Friday, July 19, 2019

Wafanyabiasha kutoka China ziarani nchini kutafuta fursa za biashara



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Wafanyabiashara kutoka Jimbo la Zhejiang, China kuja nchini kutafuta fursa za biashara

Ujumbe wa wafanyabiashara 25 kutoka Kampuni kubwa 15 za Jimbo la Zhejiang nchini China ukiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Bunge la Jimbo hilo, Mhe. Bi. GE Huijun utafanya ziara nchini kuanzia tarehe 20 hadi 23 Julai 2019 kwa lengo la kukutana na kufanya mazungumzo na wadau mbalimbali kuhusu fursa za biashara na uwekezaji zilizopo nchini.

Ziara hiyo inalenga kukuza mahusiano ya kiuchumi baina ya Jimbo la Zhejiang na Tanzania katika sekta mbalimbali za maendeleo kama vile teknolojia, mawasiliano, ujenzi na uchukuzi, afya na madini.

Mhe. GE Huijun pia atafuatana na viongozi 13 wa Serikali ya Zhejiang kwenye ziara hiyo ambayo itaanzia Zanzibar tarehe 20 Julai 2019.

Ujumbe huo ukiwa nchini, pamoja na masuala mengine, unategemea kukutana na Viongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Viongozi wa Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar kwa ajili ya kujadiliana nao kuhusu fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji zilizopo nchini.

Ukiwa Zanzibar, ujumbe huo utatembelea maeneo ya viwanda ya Amani na Fumba kwa ajili ya kujionea fursa za uwekezaji. Aidha, ujumbe huo utakutana na Mamlaka ya Uwekezaji na Uendelezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) pamoja na kukutana na wafanyabiashara wa Zanzibar kwa madhumuni ya kuanzisha ushirikiano.

Kadhalika ujumbe huo utashiriki ufunguzi wa Kongamano la Biashara kati ya Wafanyabiashara wa Tanzania na Wafanyabiashara kutoka Zhejiang utakaofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 22 Julai 2019.

Ujumbe huo unategemea kukamilisha ziara yao nchini tarehe 23 Julai, 2019.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
19 Julai 2019


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.