TANZANIA
NA MFUKO WA MAENDELEO WA ABU DHABI ZASAINI MKOPO WA MRADI WA UJENZI WA BARABARA
YA UVINZA-MALAGARASI YA MKOANI KIGOMA
Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi leo
tarehe 02 Aprili, 2018 zimesaini mkataba wa mkopo nafuu wa Dola za Kimarekani
milioni 15 kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Uvinza-Malagarasi yenye
urefu wa kilometa 51.
Hafla
fupi ya uwekaji saini wa mkataba huo imefanyika katika makao makuu ya mfuko huo
yaliyopo Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ambapo Mhandisi Mussa Ibrahim Iyombe, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa amesaini kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Mhe. Mohamed Saif Al Suwaidi Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa
Abu Dhabi amesaini kwa niaba ya Mfuko
huo.
Kusainiwa
kwa mkataba huo ni mwendelezo wa ushirikiano baina ya Tanzania na mfuko huo baada ya kukamilika kwa
awamu ya kwanza ya barabara ya Kidahwe-Uvinza (KM 77) ambayo pia ilifadhiliwa
na mfuko huo kwa mkopo nafuu wa Dola za Kimarekani milioni 57. Hivyo,
kukamilika kwa barabara ya Uvinza –Malagarasi kutaunganisha Daraja la
Malagarasi (Kikwete Bridge) ikiwa ni azma ya Serikali ya kuunganisha barabara
za Kigoma, Tabora hadi Manyoni (Singida) ambapo pia itaiunganisha nchi jirani
za Burundi na Kongo DRC.
Akizungumza
baada ya kusaini mkataba huo, Mhandisi Iyombe amesema kuwa, Serikali ya Awamu
ya Tano imedhamiria kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa kati kwa kuimarisha
miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara ambapo kusainiwa kwa mkataba huo ni
ishara mojawapo.
Mkurugenzi
Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi kwa upande wake amesema kuwa Mfuko huo
uko tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kutekeleza miradi
mbalimbali ya maendeleo nchini hususan katika kipindi hiki ambapo Serikali ya
Tanzania imeidhihirishia dunia umakini katika kutekeleza miradi mikubwa ya
maendeleo kwa kufufua nidhamu ya fedha; kupambana na rushwa pamoja na
uwajibikaji kwa manufaa ya watanzania.
Kwa
upande wake, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Umoja wa Falme za
Kiarabu Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk amesema kuwa mahusiano baina ya nchi ya
Tanzania na UAE yameendelea kukua siku hadi siku, na kwa sababu hiyo wawekezaji;
wafanyabiasha na wadau wa maendeleo wa UAE ukiwamo Mfuko wa Maendeleo wa Abu
Dhabi wamezidi kuiamini Tanzania na kuendelea kushirikiana kwa karibu.
Balozi
Mbarouk alisema kuwa, UAE ina fursa nyingi sana katika uchumi ambapo Tanzania
inaweza kunufaika nazo hususan kwenye upande wa uwekezaji, biashara na utalii. Tanzania inaweza kupata wawekezaji wakubwa kutoka UAE; kupata soko
la bidhaa zake hususan mazao ya kilimo na mifugo pamoja na kukuza utalii
kupitia familia za kifalme zinazokuja kutalii nchini lakini kwa kuvutia watalii
wanaotembelea huku hususan Dubai ili waje pia Tanzania. “Hii yote
inawezekana kutokana na mahusiano mazuri yalipo baina ya Tanzania na Umoja wa
Falme za Kiarabu yanayoendelea kukua siku hadi siku” …alisema Balozi Mbarouk.
MWISHO,
02
Aprili, 2018
ABU
DHABI, UMOJA WA FALME ZA KIARABU