Friday, April 12, 2019

Prof. Kabudi afungua rasmi Ofisi za Ubalozi wa China jijini Dodoma


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akitoa hotuba wakati wa ufunguzi wa Ofisi za Ubalozi wa China jijini Dodoma. Ufunguzi wa ofisi hizo umefanyika tarehe 12 Aprili 2019 na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Joseph Kakunda, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri anayeshughulikia uwekezaji, Mhe. Angellah Kairuki, Balozi wa China nchini, Mhe. Wang Ke, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Mussa Azan Zungu, Mzee Job Lusinde na Meya wa Jiji la Dodoma, Mhe. Prof. Davis Mwamfupe. Katika hotuba yake, Mhe. Prof. Kabudi ameupongeza Ubalozi wa China hapa nchini kwa uamuzi wa kufungua ofisi hizo na kuwataka wakazi wa Dodoma na wananchi kwa ujumla kuzitumia ofisi hizo kwa ajili ya kujiimarisha kibiashara na uwekezaji.
Sehemu ya viongozi waliohudhuria ufunguzi wa Ofisi za Ubalozi wa China jijini Dodoma wakimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (hayupo pichani) alipohutubia hafla hiyo
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akitoa hotuba yake

Sehemu ya wageni waalikwa nao wakifuatilia hotuba ya Prof. Kabudi (hayupo pichani wakati wa ufunguzi wa Ofisi za Ubalozi wa China jijini Dodoma. Katikati ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Caesar Waitara na kushoto ni Bw. Charles Mbando, Katibu wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Sehemu ya ujumbe wa China wakifuatilia hotuba ya Mhe. Prof. Kabudi (hayupo pichani)
Balozi wa China nchini, Mhe. Wang Ke akizungumza wakati wa ufunguzi wa Ofisi za Ubalozi huo jijini Dodoma. Mhe. Wang Ke alisema kuwa ufunguzi wa Ofisi hizo ni kuunga mkono kwa dhati mpango wa Serikali ya Tanzania wa kuhamia makao makuu ya nchi uliotangazwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania
Wageni waalikwa wakifuatilia hotuba ya Balozi wa China nchini (hayupo pichani)
Sehemu nyingine ya wageni waalikwa wakifuatilia hafla ya ufunguzi wa Ofisi za Ubalozi wa China jijini Dodoma
Hafla ikiendelea
Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia hotuba ya Balozi Wang Ke (hayupo pichani)
Aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini China kuanzia mwaka 1975 hadi 1984  Balozi Mstaafu, Mzee Job Lusinde akizungumza machache kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na China wakati wa hafla ya ufunguzi wa Ofisi za Ubalozi wa China jijini Dodoma
Mhe. Mussa Azan Zungu, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ambaye alimwakilisha Spika wa Bunge kwenye hafla hiyo naye akipongeza uamuzi wa China wa kufungua ofisi za Ubalozi jijini Dodoma
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi kwa pamoja na Balozi wa China nchini, Mhe. Wang Ke wakifunua kitambaa kuashiria ufunguzi rasmi wa Ofisi za Ubalozi wa China jijini Dodoma
 Mhe. Prof. Kabudi na Mhe. Balozi Wang Ke pamoja na viongozi wengine wakifurahia baada ya ufunguzi rasmi wa Ofisi za Ubalozi wa China jijini Dodoma.





Profesa Kabudi amekutana Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb.) akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi alipofika kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Wizara hiyo. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi wa kwanza kulia akimwelezea jambo Prof. Palamagamba John Kabudi, wa kwanza kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mh. Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi. 

Waziri wa Mabo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba John Kabudi wa Pili kutoka Kushoto akielezea msimamo wa Wizara yake katika kuzitangaza fursa za Uwekezaji zilizopo Zanzibar. Wa kwanza kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mwinyi.

Profesa Palamagamba John Kabudi wa Pili kutoka Kushoto akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
=====================

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba John Kabudi  (Mb.) amesema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikiwa kuwa Taifa moja linaloendelea kudumu muda wote kutokana na misingi imara iliyowekwa na Waasisi wa Taifa hilo.
Amesema yapo Makabila mengi katika Mikoa na Wilaya mbali mbali Nchini lakini muungano wa lugha moja inayozungumzwa na Wananchi wake Bara na Zanzibar imekuwa mfano kwa Mataifa mengine Duniani.
Profesa Palamagamba John Kabudi ameeleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, Vuga Mjini Zanzibar alipofika kujitambulisha baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Ameongeza kuwa yapo Mataifa mengi Duniani yaliyowahi kuunganisha Nchi zao akitolea Mfano iliyokuwa Yugoslavia na sasa imesambaratika pia Senegal na Gambia kwa upande Afrika lakini zimeshindwa kuendeleza Muungano wao.
Waziri Palamagamba John Kabudi alisema wakati Serikali zote mbili zikiendelea kuheshimu kwa kuweka Kumbukumbu za Waasisi hao ambao ni Hayati Mzee Abeid Amani Karume na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Vizazi vya sasa vinapaswa kujifunza tabia ya Viongozi hao walioacha misingi imara ya kitaifa. 

Akigusia suala la Diplomasia ya Uchumi ambayo kwa sasa Tanzania imeelekeza nguvu zake kupitia Balozi zake zilizoko nje ya mipaka ya Tanzania Profesa Palamagamba John Kabudi amesema Serikali inaendeleza mfumo wa kushawishi Wawekezaji ili kuunga mkono jitihada za Taifa za kuwa na Tanzania ya Viwanda ifikapo Mwaka 2025.
Amesema mkakati wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa Kuimarisha Uchumi wake unapaswa kuungwa mkono na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika muelekeo wa kuelekea kwenye Maendeleo ya haraka.
Akigusia Sekta ya Utalii kufanya vyema Zanzibar, Waziri Palamagamba amesema Sekta hiyo ni muhimu hivi sasa kwa mapato ya Taifa na nilazima iwekewe utaratibu wa pamoja utakaosaidia kuuza haiba ya pande zote mbili za Muungano.
Alisema vipo vivutio vinavyopaswa kutangazwa kwa pamoja Bara na Zanzibar ambavyo vinaweza kutoa nguvu ya ushawishi wa Watalii kufanya ziara ya kutembelea sehemu zote mbili kwa wakati mmoja.
Waziri huyo wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alielezea faraja yake kutokana na Zanzibar kupiga hatua kubwa katika kuimarisha Sekta ya Utalii inayotoa ajira kubwa hasa kwa Vijana.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema ushawishi wa Uwekezaji ndani ya Visiwa vya Zanzibar unapaswa kuungwa mkono na Ofisi zote za Kibalozi za Tanzania zilizopo Mataifa mbali mbali Duniani.
Alisema Zanzibar ni sehemu ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ushawishi wake kwa Wawekezaji na Mataifa ya kigeni unawajibika kusimamiwa na Mabalozi wa Tanzania kupitia Wizara yake ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Balozi Seif alimueleza Profesa Palamagamba John Kabudi kwamba Zanzibar kupitia Viongozi wake wote waliopita na waliopo hivi sasa bado wanaendeleza sera na Mikakati iliyoachwa na Muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar Hayati Mzee Abeid Amani Karume.
Alisema uimarishaji wa Miundombinu ya Mawasiliano, Ujenzi wa Nyumba za Kisasa za Maendeleo, Afya, Elimu pamoja na huduma za Maji safi na salama ni miongoni mwa Sekta zinazoendelea kuimarishwa na Viongozi wote.
Balozi Seif Ali Iddi alimweleza Profesa Palamagamba John Kabudi, kuwa Miradi iliyobuniwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwemo ujenzi wa Miji Mipya kama ule wa Ng’ambo tuitakayo katika eneo la Kwahani na Mtaa wa Chumbuni imelenga kustawisha maisha ya Wananchi wake ili kuachana na matumizi mabaya ya Ardhi ndogo iliyopo visiwani humo.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma
12 Aprili, 2019.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje akutana kwa mazungumzo na Mtaalam wa Uchumi kutoka Ujerumani


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akizungumza wakati wa kikao na Prof. Helmut Asche (kulia) ambaye ni Mtaalam wa Uchumi hususan masuala yanayohusiana na Ubia wa Kiuchumi kati ya Ulaya na Afrika (EPA) kutoka Ujerumani. Kikao hicho kilifanyika hivi karibuni jijini Dodoma.
Prof. Asche kutoka Ujerumani akizungumza kwenye kikao kati yake na Naibu Waziri, Mhe. Ndumbaro. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe akimsikiliza Prof. Asche. 
Katibu Mkuu, Dkt. Mnyepe akichangia hoja wakati wa kikao hicho
Prof. Asche akifafanua jambo kuhusu EPA wakati wa kikao kati yake na Mhe. Dkt. Ndumbaro huku wajumbe wengine wakifuatilia. Kulia ni  Bw. Jestas Nyamanga, Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. 
Dkt. Mnyepe (kulia) akiwa na Dkt. Edwin Mhede (katikati), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara wakifuatilia kikao. 
Kikao kikiendelea
Mhe. Dkt. Ndumbaro akiteta jambo na Prof. Asche mara baada ya mazungumzo kati yao
Mhe. Dkt. Ndumbaro akiwa na Prof. Asche na wajumbe wengine wakati wa chakula cha jioni kilichoandaliwa kwa heshima ya Prof. Asche.


Thursday, April 11, 2019

Vivutio vya Utalii kutangazwa Malaysia, Ufilipino, Thailand na Indonesia

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Vivutio vya Utalii kutangazwa Malaysia, Ufilipino, Thailand na Indonesia

Dodoma, 11 Aprili 2019

Makampuni 20 ya Mawakala wa Utalii na Tiketi za ndege (Tour Operators & Travel Agents) pamoja na Waandishi wa Habari kutoka katika nchi za Malaysia, Indonesia, Ufilipino na Thailand walifanya ziara ya mafunzo ya kutembelea vivutio vya utalii nchini  kuanzia tarehe 1 – 7 Aprili 2019.

Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Malaysia kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) yalijumuisha washiriki 20 ambapo Malaysia ilitoa washiriki 5, Thailand washiriki 6, Philippines Washiriki 4 na Indonesia washiriki 5.

Washiriki hao walitembelea maeneo mbalimbali yakiwemo Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro, Mbuga ya Serengeti, duka Maarufu la kuuza madini ya Tanzanite, duka maarufu la zawadi la Arusha Cultural Heritage, sehemu ya historia ya masalia ya Binadamu wa Kale la Olduvai (Oldupai) Gorge na Kijiji cha Wamasai ili kujifunza uhalisia wa maisha yao. Wakiwa kwenye maeneo hayo, wageni walifanikiwa kuona wanyama maarufu watano- big five (Simba, Nyati, Faru, Chui na Tembo) na kushuhudia makundi ya Wanyama aina ya Nyumbu, Pundamilia, na Swala ambao hufanya ziara ya mzunguko maarufu kama Great Migration.

Wageni kabla ya kuagwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii, Jaji Mstaafu Thomas Mihayo pamoja na Bibi. Devotha Mdachi, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii waliahidi kuitangaza Tanzania kama eneo jipya la utalii kwa nchi zao.

Wakati huo huo, Balozi wa Tanzania nchini Malaysia, Mhe. Dkt. Ramadhani Dau amepokea nafasi 160 za ufadhili wa masomo ya elimu ya juu (scholarships) kwenye taaluma mbalimbali zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 1.9 sawa na Shilingi bilioni 4 za Tanzania. Ufadhili huo umetolewa na Chuo Kikuu cha Selangor (University of Selangor) ambacho pia kinajulikana kama UNISEL kilichopo katika Mkoa wa Selangor, Malaysia, unahusisha masomo ya Bachelors of Civil Engineering, Bachelors of Electrical Engineering, Bachelors of Mechanical Engineering, Bachelors of Occupational Health and Safety, Bachelors of Medical Laboratory, Bachelors of Industrial Biotechnology, Bachelors of Computer Science na Bachelors of Information Technology. Hivi karibuni Watanzania watafahamishwa utaratibu wa kuomba masomo hayo.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,

Rais na Makamu Mkuu wa Chuo cha Kikuu cha UNISEL, Prof. Dkt. Mohammad Redzuan Bin Othaman akimkabidhi barua yenye kuainisha ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kwa Watanzania kwa Balozi wa Tanzania nchini Malaysia, Mhe. Dkt. Ramadhani Dau.
Dkt. Dau akiangalia miundombinu ya Chuo Kikuu cha UNISEL
Moja ya Vyumba vya madarasa

Dkt. Dau akipata maelezo kuhusu uendeshaji wa chuo hicho.
Wageni kutoka Malaysia, Indonesia, Thailand na Ufilipino walipowasili Tanzania kwa ajili ya ziara ya mafunzo kwenye vivutio vya utalii.
Wageni kutoka Malaysia, Indonesia, Thailand na Ufilipino wakipata chakula.
Balloon lililowabeba wageni kuwazungusha katika mbuga ya Serengeti.