Friday, June 21, 2019

TANZANIA YANG’ARA KATIKA MAONESHO YA UTALII SEOUL, KOREA

Ubalozi wa Tanzania Seoul, kwa kushirikiana na wadau wa Utalii kutoka sekta binafsi wameshiriki katika maonyesho makubwa ya Kimataifa ya “Seoul International Tourism Industry Fair” yaliyofanyika jijini Seoul, Jamhuri ya Korea kuanzia tarehe 6 hadi 9 Juni 2019. Maonesho hayo yaliandaliwa na Korea World Travel Fair (KOTFA) kwa kushirikiana na Seoul International Travel Mart (Seoul Metropolitan City) ambapo wadau (kampuni za utalii, usafirishaji, wamiliki wa hoteli, migahawa, vyombo vya habari) kutoka nchi mbalimbali za Asia, Ulaya, Amerika, Afrika na Mashariki ya Kati walishiriki.

Kampuni za Utalii kutoka Tanzania zilizoshiriki maonesho hayo ni Eastenders, Zara Tours, Travel Booking Guide kwa kupitia Mwakilishi wake aliye Korea, Ms. Han Bitnarae, na SAFANTA Tours & Travel ya Zanzibar.

Kupitia maonesho hayo, Tanzania iliweza kutangaza vivutio vya utalii kwa jamii ya Wakorea na mataifa mengine kwa ujumla. Aidha, kampuni zilizoshiriki ziliweza kupata wenzao wa kushirikiana nao kibiashara kupitia B2B na kuingia makubaliano ya kibiashara.

Balozi wa Tanzania Korea Kusini, Mhe. Matilda Swilla Masuka akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Tanzania katika maonesho hayo, pamoja na wageni waliotembelea banda la Tanzania.
Picha ya pamoja kati ya washiriki wa Maonesho hayo ya Utalii, Wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania Seoul, na Watanzania waishio Korea Kusini (Diaspora) ambao walikuja kuunga mkono juhudi hizo za kuitangaza Tanzania
Mwakilishi wa kampuni ya Zara Tours, Bi Leila Ansell akiongea na wateja kuhusu huduma mbalimbali zitolewazo na kampuni hiyo ambayo imeingia mkataba pia na kampuni ya kikorea ya Hyecho Trekking ambayo hupeleka watu kupanda mlima Kilimanjaro. Mazungumzo pia bado yanaendelea na makampuni mengine.   




No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.