TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Wafanyabiashara
na wawekezaji kutoka Jamhuri ya Czech watafuta fursa za biashara na uwekezaji nchini
Tanzania
Ujumbe wa wafanyabiashara na
wawekezaji kutoka Jamhuri ya Czech wamewasili nchini tarehe 13 Julai, 2019 kwa lengo
la kukutana na kufanya mazungumzo na wadau mbalimbali nchini ili kujadili fursa
za biashara na uwekezaji nchini katika sekta mbalimbali hususan afya, kilimo, miundombinu
ya barabara na reli,nishati, madini,utalii na wa ujenzi wa viwanda vya madawa na
vifaa tiba.
Ziara hiyo inatokana na juhudi
za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Ubalozi wa
Tanzania uliopo nchini Ujerumani ambao pia unawakilisha Tanzania katika Jamhuri
ya Czech na wadau wengine muhimu katika kushawishi wafanyabiashara wakubwa kuja
kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali.
Ujumbe huo wa watu kumi na mbili
(12) ukiwa nchini, pamoja na masuala mengine, unategemea kukutana na uongozi wa
Wizara naTaasisi mbalimbali zikiwemo, Wizara ya Viwanda na Biashara, Kituo cha
Uwekezaji Tanzania (TIC), Wizara ya Nishati, Wizara ya Madini, Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Bohari Kuu ya Dawa na Halmashauri ya Jiji la
Dar es Salaam.
Vilevile, ujumbe huo unategemea kushiriki katika Kongamano la
Uwekezaji wa Viwanda vya Kutengeneza Madawa na Vifaa Tiba kwa ubia kati ya
Serikali na Sekta Binafsi, lililoandaliwa na Bohari Kuu ya Dawa. Kongamano hilo
limepangwa kufanyika tarehe 17 Julai, 2019 katika Ukumbi wa Mkutano wa
Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Ziara ya ujumbe huo nchini ni
chachu ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Czech.
Kadhalika, ziara ya ujumbe huo ni moja ya mikakati ya utekelezaji wa Sera ya
Mambo ya Nje inayojikita katika diplomasia ya uchumi na kuhamasisha uwekezaji katika
sekta ya viwanda ili kutimiza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi
wa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa
kati ifikapo mwaka 2025.
Mhe. Dkt. Abdallah Saleh
Possi, Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani ambaye pia ni Balozi wa Tanzania
asiye na makazi nchini Czech ameambatana na ujumbe huo wa wafanyabiashara na wawekezaji.
Ujumbe huo kutoka Jamhuri ya
Czech unategemea kukamilisha ziara yao nchini tarehe 17 Julai, 2019.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
16 Julai 2019
Sehemu ya Wafanyabiashara na Wawekezaji kutoka Jamhuri ya Czech ukufuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa kwao na Wataalam kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) |
Sehemu nyingine ya Wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Jamhuri ya Czech |
Mkutano ukiendelea |
Mhe. Balozi Possi (wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi wa TIC na wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Jamhuri ya Czech. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.