Taarifa kuhusu ziara ya Rais wa Zimbabwe nchini
Mheshimiwa Emmerson Dambudzo Mnangagwa, Rais wa
Jamhuri ya Zimbabwe atafanya ziara ya kitaifa nchini Tanzania tarehe 28 hadi 29
Juni, 2018. Hii itakuwa ziara ya kwanza ya Mheshimiwa Rais Mnangagwa nchini
Tanzania tangu aingie madarakani mwezi Novemba, 2017.
Lengo la ziara hii ya Rais wa Zimbabwe ni
kujitambulisha kwa Rais na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tangu
aingie madarakani, Mheshimiwa Rais Mnangagwa ameshafanya ziara katika nchi za
Namibia, Zambia, Msumbiji, Angola, Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo na Botswana.
Ziara hii ni muhimu kwa Tanzania kwani itatoa fursa
ya kuimarisha na kukuza zaidi mahusiano mazuri yaliyopo ya kidiplomasia,
kihistoria, kiuchumi na kijamii kati ya nchi hizi mbili. Ziara hii pia itatoa
fursa kwa viongozi wetu kujadili masuala mbalimbali yanayohusu nchi hizi mbili
ya kikanda na kimataifa.
Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Rais Mnangagwa atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Rais Mnangagwa anatarajiwa
pia kutembelea Chuo cha Kilimo cha Wazazi Kaole Bagamoyo ambacho awali kilitumika
kutoa mafunzo kwa wapigania uhuru kutoka nchi za Kusini mwa Bara la Afrika na
Mhe. Rais Mnangagwa ni miongoni mwa waliopata mafunzo katika chuo hicho.
Mhe.
Rais Mnangagwa anatarajiwa kuondoka tarehe 29 Juni 2018 kurejea chini Zimbabwe.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 27 Juni, 2018
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.