Friday, December 3, 2021

JUKWAA LA KWANZA LA BIASHARA NA UWEKEZAJI LAFANYIKA ITALIA KWA MAFANIKIO MAKUBWA

Na Mwandishi wetu, Roma

Jukwaa la kwanza la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia limefanyika Jijini Roma kwa mafanikio makubwa, Italia na kuwakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji zaidi ya 250 kutoka nchi zote mbili hasa katika kipindi hiki cha Uviko 19.

Pamoja na mambo mengine, jukwaa hilo limewawezesha wafanyabiashara na wawekezaji kujadili fursa, uwezekano wa ubia, changamoto zinazokabili mazingira ya biashara na njia ya kuboresha mahusiano ya kibiashara kati ya Tanzania na Italia ambapo limendaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Italia kwa kushirikiana na Kituo cha Taifa cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Taifa ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA).

Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya ambapo Prof. Manya amewaeleza wawekezaji na wfanyabiashara kutoka Italia kuwa Tanzania kwa sasa imejikita kuwekeza katika miundombinu wezeshi ya uwekezaji, na kwamba hilo ndilo jambo ambalo Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Rais  Samia ameliweka suala la uwekezaji kama kipaumbele katika kuhakikisha kuwa wawekezaji kutoka nje na ndani ya nchi wanawekeza fedha na mitaji yao ili kukuza biashara na ajira kwa watanzania na kuwezesha uchumi wa Tanzania kusonga mbele

“Tanzania inathamini uwekezaji na sasa inapiga hatua kwa kuweka miundombinu wezeshi pia Tanzania kama nchi tunamshukuru Mungu kwamba lengo la njozi yetu na maono yetu ya Tanzania Development Vision (2020-2025) imeweza kufikia malengo yake miaka mitano kabla muda uliokuwa umepangwa. Ambapo lengo kubwa lilikuwa ni kuifanya Tanzania kwenda katika viwango vikubwa vya kiuchumi na mwaka 2020 Tanzania ilitangazwa na Benki ya Dunia kuingia katika Uchumi wa kati,” amesema Prof. Manya.

Kadhalika, Prof. Manya ameongeza kuwa katika miaka mitano inayokuja Tanzania inapoelekea kumaliza njozi yake, inatamani kuendelea kukuza uchumi na ikiwezekana ihame katika uchumi wa kati na kuhamia uchumi wa juu……na ndiyo maana imejikita kuwekeza katika miundombinu ya reli ya kati itakayotumika kusafirisha mizigo kwa umeme, ujenzi wa bwawa kubwa linaloweza kuzalisha umeme wa kutosha pamoja na barabara za kusafiri kutoka mashariki kwenda magharibi na kaskazini kwenda kusini.

Ameongeza kuwa Tanzania inajivunia kuwa na hali ya amani na utulivu na katika nchi za ukanda wa maziwa makuu Tanzania inajivunia kuwa na siasa safi yenye utulivu na amani ndani yake.

“Mfano tumeona mwekezaji aliyewekeza katika kilimo cha Pareto ameshuhudia kwa kusema kuwa Tanzania ni nchi ya amani na utlivu na kuwasihi Waitaliano kuja kuwekeza Tanzania,” ameongeza Prof. Manya.

Kupitia jukwaa hili, tunaamini kuwa litachagiza chachu ya uwekezaji zaidi nchini Tanzania na kukuza biashara kati ya Tanzania na Italia.

Mwitikio ni mkubwa na wameonesha utayari wa kuja kuwekeza zaidi Tanzania pamoja na kukuza biashara miongoni mwetu na tumewahahakikishia kuwa Tanzania ni sehemu salama na yenye mazingira mazuri ya Uwekezaji na wameahidi kuwekeza zaidi Tanzania.

Nae Balozi wa Tanzania Nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabiti Kombo amesema kuwa kufanyika kwa Jukwaa la biashara na uwekezaji lengo lake kubwa ni kuwavutia wafanyabiashara na wewekezaji wa sekta mbalimbali kutoka Italia kuwekeza zaidi Tanzania ili kukuza uchumi wa pande zote mbili.

“Mwitikio ni mkubwa sana na tumeitikiwa na Serikali ya Italia vizuri sana pamoja na jumuiya za Italia za kibishara na pia kwa upande wa Tanzania pia mwitikio ni mkubwa pia,” amesema Balozi Kombo.

Mwenyekiti wa Chama Wawekezaji wa Hoteli Zanzibar, Bw. Paulo Rosso amewasihi wawekezaji kutoka Italia kuwekeza kwa wingi Tanzania kwa kuwa mazingira ya biashara na uwekezaji ni tulivu na salama.

“Tanzania ni sehemu salama kuwekeza, ni nchi ya amani, tulivu kwa uwekezaji, karibuni sana kuwekeza Tanzania,” amesema Bw. Rosso

Katika Jukwaa hilo, Kampuni mbalimbali za Kiitaliano zimeonesha nia ya kuwekeza Tanzania ambazo ni pamoja na Kampuni ya utengenezaji Magari Ferari ambayo imeonesha utayari wa kuwekeza katika Gereji nchini Tanzania na Shirikisho la Uwekezaji katika Uchumi wa Buluu kutoka Italia pia limeonesha nia ya kuwekeza Tanzania.

Naibu Waziri, Wizara ya Madini Prof. Shukrani Manya akihutubia Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia Jijini Roma. Jukwa hilo limefanyika tarehe 2 na 3 Disema 2021 

 


Balozi wa Tanzania Nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabiti Kombo akiongea na wafanyabiashara waliojitokeza kushiriki Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Jijini Roma 


Sehemu ya Wafanyabiashara na Wawekezaji walishiriki katika Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Jijini Roma  







Thursday, December 2, 2021

WAWEKEZAJI ZAIDI YA 140 KUTOKA ITALIA WAWEKEZA TANZANIA

 Na Mwandishi wetu, Roma

Wawekezaji zaidi ya 140 kutoka Italia wamewekeza katika miradi mbalimbali nchini Tanzania

Takwimu hizo zimetolewa na Naibu Waziri Wizara ya Madini, Prof. Shukrani Manya alipokuwa akifungua jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika leo Jijini Roma, Italia.

Prof. Manya amasema kuwa miradi hiyo inathamani ya Shilingi bilioni 5 inayotoa ajira kwa watanzania zaidi ya 4000.

“Jukwa hili tunataka liendelee kuwa sababu ya kuchagiza uwekezaji mwingine kutoka Italia kwa kutumia teknolojia waliyonayo, kwa kutumia utalaamu walionao wa 'designing'…….na sasa waone kuwa Tanzania ni sehemu salama ya kuwekeza na Tanzania inaendelea kuweka mazingia wezeshe ya kukuza sekta ya uwekezaji na biashara,” Amesema Prof. Manya

Ameongeza kuwa kupitia jukwaa la biashara na uwekezaji biashara na uwekezaji utaendelea kuongezeka na kuongeza zaidi na hasa katika maeneo ambayo tumawaeleza hapa kupitia jukwaa hili.

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania Nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabiti Kombo amesema kuwa kufanyika kwa kongamano hili la biashara na uwekezaji lengo lake kubwa ni kuwavutia wafanyabiashara na wewekezaji wa sekta mbalimbali kutoka Italia kuwekeza zaidi Tanzania.

“mwitukio ni mkubwa na tumeitikiwa na jumuiya za kibiashara na wafanyabiashara na wawekezaji zaidi ya 250 kutoka nchi zote mbili wameshiriki katika kongamano hili,” amesema Balozi Kombo

Balozi Kombo ameongeza kuwa, Wafanyabiashara kutoka italia ni wabobezi katika sekta ya madini lakini pia katika utalii hivyo ni matumanini yake kuwa mara baada ya kumalizika kwa kongamano hilo wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Italia wataongezeka zaidi Tanzania.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Wawekezaji katika Hoteli Zanzibar, Bw. Paulo Rosso amewasihi wawekezaji kutoka Italia kuwekeza kwa wingi Tanzania kwa kuwa mazingira ya biashara na uwekezaji ni tulivu na salama.

“Tanzania ni sehemu salama kuwekeza…..nawahakikishia mimi nimewekeza Tanzania na ninaona ni sehemu salama ya kuwekeza karibuni sana kuwekeza kwa maendeleo ya Tanzania na Italia,” amesema Bw. Rosso

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela amewahakikishia wafanyabiashara na wawekezaji walioshiriki katika jukwaa hilo kuwa CRDB ipo tayari kutoa mikopo kwa watakao kuwa tayari kuwekeza Tanzania.

“Nawahakikishia kuwa Benki ya CRDB itawawezesha mikopo ya kuwekeza katika sekta mbalimbali hivyo msiwe na wasiwasi kuhusu mitaji ya kuwekeza ipo karibuni sana tuijenge Tanzania,” Amesema Bw. Nsekela.

Jukwa hilo la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia limehudhuriwa na Wafanyabiashara na Wawekezaji takribani 250 kutoka nchi zote mbili. Wafanyabiashara na wawekezaji hao ni wa sekta za utalii, kilimo, madini, na ujenzi.

Pamoja na mambo mengine, jukwaa hilo limewawezesha wafanyabiashara na wawekezaji kujadili fursa, uwezekano wa ubia, changamoto zinazokabili mazingira ya biashara na njia ya kuboresha mahusiano ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili.

Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia limeandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Italia kwa kushirikiana na Kituo cha Taifa cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Taifa ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA).

Naibu Waziri, Wizara ya Madini Prof. Shukrani Manya akihutubia Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika leo Jijini Roma 


 

Naibu Waziri, Wizara ya Madini Prof. Shukrani Manya akihutubia wafanyabiashara na wawekezaji walioshiriki katika Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika leo Jijini Roma 


Balozi wa Tanzania Nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabiti Kombo akiongea na wafanyabiashara waliojitokeza kushiriki Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika leo Jijini Roma 


Balozi wa Tanzania Nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabiti Kombo akiongea na wafanyabiashara waliojitokeza kushiriki Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika leo Jijini Roma 


Mkurugenzi wa Idara ya Diplomasia ya Uchumi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Edwin Rutageruka akitoa hotuba yake kwa wafanyabiashara (hawapo pichani) walioshiriki Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Jijini Roma  


Mwenyekiti wa Chama Wawekezaji katika Sekta ya Hoteli Zanzibar, Bw. Paulo Rosso akiongea na Wafanyabiashara na Wawekezaji walishiriki katika Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Jijini Roma  


Mmoja wa Wafanyabiashara kutoka Italia akiongea na Wafanyabiashara na Wawekezaji walishiriki katika Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Jijini Roma  


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Bw. Abdulmajid Nsekela akitoa hotuba yake kwa wafanyabiashara na Wawekezaji walishiriki katika Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Jijini Roma  


Sehemu ya Wafanyabiashara na Wawekezaji walishiriki katika Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Jijini Roma  



Wednesday, December 1, 2021

KIKAO CHA FOCAC DAKAR KIMEKUWA CHA MAFANIKIO - BALOZI MULAMULA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akizungumza baada ya kumalzika kwa mkutano wa nane wa Mawaziri wa Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC)

 


Na Mwandishi wetu, Dakar

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) amesema mkutano wa Nane wa Mawaziri wa Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) umefanyika kwa mafanikio makubwa.

Balozi Mulamula ametoa kauli hiyo jijini Dakr nchini Senegal baada ya kumalizika kwa kikao hicho kilichofanyika Novemba 29 na 30 2021 nchini humo.

Amesema kikao hicho kimekuwa cha mafanikio kwani kimepitisha maazimio makubwa na mpango kazi ambao umejikita katika kutekeleza maeneo ya kimkakati ambayo yakisimamiwa kikamilifu yatazinufaisha nchi za Afrika .

Balozi Mulamula amesema kauli ya China ya kuzihakikishia nchi za Afrika kuwa itasaidia kuanzisha viwanda vya kuzalisha chanjo za COVID 19 pamoja na dawa nyingine ni ya kujivunia na ya kupongezwa.

"Tanzania imefurahishwa na ahadi hiyo kwani jambo hilo litazifanya nchi za Afrika kuwa na uwezo wa kuzalisha chanjo na dawa nyingine kwa ajili ya kuwalinda watu wake na kuacha kutegemea msaada., kauli ya Rais Jinping ni ya kujivunia na ya lupongezwa,"amesema Balozi Mulamula.

Amesema kikao kimekuwa na mafanikio zaidi kwani mbali na kuangalia maeneo ya siku zote ya kuendeleza miundombinu na viwanda, kwa mara ya kwanza umeangalia jinsi ya kusaidia na kuendeleza wafanyabiashara wadogo na wa kati.

Amesema uamuzi wa China kwa kutoa kipaumbele katika eneo la kujenga viwanda vya kuzalisha dawa na chanjo na kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati ni wa kupongezwa mno kwani mambo hayo ndiyo ambayo Tanzania ilitilia mkazo katika taarifa yake na kuongeza kuwa wamefarijika kwamba Rais Jinping ameahidi kusaidia katika eneo hilo.

“Jambo hili ni zuri na kubwa sana, ni miongoni mwa maeneo ambayo Tanzania iliyasemea, eneo hilo ndiko watu wengi walikopata ajira hasa akina mama na vijana tunaishukuru na kuipongeza China  kwa kutoa kipaumbeele katika eneo hilo”, alisema Mhe. Waziri.

Amesema kikao hicho pia kimeangalia maeneo ya kujengea uwezo wananchi wa Afrika katika eneo la ufadhili wa masomo ambalo kwa wakati huu limekwama kutokana na mlipuko wa virusi vya Covid 19 lakini wameahidi kuendelea nalo pale hali itakapotengemaa.

Ameongeza kuwa kikao pia kimeangalia suala la kuendeleza kilimo ili kuwa na kilimo cha kisasa na kuendeleza miundombinu ya kidijitali hasa nyakati hizi ambazo ni lazima kujiunganisha kidigitali ili kujikwamua  kiuchumi.

Amesema China imesisitiza na kuweka mkazo katika eneo la kundeleza kilimo ili kuziwezesha nchi za Afrika kujikwamua na umasikini na wameahidi kutoa fedha na kuleta wataalamu kwa ajili ya kuendeleza kilimo.

Mkutano huo wa siku mbili ulijumuisha viongozi na wawakilishi kutoka Bara la Afrika na China uliangalia jinsi China ilivyotekeleza hatua za ushirikiano kwa kipindi cha miaka mitatu cha 2018-2021 kwenye  maeneo ya miradi ya kimkakati na ukuzaji wa wigo  wa biashara kati ya China na mataifa ya Afrika.


 

 

 

TANZANIA YASISITIZA KUUNGA MKONO, KUENDELEZA UHUSIANO NA CHINA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwa kwenye Mkutano wa nane wa Mawaziri wa ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika Jijini Dakar Senegal Novemba 29-30 2021.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akifuatilia Mkutano wa nane wa Mawaziri wa ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika Jijini Dakar Senegal Novemba 29-30 2021.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akimsikiliza mshiriki wakati wa Mkutano wa nane wa Mawaziri wa ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika Jijini Dakar Senegal Novemba 29-30 2021.


Washiriki wa Mkutano wa nane wa Mawaziri wa ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika Jijini Dakar Senegal Novemba 29-30 2021 wakipitia nyaraka mbalimbali za mkutano huo.

Washiriki wa Mkutano wa nane wa Mawaziri wa ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika Jijini Dakar Senegal Novemba 29-30 2021 wakifuatilia mkutano huo.


Tanzania imesisitiza kuunga mkono, kuendeleza ushirikiano, uhusiano na mshikamano ambao China umekuwa ukiuonesha  kwa nchi za Afrika.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula alipozungumza katika Mkutano wa nane wa Mawaziri wa ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika Jijini Dakar Senegal Novemba 29-30, 2021.

Amesema kwa kuangalia yaliyotokea katika kipindi hiki kigumu ambacho dunia inakipitia, China imekuwa ikishirikiana na Afrika kwa kutoa misaada mikubwa  ya fedha, wataalamu na vifaa kwa nchi za Afrika katika nyanja mbalimbali na kuwa na ushirikiano ambao umenufaisha pande zote.

Amesema kwa upande wa Tanzania China imekuwa ikisaidia katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati  ambayo imekuwa ikifanyika kwa kushirikiana na makampuni yao makubwa yanayowekeza chini .

Aidha Tanzania imeiomba China kuweka msisitizo mkubwa  katika sekta ya afya hasa katika kupambana na janga la ugonjwa wa korona unaosababishwa na virusi vya COVID 19 kwa kujengewa viwanda na kupatiwa uwezo wa kuzalisha chanjo hizo na dawa nyingine wenyewe. 

Waziri Mulamula amepongeza kauli ya Rais wa China Mhe. Xi Jinping ya kuwa nchi hiyo itatoa dozi billioni moja zaidi kwa nchi za Afrika ili kuziwezesha nchi  za Afrika kufikia lengo la kutoa chanjo kwa angalau asilimia 60 kwa watu wake ifikapo mwaka  2022.

“Tanzania imepokea taarifa hizo kwa mikono miwili na tunaishukuru serikali ya China kwani iliipatia Tanzania chanjo laki tano na tunategemea kupata  chanjo nyingine, na sasa kwa tangazo hilo China wametuhakikishia kwamba tutapata chanjo kwa kiasi kile tunachohitaji”, amesema Balozi Mulamula.

Mkutano huo ulijumuisha viongozi na wawakilishi kutoka Bara la Afrika na China na kuangalia ambavyo China ilivyotekeleza hatua za ushirikiano kwa kipindi cha miaka mitatu cha 2018-2021 kwenye  maeneo ya ujenzi wa maeneo maalum ya viwanda barani Afrika, ujenzi wa miundombinu ya nishati, usafirishaji, habari na mawasiliano, kukuza wigo  wa biashara kati ya China na mataifa ya Afrika.

Maeneo mengine ni kampeni ya mapinduzi ya kijani, mpango maalum wa mafunzo ya ufundi, kuboreha sekta ya Afya, ulinzi na usalama na ushirikiano katika masuala ya habari, utamaduni sanaa na michezo.