Sunday, January 27, 2013

Tanzania yasifiwa kwa kuwa mfano wa kuiga katika Utawala Bora


Tanzania yasifiwa kwa kuwa mfano wa kuiga katika Utawala Bora


Na Ally Kondo, Addis Ababa

Tanzania imesifiwa kwa kuwa nchi pekee duniani iliyoweza kudumisha muungano wa nchi mbili kati ya Tanganyika na Zanzibar ambao mwaka 2014 utatimiza miaka 50. Muungano huo umeelezwa kuwa ni mfano na kielelezo kizuri kwa nchi za Afrika ambazo zina ndoto ya kuungana katika siku za baadaye.

Hayo yamebainishwa katika ripoti ya Tanzania kuhusu Demokrasia na Utawala Bora iliyowasilishwa katika Mkutano wa Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali walioridhia Mpango wa Nchi za Afrika wa Kujitathmini wenyewe kiutawala bora (APRM) uliofanyika nchini Ethiopia siku ya Jumamosi tarehe 26 Januari, 2013.

Ripoti hiyo ambayo iliwasilishwa na Kiongozi wa jopo la APRM, Makao Makuu  lililotembelea Tanzania kuhakiki masuala ya Demokrasia na Utawala Bora, Bw. Barrister Akere Muna ilisifia pia pamoja na mambo mengine utulivu wa kisiasa na umoja miongoni mwa Watanzania ambao alisema umechangiwa kwa kiasi kikubwa na matumizi ya lugha ya Kiswahili.

Aidha, ripoti hiyo imeainisha mapendekezo mbalimbali ambayo Serikali inatakiwa kuyafanyia kazi ili kuboresha masuala ya demokrasia na utawala bora nchini Tanzania ambayo kimsingi yanaridhisha kwa kiasi kikubwa.
Masuala hayo ni pamoja na kero za Muungano, rushwa, uhuru wa vyombo vya habari, mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi na mizozo ya kidini.

Akitoa ufafanuzi kuhusu masula hayo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete alisema kuwa Serikali yake imeunda Kamati ya Muungano ambayo imepewa jukumu la kutafuta suluhisho la kudumu ya kero za muungano. Kupitia Kamati hiyo ya Muungano, baadhi ya kero zimeshapatiwa ufumbuzi na nyingine bado zinafanyiwa kazi lakini alisisitiza kuwa kuna matumaini ya kuzipatia ufumbuzi.

Rais Kikwete aliendelea kueleza kuwa kupitia mchakato wa kukusanya maoni kuhusu mabadiliko ya Katiba unaoendelea nchini, ana matumaini kuwa maoni yanayotolewa na wananchi, taasisi za Serikali na asasi za kiraia yatasaidia kuimarisha Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar.

Kuhusu rushwa, Rais Kikwete alieleza kuwa Serikali yake imechukua hatua kwa watu wanaotuhumiwa na rushwa kwa kupelekwa Mahakamani. Alisema miongoni mwa watu ambao wameshitakiwa ni viongozi wakiwemo waliokuwa Mawaziri na Mabalozi. Vile vile,  alisema kuna Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambavyo ni vyombo vilivyoundwa kwa lengo la kudhibiti ufisadi. Aliahidi kuwa Serikali itaendelea kuviimarisha vyombo hivyo ili viwe na mbinu za kisasa za kukabilina na rushwa.

Katika suala la uhuru wa vyombo vya habari, Rais Kikwete alisema Tanzania kuna uhuru mkubwa wa vyombo vya habari ambapo wakati mwingine baadhi yao vimefikia hata kuchapisha taarifa za uzushi kuhusu Rais, bila ya kuchukuliwa hatua. Rais Kikwete alieleza kuwa anavivumilia vyombo vya habari lakini uvumilivu huo hautakuwepo pale tu chombo cha habari kitakapo andika habari zenye mwelekeo wa kuchochea uvunjifu wa amani, utulivu wa kisiasa na umoja wa kitaifa uliopo nchin Tanzania.  

Rais Kikwete aliendelea kufafanua kuwa Tanzania ina magaezi na  majarida 763, vituo vya redio 83 na vituo vya television 26 vinavyofanya kazi kwa uhuru mkubwa bila kuingiliwa na Serikali. Alisema kuwa kama Serikali ingekuwa inabana uhuru wa vyombo vya habari isingekubali kuruhusu idadi kubwa kama hiyo.

Kuhusu mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, Rais Kikwete alisema kuwa Serikali ilichukuwa hatua stahiki na za haraka na sasa unyama huo ambao kimsingi unasababishwa na washirikina umedhibitiwa kwa kiasi kikubwa, hivyo watu watu wenye ulemavu wa ngozi sasa wanatembea bila ya hofu. Alifafanua kuwa watuhumiwa wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi walipelekwa Mahakamani na wengine wametiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo au kifo.

Kwa upande wa mizozo ya kidini, Rais Kikwete alieleza kuwa kuna watu wachache nchini wanachochea machafuko ya kidini kwa manufaa yao binafsi. Alisema Serikali haizuii uhuru wa kuabudu wa ntu yoyote isipokuwa haitamvumilia mtu ambayo anatumia kisingizio cha dini kuleta mgawanyiko miongoni mwa wananchi ambao kwa muda mrefu wameishi pamoja kwa amani licha ya tofauti za kidini walizo nazo.  

Mhe. Rais Kikwete pamoja na ujumbe wake yupo nchini Ethiopia kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika ambao ulianza siku ya Jumapili tarehe 27 Januari, 2013 na utahitimishwa siku ya Jumatatu tarehe 28 Januari, 2013.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.