Sunday, July 10, 2016

Rais Dkt. John Pombe Magufuli ampokea Waziri Mkuu wa India

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli akimpokea Waziri Mkuu wa India Mhe.  Narendra Modi mara baada ya kuwasili katika Viwanja vya Ikulu Jiji Dar es Salaam. Mhe. Modi yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili inayotarajiwa kumalizika leo.


Waziri Mkuu wa India Mhe. Modi akikabidhiwa maua na mtoto Elizabeth Jackson mara baada ya kupokelewa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiwa amesimama na Mgeni wake, Waziri Mkuu wa India Mhe. Modi wakati nyimbo za Taifa zikipigwa mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Ikulu.
Mhe. Modi akikagua gwaride la heshima mara baada ya kumalizika kupigwa nyimbo za Taifa.
Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi akisalimiana na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mama Samia Suluhu Hassan mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Mgeni wake Mhe. Modi wakipunga mkono kuwasalimia wananchi waliojitokeza kumlaki mgeni katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais Magufuli na mgeni wake Mhe. Modi wakipiga ngoma kuashiria furaha, mshikamano na ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya mataifa yao.
Rais Mhe. Dkt John Pombe Magufuli akiongoza kikao kilichofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam akiwa pamoja na mgeni wake Waziri Mkuu wa India na viongozi waandamizi wa Serikali za pande zote mbili. 
Waziri Mkuu wa India Mhe. Modi akiongea katika Kikao na Waandishi wa habari ambapo alieleza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na India na pia aliahidi Serikali yake itaendelea kutoa ushirikiano katika sekta ya Afya, Elimu, Maji na Teknolojia ya Habari, pamoja na kuzidi kuibua maeneo mapya ya ushirikiano. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dktr. John Pombe Magufuli akiongea katika kikao na Waandishi wa Habari, ambapo alisema Serikali ya Tanzania itazidi kuimarisha ushirikiano na Serikali ya India hasa katika masuala ya kiuchumi ili kuweza kuboresha maisha ya wananchi wa mataifa yao.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Mhe. Modi mara baada ya kumaliza vikao na mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Ziara ya Waziri Mkuu wa India nchini Tanzania


Serikali ya India imeahidi kuipatia Tanzania msaada wa Dola za Marekani milioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kipaumbele ili kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2020. 

Hayo yameelezwa leo Ikulu jijini Dar es Salaam na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli mara baaada ya kufanya mazungumzo na mgeni wake, Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi. Mhe. Modi aliwasili nchini jana kwa ziara ya Kitaifa ya Siku mbili.


Rais Magufuli alieleza kuwa Tanzania na India zina uhusiano mzuri wa kihistoria ambao umekuwa na faida za kijamii na kiuchumi kwa pande zote mbili. Alitoa mfano namna India ilivyofadhili ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya maji katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 178. 

Aidha, Rais Magufuli aliishukuru Serikali ya India kwa kuridhia kutoa kiasi kingine cha Dola za Marekani milioni 92 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji kisiwani Zanzibar.  Rais Magufuli alielezea pia kuridhishwa na kiwango cha biashara kati ya Tanzania na India ambacho kimekuwa kikiongezeka mwaka hadi mwaka.

 Alisema kwa mwaka 2009, Tanzania iliiuzia India bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 187, kiwango hicho kimeongezeka na kufikia Dola za Marekani bilioni 1.29 mwaka 2015.


Viongozi hao wakiwa katika mazungumzo rasmi, walikubaliana kushirikiana katika sekta mbalimbali zikiwemo za kilimo, viwanda, afya, nishati na madini.


Kwa upande wa Kilimo, Rais Magufuli alitoa wito kwa wakulima wa Kitanzania kuongeza uzalishaji wa mazao ya jamii ya kunde hususan dengu kwa kuwa yana soko kubwa nchini India. Alisema India ni soko kubwa la  mazao hayo na imeahidi kusaidia pembejeo za kilimo ili kuongeza kiwango cha uzalishaji.


Kwa upande wa viwanda, mashirika ya viwanda vidogo ya India na Tanzania yamewekeana saini mkataba ambapo mashirika hayo yatafanya tathmini nchi nzima ya kubaini rasilimali zilizopo katika maeneo mbalimbali na aina ya viwanda vidogo vinavyoweza kuanzishwa kwenye maeneo hayo. Baada ya tathmini hiyo, Serikali ya India itatoa mkopo nafuu kwa ajili ya kujenga antamizi (incubators) za viwanda vidogo nchi nzima. Kupitia antamizi hizo, wananchi watapatiwa mafunzo maalum ya uzalishaji wa bidhaa, biashara na usimamizi wa fedha na baadaye kupewa mitaji kwa ajili ya kuanza shughuli za biashara.


Kwa upande wa sekta ya Afya, Rais Magufuli alimuomba Waziri Mkuu wa India kushawishi wawekezaji kuja kuwekeza nchini katika uzalishaji wa dawa za binadamu na vifaa tiba. “Nimemuomba Mhe. Modi na amekubali kuleta wawekezaji kuzalisha madawa na vifaa tiba hapa nchini. Hiyo itaipunguzia Serikali mzigo mkubwa wa matumizi ya fedha za kigeni kutokana na uagizaji wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi. 

Sambamba na hilo, Rais Magufuli ameshukuru Serikali ya India kwa kuipatia Hospitali ya Bugando mashine maalum kwa ajili ya kupima ugonjwa saratani. Mashine hiyo inatarajiwa kuwasili nchini wakati wowote kuanzia sasa.


Kuhusu sekta ya nishati na madini, viongozi hao walikubaliana kushirikiana katika kuendeleza sekta hiyo hapa nchini. Tanzania ina utajiri mkubwa wa gesi asilia  ikiwemo Helium na madini. Hivyo ni vizuri tukishirikiana na wenzetu kuendeleza sekta hiyo.  


Rais Magufuli alihitimisha taarifa yake kwa kueleza kuwa wameazimia kushirikiana na India katika ngazi za kitaifa, kikanda na kimataifa kuhakikisha kuwa pamoja na mambo mengine, mabadiliko ya mfumo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yanafanyika ili liwe na uwiano mzuri wa uwakilishi. Aidha, wameahidi kusaidiana katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo ni tishio kubwa kwa maendeleo endelevu ya dunia ya sasa.


Waziri Mkuu wa India alikuwa katika ziara yake ya pili barani Afrika tangu kuchaguliwa kwake mwaka 2014 ambapo alitembelea nchi za Msumbiji, Afrika Kusini, Tanzania na atahitimisha ziara yake nchini Kenya.  


Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Dar es Salaam, 10 Julai 2016.



Waziri Mkuu wa India awasili nchini

Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi akipunga mkono  kusalimia wananchi waliojitokeza kumlaki mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mhe. Modi atakuwa nchini kwa ziara ya siku mbili kuanzia tarehe 09-10 Julai, 2016
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akisalimiana na Mhe. Modi mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Mhe. Modi mara baada ya kuwasili nchini. 
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda akisalimiana na Mhe. Modi mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Balozi Mbelwa Kairuki akisalimiana na Mhe. Modi mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege.

Kaimu Mkuu wa Itifaki katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. James Bwana (wa kwanza kulia) akiwaongoza Waheshimiwa Mawaziri Wakuu wakati wa mapokezi 
Mhe. Modi akipunga mkono kuwasalimia wananchi waliojitokeza kumlaki katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere

Friday, July 8, 2016

WAZIRI MAHIGA AZUNGUMZIA ZIARA WA WAZIRI MKUU WA INDIA NCHINI


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) akizungumza katika Mkutano na wanahabari kuhusu ziara ya Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi anayetarajiwa kuwasili nchini kwa ziara ya siku mbili kuanzia tarehe 9-10 Julai, 2016. Mkutano huo ulifanyika leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. Katikati ni Naibu Waziri  wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Susan Kolimba na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Aziz P. Mlima. 
Mstari wa mbele ni baadhi ya Mabalozi na Wakurugenzi kutoka Wizarani wakifuatilia Mkutano 

Katibu Mkuu Balozi Dkt. Aziz P. Mlima (katikati) akifafanua jambo wakati wa Mkutano na wanaandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam. 
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara Bi. Mindi Kisiga akifafanua jambo kwenye Mkutano na Wanahabari.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Paul Makonda (wapili kushoto) akitoa maelekezo juu ya masuala mbalimbali kuhusu ziara ya Waziri Mkuu wa India Nchini Mhe. Narendra Modi wakati wa Mkutano na Wanahabari uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam Julai.

Tuesday, July 5, 2016

Prof. Mbarawa afungua Semina kuhusu Maendeleo ya Viwanda

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (Mb.) akihutubia kwenye ufunguzi wa Semina ya Kimataifa kati ya China na Afrika kuhusu ushirikiano wa kuendeleza viwanda inayofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam Julai 5, 2016.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt Susan Kolimba (Mb.) akitoa hotuba kwenye ufunguzi wa semina ya Kimataifa kati ya China na Afrika kuhusu ushirikiano wa kuendeleza viwanda inayofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Balozi wa China hapa nchini, Mhe. Lu Youqing  naye akihutubia kwenye ufunguzi wa Semina hiyo
Baadhi ya Wadau walioshiriki katika Semina ya Kimataifa kati ya China na Afrika kuhusu ushirikiano wa kuendeleza viwanda  iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam wakifuatilia jambo. Mstari wa mbele kutoka kulia ni Prof. Ibrahim Lipumba, Prof. Moshi na Dkt. Reginald Mengi
Baadhi ya Wakuu wa Idara/Vitengo kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia semina hiyo. Kutoka kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu, Bw. Paul Kabale; Mkurugenzi wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi, Bw. Lucas Suka; Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria, Balozi Baraka Luvanda; na Mkurugenzi Idara ya Diaspora, Balozi Anisa Mbega.
Sehemu nyingine ya Wakuu wa Idara/Vitengo kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Wa pili kutoka kulia ni mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Balozi Mbelwa Kairuki, na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali watu, Bw. Nigel Msangi nao wakisikiliza kwa makini hotuba zilizokuwa zikiendelea kutolewa kwenye Semina hiyo
Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala na Usimamizi wa Raslimali watu, Bw. Hamid Mbegu; Mkurugenzi wa Miundombinu ya Kiuchumi na Huduma za Kijamii, Bw. Eliab Chodota na Mkuu wa Kitengo cha Teknologia ya Mawasiliano, Bibi. Achentalika Maunda wakifuatilia jambo wakati wa Semina.
Katibu wa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (tai nyekundu), Bw. Adam Isara naye akisikiliza hotuba za ufunguzi katika semina hiyo
Sehemu ya Washiriki wa Semina ya Kimataifa kati ya China na Afrika kuhusu ushirikiano wa kuendeleza viwanda iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam wakifuatilia Jambo.
Sehemu ya Waandishi wa Habari walio hudhuria ufunguzi wa Semina ya Kimataifa kati ya China na Afrika kuhusu ushirikiano wa kuendeleza viwanda wakitekeleza majukumu yao
Mhe. Kolimba na akijadiliana jambo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz Mlima wakati wa Ufunguzi wa Semina ya Kimataifa kati ya China na Afrika kuhusu ushirikiano wa kuendeleza viwanda
Naibu Waziri, Mhe. Suzan Kolimba akizungumza na Chombo cha Habari cha Kimataifa cha CCTV na kuelezea Faida na Madhumuni ya Semina hiyo
Picha ya pamoja mara baada ya kumaliza Ufunguzi wa Semina






TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Semina kuhusu Maendeleo ya Viwanda

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) amesema kuwa bila ya ujenzi wa miundombinu ya uhakika, Tanzania haitaweza kutimiza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025.

Alitoa kauli hiyo leo, wakati wa semina ya maendeleo ya viwanda iliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Ubalozi wa China na kufanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Mhe. Waziri alisema kuwa ili miundombinu imara iweze kujengwa nchini, katika mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga kiasi cha Shilingi trilioni 11.8 kwa ajili ya bajeti ya maendeleo na kati ya hizo asilimia 46 ni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu. “Asilimia 46 ya bajeti ya maendeleo ni kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa miradi ya miundombinu mbalimbali kama barabara, reli ya kiwango cha kimataifa, ununuzi wa ndege na meli”.  

Prof. Mbarawa aliyashukuru makampuni ya China kwa kuwekeza nchini katika miradi mbalimbali mikubwa lakini bado alitoa wito kwa makampuni mengine kutoka nchi hiyo kuja  kuwekeza kwa wingi hapa nchini.

Aliyashauri makampuni kutoka nchini China yaje kuingia ubia na makampuni ya hapa nyumbani katika uendelezaji wa miradi mbalimbali kama ya reli barabara na nishati. Aliendelea kueleza kuwa ili kuendeleza sekta ya viwanda nchini, tunahitaji msaada wa mtaji, utaalamu na elimu ya ufundi kutoka kwa marafiki zetu kama nchi ya China.

Aidha, Prof. Mbarawa alisisitiza umuhimu wa kuboresha kiwango cha uzalishaji katika sekta ya kilimo ambayo ndio imeajiri Watanzania wengi hapa nchini. “Sekta ya kilimo imekuwa ikikua kwa asilimia 4 hadi 5 hapa nchini lakini ukuaji huo haujajikita hasa katika kiwango cha uzalishaji (productivity)”. Prof. Mabarawa alisema ili watu wetu waweze kufaidika na kilimo lazima kiwango cha uzalishaji kiboreshwe na  Serikali ya awamu ya tano imejipanga kulifanyia kazi suala hilo.

Mhe. Waziri alihitimisha hotuba yake kwa kuahidi kuwa Serikali itazingatia utunzaji wa mazingira itakapokuwa inatekeleza ujenzi wa miradi mikubwa ya maendeleo iliyomo kwenye Mwaka wa Fedha 2016/2017 na miaka mingine itakayofuata.

Akizungumza awali, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Suzan Kolimba (Mb) aliishukuru Serikali ya Watu wa China kwa kuendelea kuiunga mkono Tanzania kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo. Alirejea dhamira ya Serikali ya Tanzania ya kushirikiana na China hususan katika Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika (FOCAC). Alisema Tanzania kuchaguliwa kuwa miongoni mwa nchi 4 ambazo China itahamishia viwanda vyake ni ushahidi wa wazi kuwa nchi hizi mbili zina uhusiano mzuri wa kihistoria.

Kwa upande wake, Balozi wa China nchini Tanzania, Dkt. Lu Youqing alisisitiza umuhimu wa kukuza sekta ya viwanda hapa nchini. Alisema sekta ya viwanda ikikua, itapelekea kufikiwa kwa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025, itaongeza ajira, mapato ya Serikali na hivyo kuifanya nchi kujitegemea kifedha. Alimalizia kwa kuihakikishia Tanzania kuwa nchi yake itatimiza yale yote iliyoyaahidi kwenye Mkutano wa FOCAC uliofanyika Afrika Kusini mwaka 2015.