Saturday, December 11, 2021

MAWAZIRI WA AFYA KUTOKA NCHI ZA EAC WAKUTANA MJINI ZANZIBAR

 Mkutano wa 21 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta (BLM) la Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umefanyika tarehe 10 Desemba 2021 katika Hotel Verde mjini Zanzibar.

Mkutano wa Baraza la Mawaziri ulitanguliwa na mikutano miwili ya awali iliyofanyika tarehe 6 hadi 8 Desemba 2021na tarehe 9 Desemba 2021 katika ngazi ya Wataalamu na Makatibu Wakuu mtawalia.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui (Mb) aliwakaribisha wajumbe wa mkutano huo mjini Zanzibar na kupongeza maamuzi yaliyofikiwa na sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya kwamba mkutano huo ufanyike mjini humo ili kuwapa fursa wajumbewa mkuano huo kuyafahamu maeneo ya utalii ndani ya kanda.

Vilevile alieleza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kufanyia kazi maamuzi na mapendekezo mbalimbali yanayotolewa na vikao hivyo ili yaweze kuwa na tija kwa masalahi ya wananchi  ndani ya jumuiya.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia Sekta ya Uzalishaji na Jamii, Mhe.  Christophe Bazivamo katika ufunguzi wa mkutano huo aliipongeza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mapokezi mazuri kwa wajumbe wa mkutano huo na kwa kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kupongeza jitihada mbalimbali zinazofanywa na Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kurasimisha lugha nyingine zitakazotumiwa kwenye mikutano ya jumuiya hiyo ambapo, alieleza mpaka sasa Sekretarieti ya Jumuiya hiyo inafanyia kazi taratibu za kuifanya lugha za Kiswahili na kifaransa kuwa lugha rasmi kwa ajili ya matumizi ya mikutano ya jumuiya.

Pia amepongeza juhudi zilizooneshwa na Shirika 

la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kutangaza tarehe 7 Julai kuwa siku ya Kiswahili.

“UNESCO imeonesha ni namna gani lugha ya Kiswahili ambayo ndio lugha pekee ya kiafrika yenye watumiaji wengi imeweza kuthaminiwa ulimwenguni, sisi kama jumuiya tutaendeleza jitihada za kukuza Kiswahili” alisema Mhe. Bazivamo.

Kadhalika, Mhe. Bazivamo amezisisitiza Nchi wanachama wa jumuiya hiyo kukamilisha zoezi la uandaaji wa Hati za Kusafiria za Kielekronik za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC e-Passport) ambapo, ameeleza mpaka sasa ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pekee ndio imefanikiwa kukamilisha zoezi la ugawaji wa Hati hizo za kusafiria kwa wananchi wake.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umeongozwa na Mhe. Nassor Ahmed Mazrui (Mb.) Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambaye ameambatana na Mhe. Dkt. Godwin Mollel (Mb.) Naibu Waziri, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Tanzania Bara.

Viongozi wengine walioshiriki mkutano huo ni pamoja na; Dkt. Fatma H. Mrisho, Katibu  Mkuu Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar; Dkt. Othman Mohamed Ahmed, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia - Tanzania Bara, Bw. Eliabi Chodota, Mkurugenzi Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki; na Dkt. Abdul S. Ali, Mganga Mkuu na Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia  Wazee na Watoto  wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Pamoja na Mambo mengine Mkutano wa 21 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umepokea taarifa ya utekelezaji wa maamuzi/maagizo ya mikutano iliyopita; hali ya mlipuko wa janga la UVIKO-19 Kikanda; na Utekelezaji wa program na miradi ya Afya.

Mkutano huo umehudhuriwa na nchi zote wanachama isipokuwa Jamhuri ya Rwanda na Jamhuri ya Sudan Kusini ambao walishiriki mkutano kwa njia ya mtandao.


==============================

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Godwin Mollel (Mb) akifafanua jambo wakati wa Mkutano wa 21 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika tarehe 10 Desemba 2021 katika Hotel Verde mjini Zanzibar. Pembeni yake ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui. 

Meza kuu wakiongozwa na Mwenyekiti wa mkutano huo Naibu Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Rashid Aman (wa pili kutoka kulia). Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia Sekta ya Uzalishaji na Jamii, Mhe. Christophe Bazivamo.

Mkurugenzi Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Eliabi Chodota pamoja na Mganga Mkuu na Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Abdul S. Ali  wakifuatilia mkutano.

Ujumbe wa Tanzania

Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania

Ujumbe kutoka Burundi

Ujumbe kutoka Uganda

Picha ya pamoja viongozi wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mawaziri wa Afya wa Jumuiya hiyo walioshiriki mkutano.

Mkutano ukiendelea


Thursday, December 9, 2021

MAKATIBU WAKUU WA WIZARA ZA AFYA KUTOKA NCHI ZA EAC WAKUTANA MJINI ZANZIBAR

 

Mkutano wa 21 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta (BLM) la Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika ngazi ya Makatibu Wakuu unafanyika leo tarehe 9 Desemba 2021katika Hotel Verde mjini Zanzibar.

Mkutano huu na mkutano wa ngazi ya Maafisa Waandamizi ambao ulifanyika tarehe 6 hadi 8 Desemba 2021 ni sehemu ya mikutano ya awali yenye jukukumu la kupitia na kuwasilisha agenda na mapendekezo ya masuala ya afya ya kikanda yatakayo wasilishwa katika Mkutano wa 21 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika tarehe 10 Desemba 2021.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huu unaongozwa na Dkt. Fatma H. Mrisho, Katibu  Mkuu Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. 

Viongozi wengine walioambatana naye ni pamoja na Dkt. Othman Mohamed Ahmed, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia - Tanzania Bara, Bw. Eliabi Chodota, Mkurugenzi Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, na Dkt. Abdul S. Ali, Mganga Mkuu na Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto  wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mkutano huu unafanyika mjini Zanzibar kwa lengo la kuendeleza jitihada za jumuiya katika kutangaza maeneo ya utalii ndani ya jumuiya. Vilevile kuvutia wageni na kuhamasisha utalii wa ndani kama ilivyosisitizwa katika maonesho ya Utalii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC-Tourism Expo) yaliyofanyika mapema mwezi Oktoba 2021  Jijini Arusha.

==============================

Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bi. Fatma H. Mrisho (Kulia) akifuatilia Mkutano wa 21 wa Baraza  la Mawaziri la Kisekta la Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika ngazi ya Makatibu Wakuu unaofanyika leo tarehe 9 Desemba katika Hotel Verde mjini Zanzibar. Kushoto ni Mkurugenzi Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Eliabi Chodota.

Mwenyekiti wa mkutano ngazi ya Makatibu Wakuu, kutoka Kenya, Dkt. Moses Mbaruku (kati) akiongoza mkutano huo. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia Sekta za Uzalishaji na Jamii, Mhe. Chrisophe Bazivamo na kushoto ni Mkurugenzi kutoka Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kenya, Dkt. Kuria Francis.

Ujumbe wa Tanzania 

Ujumbe wa Tanzania

Ujumbe wa Tanzania

Sehemu nyingine ya Ujumbe wa Tanzania

Ujumbe kutoka Kenya

Ujumbe kutoka Uganda

Ujumbe kutoka Burundi

RAIS SAMIA AWAONGOZA WATANZANIA SHEREHE ZA MAADHIMISHO YA MIAKA 60 YA UHURU

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewaongoza Watanzania kwenye sherehe za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Marais na viongozi wa Mataifa mbalimbali pamoja na viongozi wakuu wa Serikali.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwasalimia Watanzania kwenye sherehe za maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam  


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame katika sherehe za maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam  


Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame akisalimiana na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Mpango katika sherehe za maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam  


Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame akisalimiana na Rais Mstaafu wa Awamu ya nne Mhe. Jakaya Kikwete katika sherehe za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam    


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Hussein Ali Mwinyi akiwasili katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam kuhudhuria sherehe za maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara  


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akihutubia wananchi katika sherehe za maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam   


Baadhi ya Mawaziri na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi Pamoja na Viongozi waandamizi wa Serikali wakifuatilia maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam 


Baadhi ya Makatibu Wakuu wakifuatilia maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam 

Baadhi ya Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini wakifuatilia maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam 




Sehemu ya Mawaziri wakifuatilia maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam 





RAIS KENYATTA AWASILI NCHINI KUSHIRIKI MAADHIMISHO YA MIAKA 60 YA UHURU NA KUANZA ZIARA RASMI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akimtambulisha Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. John Simbachawene kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta wakati wa mapokezi ya Mhe. Rais Kenyatta alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimaifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam tarehe 09 Desemba 2021 kwa ajili ya kushiriki maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara pamoja na kuanza ziara rasmi ya siku mbili nchini.


Mhe. Rais Kenyatta akisalimiana na Balozi wa Kenya hapa nchini, Mhe. Dani Kazungu wakati wa hafla ya mapokezi yake
Mhe. Balozi Mulamula akiendelea na zoezi la utambulisho wa viongozi mbalimbali  wa hapa nchini  waliofika kumpokea Mhe. Rais Kenyatta 

Mhe. Rais Kenyatta akisalimiana na Bi. Felister Rugambwa, Afisa Mambo ya Nje na Mkuu wa Utawala katika Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya ambaye yupo nchini kushiriki ziara ya Rais.

Gwaride la Heshima

Mhe. Rais Kenyatta akiwa ameongozana na Mhe. Balozi Mulamula wakipita katikati ya gwaride maalum lililoandaliwa kwa  heshima yake.

Mhe. Rais Kenyatta akiwa kwenye mazungumzo na Mhe. Balozi Mulamula mara baada ya kuwasili nchini

Mazungumzo yakiendelea. Kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Mhe. Raychaelle Omamo pamoja na Balozi wa Kenya nchini, Mhe. Dani Kazungu.
























Wednesday, December 8, 2021

WAZIRI MULAMULA AKUTANA KWA MAZUNGUMZO NA VIONGOZI MBALIMBALI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula leo tarehe 08 Disemba 2021 amekutana kwa nyakati tofauti na kufanya mazungumzo na Viongozi kutoka nchi mbalimbali ambao wapo nchini kwa ajili ya kushiriki maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara yatakayofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 09 Desemba 2021.

Miongoni mwa Viongozi aliokutana nao ni pamoja na Rais Mstaafu wa Malawi, Mhe. Dkt. Joyce Banda, Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji, Mhe. Veronica Macamo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Eswatini, Mhe. Seneta Thulisile Dladla na Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Mhe. Dkt. Vicent Biruta.

Katika mazungumzo yao, Mhe. Balozi Mulamula amewakaribisha nchini  viongozi hao na kuwashukuru kwa kukubali mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan wa kuja kushiriki maadhimisho hayo pamoja na wananchi wa Tanzania. Kadhalika, viongozi hao wamekubaliana kuimarisha ushirikiano kati ya nchi zao na Tanzania kwenye maeneo mbalimbali.

Rais Mstaafu wa Malawi, Mhe. Dkt. Joyce Banda akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji, Mhe. Veronica Macamo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam  


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Eswatini, Mhe. Seneta Thulisile Dladla katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Mhe. Dkt. Vicent Biruta katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Balozi wa Rwanda nchini Tanzania Mhe. Meja Jenerali Charles Karamba.    



TANZANIA YANADI BIDHAA ZA KILIMO NCHINI MAREKANI

Na Mwandishi Wetu,

Katika kusheherekea miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara na miaka 60 ya uhusiano kati ya Tanzania na Marekani, Serikali ya Tanzania kupitia Ubalozi wake nchini Marekani imefanya Kongamano kwa njia ya Mtandao kuhusu biashara ya bidhaa za Kilimo za Tanzania.

Mkutano huo umeandaliwa kwa kushirikiana na Taasisi za Kituo cha Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Baraza la Kilimo Tanzania (ACT), Sister Cities International na Thunderbird School of Global Management. Lengo la Kongamano hilo lilikua ni kuimarisha mauzo ya bidhaa za kilimo za Tanzania nchini Marekani.

Kongamano hilo lilishirikisha wajumbe kutoka Serikali za Tanzania na Marekani, Wafanyabishara na wadau wa kilimo wa nchi hizo mbili na Taasisi za Fedha, ambapo Waziri wa Kilimo Mhe. Prof. Adolf Mkenda (Mb), ameshiriki kwenye Kongamano hilo, kadhalika, Meya wa Jiji la   Helena-West, Arkansas, Mstahiki Kevin Smith naye pia ameshiriki.

Wakati wa Kongamano hilo, fursa mbalimbali za biashara ya mazao kati ya Tanzania na Marekani zilijadiliwa. Mazao hayo ni pamoja na maparachichi, ufuta, samaki, asali, kokoa, mchele, mvinyo, pareto, na mazao ya bahari.

Akizungumza kwenye Mkutano huo, pamoja na kueleza jitihada zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha sekta ya kilimo na kuongeza mauzo ya nje, Mhe. Waziri Prof. Mkenda ameeleza pia changamoto zilizopo kwenye sekta hiyo pamoja na fursa za uwekezaji pamoja na kuwasihi wawekezaji kutoka Marekani kuwekeza katika sekta ya kilimo.

Kwa upande wake, Meya Kevin Smith ameeleza kwamba Jiji lake la Helena-West linalima mchele kwa wingi na lipo tayari kushirikiana na Tanzania katika biashara ya zao hilo.

Akizungumza kwenye Kongamano hilo, Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Dkt. Elsie Sia Kanza, ameeleza kuwa Kongamano hilo ni mwanzo wa makongamano mengine mengi ya namna hiyo, kwa sababu Ubalozi umejizatiti kuimarisha mauzo ya bidhaa mbalimbali za Tanzania nchini Marekani, hasa bidhaa za kilimo. Pamoja na mambo mengine, Balozi Kanza ameahidi Ubalozi utaendelea kushirikiana na mwekezaji au mfanyabiashara yeyote mwenye lengo la kuwekeza Tanzania.

Waziri wa Kilimo Mhe. Prof. Adolf Mkenda (Mb), akiwasilisha hotuba yake kwenye Kongamano hilo lililofanyika kwa njia ya mtandao 


Balozi wa Tanzani nchini Marekani Dkt. Elsie Kanza akiwa pamoja na wajumbe wa Ubalozi wakishiriki kwenye Kongamano hilo 


Sehemu ya Wajumbe walioshiriki katika Kongamano   


Balozi Kanza akizungumza wakati wa kongamano  


Meya Kevin Smith wa Jimbo la Helena-West Arkansas, nchini Marekani akizungumza wakati wa Kongamano



Tuesday, December 7, 2021

WAZIRI MULAMULA APOKEA HATI ZA UTAMBULISHO ZA MKURUGENZI MKAZI WA FAO

Na Mwandishi wetu, Dar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) amepokea Hati za Utambulisho za Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Dkt. Nyabenyi Tipo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Mara baada ya kupokea hati hizo Balozi Mulamula ametumia fursa hiyo kumweleza Mkurugenzi Mkazi huyo vipaumbele vya Serikali katika mpango mzima wa kuendeleza kilimo pamoja na mpango Mkakati wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa ‘Strategic Development Cooperation programme’.

Pia viongozi hao wameangalia maeneo ambayo yatapewa kipaumbele katika uwekezaji wa miundombinu, uzalishaji zaidi lakini pia kuangalia jinsi gani mazao yanayolimwa yanatunzwa vizuri.

“Tumejadili mbalimbali ikiwa ni pamoja na mpango wa FAo wa kusaidia nchi kuwa na bidhaa zinazozitambulisha nchi husika katika masoko ya kimataifa,” amesama Balozi Mulamula.

Pamoja na mambo mengine, Balozi Mulamula amemhakikishia Mkurugenzi Mkazi wa FAO kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na FAO katika kutekeleza miradi mbalimbali hasa mradi wa maendeleo wa miaka mitano.

Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Dkt. Nyabenyi Tipo amesema atahakikisha FAO inatekeleza vipaumbele vya Serikali ya Tanzania pamoja na kuongeza ushirikiano wake kwa maslahi ya pande zote mbili.

“Mara baada ya kuwasilisha Hati za Utambulisho kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, tumejadili jinsi ya kusaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi, kupunguza utapiamlo na kuona ni jinsi gani FAO inaweza kusaidia Tanzania katika kuboresha lishe kwa watanzania na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya kilimo kwa ujumla,” amesema Dkt. Tipo

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akipokea Hati za Utambulisho za Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Dkt. Nyabenyi Tipo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongea na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Dkt. Nyabenyi Tipo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Dkt. Nyabenyi Tipo akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula mara baada ya kumkabidhi Hati za Utambulisho katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Mwakilishi Msaidizi wa FAO Bwana Charles Tulahi akieleza jambo wakati wa kikao baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Dkt. Nyabenyi Tipo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Dkt. Nyabenyi Tipo wakiwa katika picha ya pamoja na badhi ya maafisa kutoka Wizarani pamoja na Ofisi za FAO