Sunday, August 25, 2024
WAZIRI CHUMI ASHIRIKI MKUTANO MAALUM WA AFYA WA TICAD 9
Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi tarehe 24 Agosti 2024, ameshiriki mkutano Maalum wa afya pembezoni ya Mkutano wa Tisa wa TICAD ngazi ya Mawaziri unaofanyika jijini Tokyo.
Mkutano huo uliongozwa na mada ya Ushirikiano Mpya kwa Usawa wa Afya Barani Afrika: Kuharakisha Ufikaji wa Huduma za Afya kwa Wote kwa Ubunifu kuelekea 2030.”
Mkutano huo uliandaliwa na Muungano wa Chanjo (GAVI) na Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) ulilenga kuangazia umuhimu wa ushirikiano na ubunifu katika kufanikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wote barani Afrika.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Bunge la Japani Mhe. Fukazawa Yoichi.
Kwa kushiriki katika mkutano huo Tanzania ilipata fursa ya kujionea namna bora ya kutoa huduma za afya kwa watu wote ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma hizo bila ya kikwazo cha kukosa hela.
WAZIRI CHUMI ASHIRIKI UZINDUZI WA LOGO YA SUMMIT YA TICAD9 2025 JAPAN
Tarehe 24 Agosti,2024, Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi ameshiriki katika hafla ya uzinduzi wa logo ya Mkutano wa Tisa wa TICAD wa Wakuu wa Nchi na Serikali utakaofanyika 2025 nchini Japan.
Uzinduzi wa Logo hiyo ya Summit ya #TICAD9 umefanyika jijini Tokyo wakati wa Mkutano wa TICAD ngazi ya Mawaziri, ambao unafanya maandalizi ya Summit hiyo inayotarajiwa kufanyika tarehe 20 - 22 Agosti 2025, jijini Yokohama, Japan.
Uzinduzi huo ullihudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka sekta za umma na binafsi za nchini
Japan ambao pia, walionesha huduma mbalimbali wanazozitoa katika nchi za Afrika.
Katika tukio hilo, Mhe. Naibu Waziri Chumi akiambatana na Balozi wa Tanzania nchini Japan Mhe. Baraka Luvanda walipata nafasi ya kusalimiana na wadau wa taasisi na kampuni za Japan zenye ubia na Tanzania.
Saturday, August 24, 2024
TANZANIA YAZISIHI NCHI ZA AFRIKA KUSHIRIKIANA KUTATUA CHANGAMOTO ZINAZOZIKABILI NCHI ZAO
Waziri Mambo ya Nje wa Japan Mhe. Yoko Kamikawa akifungua Mkutano wa
Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika ngazi ya Mawaziri unaofanyika jijini Tokyo, Japan kuanzia tarehe 24-25 Agosti 2024.
|
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Tisa wa TICAD 2024 wakifuatilia mkutano huo |
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Tisa wa TICAD 2024 wakifuatilia mkutano huo |
Washiriki wa Mkutano wa Tisa wa TICAD 2024 katika picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa Mkutano huo |
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa wito kwa nchi za Afrika kushirikiana kutafuta suluhisho la kudumu la matatizo na changamoto mbalimbali zinazozikabili nchi hizo. Pia imemewahimiza wadau wote wa maendeleo kutoka nchini Japan kuendelea kufanya biashara na kuwekeza zaidi barani Afrika ili kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya binadamu katika bara hilo ikiwa ni katika juhudi za kuendeleza amani na utulivu kikanda na kimataifa.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi alipochangia mada ya Amani na Utulivu: kuhakikisha Heshima ya Binadamu na Usalama wa Binadamu kwenye sehemu ya pili ya Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika ngazi ya Mawaziri unaofanyika nchini Japan tarehe 24-25 Agosti 2024.
Ameipongeza Japan kwa kuwa mstari wa mbele kushiriki katika jitihada za kimataifa na kuwaomba washirika wengine wa kimataifa kuiga mfano huo na kuongeza kuwa Tanzania inatambua umuhimu wa ushiriki sawa na ujumuishaji wa wanawake na wanaume, wasichana na wavulana katika kuhakikisha amani na usalama vinatamalaki.
Amesema kutokana na umuhimu huo Tanzania iko katika hatua za mwisho za kuandaa na kutekeleza Mpango wa Kitaifa wa Utekelezaji (NAP) kuhusu Wanawake, Amani na Usalama ikiwa ni utekelezaji wa Azimio Na. 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la mwaka 2000.
Amesema siku zote Tanzania imekuwa na mchango muhimu katika harakati za upatanishi, mazungumzo ya amani na njia nyingine za kidiplomasia katika kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa ndani na nje ya mipaka yake na ndio maana imefanikiwa kuondoa mizizi ya vita vya kikabila na migogoro kwa kuunganisha makabila takriban 126 na kutumia lugha moja ya Kiswahili kama lugha ya Taifa.
Ameongeza kuwa kutokana na hali hiyo Tanzania imeendelea na utamaduni wa kuwapatia hifadhi mamia ya wakimbizi na wanaotafuta hifadhi kutoka nchi jirani na zaidi na kwa sasa Tanzania inahifadhi wakimbizi na watu wanaotafuta hifadhi wapatao 237,997 huku wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.
Mkutano huo ulifunguliwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan Mhe.Yoko Kamikawa umehudhuriwa na Mawaziri, washirika wa TICAD, wawakilishi na waandaaji wenza -Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), Benki ya Dunia, Kamisheni ya Umoja wa Afrika na mashirika ya Kimataifa na kikanda, sekta binafsi na Kiraia kutoka Japan na Afrika.
Friday, August 23, 2024
NAIBU WAZIRI CHUMI AKUTANA NA NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA JAPAN
Mazungumzo yakiendelea |
Naibu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato
Chumi (Mb) amekutana na kuzungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan Mhe. Kyoto
Tsuji ofisini kwake jijini Tokyo.
Viongozi hao wamekubaliana
kuendelea kushirikiana ili kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo
kati ya Tanzania na Japan kwa manufaa ya pande mbili.
Akizungumza katika kikao
hicho Mhe. Chumi aliishukuru Serikali ya Japan kwa kuendelea kuchangia
maendeleo ya Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu,
uwekezaji, elimu, na afya.
Amesema Tanzania imejipanga
kuhakikisha inaongeza kiwango cha biashara na uwekezaji kati yake na
Japan na hivyo kuchochea ukuaji wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa manufaa ya pande zote
mbili.
Naye, Mhe. Tsuji ameelezea utayari wa Japan kuendelea
kushirikiana na Tanzania na kuimarisha uhusiano uliopo kwa manufaa ya
nchi hizo.
Amesema Japan itaendelea kushirikiana na Tanzania na kuongeza biashara na bara la Afrika ili kuhakikisha maendeleo ya kweli yanapatikana.
Mhe.
Chumia yuko nchini Japan kuhudhuria Mkutano wa Tisa wa
Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD) ngazi ya Mawaziri
utakaofanyika jijini Tokyo tarehe 24-25 Agosti 2024.
Thursday, August 22, 2024
BALOZI KOMBO AKIPONGEZA KITUO CHA DKT SALIM AHMED SALIM KWA KUTOA MAFUNZO YA STADI ZA UONGOZI NA MAJADILIANO
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amekipongeza Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim (CFR) kwa kutoa mafunzo yenye lengo la kuwanoa vijana katika masuala ya uongozi hususan kwenye stadi za Uongozi na Majadiliano.
Mhe. Balozi Kombo ametoa pongezi hizo leo Agosti 22, 2025 alipokitembelea Kituo hicho ambacho ni moja ya Taasisi zilizo chini ya Wizara kwa lengo la kujitambulisha, kufahamu majukumu yake pamoja na kuangalia maendeleo ya mradi wa jengo la vyumba vya mihadhara. Akizungumza na wanafunzi kutoka Taasisi za Umma na Sekta binafsi wanaoshiriki mafunzo ya muda mfupi kuhusu stadi za Uongozi na Majadiliano chuoni hapo, Mhe. Waziri Kombo amewataka kuzingatia mafunzo hayo ambayo yatawajenga katika masuala ya uongozi, uzalendo na majadiliano, fani ambazo ni muhimu katika ulimwengu wa sasa wa kutumia diplomasia na uhusiano na mataifa mbalimbali kunufaika kiuchumi. Amesema washiriki hao wana bahati kubwa kupatiwa mafunzo katika Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim ambacho pia baadhi ya wakufunzi wake ni Mabalozi na Wanadiplomasia wabobevu kwenye masuala ya uhusiano wa kimataifa na Diplomasia kwa ujumla. “Kwenu ninyi washiriki wa mafunzo haya mna bahati kubwa ya kufundishwa na wanadiplomasia nguli akiwemo Balozi Modest Mero ambaye ni miongoni mwa wanadiplomasia waliowahi kuhudumu kwa nafasi ya kuiwakilisha nchi yetu katika Umoja wa Mataifa nchini Marekani. Hivyo, Balozi Mero kwa wasifu wake ni fursa kubwa kwenu washiriki kupokea elimu ya masuala ya stadi za uongozi na majadiliano”, amesema Mhe. Kombo. Wakati wa ziara hii Mhe.Kombo amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Kituo hicho, Mhe. Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo hicho, Dkt. Felix Wandwe ndc, baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti ya Kituo hicho na Viongozi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki. |
Wednesday, August 21, 2024
WAZIRI KOMBO AAGANA NA BALOZI WA UFARANSA NA USWIS HAPA NCHINI.
Waziri wa Mambo ya Nje ma Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ameagana na aliyekuwa Balozi wa Ufaransa Mhe. Nabil Hajlaoui na Balozi wa Uswisi Mhe. Didier Chassot ambao wamemaliza muda wao wa uwakilishi hapa nchini.
Katika mazungumzo yao yaliyofanyika kwa nyakati tofauti katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam Mhe. Balozi Kombo amempongeza Mhe. Nabil Hajlaoui kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanya katika kipindi chake cha uwakilishi hapa nchini. “Mhe. Balozi Hajlaoui nakupongeza sana kwa kazi kubwa, nzuri na ya mfano, uliyoifanya hapa nchini, hasa katika eneo la kukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano kati ya Tanzania na Ufaransa, kwakweli hongera sana na nikutakile kila la heri huko uendako,” alisema Balozi. Naye Mhe. Balozi Hajlaoui ameshukuru kwa ushirikiano alioupata wakati wote alipokuwa nchini na hivyo kumuwezesha kutekeleza majukumu yake kwa tija na ufanisi bila ya kikwazo chochote na kuahidi kuwa atakuwa balozi mzuri wa Tanzania huko aendako. Katika tukio lingine akiagana na Balozi wa Uswisi anayemaliza muda wake nchini Mhe. Didier Chassot Balozi Kombo amemshukuru na kumpongeza kwa kushiriki kikamilifu katika kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Uswisi katika kipindi chake cha uwakilishi. Amemuahidi kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itaendelea kutoa ushirikiano kwa ajaye na kuendelea na kukamilisha masuala mbalimbali ya ushirikiano aliyoyaanzisha. Naye Mhe. Chassot ameishukuru Wizara kwa ushirikiano mzuri iliyompatia wakati wote wa uwakilishi wake hapa nchini na kuahidi kuwa atayaendelea mazuri yote alyojifunza alipokuwepo hapa nchini. |
Tuesday, August 20, 2024
WAZIRI KOMBO APOKEA MWALIKO WA RAIS SAMIA KUSHIRIKI JUKWAA LA FOCAC
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amepokea mwaliko rasmi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kushiriki Mkutano wa Kileke wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping utakaofanyika mwezi Septemba 2024 jijini Beijing nchini China.
Mwaliko huo umewasilishwa na Balozi wa Jamhuri ya Watu China nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam, pia umeainisha nafasi ya kipekee kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuzungumza katika kikao cha ufunguzi kwa niaba ya nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki pamoja na kuzungumza Katika Mkutano wa Ngazi ya Juu utakaojadili mada ya Maendeleo ya Viwanda na Kilimo cha Kisasa. Akipokea mwaliko huo kwa niaba ya Mhe. Rais, Mhe. Balozi Kombo ameelezea kuwa nafasi ya Mhe. Rais kushiriki na kuzungumza katika Jukwaa hilo itaipa nchi fursa ya kuangazia uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na China na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla, hali ambayo itasaidia vipaumbele vya maendeleo vya Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Tanzania ni kinara na kiongozi wa kupigiwa mfano kwenye Jumuiya hiyo kongwe Afrika. Aidha Balozi Kombo amemhakikishia Balozi Chen ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa Kileke wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa FOCAC ambapo Tamko la FOCAC na Mpango Kazi wa FOCAC itakuwa ni moja ya Matokeo ya Mkutano huo. Naye Balozi wa China Mhe. Chen ameelezea kufurahishwa kwa China kutokana na kupokelewa kwa mwaliko wa kuhudhuria Mkutano na kuongeza kuwa kitendo hicho kinaendelea kukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na China. Amesema China inaona Tanzania kama mshirika muhimu wa maendeleo kwa nchi za Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla na kuahidi kuwa China itaendelea kushirikiana na Tanzania. Jukwaa la Focac lilianzishwa kwa lengo la kukuza ushirikiano kati ya China na Afrika ili kuchagiza maendeleo kupitia sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi. FOCAC limekuwa jukwaa linalotoa fursa sawa kwa pande zote mbili kujadili masuala muhimu ya kimaendeleo na kutafuta majibu ya changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia ikiwemo amani na usalama na mabadiliko ya tabia nchi. |
Monday, August 19, 2024
RAIS MNANGAGWA AKABIDHI ENEO LA UJENZI WA MAKUMBUSHO YA UKOMBOZI WA AFRIKA
Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Dkt. Emmerson Mnangagwa amezindua ujenzi wa Makumbusho ya Urithi wa Afrika na kukabidhi eneo la hekta moja (1) kwa ajili ya uhifadhi wa historia ya ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika linalotambulika kama Kituo cha Ukombozi wa Nchi za SADC au “SADC Liberation Square”
Mhe. Mnangagwa alikabidhi
Kituo hicho rasmi kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya
SADC, ambapo kilipokelewa kwa niaba na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika (SADC) Mhe. Elias Magosi na kueleza kuwa Kituo hiko
kitachangia juhudi za Kanda za kuenzi michango ya Wapigania uhuru katika
harakati za ukombozi na pia ni miongoni mwa utekelezaji wa mkakati wa kuenzi
Waanzilishi wa SADC.
Kwa upande wake, Mhe.
Mnangagwa alikiri kuwa Kituo cha Ukombozi wa Nchi za SADC kitachangia uhifadhi
wa historia muhimu za ukombozi ambazo zinaendelea kuandaliwa chini ya mpango wa
kujenga Makumbusho ya SADC jijini Gaborone na ule wa kujenga Makumbusho ya
Urithi wa Afrika nchini Tanzania. Hali kadhalika, Mhe. Mnangagwa alizialika
nchi wanachama za SADC kuchangia katika kuboresha Kituo hicho kwa kuwasilisha
zana za Sanaa kutoka nchini mwao zinazoelezea historia ya ukombozi wa nchi za
kusini mwa Afrika.
Makabidhiano ya eneo hilo
yameenda sambamba na ziara ya kutembelea eneo la mradi pamoja na zoezi la kupanda
mti ambao ulipandwa na Katibu Mtendaji wa SADC, Bw. Magosi na kushuhudiwa na
Wakuu wa Nchi na Serikali walioshiriki ziara hiyo akiwemo, Mhe. João Lourenço, Rais wa Jamhuri ya
Angola, Mtukufu Mswati III, Mfalme wa Eswatini, Mhe. Andry Rajoelina, Rais wa
Jamhuri ya Madagascar, na Mhe. Mokgweetsi Masisi, Rais wa Jamhuri ya Botswana.
Ziara hiyo ilikuwa ni
muendelezo wa ratiba ya Mkutano wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliofanyika
tarehe 17 Agosti 2024. Akihutubia katika hafla ya makabidhiano ya eneo hilo, Mhe.
Mnangagwa ameeleza kuwa mradi huo unalenga kuwaenzi wanaharakati wa kweli na
wana wa Afrika waliojitoa muhanga katika kupigania ukombozi wa nchi zao. Hivyo,
ni heshima kubwa kwa mataifa yetu kutambua mchango wao na kuona fahari kuienzi
historia yetu.
Aidha, Wakuu hao wa nchi na
Serikali walitembelea pia Kituo cha uchakataji taka cha Geo Pomona cha jijini
Harare ambacho awali kilikuwa dampo na baadae kuanza kuchakata taka kwa ajili ya kuzalisha
nishati ya umeme sambamba na kutoa ajira mbalimbali kupitia shughuli za kituo
hicho.
Mradi huo una uwezo wa
kukusanya taka ngumu zenye uzito wa tani 1000 na kuzaliwa kiasi cha Megawati 16
hadi 22 za umeme kwa ajili ya kuunganisha kwenye gridi ya Taifa kwa matumizi ya
umma wa Zimbabwe.
Akihutubia katika uzinduzi
huo, Mhe. Mnangagwa ameeleza kuwa eneo hilo awali lilikuwa limekithiri kwa
uchafu na wingi wa taka na hivyo kupatikana kwa teknolojia bora na ya kisasa ya
kuchakata taka imesaidia kutunza mazingira kwa kuteketeza taka hatarishi pasipo
kuleta madhara ya kiafya kwa bianadamu, mimea, wanyama na mazingira kwa ujumla.
“Zimbabwe imeweka ahadi ya
kukiendeleza na kukisimamia kituo hiki ili kiwe cha mfano katika kuitengeneza
kanda ya kijani kwa kutunza mazingira na kuzalisha umeme” alisema Mhe.
Mnangagwa.
Aidha, alieleza kuwa miradi
kama hii ni sehemu ya jitihada za ubunifu unaohitajika ili kuiletea Jumuiya ya
SADC maendeleo na akasisitiza ni vyema kuendelea kuwa wabunifu katika kila
sekta kwa kuwa ni wazi kuwa kila nchi itajengwa na wenye nchi na sio kinyume chake.
====================================
Habari katika picha; Matukio yaliyojiri wakati wa uzinduzi wa eneo la Makumbusho ya Ukombozi wa Afrika
Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Emmerson Mnangagwa akihutubia katika ziara ya ujumbe wa SADC kwenye kituo cha kuchakata taka tarehe 8 Agosti, 2024 Harare, Zimbabwe |
Mhe. Magosi akipanda mti katika eneo la mradi wa Makumbusho ya Ukombozi wa Afrika. |
Sunday, August 18, 2024
TANZANIA YAKABIDHIWA UENYEKITI WA SADC ORGAN TROIKA
Mkutano wa Kawaida wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya
ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) leo tarehe 17 Agosti, 2024 umekabidhi
jukumu la Unyekiti wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Organ on Politics, Defence and Security)
kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Asasi hiyo ina jukumu la kusimamia masuala ya ulinzi na usalama
katika kanda ya SADC na ina mamlaka ya kuongoza na kutoa ushauri kwa nchi
wanachama katika masuala yanayohatarisha amani, usalama na utulivu katika kanda
hiyo. Majukumu hayo huratibiwa katika ngazi ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa
Asasi hiyo.
Nafasi za uongozi kwa
upande wa SADC Organ hufuata mzunguko kama ilivyo katika
nafasi ya uongozi wa SADC lakini sio nchi zote zinaweza kuwa Mwenyekiti
isipokuwa kwa kigezo cha uwepo wa hali ya ulinzi na usalama katika nchi
mwanachama. Tanzania imeshawahi kuwa Mwenyekiti mara tatu katika vipindi
tofauti: 2006/2007, 2012/2013 na 2016/2017 na sasa itaongoza kwa kipindi cha
2024/2025 ambapo itakuwa mwenyeji wa vikao vya Asasi hiyo kwa kipindi husika.
Kufuatia utaratibu
huo, Troika
ya SADC kwa mwaka 2024/2025 inaundwa na Zambia (Mwenyekiti aliyemaliza muda)
Tanzania (Mwenyekiti wa sasa) na Malawi (Makamu Mwenyekiti).
Jukumu
kubwa linalomkabili Mhe. Rais Samia katika asasi hiyo ni pamoja na kusimamia
amani Mashariki mwa DRC hivyo, ataendeleza jitihada zake pale ambapo uongozi
uliopita uliishia.
Mkutano huo pia,
umemthibitisha Mwenyekiti wa SADC ambapo, Mhe. Emerson Bambudzo Mnangagwa Rais
wa Jamhuri ya Zimbabwe amepokea jukumu hilo na nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa
SADC imeenda kwa Mhe. Andry Rajoelina Rais wa Jamhuri ya Madagascar ambapo nchi
hizo zitaongoza katika kipindi cha 2024/2025.
Akihutubia mkutano huo
Mwenyekiti wa SADC, Mhe. Mnangangwa amempongeza Mhe. Rais Samia kwa kupokea
jukumu la uenyekiti wa SADC na amemuhakikishia ushirikiano katika kufanikisha
majukumu hayo waliyokabidhiwa kwa ustawi wa kanda na wananchi wake.
Pia, ameeleza kuwa
jumuiya hiyo inaendelea kufungua fursa mbalimbali kwa ajili ya maendeleo
endelevu ya kikanda kupitia agenda yake ya kipaumbele ya maendeleo ya viwanda.
Jitihada hizo zitakuza ubunifu na kuongeza thamani ya bidhaa katika masoko ya
kikanda na kimataifa.
Kuhusu shughuli nyingine
zilizofanyika sambamba na mkutano huo Mhe. Mnangagwa ameeleza kuwa kulikuwa na
Kongamano la Uwekezaji lililoandaliwa na Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya
Kiuchumi Afrika (BADEA) na Wiki ya Viwanda ambazo zilitumika kuonesha bidhaa na
huduma mbalimbali kutoka nchi wanachama pamoja na kutoa fursa kwa
wafanyabishara kubadilishana uzoefu na kukuza mtandao wa biashara.
Shughuli nyingine
iliyofanyika ni pamoja na mhadhara wa umma ambao unasaidia katika kujenga
uelewa wa masuala ya msingi ambayo husaidia katika ubunifu na kuendelea
kuimarisha hatua za mtangamano. Hivyo ni muhimu kwa vyuo vikuu na vyuo vingine
vinavyofanana navyo kutafakari namna bora ya kuwekeza katika ubunifu ili
kuwezesha mikakati ya kikanda kupata matokeo ya kimaendeleo kwa mafanikio.
Pamoja na hayo
amesisitiza umuhimu wa kukuza sekta ya nishati, kilimo, biashara, uwekezaji na
usafirishaji na kuhimiza umuhimu wa nguvu ya pamoja katika kutatua changamoto
zake na kuiwezesha jumuiya hiyo kuinuka kiuchumi.
Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi na Serikali pia umemalizika kwa nchi wanachana kusainiwa Itifaki na matamko mbalimbali ya kikanda, kwa upande wa Tanzania imesaini Itifaki ya Ajira na Kazi, Tamko la
Kuwalinda Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi na Tamko la Kutokomeza Ugonjwa wa Ukimwi
kama Janga la Kiafya kwa Jamii ya Ukanda wa SADC ifikapo 2030.
Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa Mkutano wao Kawaida wa 44 uliofanyika tarehe 17 Agosti, 2024Harare, Zimbabwe. |