Sunday, May 29, 2022

WIZARA YA MAMBO YA NJE KUENDELEA KUTOA ELIMU KUHUSU FURSA ZITOKANAZO NA ENEO HURU LA BIASHARA LA AFRIKA

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imejipanga kuendelea kutoa elimu kwa umma na wadau mbalimbali hapa nchini kuhusu fursa zitokananzo na Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (African Continental Free Trade Area-AfCFTA) ili kuwawezesha kuzichangamkia kwa manufaa yao na nchi kwa ujumla.


Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 29 Mei 2022 jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk wakati akifungua rasmi Warsha ya Kueleimisha na Kujenga Uwezo kwa Wajumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Mkataba ulioanzisha Eneo Huru la Biashara la Afrika.


Mhe. Balozi Mbarouk amesema kuwa, watanzania wana kila sababu ya kuchangamkia fursa zinazotokana na Mkataba wa AfCFTA na kunufaika nazo kwa kuwa Tanzania ni mwanachama kamili wa mkataba huo baada ya Bunge kuuridhia mnamo mwezi Januari 2022. Fursa hizo ambazo ni pamoja na Biashara, Ajira, Uwekezaji, Teknolojia zitainufaisha nchi kwa kukuza pato la Taifa kutokana na eneo kubwa la soko, kukuza viwanda, ongezeko la biashara ndani ya Afrika na kuongezeka uzalishaji na mnyororo wa thamani.


“Ili kuwawezesha wadau kutambua na kutumia fursa za AfCFTA, Serikali imejipanga kuwa na mkakati endelevu wa kutoa elimu kwa umma. Tayari Serikali imeanza kutoa elimu na kujenga uwezo kwa wadau kwa makundi. Tayari Warsha za aina hii zimefanyika Zanzibar, Dar es Salaam, Morogoro na Mwanza na zimehusisha Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Watumishi wa Umma na Sekta Binafsi” amesema Mhe. Mbarouk.


Ameongeza kusema kuwa, AfCFTA ni muhimu kwa Tanzania katika kupanua wigo wa soko la bidhaa na huduma nje ya soko la EAC na SADC na kwamba Wizara inatumia fursa ya AfCFTA kutekeleza mikakati ya Diplomasia ya Uchumi ya kuvutia wawekezaji  nchini ilikuzalisha na kuuza kwenye soko la AfCFTA.


Pia alitumia fursa hiyo kuwaomba Wajumbe wa Kamati hiyo kuwa Mabalozi kwenye suala hilo na kushirikiana na Serikali kuendelea kutoa elimu kwa wadau ili Tanzania itumie ipasavyo fursa zitokanazo na ushiriki wake katika AfCFTA.


“Nina imani kuwa kupitia warsha hii, kila mmoja wetu atakuwa amepata elimu ya kutosha kuhusu mkataba wa AfCTA pamoja na fursa zake na mtakuwa mabalozi wazuri kwenye suala hili katika kushirikiana na Serikali” alisisitiza Balozi Mbarouk.


Akiwasilisha mada kuhusu Mkataba wa AfCFTA, Mkurugenzi wa Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Bernard Haule amesema nchi  54 za Afrika zimesaini Mkataba huo na tayari nchi 43 ikiwemo Tanzania zimeuridhia.  Amesema malengo ya kuanzishwa mkataba huo ni pamoja na kutengeneza soko moja la uhakika la kuhimili vishindo vya dunia; kujenga na kukuza uzalishaji na uwezo wa uchumi wa viwanda barani Afrika  na kuweka msingi utakaowezesha kuwa na umoja wa forodha wa Afrika.


Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe.Vincent Mbogo ameipongeza na kuishukuru Wizara kwa kundelea kutoa elimu na kushauri jitihada zaidi zitumike ili kuwafikia wananchi wa mijini na vijijini. Pia amesisitiza umuhimu wa Serikali kuwa na takwimu sahihi za mahitaji ya soko na zile za uzalishaji ili kuwe na uwiano na mwendelezo kwenye ufanyaji biashara. Vilevile elimu ya uzalishaji wa bidhaa bora na zenye viwango itolewe ili kukidhi matakwa ya Soko hilo.


“Naipongeza Wizara kwa hatua hii. Hata hivyo bado mna kazi kubwa ya kuwafikia watu wa mijini na vijijini ili kuwaeleimisha kuhusu fursa zitokanazo na soko hili muhimu. Tumieni njia mbalimbali kutoa elimu hii ikiwemo vyombo vya habari kama radio, televisheni na mitandao ya kijamii ili elimu hii iwafikie wananchi kwa wingi” alisema Mhe. Mbogo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) akifungua rasmi warsha ya siku moja iliyoendeshwa na Wizara kwa Wajumbe wa Kamati ya  ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA). Warsha hiyo imefanyika jijini Dodoma tarehe 29 Mei 2022. Kulia ni Kaimu Katibu Mkuu wa  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Fatma Mohammed Rajab
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Vincent Mbogo (Mb) (kushoto) akiwa  na Katibu wa Kamati wakati wa Warsha iliyotolewa na Wizzara kuhusu Eneo Huru la Biashara la Afrika
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Mohammed Rajab nae akizungumza wakati wa Warsha iliyotolewa na Wizara kwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama
Mkurugenzi wa Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Bernard Haule akiwasilisha mada ya kujenga uwezo kwa Wabunge kuhusu Eneo Huru la Biashara la Afrika kwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (hawapo pichani)
Sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama wakifuatilia uwasilishwaji wa mada kuhusu Eneo Huru la Biashara la Afrika
Sehemu nyingine ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama wakati wa warshailiyotolewa kwao kwa lengo la kuwaelimisha na kuwajengea uwezo kuhusu Soko Huru la Biashara la Afrika. Kushoto ni Mhe. Mustafa Mwinyikondo Rajab (Mb) na kulia ni Mhe. Felista Njau (Mb)
Wakurugenzi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakishiriki warsha. Kutoka kushoto ni Balozi Stephen Mbundi, Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama, Bw. Lawrence Mwesiga, Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Biashara, Uwekzaji na Sekta za Uzalishaji na Balozi Agnes Kayola, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda
Sehemu nyingine ya Wakurugenzi na wawakilishi kutoka Wizarani. Kutoka kushoto ni Bw. Marobe Wama, Msaidizi wa Kaimu Katibu Mkuu, Bw. Magabilo Murobi, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Diplomasia ya Uchumi na Bi. Linda Rujweka, Afisa TEHAMA
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Justine Kisoka akifuatilia warsha
Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Eliabi Chodota akifafanua jambo wakati wa warsha kuhusu Soko Huru la Biashara la Afrika 
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Vincent Mbogo (Mb) akishauri jambo kwa Wizara wakati wa warsha kuhusu Soko Huru la Biashara la Afrika
Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Muharami Mkenge (Mb) akichangia jambo wakati wa warsha
Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Abeid Ramadhani (Mb) nae akichangia jambo
Mjumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Joseph Mkindi (Mb) akitoa ushauri kwa Wizara kuhusu namna ya kunufaika na Eneo Huru la Biashara la Afrika
Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Zahor Mohamed Haji (Mb) akichangia jambo kuhusu Eneo Huru la Biashara la Afrika
Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Cosato Chumi (Mb) akichangia hoja
Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Janeth Masaburi (Mb) akitoa mchango wake wakati wa warsha hiyo
Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Abdi Hija Mkasha (Mb) nae akichangia jambo
Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Fakharia Shomar Khamis (Mb) akitoa hoja kuchangia mada kuhusu Eneo Huru la Biashara la Afrika

Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Mustafa Mwinyikondo Rajab (Mb) wakati wa warsha kuhusu Eneo Huru la Biashara Barani Afrika
Afisa Mratibu wa shughuli za Bunge katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Joshua Mponera akifuatilia matukio wakati wa warsha kwa Wabunge kuhusu Eneo Huru la Biashara la Afrika



 

TANZANIA YAPENDEKEZA MKAKATI WA PAMOJA KUPAMBANA NA UGAIDI, MAJANGA AU

Na Mwandishi wetu, Malabo

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezishauri nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kuwa na mpango mkakati wa pamoja katika kupambana na masuala ya ugaidi na majanga ya kibinadamu.

Akitoa pendekezo la Tanzania katika Mkutano wa 16 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliomalizika jana usiku Malabo, Equatorial Guinea, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) ambaye alimwakilishwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania inapendekeza Umoja wa Afrika uwe na mpango mkakati utakaosaidia kuhakikisha kuwa nchi wanachama wanakwenda pamoja lakini pia kusaidiwa kujengewa uwezo wa kupambana na vitendo vya kigaidi.

“Hakuna nchi hata moja inaweza kusema iko salama kwani vikundi vya kigaidi viko sehemu mbalimbali hivyo kwa kutumia mpango mkakati wa umoja na mshikamano ni rahisi kukabiliana na ugadi…..kwa hiyo ujumbe wetu Tanzania kwa (AU) ni kwamba twende pamoja katika kutokomeza ugaidi,” amesema Balozi Mulamula

Balozi Mulamula ameongeza kuwa Mkutano huo pia umetoa tamko la pamoja la kuimarisha utekelezaji wa mikataba mbalimbali iliyopitishwa miaka mingi pamoja na kuhakikisha Baraza la Amani na Usalama linakuwa na mpango maalum wa kufuatilia nyendo za kigaidi na kuzitokomeza.

“Baraza la Amani na Usalama pia litasaidia katika kuimarisha amani na usalama kupitia ‘stand by force’ ili kuweza kuingilia na kusaidia kuzuia machafuko pindi yanapojitokeza na kutokomeza vitendo kama hivyo vya kigaidi,” aliongeza Balozi Mulamula

Akielezea kuhusu Mkutano wa 15 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali, Balozi Mulamula alisema kuwa Tanzania imeziomba nchi wanachama kuimarisha ushirikiano na utekelezaji wa pamoja wa utoaji wa huduma za kibinadamu ikiwemo tahadhari za mapema ambazo zinahitaji kupitiwa upya, kuendelezwa na kuimarishwa kwa ajili ya kupata utabiri na tafsiri sahihi ya majanga yatakayotokea na kuyafanyia kazi ipasavyo.

Tanzania pia imeuomba Umoja wa Afrika kuwa na ushirikiano na utekelezaji wa pamoja katika utoaji wa huduma za kibinadamu hasa jukumu la kuhifadhi wahamiaji na wakimbizi.

Aidha, mkutano wa 15 na 16 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliridhia kuzizuia nchi nne ambazo kushiriki mikutano ya Umoja wa Afrika kutokana na Mabadiliko ya Serikali yasiyozingatia misingi ya Katiba ikiwemo mapinduzi ya kijeshi nchi hizo ni Mali, Burkina Faso, Guinea na Sudan. 

Kwa upande wake, Rais wa Cameroon na Mwenyekiti wa Baraza la Amani na Usalama, Mhe. Paul Biya amezitaka nchi wanchama wa Umoja wa Afrika kushughulikia masuala ya kigaidi kwa umoja na mshikamano kwani bila kufanya hivyo mambo hayo hujenga na kuchochea itikadi kali hasa miongoni mwa vijana ambao ni idadi kubwa ya watu katika Bara la Afrika.

“Zaidi ya asilimia 60 ya idadi ya watu barani Afrika ni vijana. Kwa hiyo ni lazima nchi wanchama wa Umoja wa Afrika kujitahidi kuweka mazingira mazuri ya ushirikishwaji wa vijana na wanawake katika michakato ya amani na maendeleo katika ngazi ya kitaifa, kikanda na bara,” amesema Mhe. Biya.

Wakuu wa Nchi na serikali katika Mkutano wa 16 wa Dharura waliridhia kwa pamoja kuwa kila mwaka tarehe 31 Januari kuwa siku ya Amani na maridhiano Barani Afrika na Rais wa Angola Mhe. João Lourenço atakuwa kinara ‘champion’ wa masuala ya amani.

Rais wa Equatorial Guinea, Mhe. Teodoro Obiang Nguema Mbasogo akihutubia katika Mkutano wa 16 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) uliomalizika jana usiku Jijini Malabo, Equatorial Guinea

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Bw. Moussa Faki Mahamat akihutubia katika Mkutano wa 16 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) uliomalizika jana usiku Jijini Malabo, Equatorial Guinea

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula ambaye amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 16 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) akifuatilia mkutano huo ulimalizika jana usiku Jijini Malabo, Equatorial Guinea

Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia ambaye anawakilisha pia Umoja wa Afrika, Mhe. Innocent Shiyo (mwenye tai nyekundu), Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz pamoja na watumishi wengine waandamizi wa Serikali wakishiriki katika mkutano

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia ambaye anawakilisha pia Umoja wa Afrika, Mhe. Innocent Shiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz pamoja na watumishi wengine waandamizi wa Serikali

Sehemu ya Wakuu wa Nchi na Serikali pamoja na Wawakilishi wa Wakuu wa Nchi na Serikali wakiwa katika picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa mkutano wa Mkutano wa 16 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) ulimalizika jana usiku Jijini Malabo, Equatorial Guinea

Wakuu wa Nchi na Serikali pamoja na Wawakilishi wa Wakuu wa Nchi na Serikali wakiwa katika picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa mkutano wa Mkutano wa 16 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU). Mkutano huo ulimalizika jana usiku Jijini Malabo, Equatorial Guinea  



WAKULIMA WA KUSINI WAVUTIWA NA UWEKEZAJI WA KAMPUNI YA LONGPING HIGH TECH

Wakulima wa zao la maharage ya soya wa Kanda ya Kusini wamevutiwa na aina ya uwekezaji unaotarajiwa kufanywa na Kampuni ya Longping High Tech ya nchini China, ambayo inalenga kuwawezesha wakulima wa soya katika maeneo mbalimbali nchini kuongeza uzalishaji na ubora wa zao hilo. 

Haya yamejili wakati wa ziara inayoendelea, kwa Watendaji wakuu wa Longping kutembelea maeneo yanayozalisha maharage ya soya nchini. Mkurugenzi wa Biashara za Nje na Fedha wa Kampuni hiyo Bw. Shangyang Wu akizungumza na wakulima wa Wanging’ombe Mkoani Njombe ameeleza kuwa lengo la Kampuni hiyo kuwekeza nchini kupitia wakulima hao inatokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa mahitaji ya soya kuliko kiasi wanachokizalisha nchini China, kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa baina ya Serikali ya Tanzania na China ambapo China iliahidi kuisaidia Tanzania kuongeza uzalishaji wa soya nchini na baadae kununua zao hilo kutoka kwa wakulima. 

Tumetembelea maeneo mbalimbali na kuonana na kufanya mazungumzo na wakulima, tumeridhishwa na jitihada na nia ya wakulima na serikali katika kuongeza ubora na kiwango cha uzalishaji wa soya. Nitoe ahadi kwenu kuwa tumejipanga na tupo tayari kufanya kazi na wakulima wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ili kutimiza adhima yetu ya kuona maisha ya wakulima yanaboreka kutokana na kipato kinachotokana na maharage ya soya. Tumesikia changamoto zilizopo, tutasaidia kuzitatua ili kuongeza tija kwa mkulima. Alieleza Bw. Shangyang Wu.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Waziri Kindamba kwa upande wake amewahimiza wakulima hao kuchangamkia fursa ya uzalishaji wa soya kwa kushirikiana na kampuni ya Longping kwa kuwa tayari wameshahakikishiwa soko la uhakika la nchini China. Vilevile Mhe. Kindamba aliwaeleza watendaji wa Kampuni ya Longping kuwa Serikali ya Mkoa inataoa ushirikiano wa dhati kwa pande zote mbili (Wananchi na Kampuni ya Longping) ilikuhakisha wote wanafikia matarajio yaliyokusudiwa. 

Niwasihi wananchi wenzagu hii sio fursa ya kuipoteza, tujipange kuzalisha soya kwa uwingi na ubora tutakao kubaliana kwa kuwa changamoto yetu ya muda mrefu ya ukosefu wa soko Longping wamelitatua. Niwahikikishie kuwa katika hili Serikali ya Mkoa hatupo tayari kuacha mwananchi yeyote nyuma kufikia maendeleo, tutendelea kuhimiza na kumtaka kila mmoja wetu kufanya kazi kwa bidii ili anufaike na fursa hii ya zao la soya. Alisema Mheshimiwa Kindamba. 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye mkutano baina yao, serikali na Watendaji wa Kampuni ya Longping wakulima wa Wanging’ombe wameeleza kuridhishwa kwao na mkakati wa uwekezaji wa kampuni hiyo. Aidha wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuhakisha wananchi wanapata fursa ya masoko ya mazao wanayoyazalisha. Vilevile wameeleza utayari wao wa kushirikiana na kampuni ya Longpin kwenye uzalishaji na uuzaji wa zao la soya. 

Katika hatua nyingine Watendaji wa kampuni ya Longpin wakiwa mjini Iringa walionana na kufanyamazungumzo na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Queen Sendiga. Katika mazungumzo yao walijadili namna wakulima watafikiwa na kunufaika na fursa ya uzalishaji wa soya. Mheshimiwa Sendiga aliwahikikishia wawekezaji hao kuwapa ushirikiano katika hatua zote za uwekezaji katika Mkoa huo. 

Longping High Tech ni miongoni mwa Kampuni wa kubwa nchini China inayoongoza katika uzalishaji wa mahindi ya njano, maharage ya soya na mtama. Kampuni hiyo pia imewekeza nchini Brazil kwa Dola za Marekani Bilioni 1. China inahitaji maharage ya soya kiasi cha tani milioni 155 kwa mwaka.

Wakiwa ziarani watendaji wa Longping wamepata fursa ya kutembelea mashamba ya mazao mbalimbali ya wawekezaji, kuzungumza na vikundi vya wakulima na kutembelea wazalishaji wa mbegu za mazao ya kilimo ikiwemo mahindi na soya. Ziara hiyo inahusisha mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Iringa, Njombe, Ruvuma, Mbeya na Rukwa. 

Katika ziara hiyo Watendaji wa Longping wameambatana na watendaji wa Selikali kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Kilimo, The Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania (SAGCOT) na Mkurugenzi wa Longping Tanzania Bw. Joseph Kusaga
Watendaji wa Kampuni ya Longping ya China wakizumza na wakulima wa Kilolo, Iringa walipowatembelea kwenye moja ya shamba la maharage ya soya.
Watendaji wa Kampuni ya Longping ya China wakielezewa jambo na mtaalamu wa Wakala wa Mbegu (Agricultural Seed Agency-ASA) walipotembelea moja ya shamba la Taasisi hiyo lililopo Kilolo, Iringa
Watendaji wa Kampuni ya Longping ya China wakizungumza na mtaalamu wa Taasisi ya Wakala wa Mbegu (Agricultural Seed Agency-ASA) walipotembelea moja ya shamba la Taasisi hiyo lililopo Kilolo, Iringa
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Queen Sendiga akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Kampuni ya Longping High Tech, Longping Tanzania na Afisa Mwandamizi kutoka Wizara ya Kilimo Bw. Revelian Ngaiza (wa kwanza kulia) walipomtembelea kwa mazungumzo ofisini kwake. 
Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Waziri Kindamba (aliyesimama) akizungumza kwenye mkutano baina wakulima, Serikali na Watendaji wa Kampuni ya Longping High Tech uliofanyika katika Ofisi ya Halmashauri Wanging’ombe, Njombe.
Wakulima wa Halmashauri ya Wanging’ombe wakiwa kwenye mkutano uliofanyika baina yao, Serikali na Watendaji wa Kampuni ya Longping High Tech.
Wakulima wa Wanging’ombe, Watendaji wa Kampuni ya Longping High Tech na ujumbe walioambatana nao wakifurahia jambo walipotembelea kwenye moja ya shamba la maharage ya soya
Mkutano ukiendelea Halmashauri wa Wilaya ya Kilolo, Iringa

Saturday, May 28, 2022

BALOZI KOMBO, DKT. MAKAKALA WAJADILI CHANGAMOTO ZA UHAMIAJI

Na Mwandishi wetu, 

Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo amekutana kwa mazungumzo na Kamishna Mkuu wa Uhamiaji Tanzania, Dkt. Anna Makakala katika Ofisi Ndogo za Uhamiaji Jijini Dar es Salaam. 

Pamoja na mambo mengine, viongozi hao walijadilia masuala mbalimbali yanayowahusu Watanzania wanaoishi nchini Italia, Ugiriki na maeneo mengine ya uwakilishi yanayoratibiwa na Ubalozi wa Tanzania uliopo Rome.  

Masuala mengine yaliyogusiwa katika mazungumzo yao ni changamoto mbalimbali za WanaDiaspora wanazozikabili nchini Italia na kwingineko kuhusu masuala ya Uhamiaji. 

Kamishna Mkuu wa Uhamiaji Tanzania, Dkt. Alimuahidi Balozi Kombo kufanikisha utatuzi wa changamoto zote hizo kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na ofisi za Balozi za Tanzania ulimwenguni kote ikiwemo Ubalozi wa Tanzania nchini Italia.

Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo katika picha ya pamoja na Kamishna Mkuu wa Uhamiaji Tanzania, Dkt. Anna Makakala baada ya kumalizika kwa mazungumzo yao yaliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Uhamiaji Jijini Dar es Salaam 



Friday, May 27, 2022

WAZIRI MULAMULA AMWAKILISHA RAIS SAMIA MKUTANO WA DHARURA AU

Na Mwandishi wetu, Malabo

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 15 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) unaofanyika Malabo, Equatorial Guinea tarehe 27 na 28 Mei, 2022.

Mkutano huo pamoja na mambo mengine, umejadili ajenda kuu mbili ambazo ni majanga na huduma za kibinadamu, masuala ya Ugaidi na Mabadiliko ya Serikali yasiyozingatia misingi ya Katiba. 

Akiongea wakati wa Mkutano huo, Balozi Mulamula amesema anamwakilisha Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano huo ulioitishwa na na Umoja wa Afrika (AU) kwa lengo la kuangalia na kujadili maajanga na huduma za kibinadamu pamoja na ugaidi.

“AU wameitisha mkutano huu kwa lengo la kujadili namna ya kukabiliana na majanga haya na jinsi gani Bara la Afrika linaweza kuwa na mkakati wa pamoja wa kukabiliana na majanga haya, na tunategemea baada ya kikao cha leo tutapata azimio la kukabidiliana na majanga haya katika bara letu la Afrika,” amesema Balozi Mulamula.

Kuhusu masuala ya Ugaidi, Balozi Mulamula ameongeza kuwa, Mkutano wa kesho tarehe 28 Mei, 2022 mkutano utaendelea kuangalia masuala ya kigaidi na kuona ni jinsi gani Bara la Afrika linasimama kwa umoja wake kupambana na majanga ya kigaidi.

Awali akifungua Mkutano huo, Rais wa Senegali ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mkutano huo, Mhe. Macky Sall amezisihi nchi za Afrika kuwa na umoja ambao utaziwezesha kukabiliana na majanga ya kibinadamu na mapambano dhidi ya ugaidi kwa urahisi zaidi.

Mhe. Sall amezitaka nchi za Afrika kuimarisha ushirikiano na mshikamano na kujenga uwezo wa kila nchi ili kuweza kukabiliana na majanga mbalimbali ya asili na wakati huo huo, kushughulikia changamoto za ulinzi na usalama ili kutozalisha wakimbizi na wahamaji ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano na kuunda Jeshi la Afrika (ASF) na Brigedi za kikanda pamoja na kuanzisha Vikosi Maalum    kushughulikia Changamoto za Ugaidi.

Balozi Mulamula katika mkutano huo, ameambatana na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia Mhe. Innocent Shiyo ambaye anawakilisha pia Umoja wa Afrika, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz pamoja na watumishi wengine waandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa tayari kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 15 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) unaofanyika Malabo, Equatorial Guinea tarehe 27 na 28 Mei, 2022

Waziri Mkuu wa Ethiopia Mhe. Abiy Ahmed Ali akiteta jambo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula walipokutana katika Mkutano wa 15 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) unaofanyika Malabo, Equatorial Guinea

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Bw. Moussa Faki Mahamat akihutubia katika Mkutano wa 15 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) unaofanyika Malabo, Equatorial Guinea

Rais wa Senegal na Mwenyekiti wa Mkutano wa 15 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU), Mhe. Macky Sall akitoa hotuba yake wakati wa ufunguzi wa mkutano huo leo Jijini Malabo, Equatorial Guninea

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na baadhi ya ujumbe wa Tanzania ulioshiriki katika Mkutano wa 15 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) unaofanyika Malabo, Equatorial Guinea

Rais wa Burundi, Mhe. Evariste Ndayishimiye katika picha ya pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula ambaye anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano huo

Sehemu ya Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ukiongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Innocent Shiyo,  ambaye pia anawakilisha Umoja wa Afrika, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz pamoja na watumishi wengine waandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mkutano ukiendelea

Wakuu wa Nchi na Serikali pamoja na Wawakilishi wa Wakuu wa Nchi na Serikali wakiwa katika picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa mkutano wa Mkutano wa 15 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) unaofanyika Malabo, Equatorial Guinea

Sehemu ya Wakuu wa Nchi na Serikali pamoja na Wawakilishi wa Wakuu wa Nchi na Serikali wakiwa katika picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa mkutano wa Mkutano wa 15 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) unaofanyika Malabo, Equatorial Guinea




VACANCY ANNOUNCEMENT


 

VACANCY ANNOUNCEMENT