Friday, November 13, 2015

MAREKEBISHO YA BARAZA KUU LA USALAMA YATAONGEZA TIJA- TANZANIA

Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Ramadhan Mwinyi akizugumza siku ya Alhamis wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipokuwa likijadili Taarifa ya mwaka ya Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Na Mwandishi Maalum, New  York


Tanzania imekaribisha  juhudi zinazochuliwa na  Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa za kuboresha uwazi na utendaji wenye tija wa chombo hicho juhudi ambazo pia  zinahusisha mijadala ya wazi.

Hayo yameelezwa na  Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Ramadhan Mwinyi wakati  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,  lilipokuwa likijadili Taarifa ya  Mwaka  ya Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa.

 Taarifa hiyo    iliwasilishwa siku ya  alhamisi na   Mwakilishi wa Kudumu wa Uingereza,  Balozi Matthew Rycroft ambaye nchi yake  ndiye Rais wa  Baraza Kuu la  Usalama kwa  mwezi huu wa  Novemba.

Taaria hiyo ambayo ni  ya  kuanzia  Agosti Mosi 2014 hadi Julai 31 2015 imeanisha mikutano  ya wazi na  ya ndani iliyofanywa na Baraza kwa kipindi hicho, maazimio yaliyopitishwa, taarifa za rais wa Baraza kwa  mwezi, na   ziara za kikazi zilizofanywa   na wajumbe wa Baraza. ambaye ni  Mwakilishi wa Kudumu wa Uingereza Balozi katika Umoja wa Mataifa.

Balozi Mwinyi,  amesema  mijadala  ya wazi inayoandaliwa na  Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa  inatoa fursa na kufungua milango kwa  nchi nyingi zaidi kushiriki nje ya wajumbe  15 wa Baraza  na kwamba Tanzania ni kati ya nchi ambazo zimekuwa ikishiriki mijadala hiyo ya wazi.

 Pamoja na  kupongeza juhudi hizo,  Mwakilishi huyo wa Tanzania, amesema,  ni matumaini ya Tanzania   kuwa  katika  siku za usoni,  Baraza Kuu la litaanda mijadala katika namna ambayo itawezesha wajumbe kuzingatia hoja zilizotolewa na  washiriki wengine kabla ya kupitisha matokoe ya mijadala hiyo.

Vilevile  Balozi Mwinyi amesema, juhudi zinazochukuliwa na  wadau mbalimbali za kudhibiti matumizi ya kura ya turufu hasa katika kuzuia mauaji ya halaiki, ni  juhudi sahihi na zinazopashwa kuugwa mkono.

Akizungumzia zaidi  matumizi ya kura ya turufu, Balozi Ramadhan Mwinyi ametoa wito kwa  mataifa yenye hadhi ya kutumia kura hiyo  kuhakikisha kwamba wanaitumia pale tu inapobidi na kwa kuzingatia matakwa na mamlaka zilizoainishwa  Katiba ya Umoja wa Mataifa.

“ Tuna toa wito wa Baraza kuu la Usalama la Umoja wa mataifa, kuingiza katika taarifa zake za baadaye kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,  tathmini ya   matokeo ya maamuzi  pale kura ya turufu ilipotumika na matokeo ya pale  ambapo kura ya turufu haikutumika katika maamuzi yaliyofikiwa” akasisitiza Balozi  Mwinyi.

Kuhusu  yaliyomo katika taarifa hiyo, Balozi  amesema,  Tanzania inaungana  na  nchi nyingine katika kutaka taarifa hizo  ziwe na uchambuzi wa kina na  zilizo  makini badala ya kuorothesha  kazi za Baraza hilo kama ilivyo sasa.

Tanzania pia   kupitia  Mwakilisihi wake ,  imekaribisha  namna ambavyo Baraza Kuu la Usalama linavyopanua wigo wa majadiliano na  Vyombo  vingine  zikiwamo Asasi  za kijamii na wanazuoni katika  kujadilia masuala mtambuka.

“ Hata hivyo tumegundua  kuwa  baadhi ya mada zinazojadiliwa siyo tu  zimekuwa  zikiwagawa washiriki lakini pia zinakuwa nje ya mamlaka ya Baraza. Tunaomba tukumbushe kwamba  Baraza Kuu la Usalama kama Chombo wakilishi cha  Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa, Baraza linatakiwa kujiepusha  mada ambazo  hazina tija”.

Baadhi ya wazungumzaji wengine waliochangia  taarifa hiyo ya Baraza Kuu la Usalama,  wameelezea kwamba  licha ya  utekelezaji  wa  mamlaka ya Baraza hilo katika kusimamia  Amani na usalama wa kimataifa,  Baraza limeshindwa kabisa kumaliza  baadhi ya migogoro kama  ule wa Syria ambao  umedumu  kwa muda mrefu.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.