Saturday, June 18, 2022

WAZIRI MULAMULA AFANYA MAZUNGUMZO NA WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA NORWAY

Waziri wa mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. BaloziLiberata Mulamula amefanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway, Mhe. Anniken Huifeldt katika ofisi za Wizara hiyo tarehe 17 Juni 2022  jijini Oslo, Norway.

Mazungumzo ya mawaziri hao yalihusu juu ya kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili mathalan katika diplomasia, siasa na uchumi.

Pamoja na hayo masuala mengine yaliyojadiliwa kwenye mazungmzo hayo ni pamoja na umuhimu wa kufanyika kwa mageuzi ya kiuchumi ili kuwa na maendeleo jumuishi kwa wananchi wote, uhuru wa kisisasa na uhuru wa kuongea ili kuruhusu ushirikishwaji kwa makundi yote katika jamii hususan wanawake na vijana.

Aidha, nchi za Tanzania na Norway zitaendelea kushirikiana katika masuala ya afya ili kupunguza vifo vya uzazi, vifo vya watoto na masuala mengine ya ugonjwa wa UVIKO-19.

Kadhalika viongozi hao wamejadili umuhimu wa usalama na amani katika kusaidia jamii kuinuka kiuchumi na utulivu wa kufanya shughuli za kijamii kwa maendeleo ya taifa na jamii kwa ujumla.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwa kwenye mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway, Mhe. Anniken Huifeldt tarehe 17 Juni 2022 jijini Oslo, Norway. 
Waziri Mulamula yupo nchini Norway kwa ziara ya kikazi ambapo pamoja na mambo mengine viongozi hao wamezungumza juu ya kuimarisha ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya nchi hizo mbili ili kukuza biashara, uwekezaji na utalii.

Mazungumzo yakiendelea kati ya Mhe.  Waziri Mulamula na Mhe.Anniken Huifeldt
 

Kutoka kushoto Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano katika Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga na Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Seif Kamtunda wakifuatilia mazungumzo.

Kutoka kulia Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme, Afisa Ubalozi Norway, Bi. Tunsume Mwangolombe na Afisa Mambo ya Nje, Bi. Kisa Doris Mwaseba wakifuatilia mazungumzo.

Wakibadilishana zawadi.

Picha ya pamoja Mhe. Waziri Mulamula (kati), Balozi wa Tanzania nchini Norway mwenye makazi yake nchini Sweden, Mhe. Grace Alfred Olutu  (wa tatu kulia), Balozi wa Norway nchini Tanzania, Mhe. Elisabeth Jacobsen (wa tatu kushoto) pamoja na ujumbe ulioambana na Mhe. Waziri kutoka Wizarani.


TANZANIA NA NORWAY KUANZISHA USHIRIKIANO KATIKA MASUALA YA BUNGE

Serikali ya Tanzania na Norway zimeahidi kuanzisha ushirikiano katika masuala ya Bunge kufuatia ziara ya kikazi ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika Bunge hilo tarehe 17 Juni 2022 jijini Oslo, Norway.

Kufuatia ziara hiyo Mhe. Balozi Mulamula na ujumbe wake walipata fursa ya kukutana na Wajumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje na Ulinzi wa Bunge la Norway.

Mhe. Mulamula na Wajumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje na Ulinzi walijadili kuhusu umuhimu wa ushirika kwa vyama vya siasa na madhara ya chuki na uhasama, umuhimu wa kupigania na kujenga amani na umuhimu wa maridhiano kwa vyama kunapotokea tofauti.

Masuala mengine yaliyojadiliwa ni pamoja na ulinzi na usalama katika ukanda wa Afrika na Ukanda wa Ulaya pamoja na madhara mbalimbali yanayosababishwa na migogoro inayoendelea duniani.

Hata hivyo, Waziri Mulamula ametumia wasaha huo kujadili na kamati hiyo juu ya changamoto mbalimbali zinazoendelea ulimwenguni na madhara yake kwa nchi na jamii kwa ujumla. Ameiomba Norway kuendele kufadhili Mfuko wa Afya, na kushukuru kwa michango mbalimbali kutoka katika hiyo mathalan msaada wa mapambano juu ya homa ya UVIKO-19.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongea na Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ulinzi ya Norway alipofanya ziara katika Bunge hilo tarehe 17 Juni 2022 jijini Oslo, Norway. 

Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ulinzi wa Bunge la Norway wakijadili juu ya kuimarisha ushirikiano kati ya Bunge la Norwaya na Bunge la Tanzania.

Mazungumzo yakiendelea.

Mhe. Waziri Mulamula na Ujumbe wake wakifuatilia mazungumzo.



Mazungumzo yakiendelea.


WAZIRI MULAMULA AFANYA ZIARA KATIKA KAMPUNI YA EQUINOR YA NCHINI NORWAY

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amefanya ziara katika Makao Makuu ya Kampuni ya Equinor ya nchini Norway inayojishughulisha na utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi tarehe 17 juni 2022 jijini Oslo, Norway.

Akizungumza na uongozi wa kampuni hiyo Waziri mulamula amewahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo tayari kushirikiana nao katika uwekezaji wa sekta ya gesi utaofanyika mkoani Mtwara. Hivyo ni wakati sasa mipango ya utekelezaji wa mradi huo ulioingiwa makubaliano ukawekewa mkazo zaidi.

Waziri mulamula amesema kwakuwa mradi huo baada ya kukamilika unategemewa kuwa wa kwanza kwa ukubwa barani Afrika hivyo ni fursa ya ajira kwa watanzania na italeta suluhu ya changamoto za nishati sambamba na kupunguza matatizo yaliyopo sasa.

Hivyo, ametoa rai kwa kampuni ya Equinor kuweka bajeti ya kujenga uwezo kwa watanzania ili waweze kuwa sehemu ya utekelezaji wake kwa kushiriki kazi za kitaalamu zitakazowawezesha kupata uzoefu kwaajili ya miradi mingine kama hiyo

Naye Makamu wa Rais wa Kampuni ya Equinor, Ms. Unni Merethe Skorstad alieleza kuwa kampuni yake mpaka sasa imetoa zaidi ya nafasi 1000 za ufadhili za masomo katika vyuo vikuu vya nchini Tanzania ambavyo ni pamoja na chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo Kikuu cha Zanzibar na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Baadhi ya wahitimu waliofadhiliwa na kampuni hiyo wameajiriwa na sekta za nishati za nchini Tanzania na Nje ya Nchi ikiwemo Norway na wengine wameajiriwa kufundisha katika vyuo walivyosoma.

Huduma nyingine za kijamii zinazotolewa na Kampuni ya Equinor kwa Tanzania kufuatia kuingiwa makubaliano ya uchimbaji wa gesi mkoani Mtwara ni pamoja na; kujengea uwezo juu ya uelewa wa mradi huu na manufaa yake kwa jamii itakayozunguka mradi na taifa kwa ujumla, kusaidia sekta ya elimu, afya na kuwajengea uwezo wafanyakazi katika sekta ya nishati hususani katika mafuta na gesi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na ujumbe wake wakiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa kampuni ya Equinor alipotembelea Makao Makuu ya kampuni hiyo tarehe 17 Juni 2022 jijini Oslo, Norway.

Makamu wa Rais wa Kampuni ya Equinor, Ms. Unni Merethe Skorstad akiwatambulisha kwa Mhe. Waziri Mulamula vijana wa kitanzania walioajiriwa katika kampuni ya Equinor na katika vyuo vya Norway katika fani ya mafuta na gesi.



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo na uongozi wa kampuni ya Equinor ya nchini Norway.

Makamu wa Rais wa Kampuni ya Equinor, Ms. Unni Merethe Skorstad na Mshauri Maalum wa Mawasiliano wa Kampuni ya Equinor, Bw. Tarjei Skirbekk wakiwa katika mazungumzo na Mhe. Waziri Mulamula.

Uongozi wa Kampuni ya Equinor ukifatilia mazungumzo.

Sehemu ya ujumbe wa Tanzania ukifuatilia mazungumzo.

Mazungumzo yakiendelea.

Picha ya pamoja Mhe. Waziri Mulamula na watanzania wanaofanya kazi katika kampuni ya Equinor.

TANZANIA NA NORWAY ZAWEKA MSISITIZO KUKUZA DIPLOMASIA YA UCHUMI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Norway zaweka msisitizo wa kuimarisha ushirikiano kwenye Diplomasia ya Uchumi ili kuinua shughuli za maendeleo kwa mataifa hayo na kuboresha huduma kwa jamii.

Hayo yamesemwa wakati wa mazungumzo baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Norway, Mhe. Anne Beathe Tvinnereim. Mazungumzo hayo yamefanyika tarehe 17 Juni 2022 wakati wa ziara ya Mhe. Mulamula nchini Norway.

Waziri Mulamula alieleza kuwa Tanzania kupitia sera yake ya taifa na sera ya mambo ya nje imeweka mipango imara ili kuhakikisha inainua sekta za uzalishaji hususani sekta ya kilimo, biashara na utalii. Hivyo, maeneo hayo ni ya kipaumbele kwenye ushirikiano wake na mataifa mengine.  

Hata hivyo, Tanzania kupitia sekta ya kilimo inaweza  kuzalisha mazao ya biashara na hivyo kuongeza nafasi ya ajira kwa vijana sambamba na kuinua wanawake kiuchumi. Pia katika suala hilo akafafanua umuhimu wa kuwawezesha wanawake kwani wamekuwa mstari wa mbele kuzalisha mashambani na kuwa tegemeo kwa chakula cha familia na malezi kwa ujumla. 

Aidha, akafafanua umuhimu wa ushirikishwaji na kujenga uwezo kwa makundi hayo mawili sambamba na uwezeshaji katika teknolojia ili kuyafikia malengo ya kitaifa ya uzalishaji na kuyafikia masoko ya bidhaa ya kimataifa.

Naye Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Norway alieleza kuwa Serikali yake kwasasa imeelekeza ushirikiano na mataifa mengine katika biashara badala ya utoaji wa misaada. Mabadiliko haya ni sehemu ya jitihada katika kuhakikisha mataifa rafiki ya Norway yanapiga hatua kiuchumi kwa manufaa ya pande zote mbili za ushirikiano.

Kadhalika, Mhe.Tvinnereim  alipongeza kwa jitihada zinazofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha utendaji kazi. Moja ya mafanikio ya wazi katika hilo alisema ni kufikiwa kwa makubaliano kati ya serikali na Kampuni ya Equinor ya Norway inayojishughulisha na utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi.

Pia akaongeza kusema Norway inafurahishwa na mikakati iliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukuza uchumi wa bluu na kwamba ipo tayari kushirikiana katika hilo ili kuyafikia malengo yaliyowekwa kwakuwa inao uzoefu mkubwa katika sekta hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) amefanya mazungumzo na Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Norway, Mhe. Anne Beathe Tvinnereim katika ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje ya Norway tarehe 16 Juni 2022 jijini Oslo, Norway. Waziri Mulamula yupo nchini Norway kwa ziara ya kikazi itakayomalizika tarehe 18 Juni 2022.

Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Norway, Mhe. Anne Beathe Tvinnereim akizungumza na Mhe. Balozi Mulamula  katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje ya Norway tarehe 16 Juni 2022 jijini Oslo, Norway.
Kutoka kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Norway mwenye makazi yake nchini Sweden, Mhe. Grace Alfred Olutu, Mkurugenzi Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga na Afisa Mambo ya Nje, Bi Kisa Doris Mwaseba wakifuatilia mazungumzo.

Kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme, Afisa Ubalozi, Bi. Tunsume Mwangolombe na Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Seif Kamtunda wakifuatilia mazungumzo.

Mazungumzo yakiendelea, Mhe. Tvinnereim na ujumbe wake.

Mhe. Tvinnereim akimkabidhi zawadi ya kitabu cha Diplomasia, Mhe. Balozi Mulamula.





Friday, June 17, 2022

WIZARA YA MAMBO YA NJE, CRDB PLC ZASAINI MAKUBALIANO KUTENGENEZA MFUMO WA DIASPORA DIGITAL HUB

Na Mwandishi wetu, Dar

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Benki ya CRDB Plc wamesaini Hati ya Makubaliano ya kutengeneza Mfumo wa Kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora, (Diaspora Digital Hub).

Makubaliano hayo yamesainiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Plc, Bw. AbdulMajid Nsekela katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Akiongea katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo Jijini Dar es Salaam, Balozi Sokoine amesema mfumo huo wa kidigitali utaisaidia Serikali kuwatambua, kuwasajili na kuwawezesha Diaspora wa Tanzania waliopo sehemu mbalimbali ulimwenguni kupata huduma mbalimbali na kushiriki kidigitali katika shughuli mbalimbali za maendeleo, biashara, uchumi na uwekezaji.

“Ushirikiano wa Wizara na Benki ya CRDB Plc ni wa muda mrefu na wenye mafanikio mengi katika kuendelea kusukuma gurudumu la maendeleo ya Tanzania. Wizara ina imani kuwa kupitia udhamini wa shilingi milioni 100 kutoka CRDB za kutengeneza mfumo wa Diaspora Digital Hub utaboresha huduma mbalimbali zenye kukidhi mahitaji ya Diaspora kote ulimwenguni,” amesema Balozi Sokoine

Balozi Sokoine ameongeza kuwa, mfumo huo pamoja na mambo mengine, utafungua uwezekano wa fursa zaidi za ushirikiano kati ya Wizara na Benki ya CRDB katika kazi ya uendelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya Balozi za Tanzania nje ya nchi.

Balozi Sokoine ameyataja baadhi ya mafanikio ya mfumo huo ambayo ni kutekeleza kwa vitendo azma ya Serikali ya Tanzania kuhamasisha taasisi na watumishi wake kutumia ipasavyo mifumo ya kidigitali katika kutoa huduma ili kuendana na mabadiliko ya dunia na kuongeza tija katika utoaji wa huduma.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Plc, Bw. AbdulMajid Nsekela amesema CRDB inaamini kuwa kuanza kwa Mfumo wa Kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora (Diaspora Digital Hub) utakuwa na manufaa mengi kwa Serikali na Benki ya CRDB kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kusaidia kufahamu idadi ya Diaspora walioko ulimwenguni na kutunza taarifa za watanzania walioko nje.

“Diaspora Digital Hub itasaidia pia kupata taarifa za fursa za uwekezaji nchini na kuwatambua wawekezaji wenye nia ya kuwekeza nchini, kuisaidia Serikali katika zoezi la sensa litakalo fanyika mwezi Agosti, 2022, kusaidia kupata taarifa sahihi za pamoja na kuisaidia Wizara kupanga bajeti yake” amesema Bw. Nsekela

Bw. Nsekela ameongeza kuwa mfumo huo wa kidigitali utaisaidia Benki ya CRDB kuboresha zaidi huduma zake na kuwafikia wateja wengi wakiwemo Diaspora waliopo ulimwenguni.

“CRDB inaahidi kuendelea kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika kuhakikisha mfumo wa kidigitali wa Diaspora Digital Hub unakamilika kwa wakati,” amesema Bw. Nsekela

Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi James Bwana akizungumza katika hafla hiyo amesema Mfumo wa kidigitali wa Diaspora Digital Hub utakapokamilika utaiwezesha Serikali kuwa na kanzidata ya uhakika kuhusu Diaspora kote ulimwenguni.

“Mfumo huu pia utaiwezesha Wizara kutekeleza majukumu yake kwa njia ya kidigitali ambapo uratibu wa masuala mbalimbali yanayotolewa katika mfumo huo utafanyika papo kwa papo.

Balozi Bwana aliongeza kuwa kupitia mfumo huo Serikali itaweza kufahamu kwa ufasaha idadi ya Diaspora, ujuzi, elimu walizonazo na mengine mengi. Kadhalika, Diaspora wenyewe wataweza kupata kupitia mfumo huo huduma mbalimbali kwa ajili ya mahitaji yao.

Ushirikiano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Benki ya CRDB ni wa muda mrefu tangu 2010 wakati Kitengo cha Diaspora kilipoanzishwa. Ushirikiano huo umewezesha Benki ya CRDB PLC kuwa ya kwanza kuanzisha utoaji wa huduma kwa Diaspora ambapo hadi sasa zaidi ya Diaspora 30,000 wananufaika na huduma ya Tanzanite Account.


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akiongea katika hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano baina ya Wizara na CRDB ya kutengeneza mfumo wa kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora (Diaspora Digital Hub) katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

 Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Plc, Bw. AbdulMajid Nsekela akiongea wakati wa hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano baina ya Wizara na CRDB ya kutengeneza mfumo wa kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora (Diaspora Digital Hub) katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi James Bwana akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano baina ya Wizara na CRDB ya kutengeneza 'Diaspora Digital Hub' leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akiongea katika hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano baina ya Wizara na CRDB ya kutengeneza mfumo wa kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora  


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Plc, Bw. AbdulMajid Nsekela wakisaini Hati ya makubaliano baina ya Wizara na CRDB ya kutengeneza mfumo wa kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Plc, Bw. AbdulMajid Nsekela wakionesha Hati ya makubaliano baina ya Wizara na CRDB ya kutengeneza mfumo wa kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora baada ya kumaliza kusaini hati hiyo




Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Plc, Bw. AbdulMajid Nsekela wakibadilishana Hati ya Makubaliano ya kutengeneza mfumo wa kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora



Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi James Bwana pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Fedha katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Swalehe Chondoma wakifuatilia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano ya kutengeneza mfumo wa kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Plc, Bw. AbdulMajid Nsekela katika picha ya pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na watumishi kutoka Wizarani na wafanyakazi wa Benki ya CRDB baada ya kusainiwa kwa Hati ya makubaliano 



Thursday, June 16, 2022

SERIKALI YA DENMARK YAAHIDI KUENDELEZA USHIRIKIANO NA TANZANIA

    

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) amefanya mazungumzo na Waziri wa Maendeleo wa Denmark, Mhe. Flemming Møller Mortensen (kushoto) pembezoni mwa Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nordic uliofanyika tarehe 14 Juni 2022 jijini Helsinki, Finland.

Mazungumzo baina ya Mawaziri hao yalijikita katika kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia pamoja na kuendeleza sekta za biashara na uwekezaji, uchumi wa buluu na uchumi wa kijani.

Pia Waziri Mulamula ameishukuru Denmark kwa kuendelea kuwa mdau wa maendeleo kabla na baada ya Tanzania kupata uhuru wake mwaka 1961 na kwamba Serikali ya Tanzania inaendelea kusimamia kwa karibu mipango na miradi yote iliyoanzishwa kwa ushirikiano na Serikali ya Denmark.

Waziri wa Maendeleo wa Denmark, Mhe. Flemming Møller Mortensen (wa pili kushoto) akieleza kuhusiana na maeneo ya kimkakati ambayo Serikali ya Denmark itaendelea kushirikiana na Tanzania ili kuenzi ushirikiano wa kihistoria ulioanzishwa na waasisi wa mataifa hayo mawili.

Waziri Mulamula akimkabidhi zawadi, Mhe. Mortensen

Ujumbe wa Tanzania ulioambatana na Mhe. Waziri Mulamula ukifuatilia mazungumzo.




 

TANZANIA NA SWEDEN ZAAHIDI KUONGEZA MAENEO MAPYA YA USHIRIKIANO

  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amefanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Sweden, Bw. Magnus Nilsson pembezoni mwa  Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nchi za Nordic uliofanyika tarehe tarehe 13 hadi 15 Juni 2022 jijini Helsinki, Finland

Mazungumzo ya viongozi hao yalihusu ushirikiano baina ya mataifa yao hususan kwenye sekta za biashara, mageuzi katika mifumo ya taasisi za umma, haki za wanawake na watoto.

Akielezea mafanikio yaliyopatikana kufuatia misaada mbalimbali iliyotolewa na Serikali ya Sweden,  Waziri Mulamula amesema sekta ya nishati imepiga hatua kubwa nchini ambapo mashirika yote yanayosimamia sekta hiyo yameboresha utendaji wake pamoja na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Naye Bw. Nilsson alieleza kuwa Sweden itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kihistoria baina yake na Tanzania pamoja na kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano. 

Aidha, Bw. Nilsson ameahidi kuwa Serikali ya Sweden itaendelea kusaidia eneo la mageuzi ya kisekta ikiwa ni pamoja na kuziunganisha taasisi za Tanzania na Sweden zianzishe ushirikiano kwa lengo la kupeana uzoefu na kujenga uwezo.

Kadhalika, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweka mkazo katika masuala ya watoto, usawa wa jinsia na uhuru katika masuala ya siasa. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kushoto) amefanya mazungumzo wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Sweden. Bw. Magnus Nilsson (kulia) pembezoni mwa Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nordic uliofanyika nchini Finland tarehe 13 hadi 15 Juni 2022 jijini Helsinki, Finland.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje wa Sweden, Bw. Magnus Nilsson (wa pili kulia) akizungumza na Mheshimiwa Waziri Mulamula (hayupo pichani). Pamoja naye ni ujumbe alioambana nao alipokuwa nchini Finland kushiriki Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nchi za Nordic uliofanyika tarehe 13 hadi 15 Juni 2022 jijini Helsinki, Finland.

Mkutano ukiendelea, kushoto ni ujumbe wa Tanzania ulioambana na Mhe. Waziri Mulamula.

Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Finland mwenye makazi yake nchini Sweden, Mhe. Grace Alfred Olutu na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Balozi Mindi Kasiga wakifuatilia mazungumzo.

WAZIRI MULAMULA AFANYA MAZUNGUMZO NA WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA FINLAND


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amefanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland, Mhe. Pekka Haavisto pembezoni mwa  Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nordic uliofanyika tarehe 13 hadi 15 Juni 2022 jijini Helsinki, Finland.

Serikali ya Tanzania na Finland zinashirikiana katika masuala ya ubunifu wa kutengeneza ajira, usimamizi wa fedha kwa taasisi za umma, kujenga uwezo kwenye masuala ya kodi pamoja na utawala bora.
Maeneo mengine ya kipaumbele katika ushirikiano huo ni pamoja na elimu,kuinua ubia kati serikali na sekta binafsi, kuhamasisha uwekezaji, umarishaji wa demokrasia na utawala wa sheria na kukuza biashara. 
Balozi wa Tanzania nchini Finland mwenye makazi yake nchini Sweden, Mhe. Grace Alfred Olutu na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Balozi Mindi Kasiga wakifuatilia mazungumzo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland, Mhe. Pekka Haavisto akieleza utayari wa Serikali ya Finland katika kuimarisha ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya Serikali yake na Tanzania.
Ujumbe ulioambatana na Mhe. Haavisto ukifuatilia mazungumzo.

Wednesday, June 15, 2022

WAZIRI MULAMULA ASISITIZA UMOJA NA MSHIKAMANO KWA NCHI ZA AFRIKA NA NORDIC

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amesisitiza umoja na mshikamano kwa nchi za Afrika na Nordic aliposhiriki Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nchi za Nordic uliofanyika tarehe 14 Juni 2022 jijini Helsinki, Finland.


Mkutano huo ulifunguliwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland, Mhe. Pekka Haavisto ambapo aliwakaribisha wajumbe wa mkutano huo kushiriki mjadala wa vijana wa Nordic – Afrika pamoja na ajenda nyingine za majadilianao baina ya mawaziri hao.

 

Akichangia mjadala wa vijana Mhe. Waziri Mulamula amewasihi vijana waliopata nafasi ya kushiriki katika masuala mbalimbali ya kimataifa kujitoa kwa dhati ili kuleta tija katika nchi zao pamoja na kusaidia vijana wengine kupata nafasi hizo.

 

Sambamba na hilo katika nafasi nyingine ya majadiliano ya mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika na Nordic amesisitiza juu ya umoja na umuhimu wa kushirikiana katika  kukabiliana na changamoto za ulimwengu  kwa manufaa ya wote.

 

Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nchi za Nordic pamoja na mambo mengine umejadili masuala ya amani na usalama, migogoro, mabadiliko ya Tabianchi, masuala ya kimataifa, vijana na wanawake.

Mkutano wa 19 wa Mamwaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nordic umependekeza Algeria kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 20 wa Mawaziri hao unaotarajiwa kufanyika mwaka 2024.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nordic baada ya kumalizika kwa mkutano wa 19 wa Mawaziri hao jijini Helsinki, Finland.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (kushoto) akifuatilia majadiliano katika mjadala wa vijana wa Nordic - Afrika amabo ulijikita katika namna ya kuwakwamua vijana kwa kuwapa ujuzi utakaowawezesha kujikwamua kiuchumi samabamba na kushirikikishwa katika masuala ya kijamii na taifa kwa ujumla.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland, Mhe. Pekka Haavisto ( kulia) akiongoza Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Finland uliofanyika tarehe 14 Juni 2022 jijini Helsinki, Finland.

Mkutano ukiendelea.