Wednesday, August 26, 2015

Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje akutana kwa mazungumzo na Balozi wa Japan

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Libarata Mulamula akizungumza na Balozi wa Japan nchini, Mhe. Masaharu Yoshida. Mazungumzo hayo yalijikita katika Mkutano wa Sita (6) wa Tokyo wa kujadili maendeleo ya Afrika, pia kukuza na kuboresha mahusiano kati ya Tanzania na Japan katika sekta mbalimbali zikiwemo miundombinu kama vile barabara na reli.
Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Balozi Mbelwa Kairuki (kushoto) na Afisa Mambo ya Nje, Bi Bertha Makilagi wakifuatilia mazungumzo kati ya Balozi Mulamula na Balozi Yoshida (hawapo pichani) 
Balozi Yoshida (kushoto) akielezea jambo kwa Balozi Mulamula
Mazungumzo yakiendelea
 Balozi  Mulamula (kulia) akiagana na Balozi wa Japan nchini, Mhe. Masaharu Yoshida mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.

Picha na Reginald Philip

=====================================

JAPAN YAAHIDI KUIMARISHA USHIRIKIANO NA TANZANIA

Serikali ya Japan imeahidi kuendeleza ushirikiano uliopo baina yake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha sekta ya miundombinu kama barabara, reli na bandari kwa maendeleo ya haraka nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Balozi wa Japan nchini, Mhe. Masaharu Yoshida wakati akizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.

Balozi Yoshida amesema kuwa Serikali yake itaendeleza ushirikiano na Tanzania katika kuhakikisha uchumi unakua kwa kasi zaidi kwa kuboresha sekta muhimu ya miundombinu ambapo Serikali hiyo ipo tayari kuendeleza miradi mbalimbali ambayo serikali hiyo inashirikiana na Tanzania ikiwemo barabara, reli na bandari.

Balozi Yoshida alibainisha kuwa miradi ambayo tayari inaendelea hapa nchini chini ya usimamizi wa Serikali yake ukiwemo ule wa kuboresha Reli ya Kati na barabara za juu (fly-over) katika eneo la TAZARA Jijini Dar es Salaam itajadiliwa kwa pamoja na Serikali ya Tanzania, Ubalozi na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) ili kuangalia namna miradi hiyo itakamilishwa.

“Serikali ya Japan kwa sasa inaondoka katika mfumo wa kutoa misaada na kwenda kwenye uwekezaji, hivyo Tanzania ni mdau muhimu sana katika kufanikisha azma hiyo ili kila upande unufaike”, alisema Balozi Yoshida.

Akizungumzia Bandari, Balozi Yoshida alisema kuwa nchi yake ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kuboresha Bandari ya Dar es Salaam pamoja na ile ya Kigoma ili kuimarisha biashara na nchi jirani.

Akitoa taarifa kuhusu Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD VI) ambao umepangwa kufanyika mwezi Agosti 2016 nchini Kenya, Balozi huyo alisema mkutano huo pamoja na mambo mengine utazungumzia Maendeleo ya Miundombinu ya Kikanda ikiwemo mradi wa kuimarisha miundombinu ya Nchi za Kanda ya Kati ambao Japan ipo tayari kushirikiana kikamilifu na nchi za Afrika Mashariki kwa maendeleo ya nchi hizo.

Kwa upande wake, Balozi Mulamula alimshukuru Balozi Yoshida kwa niaba ya Serikali ya Japan kwa kuisadia Tanzania kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo kwa kiasi kikubwa imechangia kuboresha maisha ya Watanzania.

“Naipongeza Serikali ya Japan kwa kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi yake ya maendeleo ambayo imelenga mahitaji halisi ya jamii na kuleta maendeleo ya haraka kuanzia ngazi za chini” alisisitiza Balozi Mulamula.

Kuhusu Mkutano wa TICAD VI, Balozi Mulamula aliipongeza Japan kwa kuwezesha mkutano huo kufanyika Afrika kwa mara ya kwanza na kupongeza agenda za mkutano huo ambazo mojawapo itahusu Maendeleo ya Miundombinu ya Kikanda ambapo Tanzania itatumia fursa hiyo kuzungumzia mradi wa kuimarisha Miundombinu ya Nchi za Kanda ya Kati (Central Corridor) kwa vile Serikali imeweka umuhimu mkubwa kwenye miradi ya aina hiyo.


-Mwisho-


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.