Thursday, August 17, 2017

Balozi wa Tanzania nchini Uturuki awasilisha Hati za Utambulisho



 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Balozi wa Tanzania nchini Uturuki awasilisha Hati za Utambulisho
Mhe. Prof. Elizabeth K. KIONDO, Balozi wa Kwanza Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uturuki Jumatano ya tarehe 16 Agosti 2017, amewasilisha Hati zake za Utambulisho pamoja na zile za Kukoma kwa Muda wa Mtangulizi wake kwa Mheshimiwa Recep Tayyip Erdoǧan, Rais wa Jamhuri ya Uturuki. Kitendo hicho kinamfanya Mhe. Kiondo kuwa Balozi wa kwanza mkaazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini humo.

Katika hafla hiyo Mhe. Balozi Kiondo alipata fursa ya kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Rais Erdoǧan kuhusu namna ya kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizo mbili katika maeneo ya uwekezaji, biashara, afya, Elimu, na mengineyo. Aidha, Mhe. Balozi Kiondo alimfahamisha Mheshimiwa Rais Erdoǧan kuwa Ubalozi  utakuwa kiungo muhimu katika kuongeza kasi ya utekelezaji wa makubaliano mbalimbali yaliyofikiwa wakati wa ziara yake nchini Tanzania mwezi Januari 2017 ambapo mikataba na makubaliano yapatayo tisa yalisainiwa.

Kufunguliwa kwa Ubalozi mpya wa Tanzania nchini Uturuki na kuanza kufanya kazi kunatoa fursa muhimu kwa wananchi wa mataifa hayo mawili kuongeza shughuli za kiuchumi hususan biashara kwa manufaa ya pande zote mbili.

Mhe. Balozi anatoa rai kwa Watanzania kujipanga vizuri na kuchangamkia fursa mbalimbali hususan za kibiashara zinazotokana na kuendelea kuimarika kwa mahusiano kati ya Tanzania na uturuki.

Mwisho-

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 17 Agosti 2017

 


Mhe. Prof. Elizabeth Kiondo, Balozi Mteule wa Tanzania nchini Uturuki akiwasilisha Hati za Utambulisho kwa Mheshimiwa Recep Tayyip Erdoǧan, Rais wa Jamhuri ya Uturuki.


Mhe. Balozi Kiondo akiagana na Mheshimiwa Rais Erdoǧan, baada ya kufanya mazungumzo kuhusu mahusiano ya Tanzania na Uturuki.
Picha ya pamoja

Monday, August 14, 2017

RAIS WA MISRI AWASILI NCHINI NA KUPOKEWA NA MWENYEJI WAKE RAIS DKT. MAGUFULI


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpokea mgeni wake Rais wa Misri Abdel Fattah Al Sisi mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA) jijini Dar es Salaam. 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na mgeni wake Rais wa Misri Abdel Fattah Al Sisi mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA) jijini Dar es Salaam. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa amesimama na mgeni wake wake Rais wa Misri Abdel Fattah Al Sisi wakati nyimbo za mataifa mawili ya Tanzania na Misri zikipigwa uwanjani hapo
 Rais wa Misri Abdel Fattah Al Sisi akikagua gwaride la Heshima mara baada ya nyimbo za Taifa kupigwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA) jijini Dar es Salaam.
Rais wa Misri Abdel Fattah Al Sisi akiangalia vikundi vya ngoma za asili mara baada ya kuwasili nchini.
 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 

Tanzania na Misri kushirikiana katika viwanda

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amesema kuwa Misri ina historia kubwa katika Nyanja mbalimbali za maendeleo yaliyofikiwa na mwanadamu katika dunia ya leo.

Kauli hiyo aliitoa jana Ikulu, Dar Es Salaam akiwa pamoja na mgeni wake, Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Mhe. Abdel Fatah Al Sisi ambaye yupo nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku mbili tarehe 14 na 15 Agosti 2017.

Rais Magufuli alisema kuwa ukizungumzia maendeleo ya uhandisi huwezi kukosa kuitaja Misri na ushahidi hadi leo upo namna ujenzi wa piramidi ulivyofanyika. Aidha, katika masuala ya dini, Rais Magufuli alisema kuwa maandiko yanabainisha kuwa Yesu Kristu alikimbilia nchi hyo alipotaka kuuwawa na Herode. 

“Kwa kuwa hata Manabii walikimbilia Misri nimeona nami shida zangu nizikimbizie huko na Mhe. Al Sisi amekubali tushirikiane ili kwa pamoja tutatue changamoto za kiuchumi zinazotukabili”. Rais Magufuli alisema.
Viongozi hao wawili wamekubaliana kushirikiana katika masuala mbalimbali ikiwemo ufugaji, kilimo, afya, elimu, utalii, ulinzi na matumizi ya maji ya mto Nile.

Kwa upande wa Ufugaji, Misri imekubali kuanzisha kiwanda kikubwa cha kusindika nyama nchini ili kukidhi mahitaji makubwa ya nyama nchini Misri na pia kutoa ajira, mapato na soko kwa wafugaji wa hapa nchini.
Aidha, Tanzania itaendelea kujifunza kutoka Misri katika sekta ya kilimo, hususan utaalamu wa umwagiliaji. “Nchi ya Misri ina eneo kubwa kidogo kuliko Tanzania lakini asilimia 95 ya eneo hilo ni jangwa ambalo huwezi kufanya shughuli za kilimo. Licha ya eneo linalotumika kwa kilimo kuwa dogo, lakini nchi hiyo inazalisha chakula cha kutosha na ziada ya kuuza nje”. Rais Magufuli alisema.

Kuhusu masuala ya afya, Misri imeahidi kuanzisha kiwanda cha kutengeneza dawa za binadamu nchini Tanzania ambapo Rais Magufuli alisema kiwanda hicho kitakapokamilika na kuanza kazi, kitaokoa fedha nyingi za Serikali zinazotumika kwa ajili kuagiza dawa nje ya nchi.
Suala la matumizi ya maji ya mto Nile, Rais Magufuli alieleza kuwa wamekubaliana na mgeni wake kuwa wataendelea kujadiliana ili kupata utaratibu mzuri wa kutumia maji hayo utakaokuwa na maslahi kwa nchi zote zinazopitiwa na mto huo.

Viongozi hao pia wamekubaliana kubadilishana uzoefu katika sekta ya utalii ambapo Misri imepiga hatua kubwa katika sekta hiyo. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, Misri inapokea watalii zaidi ya milioni 10 kila mwaka ukilinganisha na idadi ya watalii milioni 2 ambayo Tanzania inapata kwa mwaka. Hivyo, Tanzania ina mambo mengi ya kujifunza kutoka Misri ili kuongeza idadi ya watalii wa kutembelea Tanzania kwa mwaka.

Rais Nagufuli alihitimisha hotuba yake kwa kueleza kuwa Ziara ya Mhe. Al Sisi imeimarisha uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi hizi mbili ambao uliasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa zamani wa Misri, Marehemu Gamal Abdel Nasser. Alisisitiza umuhimu wa kushirikiana kibiashara kati ya nchi hizo mbili ambapo kwa takwimu zilizopo kiwango cha biashara kwa mwaka ni Dola milioni 778 na uwekezaji wa Misri nchini ni Dola milioni 887, viwango ambavyo bado ni vya chini mno.

Kwa upande wake, Rais wa Misri alipongeza hatua mbalimbali zinazochokuliwa na Rais Magufuli za kuiendeleza nchi kiuchumi pamoja na kupambana na rushwa na ufisadi. Aidha, aliahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha mtangamano ndani ya Afrika na kupata msimamo mmoja wa Bara la Afrika katika masuala mbalimbali ya kimataifa.    
Mwisho-

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 15 Agosti 2017









Waziri Mahiga akutana na Mjumbe Maalum kutoka Serikali ya Japan

Waziri wa Mambo wa Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akizungumza na Mjumbe Maalum wa Serikali ya Japan, Mhe. Ichiro Aisawa alipofika Wizarani hivi karibuni. Katika mazungumzo yao walizungumzia masuala mbalimbali yanayohusu ushirikiano kati ya nchi hizi mbili ikiwemo miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Japan.
Bw. Ichiro Aisawa nae akizungumza. Kushoto ni Balozi wa Japan nchini, Mhe. Masaharu Yoshida
Mhe. Mahiga akifafanua jambo wakati wa mazungumzo. Kulia ni Bi. Justa Nyange, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Waziri Mahiga akiagana na Bw. Ichiro Aisawa mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.



Friday, August 11, 2017

Taarifa kuhusu ziara ya Kitaifa ya Mhe. Abdel Fattah Al Sisi, Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri nchini


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 

Taarifa kuhusu ziara ya Kitaifa ya Mhe. Abdel Fattah Al Sisi, Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri nchini 

Kufuatia mwaliko wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Abdel Fattah Al Sisi, Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri atafanya Ziara ya Kitaifa nchini Tanzania wiki ijayo. Hii itakuwa ni ziara ya kwanza ya Mheshimiwa Abdel Fattah Al Sisi nchini Tanzania tangu Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli aingie madarakani. 

Lengo la ziara hii ni kuimarisha na kukuza zaidi mahusiano mazuri yaliyopo ya kidiplomasia, kiuchumi na kijamii kati ya nchi hizi mbili, ziara hii pia itatoa fursa kwa viongozi wetu kujadili masuala mbalimbali yanayohusu nchi hizi mbili, ya kikanda na kimataifa.

Mheshimiwa Rais Al Sisi atawasili nchini kupokelewa na mwenyeji wake, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, Mheshimiwa Rais Al Sisi mchana atakuwa na mazungumzo (tete-a-tete) na mwenyeji wake kabla ya kushiriki mazungumzo rasmi (official talks) na baadae jioni Mheshimiwa Rais Al Sisi atahudhuria dhifa ya kitaifa itakayoandaliwa na mwenyeji wake. 

Tanzania na Misri zina mahusiano mazuri ya kidiplomasia ya muda mrefu ambayo yamezidi kuimarika hasa katika miaka ya karibuni. Ushirikiano huu unatokana na misingi ya mahusiano na mashirikiano ya karibu sana kati ya Marehemu Baba wa Taifa na muasisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Kiongozi mashuhuri wa Misri na muasisi wa Jamhuri ya Taifa  la Kiarabu ya Misri, Marehemu Gamal Abdel Nasser. Uhusiano wa nchi hizi mbili umejengwa katika misingi ya ushirikiano na maelewano katika Nyanja za kijamii, kiuchumi, kisiasa, kiulinzi na kiusalama pamoja na medani za siasa za ushirikiano kimataifa, kutetea haki za binadamu, kuimarisha umoja na maendeleo ya Afrika, ukombozi wa Bara la Afrika na kupinga ukoloni, dhuluma na aina zote za ukandamamizaji duniani. Uhusiano huu umejengwa katika Nyanja zote za uhusiano katika sekta za huduma za kijamii na kiuchumi zikiwemo elimu, afya, kilimo, mawasiliano, usafiri, ulinzi na usalama na ushirikiano wa kimataifa.

Misri ni nchi ya pili yenye uchumi mkubwa Barani Afrika. Takwimu za mwaka 2016, zinaonesha kwamba pato la taifa (GDP) la Misri lilikuwa Dola za Kimarekani Billioni 266.213. Sekta kubwa kabisa katika uchumi wa Misri ni sekta ya huduma ( huduma za benki, mawasiliano, usafirishaji na utalii) ambayo inachangia takribani asilimia 52.5 kwenye GDP. Viwanda (manufacturing) inachangia asilimia 36.3, na kilimo asilimia 11.2.

Tanzania na Misri zinashirikiana katika ngazi za taasisi za serikali ambazo ni Taasisi ya Udhibiti wa utawala ya Misri (Administration Control Authority of Egypt) ambayo inashirikiana na Taasisi ya kupambana na kuzuia Rushwa ya Tanzania (TAKUKURU), Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Hospitali ya Rufaa ya Mnazi mmoja zimesaini makubaliano ya Ushirikiano na Hospitali ya El Shatby ya Chuo Kikuu cha Alexandria nchini Misri, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kina mashirikiano ya kubadilishana wataalamu na usimamizi wa pamoja wa Shahada za juu za uzamili na uzamivu na Chuo Kikuu cha Azhar cha Misri, Jeshi la Wananchi wa Tanzania kupitia SUMA JKT wamesaini Makubaliano ya Ushirikiano na Kampuni ya Polyserve ya Misri .

Aidha, kutokana na takwimu za kituo cha Uwekezaji (TIC) kimesajili jumla ya miradi nane kati ya mwaka 1990 hadi 2017, miradi hii ina jumla ya thamani ya Dola za Kimarekani 887.02 na kutoa ajira zipatazo 953, uwekezaji huo ni katika maeneo ya Kilimo, viwanda(mbao, mbolea, madini, dhahabu na shaba) na sekta ya Huduma.

Hivyo ziara hii ina umuhimu mkubwa sana hasa katika wakati huu ambapo msisitizo wa Serikali ni katika kujenga uchumi wa viwanda.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam
11 Agosti, 2017
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz P. Mlima akiongea na waandishi wa habari kuhusu ziara ya Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Mhe. Abdel Fattah Al Sisi itakayofanyika nchini wiki ijayo.

Balozi Mlima akiendelea na mazungumzo yake na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.


Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga akifafanua jambo kwa waandishi wa habari.(hawapo pichani)