Friday, January 25, 2013

Ufunguzi wa Mkutano wa Mawaziri wa Umoja wa Afrika (AU)


Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Bibi Nkosazana Dlamini-Zuma akitoa hotuba ya ufunguzi ya Mkutano wa Mawaziri wa Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) mjini Addis Ababa, Ethiopia. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb) akimsikiliza kwa makini Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU wakati alipokuwa akitoa hotuba ya ufunguzi ya Mkutano wa Mawaziri wa AU.


Bw. Ally Ubwa, Afisa (kulia) kutoka Kitengo cha Sheria, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa naye akisikiliza kwa makini hotuba ya Bibi Dlamini-Zuma.




Na Ally Kondo, Addis Ababa

Kamisheni ya Umoja wa Afrika imkusudia kuandaa Mpngo Mkakati wa miaka 4 (2014-2017) ambao ndani yake utakuwa na vipaumbele 8 vitakavyopendekezwa kwa ajili ya kutekelezwa katika kipindi hicho.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Kamisheni hiyo, Bibi Nkosezana Dlamini- Zuma wakati alipokuwa anafungua mkutano wa Mawaziri wa Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) ulioanza nchini Ethiopia siku ya Alhamisi tarehe 24 Junuari, 2013.

Bibi Dlamini-Zuma alivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni kuwajengea uwezo wanadamu hususan katika masuala ya elimu, afya, sayansi, utafiti, teknolojia na ubunifu; kuendeleza kilimo na usindikaji wa mazao; maendeleo ya kiuchumi shirikishi kupitia mapinduzi ya viwanda, ujenzi wa miundombinu, kilimo, biashara na uwekezaji; na kujenga na kudumisha amani, utulivu na utawala bora.

Vipeumbele vingine ni kuwashirikisha wanawake na vijana katika maamuzi, utafutaji wa mitaji, kuufanya Umoja wa Afrika kuwa ni chombo cha wanachama wenyewe kwa kujenga mfumo madhubuti wa mawasiliano na mwisho kuimarisha uwezo wa taasisi za AU pamoja na vyombo vyake vyote ili vitekeleze majukumu yake ipasavyo.

Bibi Zuma aliendelea kueleza kuwa sera, mikakati na mpango kazi wa namna ya kutekeleza maeneo yote hayo yaliyoainishwa vimeshaandaliwa, ila kinachosubiriwa ni michango ya mawazo kutoka nchi wanachama na Jumuiya za Kikanda ili zibainishe matokeo maalum ya kila eneo.

Aidha, Mwenyekiti wa Kamisherni ya AU aligusia suala la mizozo ya kisiasa inayozuka kila siku katika Bara la Afrika ambayo inazorotesha amani na utulivu katika nchi za Afrika. Alizihimiza nchi za Afrika kuwa tayari kukabiliana na machafuko ya kisiasa hususan kwa kutokomeza vyanzo vinvyosababisha kuzuka kwa mizozo hiyo.

Ili kukabiliana na tatizo la mizozo katika Bara la Afrika,  alisisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kukamilisha uundwaji wa kikosi maalum cha kijeshi ambacho kitakuwa tayari wakati wowote kupelekwa katika nchi zitazokumbwa na mizozo ya kisiasa.   

Bibi Zuma alihitimisha kwa kueleza kuwa lazima kuwe na uwiano kati ya kutafuta amani na kupata maendeleo ya kiuchumi, kwani Afrika haitaweza kupiga hatua ya kimaendeleo bila ya masuala yote hayo mawili kushughulikiwa kwa pamoja. 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.