Tuesday, February 25, 2014

Mhe. Membe awasili nchini China kwa ziara ya kikazi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akizungumza na Makamu Mkurugenzi wa masuala ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Bi. Sun Baohong mara baada ya Mhe. Membe kuwasili nchini humo kwa ziara ya kikazi ya siku tano.
Mhe. Membe akisaini Kitabu cha Wageni mara baada ya kuwasili katika Ubalozi wa Tanzania nchini China. Kulia ni Mhe. Lt. Jen. (Mstaafu) Abdulrahaman Shimbo, Balozi wa Tanzania nchini China.
Mhe. Membe katika mazungumzo. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Mbelwa Kairuki. 

Na Mwandishi Wetu, Beijing, China

MHE. BERNARD K. MEMBE (MB.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa amewasili nchini China tarehe 24 Februari 2014 nchini China kwa ziara ya siku tano, na kulakiwa na Bi. Sun Baohong, Makamu Mkurugenzi wa Masuala ya Afrika Wizara ya Mambo ya Nje China. 

Baada ya kuwasili Mhe. Membe alipokea taarifa ya maendeleo ya shuguli za ubalozi kutoka kwa Lt. Jen. (Mstaafu) Abdulrahaman Shimbo, Balozi wa Tanzania hapa China ambapo pia iligusia maeneo ambayo Mhe. Waziri atayatembelea yaani Shenzhen na Guangzhou.  Baadaye Mhe. Membe na ujumbe wake walipata chakula cha usiku na kufanya mazungumzo na Watanzania wanaoishi Beijing China kuhusu ziara yake na masuala mengine yahusuyo Tanzania. 

Katika salamu zake kwa Watanzania hao ambao walijumuika na wafanyakazi wa Ubalozi na Familia zao, Mhe. Membe alieleza baadhi ya mambo yaliomleta kwenye ziara hii ikiwa ni pamoja na maandalizi ya ziara ya Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete nchini hapa kufuatia mualiko wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China. 

Mhe. Membe alielezea pia nia yake na Wizara anayoiongoza ya kukuza na kuendeleza Diplomasia ya Michezo na kusema anaamini Serikali ya China itaridhia ombi la Tanzania la kufundisha wanamichezo thelathini wa Kitanzania kwenye michezo mbalimbali kabla ya Mashindano ya Nchi za Jumuiya ya Madola katikati ya mwaka huu.

Mwishoni Mhe. Membe aliwaelezea Watanzania hao mchakato unaoendelea Tanzania wa kupitia Katiba na hoja kuu ya Wizara ya Mambo ya Nje inayowagusa Watanzania wengi waishio ughaibuni ya Uraia wa Nchi Mbili.

Kesho Mhe. Membe na Ujumbe wake wanatazamia kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa China, Mawaziri wa Mambo ya Nje,  Biashara na Naibu Waziri wa Usalama kabla ya kuendelea na ziara yake kwneye Jimbo la Shenzhen na Guangzhou.

Kwenye ziara hii, Mhe. Membe ameongozana na Balozi Mbelwa Kairuki, Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia Wizara ya Mambo ya Nje, Bi. Nakuala Senzia Mkurugenzi  Kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Bi. Mindi Kasiga Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na maafisa waandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje.


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.