Thursday, March 31, 2022

Balozi wa Tanzania, DRC Awasilisha Nakala za Hati za Utambulisho

Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Said Juma Mshana (kushoto) akiwasilisha Nakala za Hati za Utambulisho kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje, wa DRC, Mhe. Chritophe Lutundula Pen Apala jijini Kinshasa  tarehe 30 Machi, 2022.
Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Said Juma Mshana  akiwa katika picha pamoja na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje, wa DRC, Mhe. Chritophe Lutundula Pen Apala jijini Kinshasa  tarehe 30 Machi, 2022.mara baada ya kuwasilisha Nakala za Hati za Utambulisho.

TEKNOLOJIA ILIYOLETWA NA MWEKEZAJI DIASPORA ANAYEISHI NCHINI CANADA YAVUTIA SEKTA ZA UJENZI NCHINI

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inaratibu ziara ya wiki mbili ya Mwekezaji Diapora kutoka nchini Canada, Bw. Joseph Katallah ambaye ameonesha nia ya kuwekeza katika miundombinu ya barabara.

Bw. Katallah anashirikiana na Kampuni ya Geopolymer Solutions LLC ya nchini Marekani inayomilikiwa na Bw. Rodney Zubrod ambayo imebuni teknolojia mpya ya ujenzi wa barabara  za lami na madaraja yanayotumia teknolojia hiyo. Pia teknolojia hiyo hutumia mabaki ya uchafu wa migodini na viwandani hususani viwanda vinavyotengeneza alumina na vioo. Uchafu huo kitaalamu huitwa matope mekundu.

Aidha, kampuni hiyo imefanikiwa kuwa na bidhaa nyingine zaidi ya barabara katika nchi za Canada, Uingereza na Uholanzi ambapo wametengeneza vifaa vya kuzimia moto, kupiga plasta na kuzuia kutu kwenye majengo na matanki ya kuhifadhia bidhaa mbalimbali.

Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Tagie Daisy Mwakawago ameeleza kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imefanikiwa kuwakutanisha wawekezaji hao na sekta za ujenzi nchini kwa lengo la kuinadi teknolojia hiyo mbadala ya geopolymer na matumizi yake ambayo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa nchini Canada, Marekani na Uingereza.

Akaongeza kuwa Bw. Katallah ni mmoja wa wanadiaspora ambaye amehamasika kurudisha ubunifu wake nyumbani. Pamoja na kuonesha nia ya kuwekeza katika miundombinu ya barabara pia amewekeza katika miradi ya kilimo, ujenzi wa shule (iitwayo shamba darasa kwa vijana walioishia darasa la saba hadi kidato cha sita) pamoja na ujenzi wa barabara ya mfano inayotumia teknolojia ya “nano” mkoani Singida.

Kadhalika uwezo wa teknolojia hiyo mbadala ya Geopolymer kutumia uchafu wa migodini na viwandani ni sehemu ya mikakati ya utunzaji wa mazingira. Bila kuathiri taratibu za ujenzi unatumika sasa imeelezwa kuwa teknolojia hiyo mpya italeta unafuu wa gharama za ujenzi kufuatia uwepo wa rasilimali za kutosha nchini na hivyo kuhitaji utaalamu na vifaa.

Idara za ujenzi zilizokutana na wawekezaji hao ni pamoja na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi tarehe 28 Machi 2022; Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini –TARURA tarehe 30 Machi 2022; Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) tarehe 30 Machi 2022 na Wakala wa Barabara Tanzania - TANROADS wanatarajia kukutana na wawekezaji hao tarehe 1 Aprili 2022.

Pamoja na Mwekezaji huyo Diaspora anayeishi nchini Canada Wizara kupitia idara ya Diaspora inaendelea kuhamasishaji Diaspora wengine wenye malengo ya kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini na inawahakikishia ushirikiano katika hatua za kurasimisha uwekezaji.

==========================================

Kikao kati ya Wawekezaji na Uongozi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - TAMISEMI kilichofanyika tarehe 30 Machi 2022 jijini Dodoma. 
Kulia ni Mkurugenzi wa Miundombinu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhandisi Gilbert Mwoga; kulia kwake ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Tagie Daisy Mwakawago; Rais wa Kampuni ya Geopolymer Solutions LLC kutoka nchini Marekani, Bw. Rodney Zubrod; Mhandisi Idara ya Miundombinu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhandisi, Gilbert Mfinanga na Mwekezaji mzawa kutoka nchini Canada, Bw. Joseph Katallah.

Mazungumzo yakiendelea.

===================

Kikao kati ya Wawekezaji na Wakala wa barabara Vijijini na Mijini - TARURA kilichofanyika tarehe 30 Machi 2022 jijini Dodoma.
Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Tagie Daisy Mwakawago akiteta na Mkuu wa Kitengo cha Tafiti na Udhibiti Ubora - TARURA, Dkt. Philemon Msomba wakati wa kikao pamoja na wawekezaji kilichofanyika tarehe 30 Machi 2022 kwenye ofisi za makao makuu ya TARURA jijini Dodoma.


Kikao kikiendelea.
Mwekezaji  kutoka nchini Canada, Bw. Joseph Katallah (kushoto) akifafanua juu ya teknolojia mpya ya Geopolymer na matumizi yake, pembeni yake ni Rais na mmiliki wa Kampuni ya Geopolymer Solutions LLC ya nchini Marekani, Bw. Rodney Zubrod.

Kikao kikiendelea 

Kikao kikiendelea.

Wednesday, March 30, 2022

SERIKALI YAENDELEA KUWASIHI WAWEKEZAJI KUWEKEZA NCHINI

Na Mwandishi wetu, Dar

Serikali imeendelea kuwasisitiza Wawekezaji na Wafanyabiashara kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kuwa Tanzania ni salama kwa biashara na uwekezaji na kuwasihi kuendelea kuwekeza kwa wingi. 

Akizindua Ripoti ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya nchini ya mwaka 2022 kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) amesema kuwa Tanzania ni salama kwa uwekezaji na ufanyaji wa biashara na kuwasihi wawekezaji kutoka mataifa ya Ulaya kuendelea kuwekeza kwa wingi nchini.

“Tunapoendelea na juhudi za kuimarisha mazingira ya biashara na kukuza uwekezaji nchini Tanzania, napenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha wawekezaji zaidi kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kuwekeza nchini Tanzania. Tanzania ni nchi yenye amani na utulivu na imejaaliwa kuwa na fursa nyingi za uwekezaji hasa katika maeneo ya kimkakati yakiwemo mafuta na gesi, madini, viwanda, utalii, uchumi wa bluu, kilimo na mifugo, amesema Balozi Mulamula.

Balozi Mulamula ameongeza kuwa, ripoti hiyo inaonyesha kuendelea kwa uhusiano mzuri na imara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya kwa  maslahi ya ustawi wa uchumi. Ripoti hii itatumika kama kielelezo cha uwezekano wa kuibua wa uwekezaji wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania.

Napenda kuwahakikishia wawezeji na wafanyabiashara kutoka Umoja wa Ulaya kuwa ripoti iliyozinduliwa leo tumeipokea vyema na Serikali tutaendelea kufanya kazi ya kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini ili kuwavutia zaidi wawekezaji na wafanyabiashara.

Kwa upande wake Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Mhe. Mafredo Fanti amesema kuwa Umoja wa Ulaya ni mshirika mkuu wa biashara na uwekezaji kwa Tanzania, na kuongeza kuwa makampuni ya nchi 10 za EU zilikuja kuwekeza Tanzania Dola za Kimarekani bilioni 1.5 kati ya 2013 na 2020.

“Tunaamini kuwa Tanzania inatoa fursa kubwa zaidi za uwekezaji  hivyo EU inaunga mkono sera ya Tanzania ya kuunganisha mfumo wa kisheria na kiutawala ili kuweza kuwavutia zaidi wawekezaji na wafanyabiashara kuja kuwekeza hapa nchini,” amesema balozi Fanti

Uzinduzi wa Ripoti ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya nchini, umehudhuriwa na Mabalozi wa nchi za Ulaya, Jumuiya ya wafanyabiashara wa Ulaya nchini, Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe Pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge – Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe. David Kihenzile.

Katika tukio jingine, Waziri Mulamula amekutana kwa mazungumzo na Balozi wa Nigeria nchini Mhe. Hamisu Umar Takamawa na kujadili mambo ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Nigeria katika sekta za uwekezaji, biashara, elimu, madini na uhusiano wa kimataifa.

Pamoja na mambo mengine, Waziri Mulamula amemhakikishia Balozi wa Nigeria ushirikiano wa kutosha wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake hapa nchini.



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwasilisha hotuba yake wakati wa uzinduzi wa  Ripoti ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya nchini ya mwaka 2022 Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwasilisha hotuba yake wakati wa uzinduzi wa  Ripoti ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya nchini ya mwaka 2022 Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Hamisu Umar Takamawa katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam  



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Hamisu Umar Takamawa  







Monday, March 28, 2022

MTANZANIA ANAYEISHI NCHINI CANADA AONESHA NIA YA KUWEKEZA NCHINI KATIKA SEKTA YA MIUNDOMBINU YA BARABARA

Mtanzania anayeishi nchini Canada Bw. Joseph Katallah ameonesha nia ya kuja kuwekeza nchini katika sekta ya miundombinu kwa kushirikiana na kampuni ya Geopolymer Solutions LLC ya nchini Marekani hususan kwenye ujenzi wa barabara za lami kwa kutumia teknolojia mpya iliyogunduliwa na kampuni hiyo.


Wawekezaji hao wanaoratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wapo nchini kwa ziara ya wiki moja ambapo wanatumia fursa hiyo kukutana na wataalamu wa sekta ya barabara kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini Tanzania - TARURA, Wakala wa Barabara Tanzania  - TANROADS, na Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.


Lengo la ziara ya wawekezaji hao pamoja na mambo mengine ni kuitangaza teknolojia mpya ya utengenezaji wa barabara za lami zisizotumia saruji ya kiwandani na badala yake zitatumia udongo mwekundu ambao pia unapatikana nchini.


Wawekezaji hao wameeleza kuwa Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kupewa kipaumbele katika uwekezaji wa teknolojia hiyo kufuatia uwepo wa rasilimali za kutosha hapa nchini zitakazowezesha matumizi ya teknolojia hiyo yenye gharama nafuu na rafiki kwa mazingira ili iweze kutumika kuchochea maendeleo chanya kwa Taifa.


Wakati huo huo, wataalamu kutoka sekta ya barabara wameeleza kuwa ni vema uwekezaji wa aina hiyo ukafuata taratibu zilizowekwa katika mfumo wa Serikali na kuruhusu kufanyika kwa tafiti inayopimika ili kujiridhisha na ufanisi wake katika ardhi na hali ya hewa ya Tanzania.


Vilevile, wakaeleza umuhimu wa teknolojia hiyo kufanyiwa majaribio katika maeneo korofi kufuatia wawekezaji hao kueleza ufanisi wa teknolojia hiyo katika maeneo mengi korofi ambayo kampuni zenye teknolojia nyingine zimeshindwa kukidhi na kudhibiti changamoto hiyo.


Hivyo, kikao hicho kiliazimia wawekezaji hao wakutane na wataalamu wanaoshughulikia viwango vya ubora wa barabara nchini ili kujihakikishia ubora na ufanisi wa teknolijia hiyo mpya kabla ya kufikia hatua ya kukubaliana na uwekezaji huo.  Pia uhakiki huo utasaidia kufahamu unafuu wa gharama, uokoaji wa muda, sambamba na upekee na uwezo wa teknolojia hiyo mpya ukilinganishwa na teknolojia inayotumika sasa.


Kampuni ya Geopolymer Solutions LLC inauzoefu wa kufanya kazi katika nchi za Canada, Marekani na Uingereza.  Kwa upande wa nchi za Bara la Afrika, pamoja na kutoa kipaumbele kwa Tanzania pia nchi ya Ghana imeonesha kuhitaji kujifunza teknolojia hiyo mpya.

 ==================================

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Tagie Daisy Mwakawago (Kushoto) akifafanua jambo kwenye kikao kati ya Wawekezaji wa Kitanzania wanaoishi Ughaibuni (Diaspora) na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) na Taasisi zake ambao ni; (Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini - TARURA, Wakala wa Barabara Tanzania-TANROADS) na Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kilichoratibiwa na Idara hiyo. Kulia ni Mkurugenzi Wa Barabara katika Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) Mhandisi John Ngowi.



Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) Mhandisi, Alois Matei (kulia) akitoa ufafanuzi juu ya taratibu za ugunduzi wa teknolojia mpya na uwekezaji zinavyofanyika nchini ili kuweza kurasimisha ugunduzi huo unaofanywa na Watanzania pamoja na Wawekezaji kutoka Nje. Kulia kwake ni Rais wa Kampuni ya Geopolymer Solutions, LLC, Bw. Rodney Zabrod, Bw.Amon Mahuza, Mtanzania mwenyeji aliyeambatana na wawekezaji hao na Bw. Joseph Katallal mtanzania anayeishi nchini Canada.

Wajumbe wengine kutoka sekta za Ujenzi wakifuatilia kikao hicho.

Kikao kikiendelea.

Bi. Mwakawago akizungumza na Mhandisi John ngowi na Dkt. Philemon Msomba kutoka Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TATURA) mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho.

 

TANZANIA YASHIRIKI MAKABIDHIANO YA MAJUKUMU YA BARAZA LA AMANI NA USALAMA LA UMOJA WA AFRIKA

Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Afrika, Mhe. Balozi Innocent Shiyo ameongoza ujumbe wa Tanzania katika hafla ya kupokea majukumu ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika yaliyokabidhiwa kwa Nchi 15 wanachama wapya, Tanzania ikiwemo na wajumbe wa Baraza hilo wanaomaliza muda wao.

Hafla hiyo ambayo imefanyika hivi karibuni jijini Maseru, Lesotho na kuratibiwa na Sekretarieti ya Umoja wa Afrika, ilitanguliwa na warsha iliyolenga kuwawezesha Wajumbe wa Baraza kubadilishana uzoefu na kujenga uelewa wa pamoja kuhusu majukumu ya Baraza hilo.

Wakati wa warsha hiyo ambayo ilifunguliwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa wa Ufalme wa Lesotho, Mhe. Mats’epo Ramakoae, Wawakilishi wa Kudumu wa Nchi Wanachama 15 wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika walibadilishana uzoefu kuhusu mamlaka na taratibu za Baraza hilo, vihatarishi kwa amani na usalama barani Afrika na namna ya kuimarisha ufanisi wa Operesheni za Kulinda Amani za Umoja wa Afrika. Aidha, maeneo ambayo yanakusudiwa kupewa kipaumbele na Baraza jipya pia yalijadiliwa.

Akizungumza baada ya warsha hiyo, Mhe. Balozi Shiyo alieleza kuwa, Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika na watu wa Afrika kwa ujumla wana matarajio makubwa kwa chombo hicho katika kuchangia na kuimarisha hali ya amani na usalama barani Afrika, Bara ambalo linakabiliwa na changamoto nyingi. “Tanzania chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan itaendelea kutoa mchango wake kikamilifu ikiwa ni pamoja na kutumia Baraza la Amani na Usalama kutatua changamoto za kiusalama na kuimarisha amani na utulivu barani Afrika” alisema Balozi Shiyo.

Itakumbukwa kuwa,Tanzania ilichaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika katika Mkutano wa 35 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika mwezi Februari 2022. Tanzania itahudumu kwenye Baraza la Amani na Usalama kwa kipindi cha miaka 2 kuanzia tarehe 01 Aprili 2022. Nchi 15 Wanachama wapya wa Baraza jipya la Amani na Usalama ni Burundi, Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Djibouti, Gambia, Ghana, Morocco, Namibia, Nigeria, Senegal, Afrika Kusini, Tanzania, Tunisia, Uganda na Zimbabwe.

Kwa mujibu wa Mkataba ulioanzisha Umoja wa Afrika, Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika ni chombo cha kudumu na cha maamuzi kuhusu masuala yote yanayohusu kuzuia, kukabiliana na kusuluhisha migogoro barani Afrika.

Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Afrika, Mhe. Balozi Innocent Shiyo akikabidhiwa Bendera ya Taifa kutoka kwa Mkuu wa Utawala wa Ubalozi wa Tanzania, Ethiopia, Bi. Elizabeth Rwitunga kama ishara ya kupokea rasmi majukumu ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi 15 zinazounda Baraza hilo. Hafla hiyo imefanyika hivi karibuni jijini Maseru, Lesotho. Tanzania ilichaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika katika Mkutano wa 35 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika mwezi Februari 2022. Tanzania itahudumu kwenye Baraza  hilo kwa kipindi cha miaka 2 kuanzia tarehe 01 Aprili 2022.

Mhe. Balozi Shiyo (wa nne kushoto) akiwa na wajumbe wengine wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika mara baada ya wajumbe hao wapya 15 kukabidhiwa majumu ambayo yataanza kutekelezwa rasmi tarehe 01 Aprili 2022.

Picha ya pamoja

Wajumbe wengine wakiwa na Bendera za Nchi zao mara baada ya kukabidhiwa majukumu ya Baraza la Amani na Uslama la Umoja wa Afrika.

TANZANIA, LIECHTENSTEIN KUWEKEZA KATIKA KILIMO HAI

Na Mwandishi wetu, Dar

Tanzania na Liechtenstein zimekubaliana kuweka mpango mkakati wa kuwekeza katika kilimo hai na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo katika mikoa ya Morogogo na Dodoma.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam wakati alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Liechtenstein Mhe. Dominique Hasler ambaye yuko nchi kwa ziara ya kikazi.

Katika mazungumzo hayo viongozi hao wamekubalia kuangazia maeneo mapya ya ushirikiano katika sekta za Utalii, Viwanda, na Elimu, hususan kumuendeleza mtoto wa kike katika masomo ya sayansi na teknolojia.

“Tumekubaliana mara baada ya ziara yake tuweze kuangazia namna gani tunaweza kudumisha na kuendeleza maeneo mapya ya ushirikiano baina yetu kwa maslahi ya Tanzania na Liechtenstein,” Amesema balozi Mulamula.

Nae Waziri wa Mambo ya Nje wa Liechtenstein Mhe. Dominique Hasler amesema Liechtenstein ina uhusiano imara na wa siku nyingi, na tumekuwa tukisaidia miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopo hapa nchini Tanzania hivyo kuja kwetu hap ani kuja kuiona miradi hiyo na kutuwezesha kujadiliana kwa pamoja ni namna gani tunaweza kuendele kushirikiana katika miradi hiyo.  

"Katika kikao changu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania tumejadili mambo mbalimbali ya ushirikiano baina ya nchi zetu, lakini kubwa kabisa tumekubaliana kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano," Amesema Waziri Hasler.

Waziri Hasler akiwa nchini atatembelea miradi mbalimbali ya kilimo hai inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Liechtenstein kupitia Sustainable Agriculture Tanzania (SAT) katika mkoa wa Morogoro na Dodoma.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Liechtenstein Mhe. Dominique Hasler akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje wa Liechtenstein Mhe. Dominique Hasler katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akimfafanulia jambo Waziri wa Mambo ya Nje wa Liechtenstein Mhe. Dominique Hasler katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula na Waziri wa Mambo ya Nje wa Liechtenstein Mhe. Dominique Hasler kikiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mjumbe aliyeambatana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Liechtenstein Mhe. Dominique Hasler akifafanua jambo wakati wa kikao 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Liechtenstein Mhe. Dominique Hasler na Mkurugenzi Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme (kulia mwa Balozi Mulamula). Wengine ni Viongozi walioambatana na ujumbe wa Waziri Hasler pamoja na Afisa Mwandamizi kutoka wizarani 





Friday, March 25, 2022

NGORONGORO YAIKUTANASHA SERIKALI NA MABALOZI, WAKUU WA MASHIRIKA YA KIMATAIFA NA WADAU WA MAENDELEO

Na Waandishi Wetu, Dar

*Yasema inazingatia Haki za Binadamu na kuwawezesha wale watakaoondoka kwa hiyari katika maeneo hayo

Serikali imesema haitamzuia mtu yeyote anayetaka kuondoka kwa hiyari katika eneo la Ngorongoro kwenda kuishi popote nchini na kuwataka wadau wengine kutowazuia wanaotaka kuondoka katika eneo hilo.

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damasi Ndumbaro ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Mabalozi, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Wadau wa Maendeleo kuhusu mpango wa serikali wa kutafuta suluhu ya kudumu katika eneo la Ngorongoro na Loliondo na kuongeza kuwa itawawezesha wale wote wanaotaka kuondoka kwa hiyari katika maeneo hayo.

Dkt. Ndumbaro amewaeleza Mabalozi hao kuwa mpaka sasa jumla ya kaya 164 sawa na watu 915 wamejiandikisha kuondoka Ngorongoro kwa hiyari na kwenda kuishi katika maeneo mbadala watakayopewa na Serikali ikiwa ni pamoja na kuwajengea nyumba ama kuwalipa fidia.

Waziri Ndumbaro ameongeza kuwa Serikali imeamua kuchukua hatua hiyo ili kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizojitokeza katika eneo la Ngorongoro ikiwa ni kuongeza kwa binadamu kutoka 8000 mwaka 1959 hadi kufikia 110,000 kwa sasa ikiambatana na ongezeko la mifugo kutoka mifugo 200,000 mwaka 1959 hadi kufikia mifugo 1,000,000 kwa sasa jambo linaloathiri ikolojia na uhifadhi, maendeleo ya utalii na maendeleo ya jamii ya wanaoishi Ngorongoro.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akiwa ameambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Balozi Fatma Rajabu amesema dhumuni la kuwaita Mabalozi hao pamoja na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa ni katika jitihada zinazofanywa na Serikali kuhakikisha Mabalozi na wadau wa Maendeleo wanapata taarifa sahihi kuhusu suala la Ngorongoro na Loliondo kutokana na kugubikwa na upotoshaji.

Ameongeza kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeweka utaratibu wa kuzikutanisha Wizara za kisekta na  Mabalozi, Wakuu wa Masharika ya Kimataifa na Wadau wa Maendeleo mara moja kila baada ya miezi 3 lengo likiwa ni kutoa fursa kwa Serikali kutoa ufafanuzi wa masuala mtambuka ya serikali na kuruhusu majadiliano yanayosaidia wadau hao kuwa na taarifa sahihi pamoja na kuwa na uelewa wa pamoja.

Akichangia mjadala huo, Balozi wa Ujerumani nchini, Mhe. Regina Hess ameunga mkono jitihada za Serikali za kulinda uhifadhi na mazingira katika eneo la Ngorongoro ili kukabiliana na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damasi Ndumbaro akiongea na Mabalozi, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Wadau wa Maendeleo  (hawapo pichani) Jijini Dar es Salaam  

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akiongea na Mabalozi, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Wadau wa Maendeleo  (hawapo pichani) Jijini Dar es Salaam  

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma Rajab akiongea na Mabalozi, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Wadau wa Maendeleo Jijini Dar es Salaam 

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damasi Ndumbaro (mwenye tai ya bluu) akiongoza mkutano kati ya Serikali na Mabalozi, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Wadau wa Maendeleo  (hawapo pichani) Jijini Dar es Salaam. Wengine katika meza kuu ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Francis Michael pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma Rajab.

Balozi wa Denmark nchini, Mhe. Mette Norgaard Spandet akitoa maoni yake wakati wa mjadala kuhusu jitihada za Serikali za kulinda uhifadhi na mazingira katika eneo la Ngorongoro

Balozi wa Ujerumani nchini, Mhe. Regina Hess akichangia mjadala kuhusu jitihada za Serikali za kulinda uhifadhi na mazingira katika eneo la Ngorongoro


Balozi wa Uingereza nchini, Mhe. David Concar akichangia mjadala kuhusu jitihada za Serikali za kulinda uhifadhi na mazingira katika eneo la Ngorongoro

Sehemu ya Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa pamoja na Wadau wa Maendeleo wakifuatilia mkutano 

Sehemu ya Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa pamoja na Wadau wa Maendeleo wakifuatilia mkutano 

Mawaziri, Makatibu Wakuu, Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa pamoja na Wadau wa Maendeleo katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza mkutano wao leo Jijini Dar es Salaam



MKUTANO WA 15 WA BARAZA LA KISEKTA LA KILIMO NA USALAMA WA CHAKULA WAHITIMISHWA JIJINI DAR ES SALAAM


Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula la Jumuiya ya Afrika Mashariki (SCAFS) leo tarehe 25 Machi 2022 umefikia tamati jijini Dar es Salaam.

Mkutano huu ambao umefanyika kwa kipindi cha siku 5 kuanzia tarehe 21 hadi 25 Machi 2022 umetimishwa katika ngazi ya Mawaziri ambapo awali, ulitangulia na Mkutano katika ngazi ya Wataalum Waandamizi uliofanyika tarehe 21 hadi 23 Machi 2022, na Makatibu Wakuu tarehe 24 Machi 2022. 

Miongoni mwa masuala yaliyojitokeza katika Mkutano huo ni pamoja na kujadili ripoti za; Usalama wa Chakula na Lishe wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kupitia na kutathimini utekelezaji wa maagizo na maamuzi mbalimbali yaliyofikiwa katika Mikutano ya awali ya Baraza la Mawaziri na Baraza la Kisekta, utekelezaji wa azimio la Malabo kuhusu Progaramu ya Mpango wa Maendeleo ya Kilimo Afrika (Comprehensive Africa Agriculture Development Programme - CAADP) pamoja na uwianishaji wa pembejeo za kilimo; maendeleo ya mifugo, uvuvi na ufugaji wa samaki katika Jumuiya.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano huo wa ngazi ya Mawaziri Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayesimamia Sekta za Uzalishaji na Huduma za Jamii Bw. Christophe Bazivamo ameeleza kuwa licha ya changamoto za Janga la UVIKO-Jumuiya imerekodi mafanikio makubwa katika utekelezaji wa makubaliano na maagizo ya Baraza la Kisekta na Baraza la Mawaziri. 

“Tumepiga hatua kubwa katika kuwezesha mazingira mazuri ya sekta ya kilimo kwa kuhakikisha upatikanaji na upatikanaji wa pembejeo; kuimarisha utendaji wa minyororo ya thamani ya kilimo na biashara ya bidhaa za kilimo” Amesema Bazivamo. 

Kwa upande wake mwenyekiti wa mkutano huo na Katibu Mkuu wa Uvuvi, Kilimo na Uchumi wa Buluu wa Kenya Dkt. F.O. Owino akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Uvuvi, Kilimo na Uchumi wa Buluu wa Kenya amepongeza hatua iliyofikiwa katika utekelezaji mpango uwianishaji wa pembejeo za kilimo; maendeleo ya mifugo, uvuvi na ufugaji wa samaki katika Jumuiya. 

Vilevile Dkt. Owino amepongeza dhamira za nchi Wanachama wa Jumuiya ya kuweka katika mazingira wezeshi kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya kilimo. Ameongeza kuwa uwekezaji huo utachochea ongezeko la ubora wa mazao na uzalishaji, sambamba na kuimarisha mnyororo wa thamani katika sekta ya kilimo na hatimaye kukuza biashara ya kikanda na kimataifa ya mazao ya kilimo.

Bw. Bazivamo kwa niaba ya Mkutano huo amewashukuru Washirika wote Maendeleo wakiwemo USAID Kenya na Afrika Mashariki (USAID/KEA, Idara ya Kilimo ya Marekani (USDA) na Serikali ya Ujerumani kupitia Shirika lake la GIZ, Mpango wa Kuzuia na Kukabili Ugonjwa wa Mlipuko kwa msaada wao katika kuboresha sekta ya Kilimo na Usalama wa Chakula kwenye Jumuiya. 

Katika Mkutano huo Tanzania imewakilishwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Mashauri Ndaki ambaye pia aliongoza wa Ujumbe wa Tanzania, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Antony Peter Mavunde, Makatibu Wakuu, Maafisa Waandamizi wa Taasisi na Idara mbalimbali za Serikali. Aidha, Mkutano huo umehudhuriwa na nchi zote sita (6) Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. 
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Mashauri Ndaki (Mb) ambaye pia alikuwa Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania akichangia hoja kwenye Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Dar es Salaam. Machi 25, 2022
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Antony Peter Mavunde (Mb) akifuatilia Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliokuwa ukiendelea jijini Dar es Salaam. Machi 25, 2022
Mkurugenzi Msaidizi wa Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Benjamin Mwesiga (wakwanza kushoto) akifuatilia Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliokuwa ukiendelea jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Mashauri Ndaki akisaini ripoti ya Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Dar es Salaam
Mawaziri walioshiriki Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula la Jumuiya ya Afrika Mashariki wakisaini ripoti ya Mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliokuwa uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Thursday, March 24, 2022

WAZIRI MULAMULA AMUAGA BALOZI WA UGANDA

Na Waandishi Wetu, Dar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula amemuaga Balozi wa Unganda nchini Mhe. Richard Kabonero ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika tukio hilo Waziri Mulamula amempongeza Balozi Kabonero kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kuendeleza na kudumisha uhusiano mzuri wa kihistoria uliopo baina ya Tanzania na Uganda. 

Waziri Mulamula ametaja baadhi ya mafanikio ambayo yamepatika katika kipindi cha uwakilishi wake hapa nchini, kuwa ni pamoja na kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi Choleani, Tanzania lenye urefu wa Kilomita 1443 na kukua kwa urari wa biashara kati ya Tanzania na Uganda.  

“Serikali kwa ujumla tunashukuru zaidi kwa ushirikiano uliotuonesha wakati wote ulipokuwa hapa kama Balozi na tunakuahidi kuudumisha na kuuendeleza ushirikiano huo kwa maslahi ya nchi zetu mbili (Tanzania na Uganda),” amesema Balozi Mulamula. 

Kwa upande wake Balozi Kabonero ameishukuru Serikali kwa kumpatia ushirikiano wakati wote alipokuwa akitekeleza majukumu yake hapa nchini. 

“Naomba kuishukuru sana Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mlionipatia wakati wote nilipokuwa hapa kama balozi, kwa kweli nilifarijika sana kuwa nanyi……..naahidi kuwa balozi mwema wa Tanzania asante sana,” amesema Balozi Kabonero.

Tanzania na Uganda zimekuwa zikishirikiana katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara na uwekezaji, nishati, elimu, pamoja na usafirishaji.

Katika tukio jingine, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula ameshiriki katika Mkutano wa Nchi wanachama wa Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) ulifanyika kwa njia ya mtandao na kuongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angloa na Mwenyekiti wa ICGLR Balozi Tete Antonio.

Pia Waziri Mulamula ameshiriki kufunga Mkutano wa Mabalozi (Wastaafu) katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiongea na Balozi wa Unganda nchini Mhe. Richard Kabonero ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akimkabidhi zawadi Balozi wa Unganda nchini ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi Mhe. Richard Kabonero katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Balozi wa Unganda nchini aliyemaliza muda wake wa uwakilishi Mhe. Richard Kabonero pamoja na maafisa kutoka Ubalozi wa Uganda na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki   

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akishiriki katika Mkutano wa Nchi wanachama wa Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) ulifanyika kwa njia ya mtandao. Mkutano huo umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angloa na Mwenyekiti wa ICGLR Balozi Tete Antonio. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akionge na Mabalozi (wastaafu) katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam