Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amewakaribisha wawekezaji kutoka Jamhuri ya Latvia kuja nchini kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya Kilimo na TEHAMA.
Balozi Dkt. Shelukindo ametoa wito huo leo tarehe 10 Machi, 2023 alipozungumza
na Mkurugenzi Mkuu anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Uwili katika
Wizara ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Latvia, Bw. Nils Jansons aliyemtembelea
ofisini kwake jijini Dodoma kwa lengo la kumsalimia na kumpongeza kwa kuteuliwa
hivi karibuni kwenye wadhifa huo.
Amesema Tanzania inayo ardhi ya kutosha kwa uwekezaji wa kilimo cha mazao
mbalimbali ya chakula na biashara hivyo wawekezaji kutoka Latvia ambayo ni
miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri kwenye sekta ya kilimo duniani
wanakaribishwa.
“Nimefurahishwa na ziara yako hapa Tanzania. Latvia ni miongoni mwa nchi
zinazofanya vizuri katika sekta ya kilimo duniani. Tunaunga mkono ushirikiano
na Tanzania kwenye sekta hiyo na tunawakaribisha wawekezaji wenye tija kuja
kuwekeza kwenye sekta mbalimbali hususan kilimo na TEHAMA ” alisema Balozi Dkt.
Shelukindo.
Awali akizungumza kwenye Majadiliano ya Kwanza ya Kisiasa baina ya Tanzania na
Latvia, Balozi Swahiba Mndeme, Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, amesema Tanzania
inathamini ushirikiano uliopo baina yake na Latvia na kwamba majadiliano hayo
ambayo yanalenga kuimarisha ushirikiano baina ya pande mbili, yamekuja
wakati muafaka kwa nchi hizi mbili ili kuziwezesha kujiwekea malengo na
mikakati mipya ya kuuimarisha ushirikiano ambao ulikuwa hafifu miaka ya
nyuma.
“Tanzania inathamini ushirikiano uliopo baina yake na Latvia na tunapongeza
uamuzi wenu wa kuja ili kama nchi mbili rafiki tuzungumze na kukubaliana namna
ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wetu”, alisema Balozi Mndeme.
Aidha, amesema Tanzania kupitia ushirikiano na nchi za Umoja wa Ulaya ikiwemo
Latvia imeendelea kunufaika kupitia sekta za biashara, utalii na uwekezaji huku
akitoa mfano wa sekta ya utalii ambayo kwa kiasi kikubwa imewavutia watalii
wengi kutoka nchi za Ulaya kwa takribani asilimia 80 ya watalii wote wanaoingia
Tanzania.
Amesema katika medani za kimataifa hususan agenda ya Mabadiliko ya Tabianchi,
Tanzania inazisisitiza nchi zilizoendelea ikiwemo Latvia kutimiza ahadi yao ya
kuchangia kiasi cha Dola za Marekani Bilioni Moja kila mwaka ili kuziwezesha
nchi zinazoendelea ikwemo Tanzania kukabiliana na changamoto mbalimbali
zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ongezeko la joto na ukame.
Naye, Bw. Jansons ameeleza utayari wa Serikali ya Latvia wa kushirikiana na
Tanzania katika sekta mbalimbali za manufaa kwa pande mbili na kusisitiza kuwa
nchi hiyo ina mpango wa kuteua Mwakilishi wa Heshima wa nchi hiyo hapa nchini
ili kushughulikia masuala yote ya ushirikiano.
“Naunga mkono hoja zote tulizojadiliana ikiwemo ya kuzikumbusha nchi
zilizoendelea kutimiza ahadi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Latvia inayo nia ya dhati ya kuimarisha ushirikiano na Tanzania kwa manufaa ya
pande hizi mbili,” alisema Bw. Jansons.
Kupitia majadiliano hayo, Tanzania na Latvia zimekubaliana kuimarisha
ushirikiano katika sekta za Kilimo, Tehama, Utalii, Biashara na Uwekezaji,
Mazingira na Uchukuzi hususan kwa kuimarisha matumizi bora ya Bandari.
Pia nchi hizi mbili zimedhamiria kusaini Mkataba wa Ushirikiano katika sekta ya
Anga (BASA) baada ya majadiliano ya awali kukamilika kwa ajili ya kukuza Utalii
na Biashara baina ya pande mbili; Kuunganisha Vyuo Vikuu vya Kilimo vya pande
mbili kwa ajili ya kukuza matumizi ya teknolojia katika sekta ya Kilimo; na
Kuunganisha Taasisi Kuu za Biashara na Uwekezaji za pande mbili kwa lengo la
kukuza Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Latvia ambapo hivi karibuni
ujumbe wa Wawekezaji kutoka Latvia watafanya ziara ya kikazi nchini kwa ajili
ya kufahamu na `kutumia fursa za Biashara zilizopo nchini.
Mazungumzo yakiendelea |
Balozi Dkt. Shelukindo akiagana na Bw. Jansons mara baada ya kukamilisha mazungumzo yao |
Picha ya pamoja |
.........Majadiliano ya Kwanza ya Kisiasa kati ya Tanzania na Latvia
Mkurugenzi
Mkuu anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Uwili katika Wizara ya Mambo ya
Nje wa Jamhuri ya Latvia, Bw. Nils Jansons (kushoto) akiwa na Mjumbe aliyefuatana naye, Bw. Tils Indans. |