Wednesday, April 25, 2018

Ufunguzi rasmi wa maonesho ya kipekee ya bidhaa za viwanda vya Tanzania nchini Kenya


Waziri wa Kilimo na Umwagiliaji wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Mwangi Kiunjuri akikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa wiki ya Tanzania nchini Kenya ambayo imeambatana na maonesho ya huduma, vivutio vya utalii na bidhaa za viwanda vya Tanzania yanayofanyika kuanzia tarehe 25 hadi 28 Aprili 2018 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (KICC) Jijini Nairobi, Kenya.


Mhe. Waziri Kiunjuri akihutubia wageni waalikwa (hawapo pichani) katika hafla ya ufunguzi wa Wiki ya Tanzania nchini Kenya ambayo itaenda sambamba na Maonesho ya bidhaa za viwanda, Kongamano la biashara na Maadhimisho ya miaka 54 ya Muungano wa Tanzania. Hafla hiyo imefanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Kenyatta (KICC) jijini Nairobi, Kenya tarehe 25 Aprili 2018.

Mhe. Wanjuri katika hotuba yake amesisitiza umuhimu wa kilimo cha kisasa ili kupata mazao yatakayokidhi vigezo vya ubora na kuingia katika ushindani wa biashara kimataifa utakaopelekea maendeleo ya uchumi hususan uchumi wa viwanda.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Hassan Khamis Hafidh akihutubia katika hafla ya ufunguzi wa Wiki ya Tanzania nchini Kenya ambapo alieleza kuwa tukio hili ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya marais wa Tanzania na Kenya walipokutana katika Mkutano wa 19 wa Kawaida wa Wakuu wa nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Pindi Chana akiwakaribisha wageni waalikwa katika hafla ya ufunguzi rasmi wa wiki ya Tanzania nchini Kenya.
Katika ufunguzi huo Mhe. Chana alieleza  umuhimu wa maonesho hayo ni pamoja na kuzitangaza huduma na bidhaa za viwanda  vya Tanzania ili ziweze kupenyeza katika soko la Kenya. Maonesho hayo yametoa fursa kwa wafanyabiashara kutoka Tanzania kukutana na kufanya mazungumzo ya biashara na wafanyabishara kutoka katika kampuni za Kenya.

Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Katibu wa kamati ya maandalizi ya Wiki ya Tanzania nchini Kenya, Balozi Anisa Mbega  na mjumbe kutoka Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Francis Mossongo wakifuatilia hafla ya ufunguzi.

Sehemu ya wafanyabiashara kutoka Tanzania wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa hafla hiyo. 
Sehemu nyingine ya wafanyabiashara wakifuatilia hafla ya ufunguzi huo.



Sehemu ya Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa  nchini Kenya wakifuatilia hafla ya ufunguzi.

Sehemu nyingine ya Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa  nchini Kenya wakifuatilia hafla ya ufunguzi.

Wajumbe kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii wakifuatilia hafla hiyo.
 =======================================================================
Wakati huo huo Mhe. Waziri Kiunjuri alitumia fursa hiyo kukabidhi vyeti kwa washiriki pamoja na kutembelea mabanda ya maonesho.

Mhe. Waziri Kiunjuri akikabidhi cheti cha ushiriki kwa mwakilishi wa kampuni ya Lake Group, Bw. Peter Sifa

Mhe. Waziri wa Kiunjuri akimkabidhi cheti cha ushiriki mwakilishi kutoka Kampuni ya vinywaji (Tanzania Distillers Ltd)
Mhe. Waziri Kiunjuri akikabidhi cheti cha ushiri kwa mmoja wa wafanyabiashara kutoka Zanzibar, Bw. Nassoro Omar wa Kampuni ya ZANOP.
Mhe. Kiunjuri akimkabidhi cheti mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya maonesho na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TANTRADE),  Bw. Edwin Rutageruka.

Mhe. Waziri Kiunjuri akimkabidhi cheti Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) na mwenyekiti mwenza wa kamati ya maandalizi ya Wiki ya Tanzania nchini Kenya, Bw. Godfrey Simbeye kwa kufanikisha zoezi la uratibu wa wiki hiyo.

Mhe. Waziri Kiunjuri akipokea maelezo kwa mmoja wa washiriki wa maonesho ya bidhaa kutoka Tanzania, Bw. Amir Esmail kutoka kampuni ya kahawa ya AMIMZA.

Mwambata Jeshi wa Ubalozi wa Tanzania, India apandishwa cheo

Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka H. Luvanda akimvalisha cheo cha Brigedia Jenerali A.S Mwami ambaye ni Mwambata Jeshi wa Ubalozi wa Tanzania nchini India.Brigedia Jenerali A.S Mwami ni miongoni mwa Maafisa Wakuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania ambao Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliwapandisha vyeo tarehe 12 Aprili, 2018. Awali Brigedia Jenerali Mwami alikuwa na cheo cha Kanali. Hafla hiyo fupi imefanyika katika Ubalozi wa Tanzania nchini India na  kuhudhuriwa na watumishi wa ubalozi huo.
Brigedia Jenerali Mwami akiwa kwenye picha ya pamoja na familia yake.
Balozi Baraka Luvanda akiwa katika picha ya pamoja na Brigedia Jenerali A.S Mwami
Balozi Luvanda pamoja na Brigedia Jenerali A.S Mwami wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini India.



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU ZIARA YA RAIS WA BENKI YA AfDB NCHINI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Taarifa kuhusu ziara ya Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika nchini
Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Ayodeji Adesina atafanya ziara ya siku nne (4) nchini kuanzia tarehe 25 hadi 28 Aprili, 2018 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Lengo la ziara ya Dkt. Adesina nchini ni kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Benki hiyo ambayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya miradi ya miundombinu nchini.
Akiwa nchini, Mhe. Dkt. Adesina ataonana kwa mazungumzo rasmi na Mhe. Rais Magufuli pamoja na kuzindua Barabara kutoka Dodoma kwenda Babati hafla itakayofanyika katika eneo la Mradi wa Barabara wa Mayamaya-Mela-Bonga Wilayani Kondoa.
Aidha, Dkt. Adesina atatembelea Mtambo wa Kusafirisha Umeme wa Iringa kwenda Shinyanga pamoja na Kituo Kidogo cha Umeme cha Zuzu cha Mkoani Dodoma.
Dkt. Adesina ambaye ameambatana na Makamu wa Rais wa Benki hiyo anatarajiwa kushiriki Maadhimisho ya Miaka 54 ya Muungano wa Tanzania yatakayofanyika Mkoani Dodoma tarehe 26 Aprili, 2018.
Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazoongoza kwa kupokea misaada kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Benki hiyo (ADF). Aidha, tangu kuanzishwa kwa Benki hiyo hapa nchini mwaka 1971, Tanzania imenufaika kwa kiasi cha zaidi ya Dola za Marekani bilioni 3.5 huku miradi ya maendeleo ya miundombinu ikipewa kipaumbele.
Aidha, hadi kufikia mwezi Novemba 2017 Benki ya Maendeleo ya Afrika imekuwa ikitekeleza miradi 25 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 1.9. Kati ya miradi hiyo, 22 ni ya Sekta ya Umma yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.8 huku miradi mitatu (3) ikiwa chini ya Sekta Binafsi kwa thamani ya Dola za Marekani milioni 187.0.
Kati ya miradi yote, miradi ya maendeleo ya miundombinu inachukua asilimia 73 ambapo kati yake miradi ya Barabara ni asilimia 51, Maji na Usafi wa Mazingira asilimia 12 na Nishati asilimia 10. Asilimia 27 zilizosalia zinasaidia miradi ya sekta binafsi hususan katika kilimo na ustawi wa jamii.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 24 Aprili, 2018
-Mwisho-
 

Monday, April 23, 2018

Naibu Waziri akutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Bunge la Afrika

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Susan Kolimba akisalimiana na Rais wa Bunge la Afrika Mhe.Roger Nkodo Dang Wizarani Mjini Dodoma.

Mhe. Dang amekuja nchini kwa lengo la kuishukuru Serikali kwa ushirikiano iliompa katika kipindi chote ambacho amelitumikia hilo.

Mhe.Dang anakaribia kumaliza muda wake wa kipindi cha miaka miwili wa kutumikia nafasi hiyo.  
Naibu Waziri Mhe. Dkt. Susan Kolimba akimsikiliza  Rais wa Bunge la Afrika Mhe.Roger Nkodo Dang


Saturday, April 21, 2018

Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje na Balozi wa China nchini wazungumzia maandalizi ya Mkutano wa FOCAC

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda akizungumza na Balozi wa China nchini, Mhe. Wang Ke kuhusu Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jukwaa la Ushirikiano wa Afrika na China (FOCAC) utakaofanyika mwezi Septemba, 2018 nchini China. Mkutano huo ambao utajadili masuala mbalimbali kwa maendeleo ya Bara la Afrika utatanguliwa na vikao vya maafisa waandamizi na vile vya mawaziri. Kikao kati ya Prof. Mkenda na Balozi Wang Ke kimefanyika Wizarani tarehe 21 Aprili, 2018
Maafisa kutoka Ubalozi wa China nchini wakifuatilia mazungumzo kati ya Prof. Mkenda na Balozi Wang Ke (hawapo pichani)
Prof. Mkenda akimsikiliza Balozi Wang Ke alipokuwa akimweleza kuhusu hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya Mkutano wa FOCAC utakaofanyika mwezi Septemba, 2018 nchini China
Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki nao wakifuatilia mazungumzo kati ya Prof. Mkenda na Balozi Wang Ke (hawapo pichani). Kulia ni Bi. Berha Makilagi na Bw. Halmesh Lunyumbu.
Mkutano ukiendelea
Picha ya pamoja

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU ZIARA YA WAZIRI WA SHERIA WA ISRAEL NCHINI




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 

Taarifa kuhusu ziara ya Waziri wa Sheria wa Israel nchini

Waziri wa Sheria wa Israel, Mhe. Ayelet Shaked atafanya ziara ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 22 hadi 24 Aprili, 2018. 

Akiwa nchini, Mhe. Waziri Shaked ambaye anaongoza ujumbe wa wafanyabiashara na wawakilishi wa makampuni kutoka Israel atashiriki Kongamano la Tano la Biashara kati ya Tanzania na Israel litakalofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam tarehe 23 na 24 Aprili, 2018.

Kongamano hilo ambalo linalenga kuwakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Israel, litahusisha Sekta muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania ambazo ni pamoja na Kilimo, Viwanda, Afya, Nishati na Utalii. Aidha, kupitia Kongamano hilo wafanyabiashara katika sekta hizo watabadilishana mawazo baina yao pamoja na watendaji wa Serikali ili kufikia malengo waliyopanga.

Kongamano hilo linaratibiwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na Kingdom Leadership Network Tanzania (KLNT).

Pamoja na kushiriki katika Kongamano hilo, Mhe. Waziri Shaked ameomba miadi ya kukutana na Viongozi mbalimbali Serikalini akiwemo Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Aderladus Kilangi.

Kabla ya kuhitimisha ziara hiyo, Mhe. Shaked atakutana na vyombo vya habari tarehe 24 Aprili, 2018 kwa ajili kueleza mafanikio ya ziara yake nchini. Mhe. Shaked na ujumbe wake wataondoka nchini siku hiyohiyo kurejea Israel.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 21 Aprili, 2018
-Mwisho-

Friday, April 20, 2018

Balozi Shelukindo ahimiza wafanyabiashara kuchangamkia fursa za biashara Ufaransa.

Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa Mhe. Samuel Shelukindo akizungumza katika Mkutano na wafanyabiashara nchini, uliofanyika tarehe 20 Aprili,2018, katika Ukumbi wa Kimataifa wa  Mikutano (JNICC), Jijini Dar es Salaam. 
Pamoja na mambo mengine lengo la mkutano  huo ilikuwa kuelezea fursa za masoko nchini Ufaransa kwa wafanyabiashara wa Tanzania.
Mkutano huu ulitanguliwa na ziara ya siku mbili(2), tarehe 17 na 18 Aprili,2018, jumla ya wafanyabiashara 35 kutoka Ufaransa ambao walikuja nchini kuangalia fursa za uwekezaji. 

Akiongea katika Mkutano huo Mhe. Balozi Shelukindo alisema, kuna fursa nyingi sana nchini Ufaransa hasa katika mazao ya vyakula, mbogaboga na matunda hivyo Serikali iko tayari kusaidia pale msaada wa jinsi ya kufikia hayo masoko utakapohitajika. Naye Balozi wa Ufaransa nchini Mhe. Clavier ametoa rai kwa wafanyabiashara kuutumia Ubalozi wa Ufaransa hapa nchini kwa ajili ya kupata taarifa jinsi ya kulifikia soko la Ufaransa.

Kwa mujibu wa Balozi Shelukindo mazao yanayohitajika zaidi nchini humo ni asali, mbogamboga na matunda, viungo, nyanya, kahawa, samaki, chai na cacao.


Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Frederic Clavier akiongea na vyombo vya habari katika mkutano huo.
Sehemu ya wafanyabiashara wakiwa katika mkutano huo

Sehemu  ya wafanyabiashara wakiwa katika Mkutano
Mkurugenzi wa TanTrade Bw. Edwin Rutageruka, akifafanua jambo katika mkutano huo
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, Bw. Salvatory Mbilinyi akiongea katika Mkutano huo.

Bi. Mona Mahecha, Afisa Mambo ya Nje(wa kwanza) na wajumbe wengine wakifuatilia Mkutano
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Bi Mindi Kasiga ambaye alikuwa Mshehereshaji wa Mkutano huo akiongea jambo.
Mkutano ukiendelea
Balozi Clavier akiongea na vyombo vya habari baada ya Mkutano, pembeni yake ni Balozi Shelukindo akisikiliza.
Balozi Shelukindo na Balozi Clavier akiwa katika picha ya pamoja na wafanyabiashara baada ya Mkutano.