Friday, March 22, 2019

Prof. Kabudi awasilisha taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya Wizara kwa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb.) akiwasilisha Taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2018/2019 na Taarifa kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2019/2020 mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) (hawapo pichani) wakati wa kikao kati ya Kamati hiyo na Wizara kilichofanyika kwenye Ofisi za Bunge, Dodoma tarehe 22 Machi, 2019. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe na kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  Balozi Ramadhan M. Mwinyi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), Mhe. Mussa Azan Zungu akimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb.) (hayupo pichani), wakati akiwasilisha taarifa kuhusu bajeti ya Wizara yake wakati wa kikao kati ya Kamati hiyo na Wizara kilichofanyika Ofisi za Bunge, Dodoma tarehe 22 Machi, 2019. Wakati wa kikao hicho, Mhe. Zungu alitumia fursa hiyo kwa niaba ya Kamati, kumpongeza Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua ya kupeleka haraka misaada ya chakula na dawa kwa nchi za Malawi, Msumbiji na Zimbabwe baada ya kupatwa na maafa  yaliyosababishwa na kimbunga kikali kilichozikumba nchi hizo.
Kikao kati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kikiendelea
Sehemu ya Wabunge ambao ni Wajumbe wa Kamati hiyo wakifuatilia kikao
Sehemu ya Wakurugenzi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakiwa kwenye kikao na Kamati ya Bunge ya NUU
Wajumbe wa Kamati wakimsikiliza Mhe. Waziri (hayupo pichani)
Wakuu wa Idara na Vitengo kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia kikao
Mjumbe wa Kamati akichangia hoja wakati wa kikao hicho
Sehemu nyingine ya Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara wakiwa kwenye kikao na Kamati ya Bunge ya NUU
Mjumbe wa Kamati akichangia jambo wakati wa kikao na Wizara
Mjumbe mwingine wa Kamati ya Bunge ya NUU akichangia hoja wakati wa kikao kati ya Kamati hiyo na Wizara
Mhe. Mbunge akichangia hoja 

Wakuu wa Vyombo vya usalama wajadili usalama wa bomba la mafuta

Juu na chini ni Mkutano wa Pamoja wa Uganda na Tanzania wa Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama (wawakilishi wao) walipokutana hivi karibuni kuzungumzia mambo muhimu ya usalama wa Bomba la Mafuta kati ya Tanzania na Uganda.

Kamati Maalum wakiwa katika picha ya Pamoja. Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali Yacoub Mohamed na Ujumbe wa Uganda uliongozwa na Mnadhimu Mkuu wa UPDF Luteni Jenerali Joseph Musanyufu.


Thursday, March 21, 2019

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar aitembelea Tanzania




Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Mhe. Mohammed Bin Abdulrahman Al-Thani, amewasili  nchini na kupokelewa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, jana tarehe 20 Machi, 2019. Mhe. Al-Thani atakuwa nchini kwa siku moja ambapo atakutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, kabla ya kuondoka kuelekea Rwanda.


Sehemu ya ugeni huo ukiwasili.
Wajumbe wa msafara huo wakisalimiana na viongozi wa serikali waliofika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, kuwapokea akiwemo Balozi wa Tanzania nchini Qatar  Mhe. Fatma Mohammed Rajab na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ayoub Mndeme.

Mmoja kati ya maafisa wa msafara huo akisalimiana na afisa wa Ubalozi wa Qatar nchini.

Wednesday, March 20, 2019

Waziri Kabudi afanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (Mb.) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Mhe. Khalifa Abdulrahman Mohamed Al-Marzooqi alipomtembelea katika ofisi ndogo za Wizara zilizopo Jijini Dar es Salaam tarehe 20 Machi 2019. Mazungumzo hayo yalijikita katika kujadili masuala mbalimbali ya namna ya kudumisha na kukuza uhusiano baina ya Tanzania na UAE.     
Waziri Mhe. Kabudi akimsikiliza Balozi wa Falme za Kiarabu nchini Mhe.Khalifa Abdulrahman Mohamed Al-Marzooqi walipokutana kwa Mazungumzo Jijini Dar es Salaam
Mazungumzo yakiendelea.
=====================================================================================
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mhe. Prof. Kabudi akutana kwa mazungumzo na Balozi wa UAE nchini

Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amekutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Khalifa Abdulrahman Al-Marzooqi, Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) nchini.

Katika mazungumzo yao yaliyofanyika tarehe 20 Machi 2019 kwenye ofisi ndogo za Wizara zilizopo Dar es Salaam, Prof. Kabudi alimshukuru Mhe. Balozi Al-Marzooqi kwa kupata fursa ya kukutana naye na kwamba, Tanzania inathamini mahusiano na ushirikiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Aidha, alimweleza Balozi huyo kuwa, Wizara chini ya uongozi wake itaendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa, mahusiano yaliyopo kati ya nchi hizi mbili yanaimarishwa.

Kwa upande wake, Mhe. Balozi Al-Marzooqi ametumia mazungumzo hayo kumpongeza Mhe. Prof. Kabudi kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kumhakikishia ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha mahusiano yaliyopo yanaimarishwa.

 Mhe. Balozi Al-Marzooqi aliongeza kuwa, Umoja wa Falme za Kiarabu una nia ya kuimarisha mahusiano yaliyopo na umepanga kufungua Ubalozi mdogo (Consulate General) Zanzibar. Pia, Mhe. Balozi alimuarifu Mhe. Waziri kwamba  ana mpango wa kuutembelea Mkoa wa Dodoma ili pamoja na masuala mengine, kujionea eneo walilopewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za ubalozi na makazi kwa lengo la kujipanga kuliendeleza.

Kadhalika, Prof. Kabudi na Mhe. Balozi Al-Marzooqi wamekubaliana kuendeleza ushirikiano kwenye maeneo ya uwekezaji ambapo Balozi huyo ameonesha nia ya kuendelea kushawishi wawekezaji kutoka nchini kwake kuja kuwekeza nchini hususan kwenye sekta za utalii, hoteli, viwanda na utoaji wa huduma. Pia ameahidi kuwashawishi wafanyabishara wakubwa na wadogo kutoka UAE kuja nchini ili kujionea fursa za biashara zilizopo.

Prof. Kabudi amemuhakikishia Balozi Al-Marzooqi kuwa, Tanzania ni eneo bora la uwekezaji na biashara na kwamba, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Wizara zingine zitaendelea kuweka mazingira mazuri ya kupokea wawekezaji na wafanyabiashara kutoka maeneo yote duniani.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
20 Machi 2019



 



TANZANIA YANGA’RA KWENYE MASHINDANO YA SPECIAL OLYMPICS, ABU DHABI, UAE.

Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, Balozi wa Tanzania UAE akiongozana na Bw. Timothy Shriver, Mwenyekiti wa Special Olympics International, wakiingia uwanja wa Sheikh Zayed Sports City kwenye ufunguzi wa Special Olympics pamoja na timu ya Tanzania walioshiriki Special Olympics Internationalyaliyofunguliwa rasmi tarehe 14 Machi 2019 na Mtukufu Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan, Mrithi wa Mtawala wa Abu Dhabi na Naibu Amri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi UAE.
Bonaventura Francis Anga ameshinda mbio za mita 3,000. na kupata medali ya dhabu, kwenye mashindano ya Special Olympics, Dubai.
Khalifani Ally Jihadi alishiriki mbio za mita 200 na ameshinda medali ya dhabu kwenye mashindano ya Special Olympics, Dubai.







Uzinduzi wa mashindano ya watu wenye ulemavu wa akili (Intellectual Disability) ulifanyika Abu Dhabi tarehe 14 Machi 2019 na Mtukufu Sheikh Mohamed , Mrithi wa Abu Dhabi na Naibu Amri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi, UAE. Mashindano hayo yataendelea mpaka tarehe 21 Machi 2019.  Nchi 183 zinashiriki kwenye Special Olympics.

Timu ya Tanzania wanashiriki, ikiwemo wanamichezo 15 na viongozi, na makocha pamoja na walenzi 13 Tanzania imewakilishwa na timu mbili, moja ya riadha ipo Dubai wenye wanamichezo 6, na timu ya mpira wa wavu ipo Abu Dhabi yenye wachezaji 9.

Timu ya Tanzania inaendelea kufanya vizuri katika riadha.  Wanamichezo wameweza kupata jumla ya medali 3 za dhabu, kwenye mbio za mita 200, 400, na 3000, medali ya fedha 1 na 2 za shaba.

Timu ya Tanzania ya mpira wavu imefuzu kucheza fainali kesho itakayofanyika kesho tareh 20 Machi 2019 baada ya kuifunga Marekani (USA) kwa seti 2 kwa sifuri.  Fainali kwsho ni kati ya Tanzania na Italia kwa ajili ya medal ya dhahabu au fedha.

Balozi Mgaza aahidi kuandaa mafunzo zaidi kwa wataalam wa afya nchini

Daktari Bingwa wa Watoto wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Evelyne Assenga akikabidhiwa cheti na Balozi wa Tanzania nchini Saudia Arabia, Hemedi Iddi Mgaza baada ya kumalizika kwa mafunzo ya kusimamia upumuaji kwa wagonjwa wanaolazwa ICU. Wengine katika picha ni wataalam wa afya kutoka Saudia Arabia. Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo leo, balozi huyo amesema wataendelea kuandaa mafunzo ya huduma za afya kwa wataalam mbalimbali nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo. Kauli hiyo imetolewa leo na balozi huyo wakati wa kufunga mafunzo ya siku mbili kuhusu upumuaji kwa wataalam kutoka hospitali mbalimbali nchini ikiwamo Bugando, Hospitali ya Mkoa wa Mbeya, Hospitali ya Benjamini Mkapa na Hospitali ya Mkoa wa Dodoma. Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru amesema kwamba Muhimbili itaendelea kutoa ushirikiano kwa wataalam wa afya kutoka Saudia Arabia ili kuhakikisha wataalam wabadilisha uzoefu na wenzao kutoka Saudia Arabia. Mafunzo hayo yameandaliwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana na Al balsam Cure and Care International Charity Organization.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto, Abdulhakiem Kattan wa Saudia Arabia akizungumza kabla ya shughuli ya utoaji vyeti kwa washiriki wa mafunzo ya kusimamia upumuaji kwa wagonjwa wa ICU.

Baadhi ya washiriki wakiwa kwenye mafunzo hayo leo.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto, Dkt. Martha Mkony akipokea cheti baada ya kumaliza mafunzo ya kusimamia upumuaji kwa wagonjwa wa ICU kutoka kwa Balozi wa Tanzania nchini Saudia Arabia, Hemedi Iddi Mgaza.
Daktari Bingwa wa Huduma za Usingizi wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya, Dkt. Amos Zakharia akifurahia baada ya kuwa miongoni mwa washiriki waliokabidhiwa cheti.
Baadhi ya wataalam walioshiriki mafunzo ya kusimamia upumuaji kwa wagonjwa wanaolazwa ICU.
Mtaalam wa wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU), Peter Bahati akikabidhiwa cheti na Balozi wa Tanzania nchini Saudia Arabia, Hemedi Iddi Mgaza.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto, Dkt. Jenifa Metodi akipongezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru baada ya kumaliza mafunzo hayo leo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru akiwa katika picha ya pamoja na wataalam wa afya kutoka Saudia Arabia na wenzao kutoka hospitali mbalimbali nchini.








Tanzania yashiriki mazoezi ya kijeshi ya pamoja nchini India

Kikosi cha wanajeshi kutoka nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Tanzania kinachoshiriki Mazoezi ya Kijeshi ya Pamoja nchini India yanayojulikana kama "Africa-India Field Training Exercise- AFINDEX-2019" kikiwa katika picha. Mazoezi hayo ambayo yanafanyika katika mji wa Pune nchini India yameanza tarehe 18 Machi 2019. Lengo kuu la mazoezi hayo pamoja na mambo mengine, yamelenga kujenga uwezo wa majeshi ya nchi zinazoshiriki kulinda amani katika vikosi vya Umoja wa Mataifa duniani ambapo India na Afrika inachangia wanajeshi wengi katika vikosi hivyo.  Mbali na Tanzania, nchi nyingine za Mataifa ya Afrika zinazoshiriki mazoezi hayo ya kijeshi ya pamoja na India ni Afrika ya Kusini, Benin, Botswana, Ghana, Kenya, Mauritius, Misri, Msumbiji, Namibia, Niger, Nigeria, Senegal, Sudani, Uganda, Zambia na Zimbabwe. 

Makamanda wa nchi zinazoshiriki mazoezi ya pamoja kati
 ya nchi za Afrika na India wakiwa katika gwaride la ufunguzi wa mazoezi hayo.
Picha ya pamoja


Tuesday, March 19, 2019

Tanzania yapeleka msaada wa chakula na madawa kwa nchi za Malawi, Msumbiji na Zimbabwe kutokana na kukumbwa na mafuriko


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,  Mhe. Ummy Mwalimu wakiwa na Balozi wa Malawi, Mhe. Glad Chembe Munthali (kushoto), Balozi wa Msumbiji, Mhe. Monica D.C. Mussa (wa pili kushoto) na Balozi Mdogo wa Zimambwe nchini, Mhe. Martin Tavenyika (wa tatu kushoto) wakati wa zoezi la kuwakabidhi  mabalozi hao  misaada ya dawa na chakula ambavyo Serikali ya Tanzania imetoa kwa nchi zao ambazo zimekumbwa na maafa yaliyosababishwa na mafuriko kufuatia tufani kali iliyolikumba eneo hilo la kusini mwa Afrika. Tukio hilo limefanyika kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam tarehe 19 Machi 2019

Mhe. Prof. Kabudi akisikiliza maelezo kutoka kwa Mhe. Waziri Ummy kuhusu aina ya dawa zilizotolewa msaada kwenye nchi za Malawi, Msumbiji na Zimbabwe kufuatia maafa yaliyosababishwa na mafuriko yaliyozikumba nchi hizo
Add caption
Sehemu ya magari yaliyobeba shehena ya msaada wa dawa na chakula kwa ajili ya waathirika wa mafuriko kwenye nchi za Malawi, Msumbiji na Zimbabwe kama inavyoonekana kabla ya kuanza kupakiwa kwenye ndege
Askari wa Jeshi la Ulinzi wakishusha kwenye magari na kupakia kwenye ndege misaada ya madawa na chakula ambavyo Serikali ya Tanzania imetoa msaada kwa nchi za Malawi, Msumbiji na Zimbabwe  ambazo zimekumbwa na maafa ya mafuriko kufuatia tufani kali iliyolikumba eneo hilo la kusini mwa Afrika
Askari hao wakiwajibika
Mhe. Prof. Kabudi akiwa ameongozana na Mhe. Waziri Ummy , Mabalozi na Viongozi mbalimbali mara baada ya kukamilisha zoezi la kuwakabidhi Mabalozi  misaada ya dawa na chakula vilivyotolewa na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya nchi zao zilizopatwa na maafa yaliyosababishwa na mafuriko kufuatia tufani kali iliyozikumba baadhi ya nchi za Kusini mwa Afrika. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe.
Picha ya pamoja


Mhe. Prof. Kabudi akiagana na Balozi wa Msumbiji nchini, Mhe. Monica mara baada ya kukabidhi misaada kwa nchi zao

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Mnyepe naye akiagana na Mhe. Balozi Monica

Brigedia Jenerali Francis Shirima  wa kikosi cha anga cha Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukabidhiwa jukumu la  kuipeleka misaada ya dawa na chakula katika nchi za Malawi, Msumbiji na Zimbabwe  ambazo zimekumbwa na maafa yaliyosababishwa na mafuriko kufuatia tufani kali iliyolikumba eneo la kusini mwa Afrika



Naibu Katibu Mkuu afungua mkutano kati ya Wabunge wa EALA na wadau kuhusu kilimo

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi akifungua mkutano wa Kamati ya Kilimo, Utalii na Maliasili ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) ambayo inakusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu namna ya kuboresha bajeti katika sekta ya Kilimo kwenye nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki mpaka kufikia asilimia 10. Mkutano huo umehudhuriwa na Wabunge wa Bunge hilo kutoka nchi wanachama. Ufunguzi wa mkutano  huo umefanyika katika Hotel ya Mt. Gasper iliyopo jijini Dodoma tarehe 19 Machi 2019.
Sehemu ya Wabunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa mkutano huo. Kutoka kushoto ni Mhe. Adam Omari Kimbisa, Mhe. Dkt. Oburu Oginga na  Mhe. Nooru Adan Mohammed 
Juu na Chini ni sehemu ya wadau mbalimbali waliohudhuria Mkutano huo.




Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Joachim Otaru naye akifuatilia ufunguzi wa mkutano huo
Balozi Mwinyi akiendelea kuzungumza katika ufunguzi wa Mkutano huo.
Wajumbe wengine wakifuatilia ufunguzi wa mkutano huo. Kushoto ni Mhe.Mhandisi Mohammed H. Mnyaa.

Mhe. Ramadhan Muombwa Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya Kilimo, Utalii na Maliasili ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na wadau kutoka sekta na taasisi mbalimbali waliohudhuria mkutano kuhusu namna ya kuboresha bajeti katika sekta ya kilimo kwenye nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.