Tuesday, November 30, 2021

Balozi Togolani Mavura awasilisha Nakala za Hati za Utambulisho kwa Naibu Waziri na Mkuu wa Itifaki wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea

Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Jamhuri ya Korea, Mhe. Togolani Edriss Mavura, leo tarehe 30 Novemba 2021 amewasilisha Nakala za Hati za  Utambulisho kwa Naibu Waziri na Mkuu wa Itifaki Balozi Jeongyun RYU wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea jijini Seoul.


Akiongea baada ya kupokea Nakala hizo, Balozi Ryu amempongeza Balozi Mavura kwa imani kubwa aliyopewa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kumuwakilisha nchini humo. 

Pia ametumia nafasi hiyo kumhakikishia utayari wa Wizara ya Mambo ya Nje na Serikali ya Korea kwa ujumla kumpatia ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake ikiwemo kuimarisha ushirikiano na uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Korea.

Naye Balozi Mavura alimshukuru Balozi Ryu kwa mapokezi mazuri aliyopata kutoka Serikali ya Korea tangia alipowasili nchini Korea tarehe Novemba 10, 2021, na kutenga muda wake kupokea Nakala za Utambulisho.

 Aidha, Balozi Mavura alielezea kufurahishwa kwa hali ya uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Korea unaoelekea kutimiza miaka 30 mwezi Aprili 2022. 

Vilevile, Alimfahamisha mwenyeji wake juu ya azma yake ya kuuona ushirikiano huu unazidi kuimarika siku za usoni kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na Korea.


Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Jamhuri ya Korea, Mhe. Togolani Edriss Mavura, leo tarehe 30 Novemba 2021 amewasilisha Nakala za Hati za  Utambulisho kwa Naibu Waziri na Mkuu wa Itifaki, Balozi Jeongyun RYU wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea jijini Seoul.

Makabidhiano yakiendelea, wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Utawala na Fedha wa Ubalozi wa Tanzania katika jamhuri ya Korea, Bw. Deogratius Mwanyasi akishuhudia makabidhiano hayo.
 

BALOZI MULAMULA AKUTANA NA WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA CHINA

 

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe. Wang Yi walipokutana kwa mazungumzo jijini Dakar nchini Senegal wanakohudhuria Mkutano wa Nane wa  Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) unaofanyika nchini humo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula wakisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe. Wang Yi walipokutana kwa mazungumzo jijini Dakar nchini Senegal wakati wa Mkutano wa Nane wa wa  Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) unaofanyika nchini humo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na ujumbe wake (kushoto) na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe. Wang Yi na ujumbe wake (kulia) walipokutana kwa mazungumzo jijini Dakar nchini Senegal.
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe. Wang Yi akizungumza wakati wa mazungumzo  na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula hayupo pchani jijini Dakar nchini Senegal.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akizungumza wakati alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe. Wang Yi na ujumbe wake hawako pichani  jijini Dakar nchini Senegal.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na ujumbe wake katika picha ya pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe. Wang Yi baada ya kumaliza mazungumzo yao walipokutana jijini Dakar nchini Senegal.

 

 Na mwandishi wetu,  Dakar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe. Wang Yi jijini Dakar nchini Senegal.

Katika mazungumzo yao viongozi hao wameelezea kuridhishwa kwao na ushirikiano na uhusiano imara uliopo kati ya Tanzania na China na kuahidi kuendeleza uhusiano huo kwa faida ya pande zote mbili.

Waziri Mulamula amemuhakikishia Waziri Yi utayari wa Serikali  kuendelea kushirikiana na China katika kuhakikisha Tanzania inafikia maendeleo ya kweli kwa ufanisi mkubwa.

Amemshukuru Waziri huyo kutokana na ahadi iliyotolewa awali na Rais Xi Jinping wa China wakati wa ufunguzi wa mkutano wa FOCAC ya kutoa dozi bilioni moja zaidi za chanjo ya virusi vya Covid 19 kwa bara la Afrika kwani kitendo hicho kitazisaidia nchi za Afrika kutoa chanjo ya ugonjwa huo kwa watu wengi zaidi.

Pia ameishukuru China kwa kuwa soko la bidhaa za Tanzania na amemuhakikishia Waziri huyo kuwa Tanzania iko tayari kutumia fursa ya soko la China la kuuza mazao yake ya mbogamboga na matunda ili kuongeza ujazo wa biashara na hivyo kukuza uchumi.

Pia ameelezea ambavyo Tanzania inafarijika na utayari wa China katika kuisaidia kwenye miradi mbalimbali kama ile ya  ya ujenzi wa mabwawa ya kuzalisha umeme utokanao na maji kama ya Ruhuji, mradi wa uendelezaji wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji , upanuzi wa Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete  na ujenzi wa barabara kuu katika Visiwa vya  Zanzibar miradi ambayo amesema itasaidia kuinua na kukuza uchumi wa nchi.

Naye Waziri Yi kwa upande wake ameishukuru Tanzania kwa kuendelea kuiunga mkono China na kuahidi kuendelea na harakati za kusaidia nchi zinazoendelea na kuongeza kuwa China itaendelea kuisadia Tanzania katika kufanikisha miradi mbalimbali ya kimkakati na kuielezea Reli ya TAZARA kama moja ya kielelezo cha ushirikiano huo.

Amesema China itaendelea kuunga mkono jitihada za Tanzania katika kujikwamua kiuchumi na itatoa mamilioni ya fedha ili  kukamilisha miradi ya ujenzi, uanzishwaji wa kituo cha mfano kwa ajili ya kuongeza thamani kwenye mazao ya kilimo na kuwaendeleza wafanyabiashara wadogo wadogo nchini.

Mawaziri hao wako Senegal kuhudhuria  Mkutano wa Nane wa  Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) unaofanyika nchini Senegal ulioanza tarehe 29  hadi 30 Novemba  2021.

 

 

 

MKUTANO WA NANE WA MAWAZIRI WA JUKWAA LA USHIRIKIANO KATI YA CHINA NA AFRIKA WAANZA


Rais wa Senegal  na Mwenyekiti Mwenza wa mkutano wa Nane wa  Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC)Mhe. Macky Sall akihutubia wakaati wa ufunguzi wa mkutano huo katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Abdou Diouf ulioko jijini Dakar.

Rais wa China na Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano wa nane wa  Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) Mhe. Xi Jinping na viongozi wengine ambao walihutubia katika ufunguzi wa mkutano huo kwa njia ya mtandao.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashaariki Balozi Liberata Mulamula akifuatilia ufunguzi wa Mkutano wa nane wa  Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC)jijini Dakar , Senegal.

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akizungumza kitu na mmoja wa wa shiriki wa Mkutano wa nane wa  Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) unaofanyika jijini Dakar , Senegal.


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine akifuatilia ufunguzi wa Mkutano wa nane wa  Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) unaaofanyika jijini Dakar , Senegal.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akizungumza jambo na Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine (kushoto)  huku Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar Dkt. Juma Malik Akil (kulia) akisikiliza baada ya ufunguzi wa Mkutano wa nane wa  Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC)jijini Dakar , Senegal.

Mkutano wa Nane wha  Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) umefunguliwa rasmi jijini Dakar nchini Senegal na kuhutubiwa na wenyeviti wenza kwa njia ya mtandao na moja kwa moja.

Awali mwenyekiti mwenza na Rais wa Senegal Mhe. Macky Sall alihutubia mkutano katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Abdou Diouf ulioko jijini Dakar.

Baadaye mwenyekiti mwenza ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping alihutubia mkutano huo kwa njia ya mtandao akiwa nchini China.

Mkutano huo wenye kauli mbiu ya “kuimarisha ubia wa  China na Afrika na kukuza maendeleo endelevu na kujenga jamii ya China-Afrika yenye  kesho ya pamoja katika zama mpya” unahudhuriwa pia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya China Mhe. Wang Yi na Mawaziri wengine wa Mambo ya Nje akiwamo Balozi Liberata Mulamula .

Katika ufunguzi wa Mkutano huo ulihutubiwa pia kwa njia ya mtandao na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mhe. Felix Tshisekedi, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, Rais wa Visiwa vya Comoro Mhe. Asumani Azali, Rais wa Umoja wa Afrika Mhe. Ndiya Musa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Antonio Getterez.

Viongozi hao wote kwa umoja wao wameelezea kuridhishwa kwao na ushirikiano imara uliopo kati ya China na Afrika na kupongeza juhudi zozote zinazochukuliwa katika kuimarisha zaidi uhusiano huo.

Viongozi hao pia wameelezea juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na nchi na viongozi wao katika harakati za kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Covid 19 ikiwa ni pamoja na kuhakikisha maelfu ya watu wa Afrika wanapatiwa chanjo kama njia mojawapo ya kukabiliana na virus hivyo.

Pia wameongelea juu ya hatua mbalimbali ambazo zimekuwa zikichukuliwa na nchi husika katika kuhakikisha mabadiliko ya hali ya hewa hayaleti changamoto zaidi kwa nchi zao.

 Pamoja na mambo mengine viongozi hao wamesisitiza juu ya umuhimu wa kuendelea kuzingatia uimarishaji na ukuzaji wa demokrasia, haki za binadamu, usawa wa kijinsia na utawala wa sheria katika nchi zao

Katika hotuba yake rais wa China aliahidi kutoa dozi bilioni moja za chanjo ya covid 19 kwa nchi za Afrika ikiwa ni ziada ya dozi ambazo zimeshatolewa na China kwa nchi hizo.

 

Monday, November 29, 2021

MKUTANO WA NANE WA JUKWAA LA USHIRIKIANO KATI YA CHINA NA AFRIKA KUANZA LEO

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine katika kikao cha 15 cha maafisa waandamizi kutoka nchi za Afrika na China katika kikao cha maandalizi ya Kikao cha Nane cha  Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) kilichofanyika tarehe 28 Novemba ,2021 jijini Dakar nchini Senegal.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine akiongoza Ujumbe wa Tanzania katika kikao cha maandalizi ya Kikao cha Nane cha  Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) kilichofanyika tarehe 28 Novemba, 2021 jijini Dakar nchini Senegal .

Wajumbe kutoka nchi mbalimbali za Afrika katika kikao cha maandalizi ya Kikao cha Nane cha  Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) kilichofanyika tarehe 28 Novemba, 2021 jijini Dakar nchini Senegal .

Washiriki  wa kikao cha maandalizi ya Kikao cha Nane cha  Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) kilichofanyika tarehe 28 Novemba, 2021 jijini Dakar nchini Senegal wakifuatilia kikao hicho .

Washiriki  wa kikao cha maandalizi ya Kikao cha Nane cha  Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) kilichofanyika tarehe 28 Novemba, 2021 jijini Dakar nchini Senegal wakifuatilia kikao hicho .

Ujumbe wa Tanzania katika picha ya pamoja baada ya kumalizika kwa kikao cha maafisa waandamizi kwa ajili ya kuandaa kikao cha Nane cha  Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) kilichofanyika tarehe 28 Novemba, 2021 jijini Dakar nchini Senegal .




 

Na mwandishi wetu, Dakar

 

Mkutano wa Nane wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) unaanza leo tarehe 29 hadi 30 Novemba 2021 jijini Dakar nchini Senegal.

Maafisa waandamizi kutoka katika nchi za Afrika na Jamhuri ya Watu wa China wamekamilisha maandalizi  yaliyokuwa yanahitajika ya mkutano huo, kwa kupitia na kukubaliana na nyaraka za taarifa za utekelezaji wa miaka mitatu baada ya kikao cha saba katika kikao kilichofayika tarehe 28 Novemba, 2021.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine ameongoza ujumbe wa Tanzania hicho, ambacho pia kilihudhuduriwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mpango Zanzibar Dkt. Juma Akil, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bibi Amina Shaaban, Balozi wa Tanzania Nigeria ambaye pia anaiwakilisha Tanzania nchni Senegal Dkt. Benson Bana na Balozi Ceasar Waitara Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mkutano huo wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika, utakuwa chini ya Wenyekiti Wenza wa Rais wa Jamhuri ya Senegal Mhe. Macky Sall na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping ambao pia watahutubia wakati wa ufunguzi wake.

Mkutano huo unatarajiwa kufanya maamuzi na kutoa maelekezo kuhusu utekeleaji wa masuala ya namna ya kuendelea kukabiliana na virusi vya ugonjwa wa Korona, ushirikiano kati ya China na Afrika, Ushirikiano wa Kisiasa, Ushirikiano wa Kiuchumi, Ushirikiano wa Maendeleo ya Kijamii, Utamaduni na Ushirikiano kati ya Watu na Watu, Ushirikiano wa Ulinzi na Usalama, Mapinduzi ya Kijani, Ubadilishanaji Uzoefu katika masuala ya Uongozi Bora pamoja na Maendeleo ya Kitaasisi ya Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika na mabadiliko ya tabia nchi.