Monday, June 27, 2022

WAZIRI MULAMULA AMUAGA BALOZI WA UBELGIJI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameagana na Balozi wa Ubelgiji nchini Mhe. Peter Van Acker ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini.

Akizungumza na Mhe. Balozi Peter walipokutana katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam, Waziri Mulamula amesema Tanzania na Ubelgiji zimekuwa na uhusiano wa karibu tangu nchi hiyo ilipofungua Ubalozi wake hapa nchini mwaka 1980.

“Uhusiano kati ya Tanzania na Ubelgiji umekuwa unakuwa na kuimarika………. kupitia awamu zote za serikali tumeshuhudia uwepo wa mipango ya maendeleo katika sekta za maji, elimu , nishati pamoja na biashara na uwekezaji,” amesema Balozi Mulamula.

Waziri Mulamula ampongeza Mhe. Balozi kwa kumaliza utumishi wake nchini na kuacha uhusiano kati ya Tanzania na Ubelgiji ukiwa imara.

Balozi Mulamula amesema pamoja na kwamba Balozi Peter anaondoka nchini amemhakikishia kuwa kundi la wafanyabiashara kutoka Ubelgiji litakuja nchini mwaka huu ikiwa ni mwendelezo wa kukuza ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji.

Kwa upande wake, Balozi wa Ubelgiji nchini, Mhe. Peter Van Acker ameongelea kuridhishwa kwake na uhusiano uliopo baina ya Ubelgiji na Tanzania na kuahidi kuwa balozi mwema wa Tanzania.

“Nimeishi vizuri hapa Tanzania na nimefurahia kuwa hapa wakati wote wa uwakilishi wangu, kuna mengi ya kujivunia kufanya kazi Tanzania……asante sana, amesema Balozi Acker

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa na Balozi wa Ubelgiji nchini Mhe. Peter Van Acker katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Balozi wa Ubelgiji nchini Mhe. Peter Van Acker katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akimkabidhi  Balozi wa Ubelgiji nchini Mhe. Peter Van Acker  zawadi ya picha






BALOZI MULAMULA AKUTANA NA NAIBU KATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe, Amina Mohammed jijini Kigali, Rwanda wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola. Mazungumzo hayo yaliangazia masuala makuu matatu ambayo ni mikutano inayoandaliwa na Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Usalama wa Chakula na namna dunia itakavyojikwamua kiuchumi baada ya UVIKO-19.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula  na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe, Amina Mohammed  wakifurahia jambo wakati wa mazungumzo.yao yaliyofanyika jijini Kigali, Rwanda.
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Robert Kahendaguza akiwa katika mazungumzo ya utangulizi na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe, Amina Mohammed (mwenye kilemba). Mwingine katika picha ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikino wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasiga. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akiendelea na mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe, Amina Mohammed (mwenye kilemba). Wengine wanaofuatilia ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Robert Kahendaguza; Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Balozi Mindi Kasiga na Afisa Dawati, Bi. Gloria Ngaiza.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe, Amina Mohammed (mwenye kilemba) wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wao walioshiriki katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola.

 Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe, Amina Mohammed akihojiwa na Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Runinga cha Channel 10, Bw. Ezekiel Mwamboko jijini Kigali, Rwanda wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola. Pembeni ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula

 

Saturday, June 25, 2022

BALOZI MULAMULA ATUMIA MKUTANO WA CHOGM KUITANGAZA TANZANIA

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki chini ya uongozi wa Waziri Liberata Mulamula imeendelea kutumia majukwaa ya kimataifa kuitangaza nchi na fursa zake kama sehemu ya utekelezaji wa diplomasia ya uchumi.

Katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaohitimishwa leo tarehe 25 Juni 2022 nchini Rwanda na kuhudhuriwa takribani na viongozi wa kaliba na ngazi tofauti wa nchi zote 54 za umoja huo, Tanzania ilitumia fursa hiyo kuhamasisha wawekezaji na kuja nchini.

Balozi Liberata Mulamula alionekana akifanya mazungumzo rasmi na yasiyo rasmi na Mawaziri wenzake wa Mambo ya Nje na hata Mawaziri Wakuu na Marais wa nchini mbalimbali kwa lengo la kuitangaza nchi. Alisikika akiwaambia, “Rais wetu, Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kuboresha mazingira ya biashara, hivyo milango ipo wazi, waambieni wafanyabiashara wenu waje kuwekeza Tanzania kwenye sekta mbalimbali na hasa kilimo ambacho ni moja ya kipaumbele cha Serikali ya awamu ya sita”.

Viongozi ambao Mhe. Waziri Mulamula alipata fursa ya kufanya nao mazungumzo rasmi ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Singapore, Mhe. Dkt. Vivian Balakrishnan; Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe.  Subrahmanyam Jaishankar; Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Mhe. Hina Rabbani Khar na Mke wa Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza na Mwanzilishi wa Mfuko wa Cherie Blair, Bibi Cherie Blair.

Viongozi Wakuu aliokutana nao na kuwapa salamu za Rais Samia ni pamoja na Waziri Mkuu wa Canada, Mhe. Justin Trudeau; Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame; Rais wa Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema; Rais wa Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta; na Rais wa Nigeria, Mhe.  Muhammadu Buhari.

Katika mazungumzo hayo pamoja na mambo mengine, Balozi Mulamula alihimiza ushirikiano katika biashara na uwekezaji, mafunzo, usafiri wa anga na utalii.  Alieleza namna Serikali ya awamu ya sita inavyofanya jitihada kuondoa vikwazo vya kibiashara na kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kushawishi wawekezaji wengi. Aliziomba Canada, Singapore, India na Pakistan kuleta wawekezaji wengi zaidi na hasa katika sekta ya kilimo ambayo ni kipaumbele cha Serikali ya awamu ya sita.

Kuhusu utalii, Mhe. Waziri aliziomba nchi hizo kutafsiri Filamu ya The Royal Tour iliyoongozwa na Rais Samia kwa lugha za nchi zao ili iwafikie watu wengi zaidi. Aidha, alizihimiza nchi hizo, hususan India na Singapore kuanzisha safari za moja kwa moja za mashirika yao ya ndege kati ya Tanzania na nchi hizo ili kuhamasisha utalii.

Aidha, Mhe. Waziri alihimiza ushirikiano na Singapore katika Uchumi wa Buluu kutokana na nchi hiyo kupiga hatua kubwa kwenye eneo hilo, hususan kwenye uendelezaji, usimamizi na uendeshaji wa bandari. Aligusia pia umuhimu wa kujengeana uwezo hususan katika eneo la rasilimali watu na mafunzo ya TEHAMA.

Wakati wa mazungumzo na Bibi Cherie Blair, alielezea utayari wa Mfuko wake wa Cherie Blair Foundation wa kushirikiana na Tanzania, kwenye kuwajengea uwezo wanasheria wa kuwa na ujuzi wa kutosha wa upatanishi na usuluhishi wa migogoro nje ya mahakama na kwamba mfuko huo pia, upo tayari kuisaidia Tanzania kwa kutoa msaada kwa mawakili katika kesi za Kimataifa zinazoikabili Serikali ya Tanzania.

Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola utafungwa leo jioni na Balozi Mulamula ataendeelea na mkakati wake wa kukutana na viongozi mbalimbali na atarejea nchini tarehe 26 Juni 2022.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashaiki, Balozi Liberata Mulamula akiongea na Waziri Mkuu wa Canada, Mhe Justin Trudeau wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaofanyika Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashaiki, Balozi Liberata Mulamula akiongea na Waziri Mkuu wa Canada, Mhe Justin Trudeau wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaofanyika Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022. Mwingine katika picha ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Canada, Mhe. Mélanie Joly
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongea jambo na Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame  wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Modola unaofanyika Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2025.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongea jambo na Rais wa Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Modola unaofanyika Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2025.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongea jambo na Rais wa Nigeria, Mhe.  Muhammadu Buhari  wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Modola unaofanyika Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2025.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongea jambo na Rais wa Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta  wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Modola unaofanyika Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2025.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongozana na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango kuingia kwenye ukumbi unaofanyika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa  Singapore, Dkt. Vivian Balakrishnan wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Modola unaofanyika Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2025.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa  Singapore, Dkt. Vivian Balakrishnan wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Modola unaofanyika Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2025. Balozi Mulmula alitumia fursa pamoja na mambo mengine kuwakaribisha wafanyabiashara wa Singapore kuja kuwekeza Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongea jambo na Mkurugenzi wa Afrika katika Wizara ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz. Wengine katika picha ni Maafisa wa Mambo ya Nje, Bi. Talha Waziri (kulia) na Bi. Lilian Mukasa.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashaiki, Balozi Liberata Mulamula akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Mhe. Bilawal Bhutto Zardari wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaofanyika Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashaiki, Balozi Liberata Mulamula akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe Subrahmanyam Jaishankar wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaofanyika Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashaiki, Balozi Liberata Mulamula na ujumbe wake wakiwa katika mazungumzo na na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe Subrahmanyam Jaishankar wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaofanyika Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashaiki, Balozi Liberata Mulamula (kulia) akiongea jambo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Mhe.Netumbo Nandi-Ndaitwah wakati wakielekea kwenye ukumbi unaofanyika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaofanyika Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashaiki, Balozi Liberata Mulamula akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sierra Leone, Mhe. Prof. David Francis wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaofanyika Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashaiki, Balozi Liberata Mulamula akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje wa Zambia, Mhe. Stanley Kakubo wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaofanyika Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022

















 

Friday, June 24, 2022

UJUMBE WA JIMBO LA HAUT KATANGA WAFANYA ZIARA YA KIKAZI NCHINI


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma Rajab akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na ujumbe kutoka jimbo la Haut Katanga la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) walipotembelea Ofisi za Wizara jijini Dodoma. Ujumbe huo wa watu tisa unaongozwa na Gavana wa jimbo hilo Mhe. Jacques Kyabula Katwe

Ujumbe kutoka jimbo la Haut Katanga la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) umeanza zaira ya siku 4 ya kikazi nchini. Ujumbe huo wa watu tisa unaongozwa na Gavana wa jimbo hilo Mhe. Jacques Kyabula Katwe

Pamoja na masuala mengine ziara hiyo inalenga kujionea na kujifunza namna Tanzania inavyoendesha shughuli za kilimo cha mazao ya biashara na chakula. 

Ujumbe huo umeanza zaira yake nchini kwa kutembelea Taasisi mbalimbali za serikali sambamba na kuonana na kufanyamazungumzo na viongozi waandamizi wa Serikali ikiwemo Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe, Waziri wa Madini Mhe. Dotto Biteko na Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma Rajab. Vilevile walipata fursa ya kutembelea Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Akizungumza kwa nyakati tofauti Gavana Jacques Kyabula Katwe ameeleza kuwa ziara yake nchini imetokana na kutuvitiwa kwake na namna Tanzania ilivyopiga hatua ya maendeleo katika sekta mbalimbali hususan kilimo na usimamizi wa madini.

“Kwa muda mrefu nimekuwa nikifuatalia maendeleo ya kilomo cha Tanzania kiasi cha kuweza kujitosheleza kwa chakula na pia kubakiwa na ziada ya kuuza kwa nchi za nje zenye uhitaji, nikasema sasa niwakati muafaka wa kutembelea Tanzania ili mimi pamoja na timu yangu tuweze kujifunza na kuanzisha ushirikiano katika sekta ya kilimo”. Alisema Gavana Katwe

Balozi Fatma Rajab akizungumza na Gavana huyo pamoja na ujumbe wake walipomtembelea Ofisini kwakwe jijini Dodoma ameleeza kuwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na DRC umeendelea kuimarika daima hivyo niwakati muafaka kwa pande zote mbili kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara. 

“Tumekuwa tukishirikiana baina yetu, lakini pia kupitia Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambako sote ni wanachama na sasa ninayo furaha kubwa pia kona tuko wote katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Tuendelea kuboresha mazingira ya biashara ili watu waendeshe shughuli zao kwa urahisi na uhuru zaidi na kuweza kujiongezea kipato chao binafsi lakini pia pato la Serikali za pande zote mbili”. Amesema Balozi Fatma Rajab.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe alieleza kuwa Serikali ya Tanzania kupitia Wizara yake ipo tayari kushirikiana na Jimbo la Haut Katanga katika kuendeleza kilimo. Aliongeza kusema pamoja na Tanzania kuiuzia chakula DRC bado Tanzania haiiangali nchi hiyo kama soko bali kama mbia wa maendeleo. 

“Tupo tayari kushirikiana na DRC katika kilimo, tutafanya kila litakalowezekana kuwaongezea ujuzi ili kwa pamoja tuzalishe chakula cha kutosha; naamini Tanzania na DRC tukiungana kwa dhati katika kilimo tunaweza kuzalisha chakula kwa wingi zaidi na kuweza kulisha sehemu kubwa ya Dunia” Alisema Waziri Bashe

Waziri Biteko kwa upande wake amweleza Gavana Katwe kuwa Tanzania ipotayari kuendelea kushirikiana na DRC katika biashara ya madini. Aliendelea kueleza kuwa Tanzania ipo mikono wazi muda wote kupokea fursa za biashara za madini kutoa DRC. Aidha amemhakikishia Gavana Katwe kuwa Tanzania haina urasimu katika biashara na hiyo inawakaribisha wafanyabiashara kutoka DRC kuja nchini kuuza au kuongeza dhamani ya madini kwa kuwa uwezo huo kwa sasa Tanzania tunao.

Gavana Jacques Kyabula Katwe na ujumbe wake waliwasili nchini tarehe 22 Juni 2022 na kupokelewa na Mkurugenzi wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Dkt. Anselim Mosha. Wengine waliombatana na ujumbe huo kutoka nchini DRC ni Balozi wa Tanzania nchini humo Mhe. Saidi Juma Mshana na Konseli Mkuu wa Tanzania jijini Lubumbashi Selestine Kakele. 
Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe (kushoto) na Gavana wa jimbo la Haut Katanga la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Mheshimiwa Jacques Kyabula Katwe (kulia) wakisalimiana alipotembelea Ofisi ya Wizara ya Kilimo jijini Dodoma
Gavana wa jimbo la Haut Katanga la DRC Mhe. Jacques Kyabula Katwe (kulia) akisalimiana na Mkurugenzi wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Dkt. Anselim Mosha (kushoto) alipowasili katika uwanja wa ndege wa jijini Dodoma.
Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe na Gavana wa jimbo la Haut Katanga Mheshimiwa Jacques Kyabula Katwe na ujumbe wake wakiwa katika picha ya pamoja na Watendaji mbalimbali wa Serikali kwenye Ofisi za Wizara ya Kilimo jijini Dodoma.
Gavana wa jimbo la Haut Katanga la DRC akiwa katika picha pamoja na Viongozi na Watendaji mbalimbali wa Serikali ya Tanzania Bungeni jijini Dodoma.
Waziri wa Madini Mhe. Dotto Biteko na Gavana wa jimbo la Haut Katanga Mheshimiwa Jacques Kyabula Katwe na ujumbe wake wakiwa katika picha ya pamoja na Watendaji mbalimbali wa Serikali ya Tanzania jijini Dodoma
Gavana wa jimbo la Haut Katanga la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Mheshimiwa Jacques Kyabula Katwe (wa kwanza kulia) akiwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipotembelea Bunge hilo tarehe 23 Juni 2022. 
Waziri wa Madini Mhe. Dotto Biteko (kulia) na Gavana wa jimbo la Haut Katanga la DRC Mheshimiwa Jacques Kyabula Katwe (kushoto) wakisalimiana alipotembelea Ofisi ya Wizara ya Madini jijini Dodoma
Gavana wa jimbo la Haut Katanga la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Mheshimiwa Jacques Kyabula Katwe akielezea jambo wakati wa mazungumzo baina yake Viongozi na Watendaji wa Wizara ya Madini

VACANCY ANNOUNCEMENT


 

BALOZI MULAMULA ATAKA MIGOGORO KATIKA NCHI ZA JUMUIYA YA MADOLA IMALIZWE

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amesema kuwa, licha ya wanachama wa Jumuiya ya Madola kufanya kazi nzuri katika kuimarisha misingi ya demokrasia, amani na utawala bora katika nchi zao, bado kuna changamoto nyingi zinazohitaji kutafutiwa ufumbuzi ili misingi hiyo ya maisha iweze kufanya kazi kwa ukamilifu wake.

Ametoa kauli hiyo leo tarehe 23 Juni 2022 jijini Kigali katika kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Madola kilichukuwa kinajadili masuala ya demokrasia, amani na utawala bora.

Waziri Mulamula alizitaja baadhi ya changamoto hizo na kusisitiza umuhimu wa familia ya Jumuiya ya Madola kuziangalia kwa makini na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu, kuwa ni pamoja na migogoro isiyoisha, ukosefu wa usalama na udhaifu wa vyombo vinavyosimamia masuala ya utawala wa sheria.

Balozi Mulamula katika maelezo yake alitambua jitihada zinazofanywa na jumuiya za kikanda na kimataifa za kutumia njia za kidiplomasia kuzuia migogoro na kuzisihi nchi za jumuiya hiyo kongwe kurejea katika misingi yake ya awali, ili kuhakikisha kuwa amani na utulivu vinatawala muda wote kwenye nchi hizo.

Aidha, Waziri Mulamula alitumia mkutano huo wa Mawaziri wa Mambo ya Nje, kuzishauri nchi wanachama kuangalia uwezekano wa kutumia taratibu za kujitathmini zinazotumika kwenye jumuiya nyingine za kujipima kiutawala bora.

Alitoa mifano ya taratibu hizo kuwa ni pamoja na Mpango wa Nchi za Afrika za Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM); mpango wa hiyari wa nchi zinazotekeleza malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) wa kujipima utekelezaji wa malengo hayo; mpango wa nchi wanachama wa Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu wa kujitathmini kila baada ya kipindi fulani.

Aliwafahamisha Mawaziri wenzake kuwa, Tanzania imefanyiwa tathmini hivi karibuni na Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu na kupitia tathmini hiyo, Tanzania ilipata fursa ya kueleza mazuri yaliyofanyika kuhusu utawala bora na haki za binadamu. Alisema pia kuwa nchi yake ilipata fursa ya kujifunza mazuri ya nchi nyingine kuhusu utawala bora.

Balozi Mulamula alitihitimisha hotuba yake kwa kuwakumbusha Mawaziri kuhusu programu zilizobuniwa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola na umuhimu wa kuzihuisha na kuzipa nguvu. Progaramu hizo ni pamoja na misaada katika uchaguzi ikiwa ni pamoja na kuhamasisha nchi wanachama kuendesha chaguzi za huru na haki, kutoa misaada ya kiufundi katika uandaaji wa sera, misaada katika programu za mabadiliko ya sheria, kuunda taasisi imara za kitaifa za kusimamia masuala ya haki za binadamu na kuzijengea nchi uwezo wa kutoa haki bila upendeleo.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika kiti cha Tanzania wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaofanyika nchini Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akisalimiana na Mawaziri wenzake wanaoshiriki katika mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaofanyika nchini Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa na makabrasha ya mkutano akilekea kwenye Kiti cha Tanzania kwa ajili ya kushiiki mkutano wa Mawaziri wa sJumuiya ya Madola unaofanyika nchini Rwanda.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akihojiwa na mwandishi wa Kituo cha Runimga cha Channel 10, Bw. Ezekiel Mwamboko. Aliyemshikia kipaza sauti ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,, Balozi Mindi Kasiga.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Jumuiya ya Madola wanaoshiriki katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa jumuiya hiyo unaofanyika nchini Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022.


 

Thursday, June 23, 2022

DKT. MPANGO AWASILI RWANDA KUSHIRIKI CHOGM

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amewasili nchini Rwanda tarehe 22 Juni 2022 kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa nchi za Jumuiya ya Madola (Commonwealth Heads of Government Meeting-CHOGM) unaofanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kigali.

Makamu wa Rais anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano huo ulioanza tarehe 20 Juni na utahitimishwa tarehe 25 Juni 2022.

Mhe. Makamu wa Rais, mbali ya kushiriki kwenye mkutano huo ameombwa pia miadi ya kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wakiwemo Rais wa Namibia, Mhe. Hage Geingob; Waziri Mkuu wa Mauritius; Pravind Jugnauth; Waziri Mkuu wa Canada, Mhe. Justin Trudeau na Melinda Gates.

Inaelezwa kuwa miadi hiyo ni ishara ya dhahiri ya kuendelea kuimarika kwa diplomasia ya Tanzania duniani chini ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia. Hivyo, Mhe. Makamu wa Rais anatarajiwa kutumia miadi hiyo kusisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya pande mbili na hasa ushirikiano katika eneo la uwekezaji na biashara pamoja na utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.

Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula naye yupo nchini humo kushiriki Mkutano huo katika ngazi ya Mawaziri tarehe 23 Juni 2022. Kama ilivyo kwa Makamu wa Rais, Balozi Mulamula ameombwa miadi ya kufanya mazungumzo na Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za India, Zambia, Botswana, Eswatini, Singapore na mke wa Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Mhe. Tony Blair, Bibi Cherie Blair ambaye ni mwanzilishi wa Cherie Foundation.

Wakati huo huo, mikutano ya utangalizi ya mkutano huo, inaendelea ambapo tarehe 20 hadi 23 Juni 2022 ilifanyika mikutano ya jukwaa la vijana, jukwaa la wanawake na jukwaa la biashara. Tanzania ilishiriki katika majukwaa yote hayo

Wakati wa mkutano wa jukwaa la biashara, washiriki pamoja na mambo mengine, walijadili namna bora ya kufanya biashara huku dunia ikiwa bado inakabiliwa na janga la ugonjwa wa Corona na athari za vita kati ya Urusi na Ukraine.

Ujumbe wa Tanzaia katika mkutano huo uliongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara katika Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah ambaye alieleza hatua zinazochukuliwa na Serikali ya awamu ya sita za kuboresha mazingira ya biashara na fursa lukuki za uwekezaji zinazopatikana nchini.

Kwa upande wa mkutano wa jukwaa la vijana ambapo Tanzania iliwakilishwa na vijana saba, ulisistizwa umuhimu wa kuwaendeleza vijana. Ilielezwa kuwa endapo nchi za Jumuiya ya Madola zinahitaji kufikia maendeleo ya kweli, hazina budi kuwekeza kwa vijana kwa sababu katika nchi hizo vijana ni zaidi ya asilimia 60. 

 Kuhusu mkutano wa jukwaa la wanawake, ulisisitizwa umuhimu wa kumuendeleza mwanamke ikiwa ni pamoja na kumpatia elimu ya kumiliki, kukuza na kufanya biashara, kuweka usawa wa kijinsia na kukomesha vitendo vyote vya unyanyasaji dhidi ya wanawake.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akitoa maelezo kwa  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango kuhusu maandalizi ya ushiriki wa Tanzania katika  mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaofanyika jijini Kigali, Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akifafanua jambo kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango kuhusu ushiriki wa Tanzania katika mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaofanyika jijini Kigali, Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akitoa maelezo kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango ambaye anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 26 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaofanyika jijini Kigali, Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022.
Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe.Dkt. Asha-Rose Migiro akifafanua jambo kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango kuhusu masuala ya CHOGM


Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Robert Kahendaguza akitoa utaratibu wa namna ya mikutano ya CHOGM itakavyoendeshwa kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango.

Afisa Dawati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Salma Rajab akifafanua jambo kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika kikao cha maandalizi na ujumbe wake kabla ya kushiriki kwenye mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaofanyika jijini Kigali, Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango akiongea na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango akiongea na baadhi ya viongozi wa Serikali wanaoshiriki Mkutano wa 26 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaofanyika jijini Kigali, Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022.