Tuesday, August 22, 2017

Warsha kuunganisha Mipango ya APRM na Mipango ya Serikali kufanyika Zanzibar



                                                                                          


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Warsha kuunganisha Mipango ya APRM na Mipango ya Serikali kufanyika Zanzibar


Tunapenda  kuwafahamisha kuwa warsha ya APRM itafanyika tarehe 24 – 25 Agosti 2017, kwenye hoteli ya “Golden Tulip Boutique”, Zanzibar. Warsha hiyo itahudhuriwa na Wakurugenzi na maafisa waandamizi toka idara za Mipango na Sera za Wizara, Idara na Wakala wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wapatao 50. Na pia itakuwa na watoa mada toka nchi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Zanzibar yenyewe, Afrika ya Kusini, Ghana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa.


Warsha hiyo inalenga kujenga uwezo wa Watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), katika kuoanisha (kuunganisha) Mpango Kazi wa APRM na mipango ya Maendeleo ya Zanzibar, hasa Mpango wa Kupunguza Umaskini na Kuleta Maendeleo Na. III. 


Na itajadili masuala yafuatayo: Namna ya kuunganisha Mipango ya Maendeleo ya nchi, Agenda 2063 ya Umoja wa Afrika, Malengo Endelevu ya Milenia pamoja na Mpango Kazi wa APRM; Uzoefu wa nchi nyingine za Kiafrika katika kuunganisha Mipango yao ya Maendeleo na Mpango Kazi wa APRM na Mkakati wa Tathmini na Ufuatiliaji.


Warsha hiyo inagharamiwa kwa pamoja baina ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Uchumi Barani Afrika pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania.


Mwishoni inatarajiwa kuwa washiriki wataweza kuunganisha  Mpango Kazi wa APRM na kuonda changamoto za Utawala Bora pamoja na Mipango ya Maendeleo ya Zanzibar kwa lengo la kutumia vizuri rasilimali zilizopo ili kujenga uhusiano kati ya Mipango hiyo pamoja na kukuza uwezo wa kitaasisi.


Hatua hiyo ni muhimu sana kwani itasaidia kwa kiasi kikubwa kukamilisha Taarifa ya kuondoa changamoto za Utawala Bora zilizobainishwa kwenye Ripoti ya Nchi. Na hatimaye nchi yetu itaweza kuwasilisha Ripoti ya Utekelezaji wa Mpango Kazi wa kuondoa changamoto hizo kwenye kikao cha Wakuu wa nchi wanaoshiriki mchakato wa APRM.


Inatarajiwa kuwa, kwa kutatua changamoto za utawala bora nchi itaweza kuendelea kuwa na amani na utulivu, kukuza uchumi, kuwa na maendeleo endelevu pamoja na kuharakisha Muungano wa Kikanda, na hatimaye kuwaondolea wananchi umaskini.


Tanzania ni mojawapo kati ya nchi 36 za Afrika zinazoshiriki mchakato wa APRM, nayo imeshawasilisha Ripoti yake ya kwanza kwa Wakuu Wenza wanaoshiriki mchakato huu mwaka 2013. Hivi sasa ipo katika hatua ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa kuondoa changamoto zilizobainishwa kwenye Ripoti ya Utawala Bora.


Imetolewa na APRM Tanzania
22 Agosti 2017


Monday, August 21, 2017

Waziri wa Nchi anayeshugulikia Masuala ya Afrika wa Uingereza kuzuru Tanzania


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI



Waziri wa Nchi anayeshugulikia Masuala ya Afrika wa Uingereza kuzuru Tanzania tarehe 22 na 23 Agosti 2017


Waziri wa Nchi anayeshughulikia Masuala ya Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza, Mhe. Stewart Rory atafanya ziara ya kikazi ya siku mbili nchini tarehe 22 na 23 Agosti 2017. 


Mhe. Rory anakuja nchini kwa madhumuni ya kutembelea miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Uingereza (Department for International Development – DFID).


Aidha, wakati wa ziara hiyo, Mhe. Waziri Rory amepangiwa miadi ya kuonana na Viongozi wa Serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb).

Baadhi ya miradi ambayo, Mhe. Waziri ataitembelea ni upanuzi wa Bandari ya Dar Es Salaam, Shule ya Msingi Mkoani, Bonde la Mto Msimbazi, Kiwanda cha Nguo cha Tooku kilichopo katika Eneo la Viwanda la Benjamin Mkapa, Mabibo jijini Dar es Salaam na kampuni ya Songas. 


Waziri Rory pia anatarajiwa kushiriki chakula cha mchana na vijana wa Kitanzania katika moja ya migahawa `ya kawaida katika mitaa ya jiji la Dar Es Salaam


Baada ya kukamilisha ziara yake, Waziri Rory ataondoka nchini tarehe 23 Agosti 2017 kurejea London.



-Mwisho-

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,

Dar es Salaam, 21 Agosti 2017

Thursday, August 17, 2017

Balozi wa Tanzania nchini Uturuki awasilisha Hati za Utambulisho



 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Balozi wa Tanzania nchini Uturuki awasilisha Hati za Utambulisho
Mhe. Prof. Elizabeth K. KIONDO, Balozi wa Kwanza Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uturuki Jumatano ya tarehe 16 Agosti 2017, amewasilisha Hati zake za Utambulisho pamoja na zile za Kukoma kwa Muda wa Mtangulizi wake kwa Mheshimiwa Recep Tayyip Erdoǧan, Rais wa Jamhuri ya Uturuki. Kitendo hicho kinamfanya Mhe. Kiondo kuwa Balozi wa kwanza mkaazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini humo.

Katika hafla hiyo Mhe. Balozi Kiondo alipata fursa ya kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Rais Erdoǧan kuhusu namna ya kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizo mbili katika maeneo ya uwekezaji, biashara, afya, Elimu, na mengineyo. Aidha, Mhe. Balozi Kiondo alimfahamisha Mheshimiwa Rais Erdoǧan kuwa Ubalozi  utakuwa kiungo muhimu katika kuongeza kasi ya utekelezaji wa makubaliano mbalimbali yaliyofikiwa wakati wa ziara yake nchini Tanzania mwezi Januari 2017 ambapo mikataba na makubaliano yapatayo tisa yalisainiwa.

Kufunguliwa kwa Ubalozi mpya wa Tanzania nchini Uturuki na kuanza kufanya kazi kunatoa fursa muhimu kwa wananchi wa mataifa hayo mawili kuongeza shughuli za kiuchumi hususan biashara kwa manufaa ya pande zote mbili.

Mhe. Balozi anatoa rai kwa Watanzania kujipanga vizuri na kuchangamkia fursa mbalimbali hususan za kibiashara zinazotokana na kuendelea kuimarika kwa mahusiano kati ya Tanzania na uturuki.

Mwisho-

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 17 Agosti 2017

 


Mhe. Prof. Elizabeth Kiondo, Balozi Mteule wa Tanzania nchini Uturuki akiwasilisha Hati za Utambulisho kwa Mheshimiwa Recep Tayyip Erdoǧan, Rais wa Jamhuri ya Uturuki.


Mhe. Balozi Kiondo akiagana na Mheshimiwa Rais Erdoǧan, baada ya kufanya mazungumzo kuhusu mahusiano ya Tanzania na Uturuki.
Picha ya pamoja