Mhe. Waziri Ummy akiagana na Mhe. Prof Anas mara baada ya mazungumzo yao. =======================================================
TANZANIA NA MOROCCO KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA SEKTA YA AFYA
Mhe.Ummy Mwalimu amekutana na kufanya mazungumzo na Mhe.Prof. Anas
Doukkali, Waziri wa Afya wa Falme ya Morocco pembezoni mwa Mkutano Maalum wa 4
wa Afya ya Mama na Mtoto uliofanyika jijini New Delhi hivi karibuni.
Pamoja na mambo mengine, Mawaziri hao walijadili
namna ya kukuza na kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Morocco hususan katika
Sekta ya Afya ikiwemo uzalishaji wa dawa za binadamu, mafunzo kwa wataalam wa afya,
wakiwemo Madaktari, Wauguzi hususan wa idara za wagonjwa mahututi katika Hospitali
zote za Mikoa na Wilaya.
Aidha, walijadili namna ya kubadilishana ujuzi
wa Wataalam wa Afya kwa ajili ya kuwaongezea ujuzi, kuimarisha huduma za afya katika
kukinga magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) na yanayoambukiza kama vile VVU/UKIMWI
pamoja kuimarisha huduma za mama na motto.
Kwa upande wake, Mhe. Ummy aliiomba Serikali ya
Morocco kusaidia kujenga Hospitali ya Wazazi (Maternity Hospital) jijini Dodoma
ambapo Mhe. Prof. Anas amesema atapeleka ombi hilo kwa Mfalme wa Morocco,
Mtukufu Mfalme Mohamed VI.
Katika kuhakikisha makubaliano hayo, yanatekelezwa
mapema, wamekubaliana Wizara kuteua Mtumishi Mwandamizi mmoja awe mratibu wa masuala
hayo. Pia, wamekubaliana kuwa uandaliwe Mkataba wa Ushirikiano (MoU) ili waweze
kusaini makaubaliano hayo na kuanza kuyatekeleza mapema iwezekanavyo.
Sambamba na hilo, Waziri wa Afya wa Morocco,
Mhe. Prof. Anas ameahidi kuitembelea Tanzania mwishoni mwa mwezi Februari, 2019
ili kujionea utoaji wa huduma za afya nchini, ambapo ameahidi kuja na Wataalam wa
Wizara yake pamoja na Wawekezaji kutoka Morocco hususan kwenye eneo la viwanda vya
dawa.
-Mwisho-
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.