Tuesday, February 21, 2017

Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje afungua kikao cha Makatibu Wakuu wa SADC-ISPDC

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Aziz P. Mlima, akifungua Mkutano cha Makatibu Wakuu nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa Kamati Ndogo ya Mawaziri ya Siasa na Diplomasia ya SADC (Inter State Politics and Diplomacy Sub Committee-ISPDC) unaotarajiwa kufanyika tarehe 23 na 24 Februari, 2017. Mkutano wa Makatibu Wakuu unafanyika kwa siku mbili  katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya wajumbe wa Mkutano kutoka katika mataifa ya nchi wanachama wakifuatilia mkutano.
Kaimu Mkuu wa Mabalozi Mhe. Balozi Edzai Chimonyo (wa kwanza kushoto) na wajumbe wengine wakifuatilia mkutano.
Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Dkt. Stergomena Tax (wa pili kushoto)  na wa kwanza kulia ni Balozi Simba Yahya, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakifuatilia mkutano.

Sehemu ya Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia Mkutano.

Monday, February 20, 2017

Balozi wa Tanzania nchini Comoro aagwa kwa kutunikiwa Tuzo na Rais

Balozi wa Tanzania kwenye Muungano wa Visiwa vya Comoro, Mhe. Chabaka Kilumanga akitunukiwa Nishani ya Juu (highest civilian honor) na Rais wa nchi hiyo, Mhe. Azali Assoumani hivi karibuni.

Nishani hiyo imetolewa na Mhe Azali  kwa kutambua mchango wa Balozi Kilumanga katika kudumisha uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Comoro, pamoja na kumpongeza kwa utumishi uliotukuka. 

Hafla hiyo ilifanyika Ikulu ya Comoro kwa ajili ya kumuaga Balozi Kilumanga baada ya kumaliza muda wake wa kazi nchini humo

Mhe. Rais Azali (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Kilumanga na Mkewe




Balozi Kilumanga akipongezwa na Mkuu wa Utawala Ubalozini, Bw. Mudrick Soragha mara baada ya kutunikiwa nishani na Rais wa Comoro
============================================

BALOZI WA TANZANIA VISIWANI COMORO ATUNUKIWA MEDANI YA JUU YA HESHIMA NA MHE. AZALI ASSOUMANI, RAIS WA MUUNGANO WA VISIWA VYA COMORO TAREHE 16 FEBRUARI 2017

Balozi wa Tanzania ndani ya Muungano wa Visiwa vya Comoro Mhe. Chabaka Kilumanga ametunukiwa Nishani ya Juu (highest civilian honor) na Rais wa nchi hiyo Mhe. Azali Assoumani. Mhe. Balozi ambaye aliongozana na Mkewe Bi Irene Kilumanga walishiriki katika hafla hiyo iliyofanyika Bait Salam, Ikulu ya Comoro tarehe 16, Februari 2017. Wageni waalikwa walioshuhudia  hafla hiyo ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Comoro,  Mhe. Baccar Dossar na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Comoro Mhe. Yousef Mohamed Yousef.

Hafla hiyo ilifanyika ikiwa ni sehemu ya sherehe ya kumuaga Balozi huyo ambaye amemaliza muda wake wa kazi Visiwani Comoro na kuelekea kustaaafu ifikapo tarehe 17 Machi, 2017. Mhe. Chabaka Kilumanga anakuwa ndio Balozi wa mwanzo kutunukiwa nishani hiyo miongoni mwa mabalozi wenzake wanao tumikia nchi zao Visiwani Comoro. Wakati akimtunuku medani hiyo, Mhe Azali alieleza kutambua mchango mkubwa aliofanya Balozi huyo katika kudumisha uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Comoro, pamoja na kumpongeza kwa utumishi uliotukuka. 

Kwa upande wake Mhe. Balozi alieleza kufarijika sana kwa kutunukiwa Nishahi hiyo ambayo imekuwa ni heshima kubwa kwake. Aidha, Balozi Kilumanga alipongeza juhudi za Serikali ya Mhe. Azali kwa hatua inazochukua katika kuleta maendeleo kwa wananchi wa Comoro. Pia alipendekeza kwa Serikali hiyo kuanza kufanya taratibu za kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupanua wigo wa ushirikiano baina ya Tanzania na Comoro.

Kutunukiwa kwa nishani hiyo kulikuwa ni kwa kushtukiza kwani Mhe. Balozi hakutarajia kabisa kutunukiwa nishani hiyo ambayo kwa kawaida hupewa raia wa Comoro ambao wametoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa lao. Hivyo hii imekuwa ni heshima kubwa sio tu kwa Mhe. Balozi bali pia kwa Tanzania. 

Wakati wakiagana na Mhe. Rais, Mhe. Balozi na Mkewe Bi Irene Kilumanga walieleza kuwa kamwe hawatasahau upole na ukarimu wa Wacomoro na kwamba Comoro itaendelea kuwa mioyoni mwao daima.


Friday, February 17, 2017

Balozi wa Tanzania nchini Brazil awasili rasmi Ubalozini


Balozi wa Tanzania nchini Brazil, Mhe. Emmanuel Nchimbi akianza rasmi majukumu yake ya ofisini kwenye wadhifa wa Balozi mara baada ya kuwasili rasmi kwenye Ofisi za Ubalozi wa Tanzania zilizopo kwenye makao makuu nchini humo, mjini Brasilia.

Balozi Nchimbi akiwa kwenye picha ya pamoja na Maafisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini Brazil mara baada ya kumpokea na kumkaribisha rasmi kituoni hapo.


Balozi Nchimbi (kushoto) akizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Mambo ya Nje ya Brazil mara baada ya kuwasili Wizarani hapo kwa utambulisho.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje akutana na Balozi Mteule wa Oman

Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Susan Kolimba akizungumza na Balozi Mteule wa Oman nchini, Mhe. Ali Abdullah Al Mahruqi alipomtembelea Wizarani leo, Jijini Dar es Salaam. Mazungumzo yao yalijikita katika masuala ya ushirikiano na juu ya ukamilishaji wa makubaliano ya kibiashara na uwekezaji ili kuweza kunufaika na ushirikiano wa kidiplomasia ambao umekuwa ukizidi kuimarika baina ya mataifa hayo mawili.
Mhe. Al Mahruqi akimweleza Naibu Waziri mipango ya kiutendaji ya Ubalozi wa Oman nchini na jinsi Serikali yake ilivyojidhatiti katika kuhakikisha mahusiano yaliyopo yataelekeza nguvu zaidi katika kusimamia sekta zinazogusa kukuza uchumi wa wananchi.
Mhe. Al Mahruqi akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika ofisi za Wizara, kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Abdallah Kilima.
Picha ya pamoja wakiagana mara baada ya mazungumzo.

Thursday, February 16, 2017

Mkurugenzi wa Mashariki ya Kati akutana kwa mazungumzo na Balozi Mteule wa Oman nchini

Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Balozi Abdallah Kilima (kulia) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi Mteule wa Oman hapa nchini, Mhe. Ali Abdullah Al Mahruqi. Mazungumzo yao yalijikita katika kuboresha mahusiano kati ya Tanzania na Oman kwenye sekta mbalimbali zikiwemo biashara, elimu na afya. Pamoja na hayo Balozi Kilima amemuahidi Balozi kumpatia ushirikiano wa kutosha kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakati wowote katika kutekeleza majukumu yake hapa nchini.
Mkutano ukiendelea.Kulia ni Afisa Mambo ya Nje, Bw. Odilo Fidelis


Balozi Kilima akiagana na  Balozi Mteule Ali Abdullah Al Mahruqi mara baada ya mazungumzo yao.

Wednesday, February 15, 2017

Taarifa ya Serikali kuhusu Watanzania waliopata matatizo nchini Msumbiji

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Suzan Kolimba (Mb.), amezungumza na waandishi wa habari, kufafanua suala la Watanzania waliopata matatizo ya kufukuzwa nchini Msumbiji. Pia alitumia fursa hiyo kuwaomba Watanzania wote wanaosafiri kwenye nchi nyingine kuhakikisha wanafuata sheria na taratibu ikiwemo kupata vibali halali vya kukaa kwenye nchi husika. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika na Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Innocent Shiyo na kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Mindi Kasiga.
Sehemu ya waandishi wa habari wakimsikiliza Dkt. Kolimba (hayupo pichani), alipokuwa akizngumza nao.
Mkutano na waandishi wa habari ukiendelea.
==================================================



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Taarifa kuhusu Watanzania waliopata matatizo nchini Msumbiji

Tumepokea taarifa za kukamatwa na kufukuzwa kwa raia wa Tanzania waliokuwa wakiishi katika mji wa Monte Puez ulio Cabo Delgado, Jamhuri ya Msumbiji.
Serikali ya Msumbiji imekiri kuwepo kwa operesheni maalum ya kuwakamata na kuwarudisha raia wa nchi za kigeni wanaoishi katika mji huo bila kufuata Sheria za Uhamiaji za nchi hiyo. Aidha, Serikali hiyo imetaarifu kwamba, zoezi hilo limeanzia mji wa Monte Puez kwa kuwa una raia wengi wa kigeni ikilinganishwa na miji mingine.

Kufuatia hali hiyo, Ubalozi wetu nchini Msumbiji upo eneo la tukio ili kufuatilia suala hili na mamlaka husika. Aidha, unaendelea kufanya mawasiliano ya Kidiplomasia na Serikali ya Msumbiji ili kuhakikisha usalama wa Watanzania na mali zao, unapewa kipaumbele. Inakadiriwa kuwa Watanzania wapatao elfu tatu (3,000) wanaishi na kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii katika mji huo wa Monte Puez.

Kuanzia zoezi hilo lilipoanza, Raia wa Tanzania wapatao 132 wamesharudishwa nchini. Tarehe 11/02/2017 walirejeshwa raia 58. Tarehe 14/02/2017 wamerejeshwa raia 24 na leo tarehe 15/02/2017 wamesharejeshwa raia 50.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inawahakikishia Watanzania kuwa uhusiano kati ya Tanzania na jirani yetu Msumbiji ni mzuri, na hivyo itafanya kila jitihada kuhakikisha hali ya usalama wa Watanzania na biashara zao, inarudi kuwa shwari na kwa wakati. Mwezi Desemba 2016, Tanzania na Msumbiji zilifanya mkutano wa ujirani mwema uliolenga kuimarisha ushirikiano. Mkutano huo uliofanyika kwenye mji wa Pemba, Cabo Delgado uliainisha maeneo ya ushirikiano yakiwemo masuala ya biashara na uhamiaji.

Serikali inaendelea kuwakumbusha Watanzania waishio ughaibuni, kufuata Sheria na taratibu za nchi hizo, ikiwemo kuwa na vibali halali vya makazi na biashara.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

15 Februari, 2017

Naibu Waziri Mambo ya Nje akutana na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa na Maendeleo wa Korea



Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Susan Kolimba akizungumza na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa na Maendeleo wa Jamhuri ya Korea,Mhe. Balozi Choi Jong-moon, ambaye amewasili nchini kwa ziara ya siku mbili inayotarajiwa kumalizika tarehe 15 Februari, 2017.
Mhe. Balozi Jong-moon  akizungumza na Mhe. Dkt. Kolimba, ambapo pamoja na masuala ya ushirikiano alieleza nia ya Serikali ya Jamhuri ya Korea katika kuongeza maeneo ya ushirikiano hususan katika Ujenzi wa Miundombinu, Elimu, Utalii, biashara na Uwekezaji.
Kutoka kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Justa Nyange, Mkurugenzi msaidizi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Deus Kaganda na Afisa Mambo ya Nje, Bi. Bertha Makilagi.
Wa kwanza kulia ni Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini, Mhe. Song Geum Yong pamoja na maafisa wa Ubalozi  ambao waliambatana na Mhe. Jong-moon, wakifuatilia mazungumzo.
Mazungumzo yakiendelea.
Wakiagana mara baada ya mazungumzo.
Picha ya pamoja Manaibu Waziri na wajumbe kutoka Serikali ya Tanzania na Korea.

Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje akutana na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa na Maendeleo wa Korea


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Dkt. Aziz P. Mlima akizungumza na Mhe. Jong-moon. Katika mazungumzo yao waliongelea kuhusiana na ushirikiano wa kidiplomasia, sekta ya elimu katika ufadhili wa masomo ya muda mrefu na muda mfupi pamoja na sekta nyingine za maendeleo katika kuinua uchumi wa mataifa hayo mawili.

Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia mazungumzo.

Mazungumzo yakiendelea.

Picha ya pamoja.

Picha ya pamoja ujumbe wa Serikali ya Tanzania na Korea.

Monday, February 13, 2017

Waziri akutana na Msajili wa MICT

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Msajili wa  Mfumo wa Kimataifa wa kumalizia mashauri yaliyosalia ya iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya Rwanda (MICT), Dkt. Olufemi Elias alipomtembelea katika Ofisi za Wizara jijini Dar es Saalam tarehe 13 February, 2017.
Maafisa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia mazungumzo. Kutoka kushoto ni Bw. John Pangipita pamoja na Bi.Gwantwa Mwaisaka.
Sehemu ya Maafisa waliofuatana na Msajili wakifuatilia mazungumzo. Kutoka kulia ni  Bw. Samuel Akorimo, Bw. Ousman Njikan na Bi. Tully Mwaipopo 
Mazungumzo yakiendelea