Tuesday, September 4, 2012

Ripoti ya Timu ya Waangalizi wa Uchaguzi ya SADC



Timu ya Waangalizi wa Uchaguzi ya SADC imetoa ripoti yake kuhusu uchaguzi mkuu wa Angola uliofanyika 31 Agosti 2012. Ripoti hiyo ilitolewa mjini Luanda na Mhe. Bernard Membe, Mwenyekiti wa Timu ya Waangalizi ya SADC kwa niaba ya Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC.

Ripoti hiyo ya awali ya SADC iliyotolewa rasmi tarehe 2 Septemba, 2012 imejikita katika tathmini ya mchakato wa uchaguzi hususan majumuisho ya kampeni, ushirikishaji wa wadau upigaji kura na uhesabu wa kura katika vituo.

Timu ya SADC ilikuwa na waangalizi 103 na ilitawanywa katika Majimbo 12 kati ya 18 ya nchini Angola. Taarifa ya SADC imezingatia tathmini iliyofanywa na imeainisha mapungufu yaliyojitokeza katika uchaguzi huo ikiwemo kucheleweshwa kwa usajili wa waangalizi wa kimataifa, ucheleweshwaji katika kufunguliwa kwa baadhi ya vituo vya kupigia kura, na baadhi ya wapiga kura kutokupata kwa wakati kuhusu vituo walivyopaswa kupigia kura.

Aidha, Tume ya Uchaguzi ya Angola ilipongezwa kwa matumizi ya teknohama katika uchaguzi huo katika mchakato wote wa uchaguzi hali ambayo iliongeza ufanisi katika uchaguzi huo.

Ripoti imebainisha kuwa uchaguzj ulifanyika katika mazingira ya amani na utulivu yaliyoruhusu wananchi wa Angola kujitokeza kupiga kura wakiwemo wanawake, wazee na makundi yenye mahitaji maalum kama walemavu.

Timu ya Waangalizi wa SADC imeridhika kuwa pamoja na kasoro ndogondogo zilizojitokeza ambazo hazitoshelezi kuathiri matokeo ya jumla ya uchaguzi, uchaguzi mkuu wa Angola ulifanyika katika mazingira yanayotoa fursa ya kuwa huru na haki. Mwenyekiti wa Asasi ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama aliwapongeza wadau wote wa siasa nchini Angola na kuwahimiza kufuata kanuni za uchaguzi za SADC na Sheria za Angola iwapo kutajitokeza kutoridhika kwa mchakato wa uchaguzi mkuu huo.

Zoezi la kuhesabu kura bado linaendelea na matokeo yanatarajiwa kutangazwa rasmi katika wiki ya pili ya mwezi Septemba 2012.

Timu ya SADC inatarajiwa kutoa ripoti kamili siku thelathini kumalizika kwa uchaguzi huo mkuu kulingana na Kanuni na Misingi ya Uchaguzi ya SADC.
 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.