Saturday, April 9, 2022
Friday, April 8, 2022
BALOZI MULAMULA AKUTANA NA MWAKILISHI WA HESHIMA WA TANZANIA NCHINI CZECH
Na Mwandishi wetu, Dar
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) amekutana kwa mazungumzo na Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania nchini Czech Bw. Roman Grolig katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo yao, viongozi hao wamekubaliana kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na Jamhuri ya Czech katika sekta za biashara na uwekezaji, kilimo, elimu na teknolojia.
Balozi Mulamula aliwakaribisha wawekezaji kutoka Czech kuwekeza nchini pamoja na kutia mkazo wa kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya Tanzania na Czech.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania nchini Czech, Bw. Grolig amesema ataendelea kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Czech kuja kuwekeza Tanzania kwani ni sehemu salama ya kuwekeza.
“Jamhuri ya Czech imedhamiria kuongeza ushirikiano na Tanzania na katika kutimiza azma hiyo, wafanyabiashara na wawekezaji wameonesha nia ya kuwekeza katika viwanda vya kutengeneza ndege ndogondogo Pamoja na magari makubwa hapa Tanzania,” amesema Bw. Grolig
Pia ameongeza kuwa kwa sasa Czech ipo katika mchakato wa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja hapa nchini Tanzania ili kuwawezesha wawekezaji na wafanyabiashara kusafiri kwa urahisi kuja Tanzania kutafuta fursa za uwekezaji,” amesema Bw. Grolig.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania nchini Czech Bw. Roman Grolig |
Thursday, April 7, 2022
BALOZI MULAMULA AZISIHI NCHI ZA EAC KUISHI KWA AMANI
Na Mwandishi wetu, Dar
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amezisihi nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuishi kwa amani ili kuepukana na mauaji kama ya kimbari dhidi ya Watutsi yaliyotokea nchini Rwanda 1994.
Waziri Mulamula ametoa wito huo leo jijini Dar es Salaam katika kumbukizi ya miaka 28 ya mauaji ya Kimbari.
Balozi Mulamula ameongeza kuwa Tanzania inaungana na Rwanda kukumbuka tukio hilo baya lililoacha makovu kwa rai wa Rwanda.
"Tunashukuru na tunathamini hatua zilizochukuliwa na Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame kuijenga nchi na kuponya majeraha na makovu ya mauaji yale, ni tukio baya lilitokea, tunaomba lisijirudie tena katika nchi zetu,” amesema Balozi Mulamula.
Aidha balozi Mulamula ameongeza kuwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zina mikataba inayotuongoza kuzuia mauaji na kuishi kwa amani.
Kwa upande wake Balozi wa Rwanda nchini Tanzania Mhe. Meja Jenerali Charles Karamba amesema wananchi wa Rwanda wanakumbuka tukio baya la kuuawa kwa ndugu zao lakini wanajivunia hatua zilizochukuliwa na viongozi wao na mafanikio yaliyopo leo nchini humo.
"Mauaji ya Kimbari yalituumiza sana kwa kupoteza ndugu zetu wasio na hatia lakini leo hii tunajivunia hapa tulipofika, kama taifa tumeendelea kujenga uzalendo na umoja,"amesema Balozi Karamba.
Nae Mratibu Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa (UN), nchini Tanzania, Zlatan Millisic alisema shirika hilo linatoa pole kwa kumbukizi hiyo mbaya katika historia ya Rwanda na kusema leo kumbukizi hiyo imetumika kuelimisha dunia kuwa chuki ni mbaya.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwasilisha hotuba yake katika kumbukizi ya mauaji ya Kimbari, leo Jijini Dar es Salaam |
Balozi wa Rwanda nchini Tanzania Mhe. Meja Jenerali Charles Karamba akihutubia Wanyarwanda paomja na wageni mbalimbali waliojitokeza katika kumbukizi ya miaka 28 ya mauaji ya Kimbari |
Balozi wa Comoro nchini, Mhe. Ahmed El Badaoui Mohamed Fakih akitoa hotuba yake katika kumbukizi ya miaka 28 ya mauaji ya Kimbari yaliyotokea nchini Rwanda mwaka 1994 |
Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN) Bw. Zlatan Milišić akitoa salamu za UN katika kumbukimbizi ya miaka 28 ya mauaji ya Kimbari |
Tuesday, April 5, 2022
MKUU WA MAJESHI YA ULINZI ATEMBELEA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI AFRIKA KUSINI
Mkuu
wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo amewataka Watumishi wa
Serikali wanaopata fursa ya kuiwakilisha nchi nje kuwa wazalendo na kufanya kazi
kwa bidii huku wakijua wao ni wawakilishi wa nchi kwenye maeneo waliyopangiwa.
Jenerali
Mabeyo ametoa rai hiyo hivi karibuni alipotembelea Ubalozi wa Tanzania nchini
Afrika Kusini kwa lengo la kuwasalimia Watumishi wa Ubalozi huo.
Mkuu huyo wa Majeshi amesema
kuwa, watumishi wa kada mbalimbali wanaopangiwa kufanya kazi kwenye Balozi za
Tanzania au Mashirika ya Kikanda na Kimataifa wanatakiwa kutumia fursa hiyo kuiwakilisha nchi vizuri kwa kufanya kazi kwa bidii na kuendelea kuwa wazalendo kwa nchi yao kwa maslahi mapana ya
Taifa.
“Nawapongeza kwa kuendelea
kuiwakilisha nchi yetu vizuri hapa Afrika Kusini lakini nawahimiza mchape kazi
kwa bidii na kuwa wazalendo kwa nchi yenu wakati wote”, alisisitiza Jenerali
Mabeyo.
Kuhusu hali ya nchi, Jenerali Mabeyo amewaeleza Watumishi hao kwamba, hali ya nchi na mipaka yote ni salama na kuwahimiza kuendelea kuiombea nchi na Viongozi wote akiwemo Mhe. Rais ili hali ya amani na utulivu iliyopo iendelee kuwepo.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi amemshukuru Jenerali Mabeyo kwa kutenga muda wake na kuutembelea Ubalozi huo na kuielezea hatua hiyo kuwa ni heshima kubwa kwake binafsi na Watumishi wote wa Ubalozi.
Kadhalika, alimweleza kuwa hali ya ushirikiano wa Tanzania na Afrika Kusini ni nzuri ambapo nchi hizi zinaendelea kushirikiana kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo biashara, utalii, elimu, uwekezaji na ushirikiano katika kukuza lugha ya kiswahiili.
Aliongeza kusema moja ya jukumu kubwa la Ubalozi ni kutekeleza Diplomasia ya Uchumi. Hivyo, Ubalozi unaendelea kukamilisha mpango mkakati wa kutekeleza dhana hiyo ili kuiwezesha Tanzania kunufaika na fursa mbalimbali zilizopo nchini humo zikiwemo za biashara, uwekezaji na masoko kwa bidhaa za Tanzania.
Mhe. Jenerali Mabeyo alikuwa nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ambao ulihusisha pia Jamhuri ya Msumbiji na Nchi Zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC iliyopo Msumbiji (SAMIM) ambao ulifanyika jijini Pretoria kuanzia tarehe 01 hadi 03 Aprili 2022.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo akisaini Kitabu cha Wageni mara baada ya kuwasili kwenye Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini. |
Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi akizungumza kumkaribisha Jenerali Mabeyo (hayupo pichani) Ubalozini. |
Mhe. Jenerali Mabeyo akizungumza |
Mkutano kati ya Jenerali Mabeyo na Watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini ukiendelea |
Sehemu ya Watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini wakimsikiliza Jenerali Mabeyo (hayupo pichani) alipowatembelea Ubalozini hapo |
Sehemu nyingine ya Watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini |
Mhe. Balozi Milanzi akimkabidhi Jenerali Mabeyo zawadi ya saa kama ukumbusho kwa kutembelea Ubalozini hapo |
Mhe. Jenerali Mabeyo akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Balozi Milanzi |
Mhe. Jenerali Mabeyo akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Balozi Milanzi na Mhe. Balozi Kayola |
Mhe. Jenerali Mabeyo akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini |
Monday, April 4, 2022
WAZIRI MULAMULA AFANYA MAZUNGUMZO NA WABUNGE WA EALA
Mazungumzo yakiendelea |
WAZIRI VICKY FORD AZINDUA MPANGO WA ‘SHULE BORA’ KIBAHA
Na Mwandishi wetu, Dar
Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford amezindua mpango wa elimu unaojulikana kama ‘Shule Bora’ Kibaha mkoani Pwani.
Mhe. Ford amesema mpango wa ‘Shule Bora’ utasaidia kuboresha elimu nchini Tanzania na utawasaidia zaidi ya watoto milioni nne, ambapo nusu yao watakuwa ni watoto wa kike.
“Elimu ni kipaumbele kwa Rais Samia pamoja na Waziri wa Mkuu wa Serikali ya Uingereza……….ni lengo la Serikali ya Uingereza kuisaidia watoto zaidi ya milioni 15 hapa Tanzania kupata elimu, lakini tumeanza na hawa wachache lakini pia tumezingatia usawa wa kijinsia ambapo nusu ya sehemu ya msaada huu utamnufaisha mtoto wa kike,” amesema Mhe. Ford.
Nae Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa msaada wa pound milioni 180 zilizotolewa na Serikali ya Uingereza utasaidi sana kuboresha sekta ya elimu nchini kupitia mpango wa elimu wa 'Shule Bora'.
Prof. Mkenda amesema pamoja na mambo mengine, kuwa msaada wa Serikali ya Uingereza kupitia mpango huu wa elimu utasaidia sana kuboresha mazingira ya elimu nchini ikiwa ni pamoja nan miundombinu ya shule, vitabu na sheria pamoja na mitaala inayotumika kufundishia.
“………….‘Shule Bora’ itaiwezesha Serikali yetu kufanya mapitio ya Sera ya elimu ya 1978, kuboresha Sheria ya Elimu, kuboresha mitaala ya elimu, kuangalia idadi ya walimu pamoja na wakufunzi na wahadhiri,” amesema Prof. Mkenda
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Rais – Tamisemi, Mhe. David Silinde amemhakikishia Waziri Ford kuwa fedha zote za mpango wa elimu wa ‘Shule Bora’ zitatumika kama ilivyokusudiwa ili kuwawezesha watoto wa kitanzania kunufaika na elimu.
Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akiongea na wageni (hawapo pichani) baada ya uzinduzi wa mpango wa 'Shule Bora' |
MKUTANO MAALUM WA 47 WA BARAZA LA MAWAZIRI LA EAC NGAZI YA WATAALAM UMEFUNGULIWA JIJINI ARUSHA
Mkutano Maalum wa 47 wa Baraza
la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki unafanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 4 hadi 6
Aprili 2022.
Mkutano huu unafanyika katika mpangilio ufuatao; tarehe 4 Aprili 2022 Mkutano Ngazi ya Wataalam, tarehe 5
Aprili 2022 Mkutano Ngazi ya Makatibu Wakuu na tarehe 6 Aprili 2022 Mkutano
Ngazi ya Mawaziri.
Pamoja na mambo mengine Mkutano Ngazi ya Wataalamu unaandaa taarifa ya masuala ya Fedha na Utawala itakayowasilishwa kwenye mkutano wa Makatibu Wakuu na baadae kwenye mkutano wa Mawaziri.
Mkutano ukiendelea, kulia ni ujumbe wa Tanzania ukifuatilia majadiliano katika mkutano huo. |
Meza kuu ikiongoza Mkutano. |
Mkurugenzi Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Caroline Chipeta akifatilia majadiliano katika mkutano. |
Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania |
Ujumbe kutoka taasisi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ukifuatilia majadiliano. |