Friday, November 27, 2015

Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje amuaga Balozi wa Korea Kusini

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula (kulia) akimkabidhi zawadi ya mchoro wa picha ya binti wa kimaasai na shati la kitenge alipokuwa akimuaga Balozi wa Jamhuri ya Korea Kusini, Mhe. Chung II ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi nchini. 
     
Balozi Mulamula akizungumza na Balozi Chung II .
Balozi Chung II naye akimweleza jambo Balozi Mulamula wakati wa mazungumzo yao.
Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Balozi Mbelwa Kairuki (kushoto) na Afisa Mambo ya Nje, Bw. Khatibu Makenga nao wakifuatilia kwa  mazungumzo kati ya  Balozi Mulamula na Balozi Chung II (hawapo pichani).  
Balozi Mulamula (kulia) na Balozi Chung II wakifurahia jambo kwa pamoja wakati wa mazungumzo yao
Mazungumzo yakiendelea
 Balozi Mulamula akiagana na Balozi wa Jamhuri ya Korea Kusini aliyemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini Mhe. Chung II mara baada ya kumaliza mazungumzo

Picha na Reginald Philip 

=============================================


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula amempongeza Balozi wa Jamhuri ya Korea Kusini hapa nchini, Mhe. Chung II kwa kuiwakilisha vyema nchi yake na kupelekea miradi mingi ya maendeleo ikiwemo ile ya miundombinu kukamilika.   
       
Balozi Mulamula alitoa pongezi hizo leo alipokutana na Balozi Chung II ambaye alifika Wizarani kwa lengo la kuaga baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini.

Balozi Mulamula alisema kuwa Jamhuri ya Korea Kusini imekuwa ni miongoni mwa nchi ambazo Tanzania inashirikiana nazo kwa karibu katika kutekeleza miradi ya maendeleo. Alieleza kuwa, nchi hiyo imeshiriki kikamilifu kutekeleza miradi  yenye manufaa makubwa kwa Tanzania  katika Sekta mbalimbali zikiwemo za kiuchumi, biashara na uboreshaji wa miundombinu. 

"Nakupongeza Mhe. Balozi kwa uwakilishi wako mzuri kwani katika kipindi chote ulichokuwepo nchini na kupitia Serikali yako umeweza kukamilisha miradi mikubwa ukiwemo ule wa Daraja la Kikwete lililojengwa katika Mto Malagarasi huko Kigoma” alisema Balozi Mulamula.

Aidha, alimhakikishia ushirikiano kutoka Wizarani na Serikalini kwa ujumla kwa Balozi mpya atakayeteuliwa na nchi hiyo kuja nchini.

Kwa upande wake, Balozi Chung II ambaye amekuwepo nchini kwa kipindi cha miaka mitatu aliishukuru Wizara na Serikali kwa ujumla kwa ushirikiano mzuri aliokuwa akiupata wakati wote wa uwakilishi wake. Pia aliahidi kuendelea kuitangaza Tanzania nchini kwake ili kuendeleza mahusiano mazuri yaliyopo kati ya nchi hizi mbili.

-Mwisho-





 
 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.