Wednesday, May 17, 2017

Maandalizi ya Mkutano wa 34 wa Dharura wa Baraza la Mawaziri la Afrika Mashariki yakamilika.


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Aziz P. Mlima akizungumza kwenye kikao cha Wataalamu ngazi ya Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika katika Hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam.
 Mkutano huu ni maandalizi ya Mkutano wa 34 wa Dharura wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki unaotarajiwa kufanyika tarehe 18 Mei, 2017 Hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam. 

Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama Bw. Stephene Mbundi akisisitiza wakati wa Mkutano wa ngazi ya Wataalam kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam



Sehemu ya wajumbe wakifuatilia mkutano

Katibu Mkuu Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Bw. Liberat Mfumukeko akifuatilia Mkutano.

Tuesday, May 16, 2017

Watumishi wa umma kuweni karibu na wananchi, Balozi Mwinyi

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhani Mwinyi akitoa mwongozo kwa wajumbe wa semina ya Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki  inayoendelea kufanyika kisiwani Pemba. Pamoja na mambo mengine amewahimiza wananchi kuchangamkia fursa zinazopatikana kwenye mtangamano.
Mbunge wa jimbo la Konga, Mhe. Mbarouk Ali akichangia jambo kwenye semina.
Sehemu ya wajumbe wakiendelea kusikiliza mada mbalimbali zilizokuwa zikiendelea kutolewa kwenye semina.
Afisa kutoka Ofisi za Uhamiaji Pemba Bw. Haji Kassim Haji akijibu hoja mbalimbali zilizokuwa zikitolewa na wajumbe kwenye semina juu ya upatikanaji wa Hati ya Kusafiria ya Afrika Mashariki.
Bw. Amedeusi Mzee akitoa mada kuhusu Soko la Pamoja na faida zinazopatikana kwenye soko hilo.
Luteni Kamanda. Hassan Hussein  wa KMKM naye akitolea ufafanuzi kwenye maswala mbalimbali yenayohusiana na maswala ya magendo.
Wajumbe wakisikiliza kwa makini mada na majibu ya hoja mbalimbali walizokuwa wakihitaji kufahamu kutoka kwa Bw. Amedeusi (hayupo pichani) na mjumbe kutoka JKU.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI



Watumishi wa umma kuweni karibu na wananchi,  Balozi Mwinyi



Taasisi za Serikali zimehimizwa ziwe karibu na wananchi ili ziweze kuwahudumia na kuwaelimisha juu ya huduma inazozitoa. Wananchi wengi wamekuwa wakilalamika mara kwa mara kuhusu watumishi wa umma kutotumia weledi na ubunifu katika kuwahudumia wananchi jambo ambalo likiachwa liendelee, Tanzania itaachwa nyuma ndani ya Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na ulimwengu mzima kwa ujumla.

         Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi katika semina kuhusu elimu ya mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na fursa zake inayotolewa na wataalamu wa Wizara yake kisiwani Pemba.    Semina hiyo  iliyoanza jana inafanyika kwenye uwanja wa Gombani, Pemba na itamalizika tarehe 18 Mei 2017.

         "Kuna fursa nyingi za kiuchumi katika Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki lakini kama wananchi wetu hatutawasaidia na kuwaelimisha kuhusu nyaraka na masharti yanayokidhi vigezo wataachwa nyuma na kubaki kuwa watazamaji na walalamikaji" Balozi Mwinyi alisema.

         Wajasiriamali walielezea masikitiko yao juu ya ugumu wa kupata hati za kusafiria kutokana na mlolongo wa masharti hususan, inapotokea kuwa safari ni ya ghafla. Aidha, wajasiriamali wamekuwa wakilalamika kuwa wanapata tabu kusajili bidhaa zao katika mamlaka zinazosimamia ubora wa viwango wa bidhaa, chakula na madawa kwa kuelezwa kwamba bidhaa zao ni duni, hivyo wameiomba Serikali iwawezeshe kupata teknolojia ya kisasa ikiwa ni pamoja na vifungashio.

         Balozi Mwinyi alisisitiza umuhimu wa taasisi zote bila kukiuka Sheria, kanuni na vigezo vilivyowekwa kurahisisha taratibu zao ili wananchi wapate nyaraka zinazotakiwa kwa urahisi ili iwe wepesi kwao kuchangamkia fursa za kiuchumi na kibiashara katika soko la pamoja la Afrika Mashariki.

         Akitoa ufafanuzi kuhusu upatikanaji wa hati za kusafiria, Afisa Uhamiaji, Bw. Haji Kassim Haji alisema kuwa taratibu zilizowekwa hazina lengo la kukwamisha shughuli ya mtu yeyote isipokuwa zimewekwa kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi. Katika ulimwengu wa leo ambao unakabiliwa na changamoto nyingi za kiusalama kama, ugaidi, uharamia, Biashara haramu ya binadamu, uhamiaji haramu, lazima masharti yazingatiwe ili kuepuka uwezekano wa kutokea uovu huo.

         Aidha, Balozi Mwinyi alishauri wajasiriamali wajiunge katika vikundi ili  masuala yao ikiwa ni pamoja na maombi ya hati za kusafiria yafanywe kwa pamoja wakidhaminiwa na taasisi zinazosimamia shughuli zao.



 -Mwisho-



Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,

Pemba, 16 Mei, 2017



Wananchi wa Pemba wahimizwa kuchangamkia fursa za EAC



Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga (Mb.), akizungumza kwenye ufunguzi wa semina ya Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kisiwani Pemba. Semina hiyo inatolewa kwa wajasiriamali wa Pemba ili waweze kuchangamkia fursa za mtangamano. Semina hiyo inafanyika katika Ukumbi wa Mikutano uliopo katika Uwanja wa mpira wa Gombani.
Sehemu ya wajumbe waliohudhuria semina hiyo, wa kwanza kushoto ni Mbunge wa Konde Mhe. Mbarouk Ali akiwa pamoja na washiriki wengine wakifuatilia kwa makini ufunguzi huo
Sehemu nyingine ya wajumbe wakimsikiliza kwa makini Waziri Mahiga hayupo pichani.
Naibu Waziri wa Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora wa Serikali ya Zanzibar Mhe. Khamis Juma Maalim akisoma hotuba ya ukaribisho.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi naye akielezea jambo kwenye ufunguzi wa semina hiyo ya Mtangamano wa Afrika Mashariki.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Sanday markert  kutoka Pemba, Bw.Khamis Suleiman Masoud akitoa neno la shukrani kwa Mhe. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (hayupo pichani).
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga akitoa ufafanuzi masuala mbali mbali kuhusiana na semina hiyo.
Ufunguzi wa Semina ukiendelea
Wakiwa katika picha ya pamoja.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Wananchi wa Pemba wahimizwa kuchangamkia fursa za kiuchumi katika Soko la EAC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga amewataka wakazi wa Pemba na Tanzania kwa ujumla  kuchangamkia ipasavyo fursa za Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ajili ya kujiongezea kipato.

Mhe. Waziri alieleza kuwa katika ulimwengu wa leo hakuna nchi duniani itakayoweza kujiimarisha kiuchumi peke yake bila kushirikiana na nchi nyingine.  Ndio maana hata zile nchi zilizoendekea kama Marekani na nchi za Ulaya wana umoja wao kwa madhumuni ya kuongeza nguvu na kasi ya maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Waziri Mahiga aliyasema hayo alipokuwa anafungua semina kuhusu elimu ya Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na fursa zake kwa wananchi wa Pemba ambayo itatolewa na wataalamu wa Wizara yake kwa siku nne kuanzia leo kwenye Uwanja wa Mpira wa Miguu wa  Gombani.

Mhe. Waziri alieleza kuwa kabla, wakati na baada ya ukoloni nchi za Afrika Mashariki zilikuwa na aina moja au nyingine ya Ushirikiano kwa madhumuni ya kuimarisha uchumi wa nchi zao, waliotutawala.  Aina moja ya Ushirikiano ni ule Umoja wa Huduma ambao ulianzishwa mwaka 1961. Umoja huo ulianzisha mashirika mbalimbali kama vile bandari, ndege, hali ya hewa, posta na reli ambayo yalikuwa yanaendeshwa kwa pamoja.

Alisema Tanzania ipo katika eneo la kimkakati ndani ya Jumuiya ikiwa ni pamoja na kuwa na eneo kubwa kuliko nchi zote, idadi kubwa ya watu, ukanda mkubwa wa bahari na ardhi nzuri yenye rutuba na kihistoria Pemba ni eneo lenye rutuba nzuri kuliko maeneo yote ya Afrika Mashariki. Hivyo, kutokana na sifa hizo hakuna budi wananchi wa Pemba na Tanzania kwa ujumla kujipanga vizuri ili kuchangamkia fursa hizo badala ya kubaki kuwa watazamaji na walalamikaji.

Waziri Mahiga aliongeza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina sifa nyingine ya pekee ya kuwa Muungano wa nchi mbili na kutoa wito kwa washiriki wa semina hiyo kutumia sifa ya umoja wao kuziendea na kuzichangamkia fursa za kiuchumi zilizopo kwenye Mtangamano.

"Nchi nyingi barani Afrika na duniani kwa ujumla zilijaribu kuungana lakini zilishindwa, kwa mfano nchi za Ghana, Mali na Guinea, nchi za Afrika zinazozungumza kifaransa, nchi za Misri na Syria, nchi za Afrika ya Kati na nchi za Pembe ya Afrika". “Ni sisi peke yetu hadi leo tumedumisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo juzi tu tuliadhimisha miaka 53 ya muungano huo”. Waziri Mahiga alisema. 

Aliendelea kuueleza kuwa ni jukumu la kila Mtanzania kudumisha Muungano huo ambapo kwa maneno yake alisema kuwa unaonewa wivu Afrika na duniani kote.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora wa Serikali ya Zanzibar, Mhe. Khamisi Juma Mwalim aliwasihi washiriki wa semina hiyo kuzingatia mafunzo yanayotolewa katika semina hiyo ili waweze kunufaika katika shughuli zao ikiwemo ujasiriamali.



-Mwisho-



Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,

Dar es Salaam, 15 Mei, 2017

Monday, May 15, 2017

Wapemba wapigwa msasa kuhusu Fursa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki

Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama, Bw. Stephen Mbundi akitoa mada kwenye semina ya mtangamano wa Jumuiya ya afrika Mashariki kisiwani Pemba ambapo alielezea namna Jumuiya hiyo ilivyoanzishwa, faida, fursa na changamoto mbalimbali zinazopatikana kwenye mtangamano wa Afrika Mashariki.
Bwa. Mbundi akiendelea kuelezea mada yake.
Bw. Othman Bakar Shehe akiuliza swali mara baada ya Bw. Mbundi (hayupo pichani) kumaliza kuwasilisha mada yake.
Bw. Mbundi akijibu swali lililoulizwa na Bw. Shehe (hayupo pichani).
Sehemu ya wajumbe na wajasiriamali wakisikiliza kwa makini majibu yaliyokuwa yakitolewa na Bw. Mbundi.

Friday, May 12, 2017

Wizara ya Mambo ya Nje yapokea magari ya msaada







Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) (katikati), akipokea funguo za Magari aina ya Toyota Land Cruiser  kutoka kwa  Balozi wa Kuwait hapa nchini, Mhe. Jasem Al-Najem. Anayeshuhudia makabidhiano hayo ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Aziz Mlima Makabidhiano hayo yalifanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam leo. Waziri Mahiga alisema kuwa msaada huo umetolewa na Serikali ya Kuwait kwa ajili ya kusaidia masuala ya usafiri katika kipindi hiki cha mpito ambapo Serikali inahamia Dodoma. 
Waziri Mahiga akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Serikali na Wizara yake kwa ujumla mara baada ya kupokea msaada huo. 
Balozi Al-Najem naye akizungumza na kuishukuru Tanzania kwa ushirikiano anaoumpata kwenye utendaji kazi wake hapa nchini. Alisema Serikali yake itaendelea kuisaidia Tanzania katika masuala mbalimbali ikiwemo huduma za kijamii.
Sehemu ya watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, wa pili kutoka kulia ni Afisa Ubalozi wa Kuwait haapa nchini.
Sehemu nyingine ya viongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kutoka kulia ni Mhasibu Mkuu, Bw. Paul Kabale; Mkurugenzi wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi (wa pili kutoka kulia), Bw. Mapesi Manyama, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afrika,  Bw. Suleiman Saleh; Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga, kutoka kushoto ni Maafisa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kutoka kushoto ni  na wa pili kutoka kushoto ni Bw. Hangi Mgaka
Waziri akiendelea kuongea huku Watumishi wa Wizara yake wakimsikiliza kwa makini.

Picha ya pamoja mara baada ya shughuli kumalizika.

Wednesday, May 10, 2017

Rais wa Afrika Kusini awasili nchini kwa Ziara ya Kiserikali


Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Jacob Zuma akiwa ameambatana na mkewe Mama Getrude SizakeleZuma wakishuka  kwenye ndege baada ya kuwasili nchini kwa ziara ya siku mbili inayotarajiwa kumalizika tarehe 11 Mei, 2017. 
Juu na chini Mhe. Rais Jacob Zuma na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Mhe.  Jacob Zuma Rais wa Afrika Kusini akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi mara baada ya kuwasili  leo tarehe 10 Mei 2017.
Mhe.  Rais Jacob Zuma akisalimiana na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Suleiman Saleh Kulia nia Mkuu wa Itifaki na Mkurugenzi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Grace Martin. 
Mhe. Rais Zuma akisalimiana na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Dar es salaam waliofika Uwanaja wa Ndege kwenye mapokezi rasmi yaliyoongozwa na Mhe. Dk. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Tanzania na Afrika kusini kuongeza maeneo ya ushirikiano ili kunyanyua uchumi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb.), akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa ngazi ya Mawaziri wa Kamisheni ya Pamoja ya Kitaifa kati ya Tanzania na Afrika Kusini, uliofanyika mapema leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam. Katika hotuba yake Mhe. Mahiga alieleza mkakati wa Serikali ya Tanzania na Afrika Kusini katika kuongeza maeneo ya ushirikiano hususan katika biashara na uwekezaji.
Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, Mhe. Maite Nkoana - Mashabane akihutubia katika mkutano huo ambao ulitanguliwa na mkutano wa siku mbili wa Makatibu wakuu. Pamoja na Mambo mengine, Mhe. Mashabane alieleza umuhimu wa kukuza uhusiano wa kihistoria uliopo baina ya mataifa hayo mawili ili kuwaletea maendeleo wananchi wa mataifa yote. Pia  alitumia fursa hiyo kutoa salamu za rambirambi kwa taifa la Tanzania kwa kupatwa na msiba ambao umepunguza nguvu kazi na wataalamu wa kizazi kijacho.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga akitoa utangulizi pamoja na kuratibu ratiba ya ufunguzi wa mkutano.
Sehemu ya Mawaziri wa Tanzania na viongozi waandamizi wa Serikali ya Tanzania na Afrika Kusini wakifuatilia Mkutano.
Sehemu nyingine ya Mawaziri na Viongozi wa Serikali ya Tanzania na Afrika kusini wakifuatilia Mkutano.
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na Afrika Kusini ambao pia walikua wenyeviti wa mkutano huo wakitoa ufafanuzi wa ratiba kwa Bi. Mindi wakati wa mkutano huo wa ngazi ya Mawaziri.
Picha ya Pamoja ya Mawaziri na Viongozi wa Serikali ya Tanzania na Afrika Kusini.

Tuesday, May 9, 2017

Balozi Fatma awasilisha Nakala za Hati za Utambulisho nchini Qatar

Mhe. Fatma Mohammed Rajab, Balozi Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Qatar akiwa katika mazungumzo na Mhe. Sultan bin Saad Al Muraikhi, Waziri wa Nchi, Mambo ya Nje wa Qatar. Mazungumzo hayo yalifanyika baada ya kuwasilisha Nakala za Hati za Utambulisho. Wawili hao walizungumza masuala mbalimbali kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na Qatar.

Balozi Mteule wa Tanzania nchini Qatar, Mhe. Fatma Mohammed Rajab akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Sultan bin Saad Al Muraikhi, Waziri wa Nchi, Mambo ya Nje wa Qatar ofisini kwa Mhe. Waziri. Mhe. Fatma Rajab anakuwa Balozi Mkazi wa kwanza kuiwakilisha Tanzania katika Taifa la Qatar. Mhe. Balozi alipowasili kwenye
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Doha alipokelewa na Idara ya Itifaki ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar. Aidha, wawakilishi wa Watanzania wanaoishi nchini humo walifika Uwanja wa Ndege kumlaki

Mhe. Balozi Fatma Mohammed Rajab, akiwa na viongozi wa Watanzania wanaishi nchini Qatar.