Friday, April 19, 2024

MHE. RAIS SAMIA AWAKARIBISHA WAFANYABIASHARA WA UTURUKI KUSHIRIKI MAONESHO YA SABASABA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa mwaliko rasmi kwa Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wawekezaji wa Uturuki kushiriki Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba yanayotarajiwa kufanyika nchini mwishoni mwa mwezi Juni 2024.

 

Mhe. Rais Dkt. Samia ametoa mwaliko huo wakati akifungua rasmi Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki lililofanyika leo tarehe 19 Aprili 2024 jijini Istanbul na kuhudhuriwa na zaidi ya wafanyabiashara  na wakezaji 150 kutoka nchi hizi mbili.

 

Amesema maonesho hayo ya biashara ambayo ni makubwa Afrika Mashariki hutoa fursa ya kuwakutanisha wafanyabiashara na kuwawezesha kubadilishana taarifa na uzoefu, kujua taarifa mpya za masoko na bidhaa pamoja na  kuuza bidhaa zao.

 

Kadhalika Mhe. Rais Samia ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Uturuki kuja kuwekeza nchini na kuitaja Tanzania kama nchi yenye fursa lukuki kama vile ardhi yenye rutuba kwa ajili ya kilimo, Hifadhi za wanyama kwa ajili ya utalii, nishati, madini ikiwemo Tanzanite ambayo hupatikana nchini Tanzania pekee na fursa za biashara na uwekezaji.

 

 Amesema Serikali yake imeendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji  ambapo pamoja na mambo mengine imewekeza katika kujenga miundombinu inayoiunganisha Tanzania na nchi nyingine jirani ikiwemo Reli ya Kisasa ya SGR.

 

Vilevile, Mhe. Rais Samia alitumia fursa hiyo kuzipongeza Wizara za Mambo ya Nje za nchi hizi mbili kwa kuandaa kwa mafanikio Kongamano hilo ambalo ni jukwaa muhimu katika kukuza ushirikiano kwenye sekta ya biashara na uwekezaji.

 

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Uturuki, Mhe. Cevdet Yilmaz ambaye alishiriki Kongamano hilo, amesema nchi yake itaendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania katika sekta ambazo nchi hiyo imepiga hatua ikiwemo Utalii, Usafirishaji, Biashara na Uwekezaji.

 

Awali akizungumza kwenye Kongamano hilo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesisitiza umuhimu wa nchi hizi mbili kushirikiana na Sekta Binafsi katika kufikia malengo ya kukuza uchumi kwa manufaa ya wananchi wa mataifa haya.

 

Kadhalika ametoa rai kwa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Tanzania kuunga mkono juhudu nyingi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na mataifa mbalimbali ikiwemo Uturuki ili kutengeneza mazingira wezeshi ya ufanyaji biashara za kuvuka mipaka kwa Watanzania.

 

Mhe. Rais Samia yupo nchini Uturuki kwa ziara ya kitaifa kufuatia mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Mhe. Recep Tayyip Erdogan.

Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akifungua rasmi Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki lililofanyika jijini Istanbul, Uturuki tarehe 19 Aprili 2024. Pamoja na mambo mengine Mhe. rais Samia alitumia nafasi hiyo kuwaalika wafanyabiashara kutoka Uturuki kushiriki Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Juni 2024

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji akizunumza wakati wa Kongamano la Baishara kati ya Tanzania na Uturuki

Mhe. Rais Dkt. Samia akiwa na Makamu wa Rais wa Uturuki, Mhe. Cevdet Yilmaz pamoja na viongozi wengine akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba wakati wa Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uturuki
Makamu wa Rais wa Uturuki, Mhe. Cevdet Yilmaz akizungumza wakati wa Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uturuki

Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki likiendelea
Mhe. Rais Samia na Makamu wa Rais wa Uturuki, Mhe. Yilmaz na viongozi wengine wakiwa wamesimama kwa ajili ya heshima ya nyimbo za mataifa haya mawili zikipigwa wakati wa ufunguzi rasmi wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki lililofanyika Jijini Istanbul tarehe 19 Aprili 2024


Mkurugenzi wa Biashara za Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki Balozi John Ulanga (mwenye tai y abuluu) akiwa na wageni waalikwa na wafanyabiashara kutoka Tanzania kwenye Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uturuki.

Mkurugenzi wa Sheria atika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Dkt. Gift Kweka akiwa na Afisa Mambo ya Nje, Bi. Mariam Killo wakishiriki Kongamano la Baiashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki

Kongamano likiendelea

Sehemu ya Wafanyabiasha na wawekezaji wa Uturuki wakishiriki Kongamano

Mhe. Waziri Makamba akibadilishana mawazo na mmoja wa wageni waalikwa walioshiriki Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki

Kongamano likiendelea

Sehemu ya washiriki wa Kongamano

Mhe. Rais Samia na Viongozi wengine wakishiriki sehemu ya utaratibu wa ufunguzi wa Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uturuki



 

Thursday, April 18, 2024

WIZARA YA MAMBO YA NJE YAJIVUNIA KUIMARIKA KWA DIPLOMASIA, MIAKA 60 YA MUUNGANO


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) ametaja mafanikio ya Wizara katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano wa Tanzania.

Mhe. Balozi Mbarouk ametaja mafanikio hayo jijini Dodoma Aprili 18, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari kuelezea mafanikio ya Wizara katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano wa Tanzania. 

Balozi Mbarouk amesema Wizara inajivunia kuendelea kuimarika kwa ushirikiano na uhusiano kati ya Tanzania na nchi mbalimbali duniani na hivyo kupata mafanikio katika sekta mbalimbali kupitia ushirikiano wa uwili na ujirani mwema baina yake na mataifa mengine, 

“Mafanikio haya yamepatikana kupitia ushirikiano uliopo ambao unatekelezwa kupitia taratibu maalum ikiwemo mikutano ya Tume za Ushirikiano wa Pamoja. Ushirikiano huu umeleta mafanikio kupitia kusainiwa Mikataba na Hati za Makubaliano (MoUs) ili kutekeleza maeneo mahsusi katika sekta mbalimbali za siasa, kiuchumi na kijamii,” alisema. 

Amesema kupitia mikutano hiyo Tanzania imenufaika na kuongezeka kwa biashara na uwekezaji ambapo bidhaa za kilimo, mifugo, matunda na mbogamboga zimepata masoko katika nchi mbalimbali. 

Amesema Tanzania imenufaika na fursa za mafunzo ya muda mrefu na mfupi yanayofadhiliwa na nchi mbalimbali ikiwemo Uingereza, Uturuki, Marekani, Misri, India, Indonesia, China, Hungary, Japan, New Zealand, Australia, Urusi, Ujerumani, Cuba, Korea, Yugoslavia, Uholanzi, Ubelgiji, Algeria, Sudan, Saudi Arabia, Thailand na Pakistan. 

Amesema Tanzania imefanikiwa kuwa sehemu ya kuanzishwa kwa jumuiya za kikanda kama Umoja wa Afrika; Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Nchi zilizo katika Maziwa Makuu (ICGLR) na kupitia uanachama katika jumuiya hizo Tanzania imetekeleza programu katika sekta mtangamano za siasa, ulinzi na Usalama; Miundombinu; Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji. 

“Tanzania imekuwa sehemu ya utekelezaji wa dhana ya kutatua changamoto za kidunia kwa pamoja yaani Multilateralism, kuwa mbia anayeaminika na kukubalika katika maamuzi mbalimbali duniani hasa katika mashirika ya kimataifa hususan Umoja wa Mataifa na kuwa mbia kwenye vyombo mbalimbali ikiwemo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa; Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa; Benki ya Dunia na Shirika la Biashara Duniani (WTO),” alisema. 

Ameongeza kuwa Tanzania imekuwa sehemu ya maamuzi katika maeneo ya mazingira na mabadiliko ya tabia nchi; ulinzi na usalama; utatuzi wa migogoro; maendeleo endelevu na utafutaji rasilimali kwa ajili ya maendeleo ambapo kupitia jukwaa hilo imepata fursa ya kutoa misimamo yake kwa masuala muhimu ikiwemo mgogoro wa Isarel na Palestina na suala la Sahara Magharibi na kuwa sehemu ya kuunga mkono Sera ya Kutofungamana na Upande wowote (NAM) na kuunga mkono ajenda ya msimamo wa Kundi la 77 na China katika majukwaa ya Kimataifa kwa maslahi mapana ya Taifa. 

Amesema Tanzania inajivunia mchango wake katika juhudi za kulinda Amani Duniani na hivyo kutekeleza malengo ya Sera Mpya ya Mambo ya Nje na moja ya malengo mahsusi ya Umoja wa mataifa. 

Amesema pia Tanzania imekuwa ikishiriki kulinda Amani kupitia Misheni za Kikanda ikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC); Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa na baadhi ya maeneo ambayo Tanzania imechangia walinda amani ni pamoja na Lebanon; Darfur; Abyei; Liberia; Sudan Kusini; Sudan; DRC; Msumbiji na Afrika ya Kati na kuongeza kuwa Tanzania imeshiriki kikamilifu katika utatuzi wa migogoro kwa njia ya mazungumzo na diplomasia kwenye nchi na maeneo mbalimbali ikiwemo, Darfur; Cambodia; Sudan Kusini; Burundi na Kenya. 

Amesema Tanzania kuwa mwenyeji wa Taasisi za Kimataifa kama ishara ya kuaminika na kukubalika na nchi nyingine. Tanzania imeendelea kufungua Balozi na Ofisi za Uwakilishi katika nchi mbalimbali za kimkakati ikiwa ni sehemu ya kuimarisha utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje hususan Diplomasia ya Uchumi. 

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imefungua Balozi mpya mbili za Vienna, Austria na Jakata, Indonesia na Konseli Kuu mbili za Lugumbashi na Guangzhou, China ambapo ufunguzi wa Balozi hizo unaifanya Tanzania kuwa na Balozi na Ofisi za Uwakilishi 45 na Konseli Kuu TANO huku ikiwa ni mwenyeji wa nchi na mashirika ya kimataifa zaidi ya 90 zikiwemo Konseli Kuu ambazo baadhi yake zipo Zanzibar kama vile China, Oman, India na Umoja wa Falme za Kiarabu. 

Amesema Tanzania imefanikiwa kutoa viongozi mahiri kuongoza taasisi za kikanda na kimataifa ikiwa ni ishara ya kuaminiwa na mataifa mengine na kutaja baadhi ya nafasi hizo kuwa ni uteuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano wa Kilele wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia Barani Afrika utakaofanyika Paris, Ufaransa mwezi Mei 2024. 

Amesema Tanzania pia ilitoa Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambapo Dkt. Salim Ahmed Salim aliongoza Vikao Vinne vya Baraza hilo mwaka 1979 na 1980 na Dkt. Salim Ahmed Salim alihudumu kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Afrika (OAU). Watanzania wengine ni Dkt. Asha-Rose Migiro kuwa Naibu Katibu Mkuu wa kwanza kutoka Afrika; Balozi Getrude Mongela kuwa Rais wa Bunge la Afrika; Dkt. Stergomena Tax kuwa katibu Mtendaji wa SADC; Balozi Juma Mwapachu katibu Mkuu wa EAC; Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb.), Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR); Profesa Anna Tibaijuka kuwa Naibu Katibu Mkuu na Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-HABITAT) na Mkuu wa Ofisi za Umoja wa Mataifa Nairobi (UNON), Bi. Joyce Msuya, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb.) kuchaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU). Dkt. Tulia ni mwanamke wa kwanza kutoka barani Afrika kushika wadhifa huo. 

Amesema Tanzania imechangia katika juhudi za kubidhaisha Kiswahili ndani na nje ya nchi na kutoa ushawishi wa matumizi yake kama nyenzo ya diplomasia, usuluhishi wa migogoro; ukombozi na uhuru katika nchi za bara la Afrika. 

Amesema Viongozi wa Tanzania katika awamu zote na sasa wakiongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango; Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi; Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) wamekuwa wakifanya ziara za kimkakati katika nchi mbalimbali kwa lengo la kukuza na kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na nchi hizo. 

Amesema Wakuu wa Nchi waliotembelea Tanzania katika miaka ya hivi karibun ni pamoja na: Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni; Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame; Rais wa Burundi, Mhe. Everiste Ndayishimiye; Rais wa DRC, Mhe. Felix Tshisekedi; Rais wa Msumbiji, Mhe. Fillipe Nyusi; Rais wa Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema; Rais wa Malawi, Mhe. Lazarous Chakwera; Rais wa Poland, Mhe. Andrzej Duda; Rais wa Ujerumani, Mhe. Frank-Walter Steinmeier; Rais wa Romania, Mhe. Klaus Werner Iohannis; Rais wa Hungary, Mhe. Katalin Novak; Rais wa Indonesia, Mhe. Joko Widodo; Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris; Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Valdes Mesa; Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Abiy Ahmed na Naibu Waziri Mkuu wa China Mhe. Liu Guozhong na Rais wa Kenya, Mhe. William Ruto. 

Amesena Serikali imeimarisha ushiriki wa Watanzania waishio Nje ya Nchi na Raia wa Nchi nyingine Wenye Asili ya Tanzania katika maendeleo ya Taifa na kuchukua hatua za Kisera kwa kujumuisha masuala ya Diaspora katika mapitio ya Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 na imekamilisha mfumo wa kiditali wa kukusanya na kutunza taarifa za Diaspora ambapo mpaka sasa Diaspora wa Tanzania wapatao 1403 wamejiandikisha katika mfumo huo na hivyo kuiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi za idadi ya Diaspora, mahali walipo, ujuzi na uzoefu walionao huku mfumo pia ukiwawezesha Diaspora kupata taarifa kuhusu fursa na huduma mbalimbali zinazotolewa na Serikali na sekta binafsi nchini. 

Amesema Serikali iko katika hatua za kukamilisha kutoa Hadhi Maalum (Special Status) kwa Raia wa Nchi Nyingine Wenye Asili ya Tanzania ili kuwezesha kuchangia ipasavyo katika maendeleo ya Taifa.


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) akiongea na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Miaka 60 Muungano wa Tanzania katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma.
Waandishi wa Habari wakimsikiliza Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) alipokuwa akiongea nao kuhusu mafanikio ya Miaka 60 Muungano wa Tanzania katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) akisisitiza jambo wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Miaka 60 Muungano wa Tanzania katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma.
Waandishi wa Habari wakimsikiliza Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) hayupo pichani alipokuwa akiongea nao kuhusu mafanikio ya Miaka 60 Muungano wa Tanzania katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma.

MHE. RAIS SAMIA ATUNUKIWA SHAHADA YA HESHIMA YA UDAKTARI NCHINI UTURUKI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu ametunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari (Honoris Causa) katika Uchumi na Chuo Kikuu cha Ankara cha nchini Uturuki ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake katika kuboresha maisha ya watanzania kupitia mageuzi mbalimbali pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na nchi mbaimbali duniani ikiwemo Uturuki.


Akizungumza kupokea tuzo hiyo kwenye hafla iliyofanyika katika Chuo hicho jijini Ankara leo tarehe 18 Aprili 2024, Mhe. Rais Samia amelishukuru Baraza la Chuo kwa kumpatia heshima hiyo kubwa kwake na kwa Watanzania wake kwa waume na  kukipongeza Chuo hicho kwa kuendelea kutoa elimu yenye ubora na kuiweka Uturuki kuwa miongoni mwa nchi zinazotoa elimu ya juu bora duniani.

 

“Nilipopokea taarifa kuhusu kutunukiwa shahada hii nilijiuliza, wametumia vigezo gani hadi kufikia uamuzi huu, Waziri wangu wa Mambo ya Nje alinipatia orodha yenye vigezo hivyo nikakubali, nawashukuru sana” alisema Rais Dkt. Samia

 

Mhe. Rais Samia amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Uturuki katika kufikia malengo yake ya kukuza  uchumi kupitia ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, kilimo, uwekezaji na ushirikiano baina ya watu wa nchi hizi mbili.

 

Baraza la Chuo Kikuu cha Ankara kwa kauli moja liliamua kumtunukia Mhe. Rais Dkt. Samia Shahada hiyo ya heshima, kwa kutambua Uongozi wake wa kipekee ambao umeleta mageuzi makubwa ya kijamii, kisiasa, na kiuchumi nchini Tanzania. Mageuzi  hayo yameboresha ustawi wa Watanzania; na kuimarisha sifa ya Tanzania ulimwenguni; na yamekuza mahusiano ya kibiashara, kiuchumi na kisiasa kati ya Tanzania na nchi nyingine, ikiwemo Uturuki.


Hafla ya kukabidhiwa tuzo hiyo imeongozwa na Prof. Necdet Ãœnüvar, Mkuu wa Chuo, na kushuhudiwa na Wahadhiri  na wanafunzi wa Chuo hicho pamoja na viongozi mbalimbali kutoka Serikali ya Tanzania na Uturuki akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Muhammed Mussa.

Shahada hii ni ya pili kwa Mhe. Rais Samia kutunukiwa kutoka ugenini ambapo Shahada ya kwanza ya aina hiyo alitunukiwa na Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru cha nchini India mwezi Oktoba 2023.

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ankara cha nchini Uturuki,  Prof. Necdet Ãœnüvar, akimtunuku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Shahada ya Heshima ya Udaktari (Honoris Causa) katika Uchumi katika hafla iliyofanyika Chuoni hapo tarehe 18 Aprili 2024 wakati wa ziara ya kitaifa ya Mhe. Rais Samia nchini humo.
Mhe. Rais Dkt. Samia akiwa katika picha ya pamoja na Prof. Ünüvar pamoja na Waziri anayeshughulikia masuala ya Familia na Huduma za Jamii wa Uturuki, Mhe.Mahinur Ozdemir Goktas mara baada ya kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari katika Uchumi na Chuo Kikuu cha Ankara

Mhe. Rais Dkt. Samia akifuwa ukumbini kabla ya kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari katika Uchumi na Chuo Kikuu cha Ankara. Kutoka kulia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akifuatiwa na Prof.Ünüvar pamoja na Mhe. Waziri Mahinur



Taratibu mbalimbali zikiendelea kabla ya Mhe. Rais Samia kutunukiwa Shahada yake ya Udaktari. Pichani ni viongozi wakiwa wamesimama kwa heshima ya nyimbo za mataifa yao

Mhe. Rais Dkt. Samia akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Chuo cha Ankara, Wakufunzi na Viongozi mbalimbali