Mhe. Balozi Mwanaidi Sinare Maajar (kulia), Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Marekani na Mexico akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watanzania (Singo na Godlisen) waliokutana naye kwenye Chuo Kikuu cha Des Moines Jimboni Iowa kabla ya kuanza Mkutano wa Iowa - Tanzania mjini Des Moines tarehe 16 Oktoba, 2012.
Mhe. Balozi Mwanaidi Sinare Maajar (kushoto) akisalimiana na Dkt. Allan Hoffman, Rais Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Santa Barbara, Carlifornia ambaye naye alijumuika na Watanzania kwenye mazungumzo hayo na Balozi Maajar kabla ya Mkutano wa Iowa - Tanzania kuanza.
Rais wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ijulikanayo kama Empower Tanzania, Bw. Phil Latesa akizungumza na Dkt. Allan Hoffman na Bw. Singo baada ya mkutano na Mhe. Balozi Maaar (hayupo pichani).
Mhe. Balozi Mwanaidi Maajar akisalimiana na Watanzania waishio Des Moines Iowa.
Mhe. Balozi Maajar akiwa katika picha na Bw. Singo, alipokutana na Watanzania kabla ya kuhudhuria Mkutano wa II wa Iowa – Tanzania pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Chakula ujulikanao kama World Food Prize unaoendelea mjini Des Moines, Iowa.
Mhe. Balozi Mwanaidi Sinare Maajar akiwa katika picha ya pamoja na Bi. Mindi Kasiga (kulia), Afisa Mwandamizi (Mawasiliano) katika Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Marekani na Mexico kabla ya kuhudhuria Mkutano wa II wa Iowa – Tanzania pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Chakula ujulikanao kama World Food Prize unaoendelea mjini Des Moines, Iowa.
Picha na habari kutoka kwa Mindi Kasiga, Ubalozi wa Tanzania - Washington, DC.
Mhe. Balozi Maajar akutana na Watanzania mjini Iowa
Des Moines, Iowa
16 Oktoba, 2012
BALOZI wa Tanzania nchini Marekani na Mexico Mhe. Mwanaidi Sinare Maajar amewaasa Watanzania waishio Jimbo la Iowa mjini Des Moines kujitokeza na kutoa maoni yao kuhusu suala la uraia wa nchi mbili kwenye mchakato wa mabadiliko ya katiba unaoendelea nchini.
Balozi aliyasema hayo alipokutana na Watanzania hao kabla ya kuhudhuria Mkutano wa II wa Iowa – Tanzania pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Chakula ujulikanao kama World Food Prize unaoendelea mjini Des Moines, Iowa.
Alitoa mfano wa kwake binafsi alipokuwa mwanasheria na mwanaharakati ambapo kupitia taasisi mbalimbali walifanikiwa kushawishi na hatimaye kubadilisha sheria zilizowabana wanawake kuwa na haki sawa na wanaume nchini Tanzania.
“Hakuna ushawishi mzuri kama ule unaotoka kwenu nyie wenyewe Wana Diaspora, kwani nyie ndio mliovaa kiatu cha uraia wa nchi mbili na mnajua kinabana wapi” alisisitiza Balozi na kuwaomba wajitokeze kwa wingi kutoa maoni yao sasa wakati muda unaruhusu kufanya hivyo.
Aliongeza kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba amethibitisha ugumu uliopo kwa wajumbe wa tume hiyo kusafiri nje ya nchi kukusanya maoni, hivyo aliwataka Watanzania waishio nje ya nchi watembelee tovuti ya mabadiliko ya katiba na kutoa maoni yao http://www.katiba.go.tz
Sambamba na kutoa maoni, Mhe. Maajar aliwaasa Watanzania wa Des Moines kujipanga ili kuunda umoja wa Watanzania ili waweze kushughulikia masuala yanayowahusu kwa pamoja. Alisema Marekani ni nchi kubwa na Watanzania waishio majimbo mengine wameitikia wito huo na sasa kuna Jumuiya za Watanzania kwenye majimbo mengi nchini Marekani.
“Kwenye jimbo hili, ni muhimu sana kuwa na Jumuiya madhubuti ili kutumia fursa hii inayojitokeza kila mwaka ya Mkutano wa World Food Prize, kukutana na viongozi wanaokuja kutoka nyumbani au hata sisi kutoka ubalozini” alihimiza.
Kwa upande wao, Watanzania waishio mjini hapa walimshukuru Balozi Maajar kwa kukutana nao na kuahidi kutekeleza yale yaliyoongelewa. Pia walipendekeza ubalozi wa Tanzania Washington D.C. ujaribu kuboresha njia za mawasiliano ya kisasa kama vile Facebook na Tweeter ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi ambao kutokana na kubanwa na kazi, hawapati nafasi ya kutembelea tovuti ya ubalozi.
Mhe. Balozi yupo mjini Des Moines, IA kwa siku mbili ambapo baadaye leo atahutubia Mkutano wa II wa Iowa – Tanzania kama mgeni rasmi ulioandaliwa na Empower Tanzania, Taasisi isiyo ya Kiserikali yenye makao makuu yake hapa Des Moines, Iowa. Kesho tarehe 17 Oktoba 2012, ataendesha mjadala wa Kukata Njaa kabla ya kuhudhuria ufunguzi rasmi wa Mkutano huu wa World Food Prize.