TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA YA MASHARIKI WAMWITA KAIMU BALOZI WA MAREKANI WIZARANI
Tarehe 19 June, 2019, Ubalozi wa Marekani Nchini Tanzania ulitoa taarifa katika mitandao ya kijamii “Twitter” kuhusu angalizo la kiusalama “security alert”. Angalizo hilo la kiusalama lilitokana na uvumi unaodaiwa na ubalozi huo kusambaa kuhusu uwezekano wa kutokea kwa shambulio katika baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ulimwita katika ofisi ndogo za Wizara zilizopo Jijini Dar es Salaam, Kaimu Balozi wa Marekani Bi Janine S. Young ili kutoa ufafanuzi wa “twitter” yao.
Ubalozi wa Marekani ulimtuma Mwakilishi wa Kaimu Balozi wa Marekani Bi. Janine S. Young kuonana na uongozi wa Wizara ambapo amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe.
Bi Janine S. Young ameutambua ujumbe huo na kukiri kuwa umetumwa na ubalozi wa Marekani hapa nchini.
Katika ufafanuzi wake amekiri kuwa Ubalozi umefanya makosa ya kutoa tetesi ambazo hazikuwalenga raia wa Marekani pekee bali raia wote wakitambua kuwa Ubalozi hauna mamlaka ya kufanya hivyo jambo lililosababisha taharuki kwa wananchi na wageni wanaotarajia kuitembelea Tanzania.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeukumbusha Ubalozi wa Marekani umuhimu wa kuzingatia sheria za nchi na taratibu za kidiplomasia zinazokubalika duniani kote katika utoaji wa taarifa za aina hii.
Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe amewataka wananchi na Jumuiya za Kimataifa pamoja na wageni mbalimbali waliopo nchini na wanaotarajia kuitembelea Tanzania kuendelea na shughuli zao kama kawaida kwani mpaka sasa hakuna taarifa yeyote iliyothibitishwa ya kuwepo kwa tishio la aina hiyo hapa nchini na kwamba Vyombo vya Ulinzi na Usalama vimejizatiti kukabiliana na matishio yeyote.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar Es Salaam.
20 Juni, 2019
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.