Tuesday, September 29, 2015

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje akutana kwa mazungumzo na Balozi wa Uturuki nchini

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Mahadhi Juma Maalim (Mb) akisalimiana na Balozi wa Uturuki nchini, Mhe. Yasemine Eralp ambaye alifika Wizarani kwa ajili ya mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili. 
Mhe. Mahadhi  akizungumza wakati wa mkutano wake na Mhe. Eralp.
Mhe. Eralp akizungumza huku Mhe. Mahadhi akimsikiliza
Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Joseph Sokoine (katikati) kwa pamoja na Bw. Adam Isara, Katibu wa Naibu Waziri na Bi. Felister Rugambwa, Afisa Mambo ya Nje wakifuatilia mazungumzo kati ya Mhe. Mahadhi na Mhe. Eralp (hawapo pichani).
Mazungumzo yakiendelea.

Monday, September 28, 2015

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Taarifa zaidi kuhusu Mahujaji kutoka Tanzania waliofariki na kujeruhiwa huko Saudi Arabia

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kupitia Ubalozi wake mjini Riyadh, Saudi Arabia imepokea taarifa kuwa hadi kufikia tarehe 27 Septemba, 2015 watu waliopoteza maisha kufuatia tukio la mkanyagano (stampede) wa Mahujaji waliokuwa wakielekea Jamarat kutupa vijiwe huko Mina nje kidogo ya mji wa Makkah, lililotokea siku ya Alhamisi tarehe 24 Septemba, 2015 wameongezeka na kufikia 769 na majeruhi 934.

Aidha, Wizara kupitia Ubalozi huo inaendelea kufuatilia hatma ya Mahujaji wa Tanzania waliopotea katika tukio hilo la ajali ambapo hadi sasa Mahujaji wa Tanzania wapatao 50 bado hawajaonekana. Vikundi wanavyotoka Mahujaji hao na idadi yao ni kama ifuatavyo:-

1.  Ahlu Daawa-Mahujaji  30;
2.  Khidma Islamiya-Mahujaji 16; na
3.  TCDO-Mahujaji 4

Vile vile juhudi za Ubalozi kwa kushirikiana na Tanzania Hajj Mission na viongozi wa vikundi vilivyopoteza Mahujaji wao zimefanikiwa kuutambua mwili wa hujaji mmoja aliyefariki dunia anayejulikana kwa jina la Shafi Khamis Ali kutoka kikundi cha Ahlu Daawa. Kutambuliwa kwa mwili wa hujaji huyo kunafanya idadi ya Mahujaji wa Tanzania waliofariki dunia katika ajali hiyo kufikia watano (5).

Pia, Wizara kupitia Ubalozi wake imepokea taarifa ya kupatikana kwa hujaji mwingine anayeitwa Nasra Abdullah akiwa hai naye kutoka kikundi hicho cha Ahlu Daawa.

Kuhusu majeruhi, taarifa kutoka Ubalozini zinaeleza kuwa, hujaji mmoja aliyejulikana kwa jina la Mahjabin Taslim Khan alipata majeraha yaliyopelekea kukatwa mguu na kwa sasa anaendelea kupata matibabu huku hali yake ikiendelea vizuri.

Ubalozi unaendelea na juhudi za kuwatafuta Mahujaji wengine wa Tanzania ambao bado hawajaonekana kwa ajili ya kubaini wale waliofariki au majeruhi wanaoendelea kupatiwa matibabu.

Mahujaji wengine wa Tanzania wapo salama ambapo tarehe 26 Septemba, 2015 walimaliza ibada ya hija na tarehe 28 Septemba, 2015 wameanza safari ya kurejea nyumbani.

Wizara inaendelea kuwaomba Wananchi kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu wakati Serikali ikiendelea kufuatilia.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam

28 Septemba, 2015

Sunday, September 27, 2015

Tanzania yafaulu kupata bilioni 992.8 za MCC


Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa na Bi. Dana Hyde, Mtendaji Mkuu wa MCC mara baada ya kumaliza mazungumzo yaliyofanyika kwenye Hoteli ya Marriot Jijini New York. 









THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

                                                                                                                        PRESIDENT’S OFFICE,

      STATE HOUSE,
              1 BARACK OBAMA ROAD,  
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.





TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Sasa ni Rasmi: Tanzania kupata mabilioni mengine ya MCC
·      Yafaulu mtihani wa kupata bilioni 992.8 za kuboresha sekta ya umeme
·      Yafanikiwa baada ya kutimiza masharti yote likiwemo la kupambana na rushwa
·      Zitaanza kutolewa mwakani baada ya kupigiwa kura na Bodi ya MCC

Tanzania imetimiza masharti yote ya kupatiwa raundi ya pili ya fedha za maendeleo kutoka Shirika la Maendeleo ya Milenia la Millennium Challenge Corporation (MCC) la Marekani na itaanza kupata na kunufaika na mabilioni hayo ya fedha baada ya wajumbe wa Bodi ya MCC kupiga kura ya kuidhinisha kutolewa kwa fedha hizo chini ya Mpango wa MCC-2.

Habari hizo njema zimetangazwa Jumamosi, Septemba 26, 2015, kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, na Mtendaji Mkuu wa MCC, Bi. Dana J. Hyde katika mkutano uliofanyika katika Hoteli ya JW Marriot Essex House, New York, na kuhudhuriwa na watumishi waandamizi wa MCC akiwamo Bwana Kamran Khan, Makamu wa Rais wa Operesheni za MCC. Rais Kikwete yuko New York kuhudhuria shughuli za mwaka huu za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

“Hongera Mheshimiwa Rais kwa sababu nchi yako, Tanzania imetimiza masharti yote ya kupata fedha nyingine chini ya mpango wa MCC - 2, ikiwa ni pamoja na uongozi wa MCC kuridhika kuwa Tanzania inachukua hatua za dhati kupambana na rushwa,” Bi. Hyde amemwambia Rais Kikwete na viongozi wengine wa Tanzania akiwamo Waziri wa Nchi za Fedha wa Zanzibar, Mheshimiwa Yusuf Omar Mzee.

Bi. Hyde amemwambia Rais Kikwete kuwa Bodi ya MCC, katika mkutano wake wa Septemba 17, mwaka huu na chini ya Mwenyekiti wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Bwana John Kerry, imeafiki kuhusu kipengele pekee kilichokuwa kimebakia katika masharti ya kupata fedha za MMC kuwa ni kweli Tanzania inakabiliana ipasavyo na rushwa na kuchukua hatua stahiki kukabiliana na janga hilo la rushwa.

MCC imetoa taarifa ya kuthibitisha kuwa Tanzania imetimiza masharti ya kuiwezesha kufaulu kupata raundi ya pili ya fedha za maendeleo na pia imetoa taarifa ya kuthibitisha kuwa ni kweli Bodi ya MCC imeridhishwa na hatua zinazochukuliwa kukabiliana na rushwa.

Tofauti na fedha nyingi zinazotolewa na wafadhili wengi duniani, fedha za MCC hazitakiwi kurudishwa na nchi inayopewa fedha hizo na pia nchi husika hupewa uhuru wa kuchagua aina ya miradi ya maendeleo ambayo inaitaka igharimiwe na fedha hizo.

Miongoni mwa wajumbe wengine wa Bodi ya MCC ni pamoja na Waziri wa Fedha wa Marekani ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi, Mwakilishi wa Biashara wa Marekani duniani, Mwendeshaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), nafasi ambayo kwa sasa anaikaimu Bwana Alfonsi Lenhardt, 

Mtendaji Mkuu wa MCC Bi. Hyde na Rais wa Taasisi ya International Republican Institute (IRI) Balozi Mark Green.
Mabalozi Lenhardt na Green walikuwa mabalozi wa Marekani katika Tanzania wakati wa majadiliano, upitishaji na utekelezaji wa MCC–1.

Bi Hyde amesema sasa linalobakia ni kwa wajumbe wa Bodi kupelekewa muhtasari wa kuidhinisha mabilioni hayo kwa Tanzania ambayo chini ya mpango wa uwekezaji wa MCC–2 yatakwenda katika kuboresha huduma za umeme katika Tanzania ikiwa ni pamoja na kusambaza umeme katika vijiji vingi zaidi nchini. Kiasi cha asilimia 46 ya Watanzania kwa sasa wanapata umeme kutoka asilimia 10 ya mwaka 2005 na sehemu kubwa ya asilimia hiyo imetokana na msaada wa MCC-1.
Chini ya Mpango huo wa pili wa MCC, Tanzania itapatiwa kiasi cha dola za Marekani milioni 472.8 (sawa na sh. bilioni 992.80). Kwa kutilia maanani kiasi cha dola milioni 698 (sawa na sh. trilioni 1.46) ambazo zilitolewa chini ya MCC-1 basi Tanzania itakuwa imepata jumla ya dola za Marekani trilioni 2.45 za maendeleo kutoka Marekani katika kipindi cha miaka 10 tu iliyopita. Fedha za MCC-2 zitaanza kutolewa mwakani, 2016.

Kiasi kilichotolewa kwa Tanzania wakati wa MCC-1 ndicho kilikuwa kiasi kikubwa zaidi ambacho kimepata kutolewa na Marekani chini ya Mpango huo wa Millennium Challenge Corporation na kwa kupita MCC-2 Tanzania itakuwa ni nchi ambayo itakuwa imepata kiasi kubwa cha fedha za maendeleo chini ya MCC duniani.

Fedha zilizotolewa chini ya MCC -1 zilitumika kujenga Barabara za Tunduma-Sumbawanga, Tanga-Horohoro na Namtumbo-Songea-Mbinga.

Aidha, fedha hizo zilitumika kujenga upya mfumo wa huduma za maji kwa ajili ya miji ya Dar es Salaam na Morogoro na zilitumika kusambaza umeme katika vijiji vya mikoa 10 ya Tanzania Bara.

Fedha hizo vile vile zilitumika kutandaza njia ya pili ya kusafirisha umeme chini ya Bahari ya Hindi kati ya Bara na Tanzania Visiwani na pia zilitumika kujenga barabara zote kuu za Kisiwa cha Pemba na baadhi ya barabara za Unguja kwa kiwango cha lami.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
27 Septemba, 2015