Tuesday, November 16, 2021

MAJALIWA AFUNGUA KONGAMANO LA BIASHARA KATI YA TANZANIA NA UINGEREZA

 

Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza kufungua Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uingereza lililofanyika jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akizungumza wakati wa Kongamano la biashara kati ya Tanzania na Uingereza lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza na Mjumbe maalum wa Waziri Mkuu wa uingereza anayeshughulikia masuala ya biashara kwa Tanzania Bw. Lord Walney ambaye yuko nchini kuhudhuria Kongamano hilo.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Bw. Dotto James katika Kongamano la biashara kati ya Tanzania na Uingereza lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya Viongozi waandamizi wa Serikali ya Tanzania wakimsikiliza Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alipofungua Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uingereza jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya washiriki wa Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uingereza wakifuatilia kongamano hilo jijini Dar es Salaam.



Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amefungua Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uingereza lililowakutanisha wafanyabiashara zaidi ya 300 kutoka Tanzania na Uingereza jijini Dar es Salaam.

Mhe. Majaliwa amewataka wafanyabiashara wa Uingereza kuja kwa wingi nchini kuwekeza na kufanya biashara kwani Serikali ya Tanzania iko tayari kuwapokea wakati wowote.

‘‘Kwanza niishukuru Serikali ya Uingereza kwa kuonesha  nia na utayari wa kuwekeza nchini, nichukue fursa hii kuwakaribisha sana na kuwaahidi kuwa Tanzania iko tayari kuwapokea wakati wowote, na niwaombe muendelee kuja kwa wingi kuwekeza,’’ amesema Waziri Mkuu.

Mhe. Majaliwa pia ametoa shukurani kwa Mjumbe Maalum wa Waziri Mkuu wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya biashara kwa Tanzania Bw. Lord Walney kwa kazi nzuri ya kuitangaza Tanzania. Bw. Walney pia yuko nchini kuhudhuria Kongamano hilo la Wafanyabiashara wa Tanzania na Uingereza.

Amesema ni matumaini yake kuwa wafanyabiashara wa Tanzania na Uingereza wataendelea kuimarisha mahusiano yao ambayo yatakuza uchumi wa Tanzania na kutoa  ustawi kwa wale watakaoshiriki katika mnyororo wa uwekezaji kati ya nchi hizo.

Amesema Tanzania imeboresha mazingira yake ya uwekezaji ili kuvutia zaidi wawekezaji na kuongeza kuwa Tanzania iko tayari kuvutia uwekezaji katika maeneo ya kilimo, utengenezaji dawa, uvuvi, gesi na mafuta, alizeti, kuchakata mazao ya kilimo na mengineyo na hivyo kutengeneza ajira kwa vijana na kuongeza mapato ya serikali.

Amesema Tanzania inahitaji mitaji na teknolojia kutoka Uingereza ili kuboresha na kuutumia ukanda wa mwambao wa bahari ya Hindi kutoka Tanga hadi Mtwara na hivyo kukuza uchumi wa  nchi na kuitaka Sekta binafsi kutumia vizuri kikao hicho kwa kuzungumzia maeneo wanayoweza kufanya biashara na wawaalike kuja nchini kuwekeza na wawe sehemu ya uwekezaji huo ili kuwahakikishia usalama wa uwekezaji wao.

Katika Kongamano hilo kumefanyika mijadala kati ya Serikali ya Tanzanaia na Serikali ya Uingereza, wafanyabiashara na wafanyabiashara na Serikali na wafanyabiashara ili kupata uelewa wa pamoja wa jinsi mambo yalivyo na hivyo kuvutia uwekezaji na kukuza biashara baina ya nchi hizi mbili kwa  manufaa ya pande mbili.

Awali kizungumza katika Kongamano hilo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula amesema kufanyika kwa kongamano hilo ni utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi kwa vitendo kwa kuvutia uwekezaji na kukuza biashara nchini na kuongeza uwepo wa biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza kunaonesha uhusiano mkubwa uliopo baina ya Tanzania na Uingereza na kuna haja ya kuendelea  kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizo.

Kongamano hilo lina lengo la kuhamasisha Wafanyabiashara wa Uingereza kuja kwa wingi kuwekeza nchini na wafanyabiashara wa Tanzania kuuza bidhaa zao kwa wingi zaidi nchini Uingereza. Kongamano hilo pia limelenga kubadilishana uzoefu kwa wafanyabiashara wa nchi hizo ikiwa ni  pamoja na kujadili fursa na Changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya Biashara na Uwekezaji katika pande zote mbili na namna bora ya kuzitumia fursa hizo.

 


 


 

 

 

 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.