CHECK
AGAINST DELIVERY
HOTUBA
YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA,
MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWA WANANCHI, TAREHE 31 JANUARY, 2013
Utangulizi
Ndugu Wananchi;
Kama ilivyo ada naomba
tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwenye Rehema, kwa kutujaalia uzima na
kutuwezesha kuzungumza kwa mara
nyingine kwa kutumia utaratibu wetu huu mzuri wa mawasiliano baina ya Rais na
wananchi wa Tanzania kila mwisho wa mwezi.
Siku ya leo nitazungumzia safari yangu ya Ufaransa, Uswizi na
Ethiopia. Pia nitazungumzia ujenzi wa bomba
la kusafirisha gesi asili kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam.
Safari za Kikazi Nje ya Nchi
Ndugu Wananchi;
Safari
yangu ya Ufaransa, Uswizi na Ethiopia ilikuwa na manufaa makubwa kwa nchi
yetu. Nchini Ufaransa licha ya
kuimarisha uhusiano wa kirafiki baina ya nchi zetu, tumepata wawekezaji wengi
wakubwa wenye nia thabiti ya kuja kuwekeza hapa nchini. Pia tumekubaliana kuanza mazungumzo ya kuwa
na mpango mwingine wa ushirikiano.
Mpango wetu wa sasa ulioanza mwaka 2006 uliisha mwaka 2010. Mpango ule ulitusaidia sana kuboresha huduma
za maji katika miji ya Utete mkoani Pwani na Mpwapwa mkoani Dodoma.
Katika
mkutano wa Kongamano la Uchumi wa Dunia uliofanyika Davos, Uswizi,
tumehakikishiwa ushirikiano katika kuendeleza juhudi zetu za kuleta mapinduzi
ya kijani ili tujihakikishie usalama wa chakula na kupunguza umaskini vijijini
na kukuza uchumi wa nchi yetu. Aidha,
tulipata bahati ya kushirikishwa katika mjadala wa kuanzishwa kwa programu
kubwa ya kuzisaidia nchi za Afrika kutatua matatizo ya upatikanaji wa umeme. Naamini programu hiyo ikitekelezwa na wakubwa
kuheshimu kauli na ahadi zao itakuwa msaada mkubwa kwa maendeleo ya nchi za
Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Ndugu Wananchi;
Nchini
Ethiopia tulishiriki katika mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa
Afrika na katika kikao cha African Peer Review Mechanism (APRM) ambapo taarifa ya
tathmini ya utawala bora ya Tanzania na Zambia iliyofanywa na APRM ilijadiliwa. Kwa jumla hatuna mahali tuliponyooshewa
kidole kuwa tunafanya vibaya. Tumepongezwa
katika mambo mengi na tumepewa ushauri kwa baadhi ya maeneo waliyoona hatuna
budi kuyaboresha. Nilipata nafasi ya kusema
ambayo niliitumia kufafanua baadhi ya mambo yaliyokuwamo kwenye taarifa. Niliwashukuru na kuahidi kuufanyia kazi
ushauri uliotolewa. Tathmini ya nchi
yetu ilipitishwa kwa kauli moja.
Vurugu
za Kupinga Gesi Kusafirishwa Kutoka Mtwara
Ndugu wananchi;
Kama
mtakavyokumbuka tarehe 8 Novemba, 2012 kule Kinyerezi, Wilaya ya Ilala hapa Dar
es Salaam, niliweka jiwe la msingi la ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asili
kutoka Mtwara na Songosongo kuja Dar es Salaam.
Karibu na mwishoni mwa Desemba, 2012 kukafanyika maandamano mjini Mtwara
kupinga ujenzi wa bomba hilo. Katika
maandamano yale na baadaye kwenye kauli za wanasiasa na wanaharakati yakatolewa
madai kuwa gesi hiyo itumike kwa maendeleo ya Mtwara na kwamba yale
yanayotakiwa kufanyika Dar es Salaam yafanyike Mtwara. Pia, zilitolewa shutuma nyingine dhidi ya
Serikali eti kuwa kwa miaka mingi imewasahau na haiwajali wananchi wa Mikoa ya
Kusini na ujenzi wa bomba hilo ni muendelezo wa hayo. Kauli mbalimbali za
wanasiasa na wanaharakati ni kama vile ziliongeza mafuta kwenye kaa la moto na
kuuchochea mpaka kukatokea matukio yaliyotusikitisha na kutshtua sote. Baadhi ya ndugu zetu wamepoteza maisha na
mali za watu na Serikali kuharibiwa.
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba
yangu ya kuaga mwaka 2012 na kuukaribisha mwaka 2013, tarehe 31 Desemba, 2012,
nililisemea jambo hili. Leo mwezi mmoja
baadae, napenda kusisitiza mambo mawili.
Kwanza kwamba, si kweli kuwa Serikali inapuuza Mikoa ya Kusini. Na pili, kwamba kujenga bomba la kuipeleka gesi
Dar es Salaam hakuinyimi Mikoa ya Mtwara na Lindi fursa ya kunufaika na gesi iliyopo
Mtwara.
Ndugu Wananchi;
Serikali imefanya,
inafanya na ina mipango ya kufanya mambo mengi mazuri kwa ajili ya kuleta
maendeleo katika Mikoa ya Mtwara na Lindi.
Ipo mipango ya kuboresha miundombinu, huduma za kiuchumi na kijamii
pamoja na kukuza uchumi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanda vikubwa na
vidogo. Serikali ya Awamu ya Tatu chini
ya uongozi wa Rais Mstaafu, Mheshimiwa Benjamin Mkapa, ilijenga daraja katika Mto
Rufiji maarufu kama Daraja la Mkapa. Hii
ilikuwa ni hatua kubwa ya awali katika safari ya kutatua matatizo ya usafiri ya
Mikoa ya Kusini. Serikali ninayoiongoza
mie iliachiwa kazi ya kukamilisha ujenzi wa barabara za lami kufikia darajani
na kuunanisha Mkoa wa Mtwara na Mkoa wa Ruvuma.
Kazi hiyo, tumeitekeleza vizuri na sasa tunakaribia kuimaliza. Tulikamilisha ujenzi wa barabara ya kutoka
Mnazi-Mmoja hadi Nangurukuru. Mwaka 2009
tukaanza ujenzi wa barabara ya kilomita
56 kutoka Somanga hadi Ndundu (darajani).
Ujenzi wa kilometa 36 za
mwanzo ulienda vizuri. Bahati mbaya
ujenzi wa kilomieta 20 za mwisho
umechelewa sana kwa sababu ya mmiliki wa kampuni iliyokabidhiwa kufanya kazi
hiyo kufariki. Kwa sababu hiyo, kampuni
ilipata mtikisiko kiasi na kusababisha kazi kutotekelezwa kwa kasi
tuliyoitarajia. Sasa mambo yametengemaa
na kazi inaendelea kwa kasi nzuri.
Matumaini yetu ni kuwa ifikapo mwezi Desemba, 2013 kazi hiyo itakuwa
imekamilika.
Hali
kadhalika, Rais Mstaafu, Mzee Benjamin Mkapa alituachia jukumu la kumaliza
ujenzi wa Daraja la Umoja katika mto Ruvuma na ujenzi wa barabara ya lami
kuanzia Mikoa ya Mtwara na Ruvuma.
Tumelikamilisha Daraja hilo na ujenzi wa barabara ya lami kutoka Masasi hadi
Mangaka umekamilika. Mchakato wa kujenga
barabara ya kwenda Songea na kwenda Darajani umefikia mahala pazuri. Tenda ya ujenzi wa barabara kutoka Tunduru
hadi Mangaka mpaka Darajani imeshatangazwa.
Kama mambo yataenda sawa miezi mitatu ijayo mjenzi atapatikana. Wakati huo huo ujenzi wa barabara kutoka
Namtumbo hadi Songea – Mbinga na Namtumbo – Tunduru unaendelea. Hivyo basi, kwa barabara ya “Mtwara Corridor” kazi iliyobaki ni kutoka Mbinga kwenda
Mbambabay ambayo tutaifanya wenyewe kama tulivyofanya kwa Mnazi Mmoja –
Nangurukuru na Somanga – Ndudu na Daraja la Umoja.
Ndugu Wananchi;
Ipo pia mipango
ya kuipanua na kuijenga upya bandari ya Mtwara ili iweze kuhudumia mahitaji ya utafutaji
na uchimbaji wa gesi baharini, kuhudumia na kuvifanyia matengenezo vyombo
vinavyotumika katika utafiti, uchimbaji na uendelezaji wa gesi. Pia iweze kuhudumia shughuli za kiuchumi
zitakazotokana na uchumi wa gesi pamoja na zilizopo sasa. Nilipozungumza na makampuni ya utafutaji gesi pale
Mtwara tarehe 25 Julai, 2011 waliomba nikubali bandari ya Mtwara iwe mahali pa
kuhudumia vyombo vyote vinavyofanya shughuli ya utafutaji na uchimbaji wa gesi
na mafuta katika pwani ya Afrika ya Bahari Kuu ya Hindi. Pia waliomba kuwa sehemu hiyo ya bandari iwe
bandari huru. Niliwakubalia bila ya
kusita na tayari eneo la hekta 110 zimeshatengwa
na kutangazwa rasmi kuwa bandari huru.
Vile vile waliomba wapewe sehemu ya bandari ya sasa kuendeshea shughuli
na eneo la kujenga kituo cha mitambo ya kuchakata gesi na kusafirisha nje.
Ndugu Wananchi;
Baada ya kuzungumza
na makampuni ya utafutaji gesi na mafuta na kuelezwa mahitaji yao nilibaini
kuwa bandari ya Mtwara inahitaji kupanuliwa na kujengwa upya. Bahati nzuri viongozi wa Mamlaka ya Bandari
walikuwepo na walinihakikishia kuwa watafanya hivyo.
Tayari eneo la
bandari limeongezwa kutoka hekta 70.68
hadi 2,693.68. Eneo la bandari huru limeshatengwa hivyo hivyo
na eneo la kampuni ya Dangote na makampuni ya gesi yaliyopo. Aidha, mchakato wa kupanua bandari iliyopo,
kujenga gati mpya na kuendelea na ujenzi hadi maeneo ya Msanga Mkuu ipo katika
hatua mbalimbali za matayarisho na utekelezaji.
Ndugu Wananchi;
Kwa
upande wa Mkoa wa Lindi mipango ya kupanua na kuijenga upya bandari ya Lindi
imefikia hatua nzuri. Naibu Waziri wa
Uchukuzi, Mhe. Dkt. Charles Tizeba alithibitisha hayo tarehe 1 Desemba, 2012
nilipotembelea bandari hiyo wakati wa ziara yangu ya Mkoa wa Lindi ya tarehe 1 mpaka
5 Desemba, 2012. Hali kadhalika mipango
ya kujenga bandari ya Kilwa iko mbioni.
Tena kwa upande wa Mkoa wa Lindi moja ya makampuni yaliyogundua gesi
baharini wameamua kujenga bandari na kituo cha kuchakata na kusarifisha gesi nje
ya mkoa huo kama ilivyo kwa Mtwara.
Naambiwa wametambua maeneo matatu, kilichobakia ni kuamua mojawapo ili ujenzi
uanze.
Ndugu Wananchi;
Nilipotoka bandari ya
Mtwara, siku ile nilitembelea Chuo cha VETA na kuzungumza na viongozi wa VETA
taifa na wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuhusu kuwa na mitaala ya
kutoa mafunzo mahsusi yanayohitajika na sekta ya gesi na mafuta. Nilisisitiza kwamba tuwapatie vijana wetu
mafunzo yatakayowawezsha kuajiriwa na makampuni ya gesi na yale yatakayokuwa
yanatoa huduma kwa makampuni hayo.
Nilisema tusipofanya hivyo, makampuni hayo yataajiri watu kutoka nje na
hatutakuwa na sababu ya kuwalaumu wala kulalamika.
Nafurahi kwamba
agizo langu hilo limefanyiwa kazi ipasavyo.
Hivi sasa katika chuo cha VETA Mtwara mafunzo hayo yanatolewa. Kampuni ya PetroBrass ya Brazil inaendesha
mafunzo ya sekta ya gesi kwa vijana 25 kutoka mkoani Mtwara. Aidha, chuo cha VETA kwa kushirikiana na
Kampuni ya Gesi ya Uingereza (British Gas) na Volunteers Service Overseas ya
Uingereza, kinatekeleza programu ya miaka mitatu iitwayo Enhancing Employerbility Through
Vocational Training. Programu
hii inalenga kutoa kozi zitakazowafanya
wahitimu kuweza kuajiriwa katika sekta ya gesi.
Programu hii ilifunguliwa na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Mohamed
Gharib Bilal, tarehe 26 Novemba, 2012.
Ndugu Wananchi;
Chini ya
programu hii, walimu wa masomo yanayohusiana na gesi wanaongezewa ujuzi ili
waweze kufikia viwango vya kimataifa.
Vile vile, Wizara ya Nishati na Madini imetoa upendeleo maalum wa
kudhamini wanafunzi 50 kutoka mkoa
wa Mtwara kusoma chuoni hapo ambao tayari wameshahitimu mafunzo ya msingi ya
uunganishaji vyuma viwandani. Mchakato
wa kuwapata wanafunzi 50 kwa ajili
ya mafunzo kama hayo kutoka mkoa wa Lindi unaendelea. Nimeambiwa mpaka wameshawapata vijana 25 bado
25.
Hali
kadhalika, Wizara ya Nishati na Madini inadhamini wanafunzi 10 kupata mafunzo katika
Chuo Kikuu cha Dodoma ambako kozi za mafuta na gesi zinatolewa. Kipaumbele kwa udhamini huu unatolewa kwa
wanafunzi wa mikoa ya Mtwara na Lindi wenye sifa za kudahiliwa katika mafunzo
haya. Wamepatikana watatu. Wataalamu hawa na wengine wa fani mbalimbali
za gesi na mafuta watafundishwa kwa kiwango cha shahada ya kwanza na baadae
uzamili na uzamivu ili nchi yetu ijitosheleze kwa wataalamu wa sekta hii.
Kupanga
Mji wa Mtwara
Ndugu Wananchi;
Baada
ya kutembelea bandari ya Mtwara na Chuo cha VETA, nilikaa na kuzungumza na
viongozi wa Serikali na Manispaa ya Mtwara.
Katika mazungumzo yangu nao niliwasisitizia umuhimu wa kuwa na mpango
kabambe wa kuendeleza mji wa Mtwara – (Mtwara Masterplan) Mpango ambao utawezesha kujengwa mji mkubwa wa kisasa
unaokidhi mahitaji ya mji wa uchumi wa gesi.
Niliwataka wahakikishe kuwa kuna maeneo ya viwanda, biashara, makazi,
mahoteli, huduma za afya, elimu, mapumziko na burudani, viwanja vya michezo na
kadhalika. Kazi ya kutayarisha Masterplan hiyo imeanza na Manispaa ya
Mtwara inashirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi.
Kwa upande wa
uwekezaji nafahamu kuwa mpaka sasa makampuni 51 yameonyesha nia ya kuwekeza Mtwara katika viwanda, hoteli,
shughuli za uchukuzi na huduma hasa kwa sekta ya gesi. Wanachosubiri ni kutengewa maeneo ya kujenga,
waanze. Hivyo kukamilika mapema kwa Masterplan ya mji wa Mtwara kutasaidia
kuongeza kasi ya uwekezaji huu kufanyika.
Viwanda hivi vyote vitasaidia kuongeza ajira kwa vijana wa Mtwara na
Watanzania kwa jumla. Nimeambiwa kwa
mfano, wakati wa ujenzi wa kiwanda cha saruji watu zaidi ya 7,000 wataajiriwa.
Ndugu Wananchi;
Kabla
hata ya ugunduzi wa gesi iliyoko baharini, tulikuwa na mipango ya kutumia gesi
ya Msimbati (Mnazi Bay) kwa ajili ya kuzalisha umeme, kuzalisha mbolea na
kutumika katika kiwanda cha saruji. Kwa
upande wa umeme kulikuwa na mpango wa kujenga mtambo wa kuzalisha Megawati 300 kwa kushirikiana na
mwekezaji binafsi. Bahati mbaya wakati
wa matatizo ya kifedha ya dunia mwaka 2009 mwekezaji huyo akashindwa kupata
mkopo, hivyo mradi ukasimama kutekelezwa.
Haukufa wala haukuhamishiwa Dar es Salaam au Bagamoyo kama ambavyo
imekuwa inapotoshwa kwa makusudi. Mradi
huo bado upo, tena mpango wa sasa ni kujenga Megawati 600 zitumike Mtwara na zingine kuziingiza kwenye gridi ya
taifa kupitia Songea.
NduguWananchi;
Kwa upande wa
kiwanda cha mbolea, wawekezaji wengi wameshajitokeza tangu mwaka 2008 mpaka
sasa. Mchakato umefanyika wa kuchambua
wawekezaji wenye sifa na kutambuliwa.
Mambo mawili yamechelewesha utekelezaji kuanza. Jambo la kwanza ni wawekezaji na kampuni ya Artumas
iliyokuwa mbia na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (T.P.D.C) wakati ule,
kushindwa kukubaliana nao juu ya bei ya kuwauzia gesi. Wawekezaji walitaka bei ya gesi ipunguzwe,
lakini kampuni ya Artumas na T.P.D.C. hawakuwa tayari kupunguza zaidi ya kiasi
walichopunguza, ambacho wawekezaji bado waliona hailipi kwa kuzalisha mbolea.
Sababu ya pili ni matatizo ya kifedha
yaliyoikumba kampuni ya Artumas katika kipindi hicho. Kufuatia machafuko ya masoko ya fedha na
mdororo wa uchumi wa dunia mwaka 2008/2009 kampuni ya Artumas iliathirika na
kulazimika kuuza hisa zake kwa wawekezaji wengine. Katika kipindi hicho ilichopitia kampuni,
mazungumzo na uwekezaji wa kiwanda cha mbolea hayakuweza kupewa kipaumbele. Mtazamo wa sasa wa wabia wapya na T.P.D.C. ni
kuwa wao wenyewe sasa wawekeze katika ujenzi wa kiwanda cha mbolea. Serikali
imekubali rai yao hiyo na wanaendelea na matayarisho.
Ndugu Wananchi;
Kwa
upande wa kiwanda cha Saruji kitakachojengwa na kampuni ya Dangote
ucheleweshaji ulikuwa kwa sababu mbili.
Kwanza, kampuni ya Dangote iliomba eneo zaidi ya ililokuwa imeomba na
kupewa. Hoja yao ilikuwa kwamba eneo la
ziada walilokuwa wanaliomba ndilo lenye malighafi nyingi na bora kwa
utengenezaji wa saruji. Hivyo, waliamua
kusubiri mpaka watakapopewa eneo hilo.
Bahati mbaya
eneo hilo lilikuwa linamilikiwa na mtu mwingine na alikuwa na hati miliki
nalo. Halmashauri ya Mtwara iliomba
Serikali eneo hilo litwaliwe na baadaye ipewe kampuni ya Dangote. Serikali
ilikubali. Hata hivyo, mchakato
ulichukua muda na hata pale ulipokamilika mwenye eneo aliupinga uamuzi wa
Serikali Mahakamani. Kesi ilichukua muda
kusikilizwa na kumalizika. Bahati nzuri
Serikali ikashinda na mara baada ya uamuzi wa Mahakama ndipo kampuni ya Dangote
ikamilikishwa eneo hilo.
Kampuni nayo
ilichukua muda kuanza. Hivi sasa, timu
yake ipo kwenye eneo na mradi uko tayari kuanza kutekelezwa. Niliambiwa kuwa katika magari yaliyopigwa
mawe katika fujo za Mtwara ni pamoja na lile la mradi huu. Huo ndiyo ukweli kuhusu ujenzi wa kiwanda cha
saruji cha Dangote. Madai kuwa kiwanda
hicho kimehamishiwa Bagamoyo si ya kweli.
Ni uzushi wa makusudi wa watu
wenye nia mbaya na Serikali. Huwezi
kudai kuwa mtetezi wa wananchi wa Mtwara kwa hoja za uongo na kufanya upotoshaji
wa makusudi kabisa.
Ndugu Wananchi;
Ujenzi
wa bomba la gesi ndiyo uliozua mzozo wote huu.
Zilijengwa hisia kuwa gesi yote inapelekwa Dar es Salaam na kwamba Mtwara
itakosa gesi na maendeleo yatayotokana na gesi hiyo. Na, wengine wakasema gesi inapalekwa Bagamoyo
ili kuzidisha chumvi na kupandikiza chuki kwa wananchi dhidi ya Serikali kwamba
Rais anapeleka gesi kwao. Kwanza, Kinyerezi iko Ilala na siyo Bagamoyo. Pili, ukweli ni kwamba pale Mtwara kuna gesi
nyingi ya kutosheleza mahitaji ya Mtwara, Lindi na Dar es Salaam na kubaki. Gesi itakayoletwa Dar es Salaam ni asilimia 16 tu ya gesi yote iliyoko Mtwara
kwa miaka ishirini ijayo. Hivyo asilimia
84 ya gesi itabaki Mtwara kwa
ajili ya kuuzwa nje ya nchi na kupelekwa kwingineko nchini.
Kwa
sababu hiyo, ndugu zetu wa Mtwara hawana sababu ya kuwa na wasiwasi. Ipo gesi
ya kutosha kwa mahitaji ya sasa na ya miaka mingi ijayo. Viwanda vinavyotumia gesi kama mali ghafi na
vile vinavyohitaji gesi kama nishati vyote vitapata gesi ya kutosha. Kwa upande wa uzalishaji umeme hali kadhalika
ipo gesi ya kutosha kuzalisha umeme mwingi zaidi. Hivi sasa tunacho kituo kinachozalisha umeme
wa megawati 15 unaotumika Mtwara,
Lindi, Tandahimba, Newala, Masasi, Nachingwea, Ruangwa, na Mtama. Bado umeme
huo hautumiki wote hivi sasa.
Ndugu Wananchi;
Nayaeleza
yote haya kuwathibitishia wananchi wa Mtwara kuwa tunawathamini sana na
kuwajali. Mimi nitakuwa mtu wa mwisho kuwapuuza
na kuwatupa mkono wananchi wa Mikoa ya Kusini.
Aidha, sitakuwa tayari kuwaruhusu watu au mtu ye yote Serikalini
kuwapuuza wananchi wa Mikoa ya Kusini au mkoa wo wote hapa nchini. Hiyo haitakuwa sawa. Nilishasema siku za nyuma na napenda kurudia
tena leo kuwa kwangu mimi hakuna mkoa ulio bora kuliko mwingine. Ni kutokana na msimamo wangu huo ndiyo maana
tumeelekeza nguvu na rasilimali nyingi za Serikali katika mikoa iliyokuwa inadaiwa kuwa imesahauliwa. Kazi ya ujenzi wa barabara za lami iliyofanyika
na inayoendelea kufanyika katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Rukwa, Kigoma
na Kagera inajieleza yenyewe. Mipango ya kuboresha Kiwanja cha Ndege cha Mtwara
kufikia hadhi ya kimataifa na uboreshaji wa viwanja vya ndege vya Lindi na
Kilwa ni ushahidi mwingine kati ya mambo mengi tunayoweza kuyataja.
Ndugu Wananchi;
Haya
niliyoyasema ni sehemu ndogo tu ya yale yaliyofafanuliwa na kuelezwa kwa kina
na Mawaziri na Wakuu wa Idara husika za
Serikali na Mashirika ya Umma pale Mtwara
katika mkutano wa Waziri Mkuu na viongozi wa Serikali, dini, vyama vya siasa na
wazee wa Mkoa wa Mtwara tarehe 29 Januari, 2013.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kutumia nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo
Pinda, kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanya kule Mtwara. Uvumilivu wake, usikivu wake na utulivu wake
vimesaidia sana kulivusha taifa katika moja ya mitihani mikubwa ambayo ingeikuta
nchi yetu tangu Uhuru. Nawapongeza Mawaziri
na Wakuu wa Mashirika ya Umma na Idara za Serikali kwa mchango wao muhimu
walioutoa, uliosaidia kufafanua masuala ambayo yalikuwa hayaeleweki
vizuri. Kwa wao nawasisitiza na
kuwakumbusha wajibu wao wa kuelimisha jamii kuhusu shughuli wazifanyazo. Wakifanya hivyo mara kwa mara migongano
haitakuwepo na wapotoshaji hawatapata nafasi.
Ndugu Wananchi;
Nitakuwa
mwizi wa fadhila kama sitawashukuru viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, madhehebu
ya dini, viongozi wa jamii, wazee, wana-Mtwara na makundi mbalimbali ya jamii, kwa
muda waliotumia kuzungumza na Waziri Mkuu na kuwasikiliza wasaidizi wake
wakifafanua masuala mbalimbali.
Uvumilivu wao na uelewa wao ndivyo vilivyosaidia kurejesha hali kuwa ya
kawaida. Nawaomba nao sasa, wote kwa
pamoja washirikiane na Serikali kuelimisha umma kuhusu ukweli wa mambo. Pia watumie nafasi hiyo kutahadharisha jamii na
kuwataka watu kuwa waangalifu na kupima maneno wanayoambiwa na watu. Wajiepushe na maneno au vitendo vinavyofarakanisha,
kuchonganisha na kupandikiza chuki dhidi ya watu au Serikali. Waambieni kuwa
ghasia hukimbiza wawekezaji kwani wakipata hofu kuwa hali ya amani na usalama
ni ya mashaka, watatoka kwenda kuwekeza kwingine. Vyema iwe hapa hapa nchini, lakini wanaweza
kwenda nchi nyingine na sisi kupoteza kabisa.
Ndugu Wananchi;
Nawapa
pole wananchi wa Mtwara na Masasi kwa usumbufu walioupata kutokana na ghasia
zilizofanywa. Nawapa pole waliofiwa na
kujeruhiwa. Nawapa pole waliopoteza au
kuharibiwa mali zao. Kwa kweli inasikitisha
na kufadhaisha kuona watu wanafanya vitendo vya kuua, kuchoma moto nyumba za
watu na majengo ya Serikali pamoja na , kuharibu na kuiba mali za watu. Huu ni uhalifu ambao hauna maelezo na haukubaliki. Tunaviachia vyombo husika vya dola na sheria kutimiza
wajibu wao. Kwa waliohusika iwe fundisho
kwao na kwa wengineo kutokubali kutumika kwa maslahi ya watu wengine siku
zijazo. Sasa wameachwa pekee yao wakati
wenzao wako huru na kufaidi maisha
Ndugu Wananchi;
Hili sakata la
bomba la gesi limefika mahali pazuri.
Yaliyopita si ndwele tugange yajayo.
Mungu
Ibariki Afrika!
Mungu
Ibariki Tanzania!
Asanteni
Sana kwa Kunisikiliza!
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.