Monday, July 23, 2018

Tanzania na Korea zakubaliana kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tanzania imeiomba Jamhuri ya Korea iendelee kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo Serikali ya awamu ya tano imeifanya kuwa ya kipaumbele katika kufikia azma ya uchumi wa viwanda.

Kauli hiyo ilitolewa leo Ikulu jijini Dar Es Salaam na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) mbele ya waandishi wa habari akiwa na mgeni wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Mhe. Lee Nak-yon.

Miradi ambayo Mhe. Waziri Mkuu aliitaja ni pamoja na ujenzi wa Daraja la Kigongo-Busisi mkoani Mwanza lenye urefu wa mita 3200, barabara ya Chaya mkoani Tabora yenye urefu wa kilomita 42 na ujenzi wa barabara ya juu ya bahari kutoka ufukwe wa Coco, Osterbay hadi Aga Khan, Upanga jijini Dar Es Salaam yenye urefu wa kilomita zaidi ya sita. Miradi mingine ni ujenzi wa hospitali tano za rufaa katika kanda mbalimbali nchini na ujenzi wa reli ya kisasa ya kiwango cha kimataifa utakaotekelezwa kwa awamu tano ambapo awamu ya kwanza na ya pili kutoka Dar Es Salaam - Morogoro hadi Dodoma umeshaanza kwa kutumia Fedha za ndani.

Mhe. Majaliwa kabla ya kuzungumza na wana habari alikuwa na mazungumzo rasmi na mwenyeji wake na baadaye viongozi hao walishuhudia uwekaji saini wa Mkataba wa kuondoa hitaji la viza kwa wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na utumishi baina ya Tanzania na Korea.

Mkataba huo kwa upande wa Tanzania ulisainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga na kwa upande wa Korea, Makamu wa Kwanza wa Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Lim Sung- Nam aliweka saini kwa niaba ya Serikali yake.

Katika ziara hiyo, Mhe. Lee pamoja na mambo mengine alitembelea Kituo cha Kutunzia kumbukumbu cha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa ambacho ujenzi wake ulitokana na mkopo wa masharti nafuu wa benki ya Exim ya Korea. Aidha, alitembelea hospitali ya Mnazi mmoja na kutoa msaada wa gari mbili za kubebea wagonjwa.

Wakati wa mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Mhe. Majaliwa alitumia fursa hiyo kuwakarabisha wafanyabiashara wa Korea kuja kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii.

Kuhusu utalii, Waziri Mkuu Majaliwa alieleza kuwa Korea imekubali kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini ili kuhamasisha watalii wengi kutoka nchi hiyo kuvitembelea na kubainisha kuwa michoro ya tingatinga ambayo asili yake ni Tanzania inapendwa sana nchini humo.

Katika ziara hiyo, Mhe. Lee amefuatana na wafanyabiashara wakubwa ambao watafanya mkutano na wafanyabiashara wa Tanzania siku ya Jumatatu tarehe 23 Julai 2018 unaolenga kuangalia namna watakavyoweza kushirikiana katika uwekezaji kwenye sekta mbalimbali hapa nchini.

Mhe. Majaliwa alieleza kuwa Serikali ya Tanzania inasifu na kuunga mkono jitihada zinazofanywa kati ya Korea Kusini na Korea Kaskazini za kumaliza tofauti zao kupitia mazungumzo ya amani.

Alihitimisha kwa kuwahakikishia wananchi kuwa Korea inaridhishwa na jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano za kuinua uchumi wa Tanzania na kwamba nchi hiyo itaendelea kuunga mkono jitihada hizo. Aidha, Korea inasifu uwepo wa amani nchini na kuwasihi Watanzania waendelee kuitunza kwa kuwa ndio msingi wa maendeleo duniani.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam
22 Julai 2018


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akisalimiana na Mgeni wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Mhe. Lee Nak-yon walipokutana kwa ajili ya kufanya mazungumzo jijini Dar Es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga (kulia) na Makamu wa Kwanza wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea, Mhe. Lim Sung- Nam wakiweka saini Mkataba wa kuondoa hitaji la viza kwa wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na utumishi wanaposafiri baina ya nchi hizo mbili. 

Sunday, July 22, 2018

Waziri Mkuu wa Korea atembelea NIDA na Hospitali ya Mnazi Mmoja

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Kangi Lugola (Mb.) akisalimiana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea Mhe. Lee Nak-Yon mara baada ya kuwasili kwenye kituo cha kutunzia kumbukumbu cha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kilichopo Kibaha. Kituo hicho kilijengwa kwa Mkopo wa masharti nafuu kutoka Korea kupitia Banki ya Exim.
Mhe. Nak-Yon akiweka saini katika kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili kwenye kituo hicho. 
Mhe. Nak-Yon (katikati) akisiliza maelezo ya namna kituo cha kutunzia kumbukumbu cha mamlaka ya vitambulisho vya taifa kinavyotekeleza majukumu yake. wengine katika picha wa pili kutoka kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  Mhe. Augustine Mahiga (Mb.), Mhe. Lugola Balozi wa Korea nchini Mhe.Song Geum-young.


Maafisa wa vyombo vya Ulinzi na Usalama nchini wakifuatilia kwa makini maelezo yaliyokuwa yanaendelea kutolewa kwa mgeni rasmi.
Juu na chini ni seemu ya ujumbe wa mhe. Nak-Yon pamoja na ujumbe kutoka Tanzania wakisikiliza maelezo yaliyokuwa yanatolewa.  
Mhe. Nak-Yon akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza ziara yake kwenye kituo hicho cha kuhifadhia kumbukumbu cha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).



 *******Hospitali ya Mnazi Mmoja*******

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Suleiman(TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo (Mb.) akisalimiana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea Mhe. Lee Nak-Yon mara baada ya kuwasili kwenye Hospitali ya Mnazi Mmoja. Katika hospitali hiyo, Mhe. Waziri Mkuu alipata fursa za kutembelea wagonjwa na kujionea utendaji kazi kwenye hospitali hiyo. Aidha, alipewa nafasi ya kumchagulia jina mtoto aliyezaliwa siku chache zilizopita hospiyalini hapo. Mhe. Nak-Yon pia alikabidhi msaada wa Magari mawili ya kubebea wagonjwa kwenye hospitali hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam tarehe 22.07.2018.
Mhe. Jafo akimtambilisha kwa Waziri Mkuu, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Sophia Mjema mara baada ya kuwasili hospitali ya Mnazi Mmoja. 
Mhe. Nak-Yon akipata maelezo kutoka kwa mmoja wa Madaktari wa Mmnazi mmoja kuhusu matumizi ya kifaa cha maabara.  
Mhe. Nak-Yon akisalimiana na wagonjwa waliokuwepo hospitalini hapo
Mhe. Nak-Yon akimkabidhi zawadi mmoja wa wamama aliyejifungua Mtoto wa kike ambaye mtoto wake alipewa jina Laura na Mwaziri Mkuu huyo.
Mhe. Nak-Yon akikabidhi msaada wa magari mawili ya kubebea wagonjwa kwa Mhe. Jafo mara baada ya kumaliza kuitembelea Hospitali hiyo.
Mhe. Nak-Yon akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali waliohudhuria tukio la kukabidhiwa kwa magari hayo. 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea Mhe. LEE NAK-YON awasili nchini

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb.) akimsuburia mgeni wake Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea Mhe. Lee Nak-Yon akishuka kwenye ndege yake mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Juliusi Nyerere jijini Dar es Salaam, Mhe. Nak - Yon yupo nchini kwa ziara ya siku tatu ambapo atafanya mkutano na mweyeji wake, kisha watasaini Mkataba wa kuondoa hitaji la Viza kwa watu wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na za utumishi. Pia ataenda Ikulu kumsalimia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, atatembelea Makumbusho ya Taifa, Hospitali ya Mnazi Mmoja na Kituo cha utunzaji taarifa cha NIDA kilichopo Kibaha. 
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Majaliwa akisalimiana na Waziri wa Mkuu wa Korea Mhe. Nak-Yon mara baada ya kuwasili nchini.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga (Mb.), naye akisalimiana na Waziri Nak-Yon mara baada ya kupokelewa na Mhe. Majaliwa, wa kwanza kulia ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Isack Kamwele naye akisubiria kusalimiana na Waziri Mkuu wa Korea.
Mhe. Nak - Yon akisalimiana na Balozi wa Tanzania nchini Jamhuri ya Korea Mhe. Matilda Masuka
Mhe. Majaliwa pamoja na mgeni wake Mhe. Nak - Yon  pamoja na Dkt. Mahiga wakitizama kikundi cha ngoma kilichoandaliwa kusherehesha kwenye mapokezi hayo 

Friday, July 20, 2018

Makatibu Wakuu Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara ya Habari wakutana kwa kikao kazi

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda (kushoto) pamoja na mwenyekiti mwenza Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bi. Suzan Mlawi wakiongoza kikao kazi cha pamoja baina ya wizara hizo mbili kilichofanyika wizarani jijini Dodoma tarehe 20 Julai 2018.

Wakurugenzi na maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakifuatilia kikao ambacho ni sehemu ya vikao vinavyofanywa na Wizara ya Mambo ya nje katika kuratibu na kufanya ufuatiliaji wa masuala mbalimbali ya kikanda na kimataifa yanayotekelezwa na sekta nyingine nchini.

Thursday, July 19, 2018

Ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

ZIARA YA WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA KOREA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Mhe. Lee Nak-yon atafanya ziara ya kikazi nchini kwa mwaliko wa mwenyeji wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), kuanzia tarehe 21 hadi 23 Julai 2018. Ziara hiyo itakuwa ya kwanza kufanywa na kiongozi wa ngazi ya juu kutoka Jamhuri ya Korea tangu nchi zetu mbili zianzishe mahusiano ya kidiplomasia mwaka 1992. 

Madhumuni ya ziara hiyo ni kuimarisha ushirikiano na uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili na kufungua zaidi fursa za ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi katika ngazi na sekta mbalimbali. Mhe. Waziri Mkuu Lee atafuatana na ujumbe mzito wa maafisa wa Serikali, wabunge na wafanyabiashara wakubwa. Ujumbe wa wafanyabiashara utakaoongozana na Mhe. Lee unatarajiwa kukutana na wenzao wa Tanzania katika Mkutano wa Pili wa Jukwaa la Wafanyabiashara uliopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam tarehe 23 Julai 2018. Mkutano wa kwanza ambao ulikuwa na mafanikio makubwa ulifanyika Seoul mwezi Februari 2018.

Mhe. Lee Nak-yon atawasili nchini saa kumi na mbili na nusu jioni (12:30) ya tarehe 21 Julai 2018 na atapokelewa na mwenyeji wake Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Siku inayofuata, Waziri Mkuu Lee na mwenyeji wake Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), watafanya mazungumzo rasmi jijini Dar es Salaam na baadaye watashuhudia uwekaji saini wa mkataba wa kuondoa hitaji la visa kwa wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na za utumishi (diplomatic and official/service passport). Aidha, Mhe. Lee atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa ajili ya kusalimiana.

Jamhuri ya Korea ni mshirika mkubwa wa maendeleo wa Tanzania ambapo kupitia  Shirika la Kimataifa la Maendeleo (KOICA) na Mfuko wa Ushirikiano wa Uchumi na Maendeleo (EDCF) yamekuwa yakitoa misaada na mikopo mingi ya masharti nafuu kwa Tanzania ikiwemo misaada ya fedha katika bajeti, ujenzi wa miundombinu ya jamii, mafunzo ya muda mfupi na mrefu, wataalamu mbalimbali wa kujitolea, vifaa na mashine kwa ajili ya sekta mbalimbali ikiwemo ya afya.

Baadhi ya miradi ambayo imegharamiwa na Serikali ya Korea ni pamoja na Mradi wa kuboresha Huduma ya Mama na Mtoto katika Hospitali ya Chanika, Mradi wa Mfumo wa Usajili wa Meli na Mabaharia kwa Njia ya Mtandao Zanzibar, Mradi wa Ujenzi wa Hospitali ya Taifa ya Taaluma na Tiba (MUHAS) kampasi ya Mloganzila na ujenzi wa daraja katika mto Malagarasi.

Vile vile, Korea ni mshirika mkubwa katika kusaidia maendeleo ya Bara la Afrika ambapo hivi karibuni katika mkutano wa Sita wa Jukwaa la Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea na Africa (KOAFEC VI) uliofanyika mwezi Mei 2018, Busan, Korea ambapo Serikali ya Korea ilitangaza msaada wa Dola za Marekani bilioni 5 kwa ajili ya Bara la Afrika kwa kipindi cha mwaka 2018/2020. Tanzania ni miongoni mwa nchi zitakazonufaika na msaada huo.



Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam
19 Julai 2018

Wednesday, July 18, 2018

Mabalozi wanne waagwa jijini Dar Es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) aliyesimama katikakti akiwa katika picha ya pamoja na Waheshimiwa Mabalozi waliomaliza muda wao wa uwakilishi nchiniTanzania. Mabalozi hao, wakwanza kutoka kushoto ni Balozi wa Norway, Mhe. Hanne-Marie Kaarstad, Balozi wa Malawi, Mhe. Hawa Olga Ndilowe, Balozi wa Sweden, Mhe. Katarina Rangnitt na Balozi wa Canada, Mhe. Ian Myles. Mhe. Dkt. Mahiga aliandaa hafla ya kuwaaga Mabalozi hao iliyofanyika jijini Dar Es Salaam tarehe 17 July 2018. Katika hafla hiyo, Dkt. Mahiga aliwashukuru Mababalozi hao kwa niaba ya Serikali zao kwa mchango mkubwa wanaotoa kuboresha sekta mbali mbali hapa nchni zikiwemo za Elimu, Afya, Biashara, Kilimo pamoja na Miundombinu. Aidha, Mabalozi pia walipata nafasi ya kutoa neno la shukrani kwa Wizara pamoja na watumishi wake kwa ujumla kwa kuwapa ushirikiano wa kutosha uliowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi hapa nchini.
Dkt. Mahiga akizungumza kwenye hafla ya kuwaaga Waheshimiwa Mabalozi walio maliza muda wao wa uwawakilishi nchini.

Sehemu ya Mabalozi walio hudhuria hafla hiyo wakisimsikiliza kwa makini Mhe. Dkt. Mahiga (hayupo pichani).
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya naAmerika, Bw. Jestas Nyamanga (kulia) pamoja na Balozi Rangnitt nao wakimsikiliza kwa makini Dkt. Mahiga.
Sehemu nyingine ya Mabalozi waliohudhuria hafla hiyo
Mabalozi walio maliza muda wa uwakilishi nchini wakigonga glasi na Waziri Mahiga ikiwa ni ishara ya kuwatakia Viongozi wa Nchi zao Afya njema na Baraka tele kwenye kufanikisha gurudumu la maendeleo.
Dkt. Mahiga akimkabidhi Balozi wa Sweden picha ya mchoro wa Tembo wa Tatu pamoja na Mlima Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya kuendelea kuikumbuka Tanzania pamoja na kuendelea kuvitangaza vivutio vinavyopatikana nchini. 
Balozi wa Malawi naye alipewa Picha yenye tembo wa Tatu na mlima Kilimanjaro
Dkt. Mahiga akimkabidhi Balozi wa Norway picha inayofanana na wenzake isipokuwa yake ilikuwa na Michoro ya Wanyama aina ya Twiga, Tembo pamoja na Mlima Kilimanjaro.
Balozi wa Canada naye alipata zawadi ya picha yenye mchoro wa Tembo pamoja na Mlima Kilimanjaro, kwa pamoja Mabalozi hao walionyesha kuzifurahia zawadi hizo.
Dkt. Mahiga akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi waliomaliza muda wa uwakilishi nchini pamoja na Mabalozi ambao bado wanaendelea kuziwakilisha nchi zao. 











Tuesday, July 17, 2018

Waziri Mahiga apokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Kenya nchini

Balozi Mteule wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Dan Kazungu akiwasilisha Nakala za Hati za Utambulisho kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb.). Mara baada ya kuwasilisha nakala hizo Mhe. Mahiga na Balozi Kazungu walipata fursa ya kuzungumza kuhusu kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya hususan kwenye sekta za biashara, uchumi na elimu. Tukio hilo lilifanyika kwenye Ofisi Ndogo ya Wizara iliyopo Jijini Dar es Salaam tarehe 16 Julai, 2018. 
Dkt. Mahiga akiendelea na mazungumzo na Balozi Mteule wa Kenya hapa nchini
Sehemu ya Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia mazungumzo kati ya Dkt. Mahiga na Balozi Mteule wa Kenya nchini. Kushoto ni Bibi Judica Nagunwa na Bw. Magabilo Murobi
Balozi Kazungu akimweleza jambo Dkt. Mahiga
Mazungumzo yakiendelea kati ya Dkt. Mahiga na Balozi Kazungu
Picha ya pamoja.
Dkt. Mahiga akiagana na Balozi Mteule wa Kenya nchini Tanzania. 






Thursday, July 12, 2018

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU FURSA ZA MASOMO


TAARIFA KWA VYOMBO VY HABARI

FURSA ZA UFADHILI WA MASOMO
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imepokea fursa za ufadhili wa masomo katika kozi mbalimbali kutoka Serikali ya Saudi Arabia.

Mafunzo hayo yatatolewa katika Chuo Kikuu cha Imam Abdulrahman bin Faisal kilichopo Saudi Arabia. Taarifa kamili kuhusu ufadhili, kozi na taratibu zote za namna ya kuomba zinapatikana kupitia tovuti ya Chuo hicho www.iau.edu.sa
 

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje Na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam
12 Julai, 2018


Tuesday, July 10, 2018

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki yaendelea kutoa huduma kwenye maonesho ya sabasaba

Balozi Ramadhani Mwinyi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (wa pili kushoto) akifafanua jambo kwa mteja aliyetembelea banda la Wizara kwenye maonesho ya sabasaba

Balozi Ramadhani Mwinyi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, akisaini kitabu cha wageni alipotembelea banda la Wizara hiyo kwenye maonesho ya 42 ya biashara ya kimataifa yanayoenedelea jijini Dar es Salaam.
Mhe. Balozi Rajab Luhwavi Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Msumbiji (wa kwanza kulia) akizungumza na baadhi ya watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alipotembelea banda la Wizara hiyo kwenye maonesho ya sabasaba.



Balozi Mohamed Haji Hamza Mkurugenzi wa ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje Zanzibar (kushoto) akisikiliza maelezo kutoka kwa mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia Bw. Shoo Innocent alipotembelea banda la Wizara kwenye maonesho ya sabasaba 

Bw. Zakariyya Kera Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akisaini kitabu cha wageni alipotembelea banda la Wizara hiyo kwenye maonesho ya sabasaba

Bw. Teodos Komba akifanunua jambo kwa mteja aliyembelea banda la Wizara kwenye maonesho ya sabasaba

Wanafunzi kutoka Dar es Salaam Islamic Secondary School wakipewa maelezo walipotembelea banda la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwenye maonesho ya sabasaba


Balozi Ramadhani Mwinyi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiangalia bidhaa kwenye maonesho ya sabasaba

Balozi Ramadhani Mwinyi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiangalia bidhaa kwenye maonesho ya sabasaba

Balozi Ramadhani Mwinyi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiangalia maonesho ya kazi ya ubunifu wa teknolojia kutoka kwa Wataalam wa Taasisi ya Mafunzo ya Ufundi Zanzibar

Balozi Ramadhani Mwinyi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akitoka kuangalia bidhaa kwenye jengo la Zanzibar katika maonesho ya sabasaba