TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Kenya , Mhe.
Mwai Kibaki anatarajia kuwasili nchini tarehe 20 Februari, 2013 kwa ziara ya
kitaifa ya siku mbili. Ziara hiyo ya
Mhe. Rais Kibaki inafuatia mwaliko wa Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania . Aidha, ziara
ya Mhe. Rais Kibaki inafanyika kufuatia ziara ya Mhe. Rais Kikwete nchini Kenya mwezi
Septemba, 2012.
Mhe. Rais Kibaki ambaye anatarajiwa
kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 20 Februari, 2013 saa 9.00 alasiri,
atapokelewa na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Jakaya Mrisho Kikwete.
Akiwa
hapa nchini, Mhe. Rais Kibaki atafanya mazungumzo rasmi na Mhe. Rais Kikwete
tarehe 20 Februari 2013 kabla ya kushiriki katika Dhifa ya Kitaifa itakayoandaliwa
kwa heshima yake na Mhe. Rais Kikwete, Ikulu, Dar es Salaam .
Mhe.
Rais Kibaki anatarajiwa pia kukutana na
Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam tarehe 21 Februari, 2013, kuzindua
Barabara ya Mwai Kibaki na kutembelea Gereza Kuu la Ukonga Jijini Dar es Salaam
ili kujionea shughuli mbalimbali zinazolenga kuwarekebisha Wafungwa kuwa Raia
wema na kuwapa mafunzo ya kiufundi kuwawezesha kujitegemea wanapomaliza vifungo
vyao. Shughuli hizo ni pamoja na ushonaji, useremala na kilimo cha kisasa.
Mhe.
Rais Kibaki ataondoka nchini tarehe 21 Februari, 2013 kurejea nchini kwake.
IMETOLEWA NA: WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, DAR ES
SALAAM.
19 FEBRUARI, 2013
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.