Wednesday, April 17, 2024

MHE. RAIS SAMIA AWASILI NCHINI UTURUKI KWA ZIARA YA KITAIFA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewasili katika jijini Ankara, Uturuki leo tarehe 17 Aprili 2024 kuanza ziara yake ya kitaifa ya siku nne inayofanyika  kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Uturuki, Mhe. Recep Tayyip Erdogan.

 

Mara baada ya kuwasili Mhe. Rais Samia alilakiwa na Waziri anayeshughulikia masuala ya Huduma za Jamii na Familia, Mhe. Mahinur Ozdemir Goktaş.

 

Akiwa nchini Uturuki, Mhe. Rais Samia atapokelewa rasmi na mwenyeji wake Mhe. Rais Erdogan katika Ikulu ya nchi hiyo jijini Ankara tarehe 18 Aprili 2024. Viongozi hao pamoja na mambo mengine watashiriki mazungumzo rasmi na dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na Mhe. Rais Erdogan kwa heshima ya Mhe. Rais Samia.

 

Siku hiyohiyo Mhe. Rais Samia atatunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari katika Uchumi na Chuo Kikuu cha Ankara kutokana na chuo hicho kutambua uongozi wake wa kipekee ambao umeleta mageuzi makubwa ya kijamii, kisiasa na kiuchumi ambayo yameboresha ustawi wa Wtanzania na kuimarisha sifa ya Tanzania ulimwenguni pamoja na kukuza uhusiano wa kibiashara, kiuchumi na kisiasa kati ya Tanzania na nchi nyingine ikiwemo Uturuki.

 

Mhe. Rais Samia ataondoka Ankara tarehe 19 Aprili 2024 kuelekea Istanbul, mji mkuu wa kibiashara wa Uturuki kwa ajili ya kufungua rasmi  Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki ambalo litahudhuriwa pia na Makamu wa Rais wa Uturuki, Mhe. Cevdet Yılmaz.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Waziri anayeshughulikia masuala ya Familia na Huduma za Jamii wa Uturuki, Mhe.Mahinur Ozdemir Goktas mara baada ya kuwasili nchini Uturuki kwa ajili ya kuanza ziara ya kitaifa itakayofanyika kuanzia tarehe 17 hadi 21 Aprili 2024

Mhe. Rais Samia akisalimiana na Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Iddi Bakari mara baada ya kuwasili nchni humo kwa ziara ya kitaifa. Wanaoshuhudia ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (wa nne kushoto) pamoja Balozi wa Uturuki nchini Mhe. Dkt. Mehmet Gulluoglu (kulia)

Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan akiwa katika mazungumzo na Mhe. Mahinur mara baada ya kuwasili nchini Uturuki kwa ziara ya kitaifa






 

WAZIRI MAKAMBA AKUTANA KWA MAZUNGUMZO NA MWENYEKITI WA UMOJA WA URAFIKI WA WABUNGE WA TANZANIA NA UTURUKI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba amekutana kwa mazungumzo na Mbunge wa Bunge la Uturuki na Mwenyekiti wa Umoja wa Urafiki wa Wabunge wa Tanzania na nchi hiyo, Mhe. Zeki Korkutata.

 

Katika mazungumzo yao ambayo yamefanyika tarehe 16 Aprili 2024 jijini Ankara, ikiwa ni sehemu ya kukamilisha maandalizi ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inayotarajiwa kufanyika nchini humo kuanzia tarehe 17 hadi 21 Aprili 2024 viongozi hao wamejadili maeneo muhimu ya ushirikiano ambayo pia yatajadiliwa kwa uzito wa juu wakati wa ziara hiyo.

 

Mhe. Makamba amesema miongoni mwa masuala muhimu nchi hizi mbili zitayapa kipaumbele kupitia ziara hii, ni  pamoja na kufanyika haraka kwa mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kwenye masuala ya Uchumi baina ya Tanzania na Uturuki.

 

Amesema kupitia tume hii nchi hizi mbili zitapata fursa ya kujadili kwa kina sekta za ushirikiano wa kimkakati baina yake na kuandaa mikakati ya utekelezaji wa makubaliano yote yatakayofikiwa wakati wa ziara hii ya kihistoria.

 

Mhe. Makamba amesema kuwa, Uturuki ni nchi muhimu wakati huu  ambapo  Tanzania imejikita katika kukuza uchumi wake kupitia ushirikiano na nchi mbalimbali na kwamba ana imani kwamba Tanzania itanufaika kupitia sekta ambazo nchi hiyo imepiga hatua za kiuchumi na kimaendeleo kama viwanda, usafirishaji, utalii na nishati.

 

Amesema Kngamano la Biashara na Uwekezaji litakalofanyika wakati wa ziara ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan litakuwa ni chachu ya kuongeza kasi zaidi ya kukuza urari na ujazo wa biashara baina ya nchi hizi mbili.

 

Vile vile amesema wakati wa ziara hiyo hati nane za ushrikiano kwenye sekta za kimkakati ikiwemo Elimu, Uwekezaji na ushirikiano katika masuala ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu  zitasainiwa.

 

Pia alitumia fursa hiyo kumkaribisha Mhe. Korkutata kutembelea Tanzania hususan Bungeni ili kujionea utendaji wa shughuli za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  

Kwa upande wake, Mhe. Korkutata amesema Uturuki inathamini ushirikiano uliopo baina yake na Tanzania na kwamba ziara ya Mhe. Rais Samia ni ishara kuwa nchi hizi mbili zimedhamiria kuupeleka ushirikiano huo katika hatua nyingine ya juu kwa manufaa ya wananchi wa pande hizi mbili.

 

Mhe. Mhe. Makamba yupo nchini Uturuki kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya ziara ya kitaifa ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ambapo mbali na kukutana na Mhe. Korkutata pamoja na kutembelea Bunge la Uturuki, Mhe. Makamba pia amekutana kwa mazungumzo na mwenyeji wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Mhe. Hakan Fidan.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akizungumza na Mbunge na Mwenyekiti wa Umoja wa Urafiki wa Wabunge wa Tanzania na Uturuki Mhe. Zeki Korkutata (hayupo pichani) ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini humo
Mhe. Korkutata naye akizungumza. Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Iddi Bakari na kulia ni Mkalimani wa Mhe. Korkutata
Mazungumzo yakiendelea

Mazungumzo yakiendelea



Mazungumzo yakiendelea. Wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme
Mkuu wa Utawala katika Ubalozi wa Tanzania nchini Uturuki, Bw. Mashaka Chikoli (kushoto) pamoja na Afisa Mambo ya Nje, Bi. Clementina Msafiri wakifuatilia mazungumzo.

Mhe. Waziri Makamba akipokea zawadi kutoka kwa Mhe. Korkutata




 

Tuesday, April 16, 2024

NJE SPORT YAIZIBUA BILA HURUMA MAMLAKA YA AFYA YA MIMEA NA VIUATILIFU

Timu ya Nje – Sport wanaume imeizibua bila huruma magoli 2 kwa buyu Timu ya Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) katika mchezo uliofanyika kwenye  viwanja vya Shule ya sekondari ya Iliboru jijini Arusha leo Aprili 16, 2024.

Magoli hayo yamepachikwa wavuni na washambuliaji hatari wa timu hiyo, Bw. Mikidadi Magola, Goli la kwanza na goli la pili likiwekwa kimyani kwa ustadi mkubwa na Bw. Mukrimu Mustafa. 

Kocha wa timu hiyo, Bw. Shabani Maganga aliwapongeza wachezaji wake kwa kufuata maelekezo yake pamoja na kucheza vizuri na kuifanya timu yake kubeba alama tatu muhimu katika mzunguko wa kwanza

Katika mchezo mwingine timu ya Wanawake ya mpira wa pete ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Nje Sports) imepokea kichapo cha magoli 52 kwa 7 kutoka  timu ya Ikulu. 

Mmoja wa wachezaji wa timu hiyo, Bi. Pili Sukwa ameeleza kuwa licha ya kichapo hicho, Timu yake imeendelea kuimarika na ameahidi kufanya vizuri katika michezo inayofuata.

 Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wameungana na mamia ya watumishi wenzao kushiriki michezo ya Mei mosi ambapo maadhimisho ya kitaifa yamepangwa kufanyika Mkoani Arusha.

Timu ya mpira wa Miguu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakiwa katika picha ya pamoja muda mfupi kabla kuingia uwanjani kucheza dhidi ya Timu ya Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA)

Timu ya Mpira wa Miguu ikifanya mazoezi ya kupasha viungo.



Mechi kati ya Nje na Hazina FC ikiendelea katika uwanja wa Ujenzi mjini Morogoro

Mshambuliaji machachari wa Nje Sports Bw. Mukrimu Mustafa akipongezwa na kocha wa Nje FC katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Ilboru mjini Arusha


Kepteni wa Nje FC akipatiwa matibabu mara baada ya kuchezewa rafu na mchezaji wa timu pinzani.

Wachezaji wa Nje FC wakiburudika mara baada ya kupata ushindi wa 2 - 0.

Timu ya mpira wa pete ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Ikulu muda mfupi kabla kuingia uwanjani kucheza mchezo wa raundi ya kwanza.

Timu ya mpira wa pete ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakipasha viungo muda mfupi kabla kuingia uwanjani kucheza dhidi ya Timu ya Ikulu


Juu na chini Mchezo ukiendelea.




 

WAZIRI MAKAMBA AWASILI UTURUKI KUELEKEA ZIARA YA KITAIFA YA MHE. RAIS SAMIA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba amewasili Ankara, Uturuki leo tarehe 16 Aprili 2024 na kukutana kwa mazungumzo na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Mhe. Hakan Fidan.


Pamoja na mambo mengine viongozi hao wamejadili kuhusu kukamilika kwa maandalizi ya ziara ya kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan itakayofanyika nchini humo kuanzia tarehe 17 hadi 21 Aprili 2024.


Wakati wa ziara ya Mhe. Rais Samia ambayo inafanyika kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Uturuki, Mhe. Recep Tayyip Erdoğan viongozi hao watashuhudia kusainiwa kwa Hati za Makubaliano nane (8) katika sekta za Elimu, Utalii, Utunzaji Nyaraka na ushirikiano katika masuala ya Diaspora. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mhe.  Hakan Fidan baada ya kuwasili nchini Uturuki kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya ziara ya kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan nchini humo
Mhe. Makamba akiwa katika mazungumzo na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mhe. Hakan Fidan


Mhe. Waziri Makamba na Mhe. Waziri Fidan wakiwa na ujumbe walioongozana nao wakati wa mazungumzo yao. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme na Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Iddi Bakari. Wa pili kulia ni Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Mhe. Mehmet Gulluoglu