Wednesday, June 8, 2022

BALOZI SOKOINE AMWAKILISHA BALOZI MULAMULA KATIKA MKUTANO WA 114 WA BARAZA LA MAWAZIRI WA OACPS


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine akiongoza Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya OACPS unaofanyika jijini Brussels, Ubelgiji akimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na Rais wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) Mhe. Sylvie Baïpo Temon (katikati) akizungumza wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo jijini Brussels nchini Ubelgiji. 


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine akiwa katika Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya OACPS unaofanyika  jijini Brussels, Ubelgiji akimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na UShirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mulamula.Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Mhe. Jestas Nyamanga na kulia ni Bi Agness Kiama akimwakilisha Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Marekani Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.


Baadhi ya washiriki  kutoka nchi wanachama Jumuiya ya OACPS wakifuatilia ufunguzi wa mkutano Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa jumuiya hio unaofanyika jijini Brussels nchini Belgium

Baadhi ya washiriki  kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya OACPS wakifuatilia ufunguzi wa mkutano huo unaofanyika jijini Brussels nchini Belgium


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine amwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula katika mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya nchi za Afrika, Caribbean na Pasifiki (OACPS) unaofanyika jijini Brussels, Ubelgiji.

Mkutano huo wa siku mbili unajadili masuala mbalimbali ukiwemo mustakakabali wa maendeleo ya Jumuiya hiyo na namna nchi wanachama zinavyoweza kuendelea kukuza ushirikiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo na Umoja wa Ulaya, ambaye ni mbia wa maendeleo wa muda mrefu.

Mkutano huo pia unajadili maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya hiyo unaotarajiwa kufanyika mwezi Desemba, 2022 nchini Angola.

Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Sokoine amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya OACPS katika kuhakikisha vipaumbele vya nchi vinatekelezwa hususan katika sekta za kilimo, viwanda na biashara, uvuvi na madini ili nchi iweze kunufaika.

Mkutano huo unakutanisha nchi wanachama 79 wa Jumuiya hiyo ambao kwa mara ya kwanza baada ya miaka miwili wajumbe wake wanakutana ana kwa ana tangu dunia ilipokumbwa na janga la  UVIKO 19, wajumbe wengine  walioshindwa kuhudhuria wanashiriki kwa njia ya mtandao.

Baraza la Mawaziri la nchi wanachama wa OACPS ni chombo cha maamuzi cha Jumuiya hiyo ambacho kinahusika na utekelezaji wa maazimio yanayopitishwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali.

Baraza hilo linaundwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka kwa Nchi wanachama na hukutana mara mbili kwa mwaka kujadili utekelezaji wa maazimio  yaliyofikiwa kwenye mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya hiyo.

WAZIRI MULAMULA ATOA WITO KWA JUMUIYA ZA KIKANDA KUSHIRIKIANA KATIKA KUTEKELEZA MAKUBALIANO YA AfCFTA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula ametoa wito kwa Jumuiya za kiuchumi za Kikanda za Afrika kushirikiana katika utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kwenye Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).

Waziri Mulamula amebainisha hayo alipokuwa akifungua Mkutano wa Pili (2) wa Uratibu wa Watendaji Wakuu wa Jumuiya za Kiuchumi za Kikanda (RECs) kuhusu utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika uliofanyika tarehe 7 Juni 2022 jijini Arusha.

Mkutano huo uliohudhuriwa na Wakuu wa Jumuiya za Kuichumi za Kikanda ulilenga kuwakutanisha Wakuu hao na Sekretariati ya AfCFTA ili kwa pamoja waweze kujadili na kuweka mikakati endelevu ya utekelezaji wa makubaliano ya AfCFTA. Mikakati hiyo ni pamoja na kubuni namna ya kupata rasilimali zitakazoiwezesha Sekretariati ya AfCFTA kuendesha shughuli zake bila kutegemea ufadhili wa nchi za nje, na kuandaa mfumo wa pamoja wa ushirikiano utakaoziwezesha pande zote mbili kutekeleza makubaliano ya AfCFTA kwa ufanisi.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano huo Waziri Mulamula alieleza kuwa uchumi wa Afrika utaendelea kukua kwa kasi zaidi endapo nchi za Afrika zifanikiwa kuunganisha shughuli za kiuchumi ikiwemo kuendesha biashara baina yetu wenyewe. Waziri Mulamula aliongeza kusema, anamatarajio makubwa kuwa ndoto za waasisi wa Umoja wa Afrika za kuwa na Afrika yenye umoja na iliyounganishwa kiuchumi zinaenda kutimia siku za usoni.

“Nina imani kubwa kuwa uwepo wa mikutano ya mfumo huu unaounganisha Sekretariati ya Eneo Huru la Afrika na Watendaji wa Jumuiya za Uchumi za Kikanda, utawezesha kupatikana kwa mapendekezo ya sera zinazotekelezeka na kujenga ushirikiano thabibiti ambao utawezesha kutatua changamoto mbalimbali zinazokwamisha ustawi wa biashara miongoni mwa nchi za Afrika, na hatimaye kufikia ndoto za waasisi wetu za kuwa na Afrika iliyounganishwa kiuchumi”. Alisema Balozi Mulamula

Vilevile Waziri Mulamula alieleza kuwa pamoja na jitihada za kuendelea kushirikiana katika kutekeleza makubaliano ya AfCFTA ni muhimu pia kwa Jumiya za Kiuchumi za Kikanda na Serikali za Afrika kuendelea kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji inayounganisha bara la Afrika ambayo itasadia kwa kiasi kikubwa kuokoa gharama na muda wa usafirishaji wa bidhaa na huduma miongoni mwa Nchi za Afrika.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya AfCFTA, Mhe. Wamkele Mene alisema kuwa utekelezaji wa Mkataba wa AfCFTA ni wa lazima kwa maendeleo ya Afrika hivyo ni muhimu pia kwa sekta binafsi kupewa kipaumbele kwenye utekelezaji wa makubaliano ya AfCFTA.

Mhe. Wamkele aliendelea kusisitiza kuwa ni muhimu kwa nchi za Afrika kuendelea kuhimiza katika ukuzaji wa viwanda na kuwekeza katika kuboresha bidhaa zake, ili kumudu ushindani wa soko la kimataifa na hatimaye kuweza kunufaika na soko kubwa katika biashara ya kimataifa na kuongeza mchango wake katika pato la Dunia.

“Inasikitisha kuona kwamba nchi 55 za Afrika kwa sasa zinachangia asilimia 2 tu ya pato la biashara ya duniani na asilimia 3 ya Pato la Dunia huku Singapore, jiji lenye ukubwa wa maili 600 za mraba pekee, likichangia asilimia 6.2 ya biashara ya kimataifa”. Alisema Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya AfCFTA Mhe. Wamkele.

Aidha, Mhe. Wamkele alisisitiza umuhimu wa ushirikiano thabiti na utendaji wa karibu kati ya RECs na Sekretarieti ya AfCFTA ili kuhakikisha kuwa matokeo ya AfCFTA yanawiana na maendeleo ya kikanda katika ushirikiano na ukuajia wa biashara.

Mkutano huu umefanyika ikiwa ni utelekezaji wa agizo la Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali ambalo uliielekeza Sekretariati ya AfCFTA, Tume ya Umoja wa Afrika na RECs kukaa pamoja na kuandaa mfumo wa ushirikiano sambamba na kuoanisha programu na shughuli zao ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa makubaliano ya AfCFTA
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akifungua Mkutano wa Pili (2) wa Uratibu wa Watendaji Wakuu wa Jumuiya za Kiuchumi za Kikanda (RECs) kuhusu utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika uliofanyika jijini Arusha.
Sehemu ya Meza Kuu wakifuatilia Mkutano uliokuwa ukiendelea
Mkurugenzi wa Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Bernard Haule, akifuatilia Mkutano wa Pili (2) wa Uratibu wa Watendaji Wakuu wa Jumuiya za Kiuchumi za Kikanda kuhusu utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika uliokuwa ukiendelea jijini Arusha
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Pili (2) wa Uratibu RECs kuhusu utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika uliofanyika jijini Arusha.

Katibu Mkuu wa Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Peter Mathuki akizungumza kwenye Mkutano wa Pili (2) wa uratibu wa RECs kuhusu utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika uliofanyika jijini Arusha.
Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya AfCFTA Mhe. Wamkele Mene akisisitiza jambo kwenye mkutano wa Mkutano wa Pili (2) wa Uratibu wa RECs kuhusu utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika uliofanyika jijini Arusha.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula, Watendaji wa RECs na Viongozi Waandamizi kutoka Serikalini na Sekta binafsi wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mkutano wa Pili (2) wa Uratibu wa RECs kuhusu utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika uliofanyika jijini Arusha kufikia tamati.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwasili katika ukumbi wa mikutano wa Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Alioambatana nao mstari wa mbele ni Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya AfCFTA Mhe. Wamkele Mene (wa kwanza kulia), Katibu Mkuu wa Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Peter Mathuki (wapili kulia), Rais wa Baraza la Biashara la Afrika Dkt. Amany Asfour (wa pili kushoto) na Naibu Katibu Mkuu wa Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki anayesimamia Sekta za Uzalishaji na Huduma za Jamii Mhe. Chritophe Bazivamo