Gavana wa Kaunti ya Uasin Gishu, Mhe. Jackson K. Mandgo akivishwa vazi la kabila la Wamaasai kutoka Tanzania na kukabidhiwa mkuki na Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe.Dkt.
Pindi Chana wakati wa sherehe ya siku ya Tanzania zilizofanyika sambamba na maonesho ya Jua
Kali/Nguvu Kazi ===============================================
Gavana wa Kaunti ya Uasin
Gishu nchini Kenya, Mhe. Jackson K. Mandgo amezishauri Serikali za Nchi
Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuweka bidhaa za wajasiriamali katika
maduka makubwa (super market) ili wananchi kuzinunua na kuacha tabia ya
kuthamini bidhaa za kutoka nje.
Gavana Mandgo aliyasema
hayo wakati wa kusherehekea siku ya Tanzania iliyofanyika sambamba na maonesho
ya 19 ya Afrika Mashariki ya Jua kali/Nguvu Kazi yanayoendelea katika Viwanja
vya michezo vya Kaunti ya Uasin Gishu mjini Eldoret Kenya ambapo alikuwa mgeni
rasmi kwenye siku ya Tanzania. Mhe. Mandgo alisema kwamba bidhaa za
wajasirimali kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zinakidhi
vigezo vya kuuzwa katika maduka hayo kutokana na kuwa na ubora wake.
Katika maonesho ya Jua
Kali/Nguvu Kazi kila nchi husherehekea siku yake kwa kutangaza bidhaa na
utamaduni wake. Tanzania ilitumia fursa hiyo kusherehekea miaka 57 ya Uhuru wa
Tanzania Bara iliyoadhimishwa nchini kote tarehe 9 Desemba 2018.
Gavana Mandgo alisema
kwamba wajasiriamali wanauwezo mkubwa wa kutengeneza bidhaa bora
ambazo kwa bahati mbaya hazipatikani katika maduka makubwa (super makert) hivyo
alitoa wito kuwa wakati umefika sasa kwa bidhaa hizo kuuzwa katika maduka hayo.
Aidha alizishauri nchi za
Jumuiya ya Afrika Mashariki kuvitumia Vituo vya Elimu za Ufundi kama VETA
hapa nchini, kutoa taaluma zaidi kwa wajasiriamali kwa lengo la kuzalisha
bidhaa zenye ubora na viwango vya kimataifa.
Alisema kwamba
Serikali ya Kenya hususan Kaunti ya Uasin Gishu ya Eldoret itapeleka
Mswada katika Baraza lake kwa kufanyia marekebisho ya sheria ya kutoa vyeti kwa
wajasiriamali ambao watatahiniwa kwa ubora wa bidhaa ambazo
wanazalisha badala ya kufanya mitihani ya kuandika.
Pia alizitaka ofisi zote za
Serikali ya Kaunti ya Uasin Gishu, kutumia samani zinazotengenezwa na
wajasiriamali kutokana na kuwa ni madhubuti na zenye
ubora kuliko zilivyotengenezwa kutoka nje ya Afrika Mashariki.
Gavana Mandgo ameipongeza
Tanzania kwa kusherehekea miaka 57 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.