Thursday, May 10, 2018

Yanayojiri katika ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje nchini Israel

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Dkt, Mahiga atembelea taasisi ya Save the Children Haert ya Israel

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga ameshukuru Ushirikiano kati ya Taasisi ya Moyo ya Save the Children Heart ya Israel na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa kuokoa maisha ya watu wengi nchini, hususan watoto.

Waziri Mahiga alitoa shukrani hizo leo alipoitembelea taasisi hiyo jijini Tel Aviv, Israel akiwa anaendelea na ziara yake ya siku tatu aliyoianza jana. "Zamani nilijua kuwa mtu akizaliwa na maradhi ya kurithi, mtu huyo hawezi kuishi lazima atakufa, lakini uwepo wa taasisi yenu kumenifanya niondoe itikadi hiyo" Dkt. Mahiga alisema.

Taasisi ya Moyo ya Save the Children Heart imeisifu Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kuwa ni moja ya Taasi bora kusini mwa Jangwa la Sahara na kwamba ina uwezo na wataalam wa kufanya upasuaji bila ya kupeleka wagonjwa nje ya nchi. "Serikali inachotakiwa kufanya ni kuiboresha taasisi hiyo kwa kujenga majengo mapya na kuipatia vifaa zaidi na itakapofanya hivyo itaokoa maisha ya watu na fedha nyingi ambazo zingelitumika kugharamia matibabu nje ya nchi".  Mkurugenzi wa taasisi hiyo alishauri.

Mkurugenzi wa Taasisi hiyo alimweleza Dkt. Mahiga kuwa taasisi ilianzishwa miaka ya 90  kwa madhumuni ya kuokoa maisha ya watoto wenye maradhi ya moyo duniani kote, hususan katika nchi zinazoendelea. Hadi sasa imeshatoa matibabu kwa zaidi ya watoto 460,000 wenye maradhi ya moyo kutoka Afrika, Amerika, Asia na kwingineko.

Shughuli za taasisi hiyo inajumuisha kutibu wagonjwa, kutoa mafunzo kwa madaktari na wakufunzi na kusambaza madaktari katika nchi mbalimbali kuendesha upasuaji kwa kipindi maalum. Madaktari waliopewa mafunzo na taasisi hiyo wanaendelea kupata miongozo ya taasisi wanaporejea katika nchi zao kwa ajili ya kufanya matibabu.

Mhe. Waziri alipokuwa katika taasisi hiyo alipata fursa ya kuonana na Watanzania wanaosoma na wengine wanaopata matibabu ya maradhi ya moyo katika taasisi hiyo. Aidha, alioneshwa watoto wawili wanaougua maradhi ya moyo kutoka Nymmar na Romania ambao kwa mujibu wa Mkurugenzi alisema ndio wa kwanza kupokelewa kutoka nchi hizo.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Israel
10 Mei 2017


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe, Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) akiongea na wawakilishi wa Taasisi ya Moyo ya Save the Children Heart ya Israel mara baada ya kuwasili katika taasisi hiyo kujionea namna inavyoendesha shughuli zao. 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe, Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) akimjulia hali mmoja wa watoto kutoka Tanzania anayepata tiba ya maradhi ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Save the Children Heart ya Israel

Kutoka kulia, mtu wa kwanza na wa pili ni Watanzania wanaosomea fani za tiba za maradhi ya moyo katika taasisi ya Save the Children Haert wakiongea na Mhe. Waziri wakati alipoitembelea taasisi hiyo jijini Tel Aviv, Israel leo.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Save the Children Heart ya Israel akitoa maelezo kwa Mhe. Waziri hayupo pichani namna taasisi hiyo inavyofanya kazi.

Wanne kutoka kushoto ni wanafunzi kutoka Tanzania wanaosomea fani ya tiba ya maradhi ya Moyo wakimsikiliza Mkurugenzi wao hayupo pichani.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe, Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) akimkabidhi zawadi Mkurugenzi wa Taasisi ya Save the Children Heart/

Kaimu Mkurugenzi wa Mashariki ya Kati kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Suleiman Salehe akibadilishana mawasiliano na wanafunzi wanaosomea fani ya tiba ya maradhi ya moyo kutoka Tanzania.


Ulinzi wa Mpaka kwenye Ukanda wa Ghaza
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe, Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) akisalimiana na Afisa Usalama kutoka Kitengo cha Protection Unit alipowasili katika eneo la Netiv Haasara lililopo Ghaza ambapo ni mpakani na eneo la Palestina linalotawaliwa na Hamas.
Mkazi wa eneo la Netiv Haasara, Ghaza, Bibi Hila Fenton akitoa maelezo kwa Mhe. Waziri na wajumbe wengine kuhusu madhila wanayokutana nayo wananchi wa Israel wanaoishi karibu na mpaka wa Ghaza.



Bibi Hila Fenton akionesha mabaki ya gruneti la kwanza kabisa kurushwa kutoka Palestina na kuangukia kwenye eneo wanaloishi mwaka 2001/

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe, Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) akipokea maelekezo alipowasili eneo la mpaka katika ukanda wa Ghaza lililojengwa ukuta/
Wageni wanaofika katika eneo la mpaka huu wanaombwa kuandika ujumbe wa matumaini katika mawe yaliyotengenezwa kwa sanaa ya aina yake na kuyabandika kwenye ukuta unaozuia maguruneti kupita. Hapo Mhe, Waziri na Balozi wa Tanzania nchini Israel, Mhe. Job Masima wakibandika vijiwe vyenye ujumbe wa kuleta matumaini kwenye ukanda wa Ghaza.

Bi. Kisa Mwaseba naye akibandika ujumbe wake

Sehemu ya ukuta wa sengenge unaotenganisha mpaka wa Israel na Palestina katika Ukanda wa Ghaza.

Sehemu ya ukuta uliojengwa imara kuzuia vijiji vya Israel vilivyo mipakani visifikiwe na mashumbulizi ya magruneti.


Eneo la Ukaguzi wa Malori ya mizigo

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akipata maeleozo kutoka kwa Meneja wa Usalama wa ukaguzi wa malori ya mizigo yanayokwenda Palestina kutoka Israel na kinyume chake.

Meneja wa Usalama anatoa maelezo namna kazi ya kukagua malori ya mizigo inavyofanywa kwa uangalifu mkubwa ili kuzuia uwezekano wowote wa kupitisha vilipuzi au vifaa vya kuundia vilipuzi.

Baadhi ya Malori ya mizigoAdd caption

baadhi ya mizigo ambayo imekamilika kukaguliwa inasubiri kusafirishwa/Add caption

Eneo la ukaguzi wa maslori ya mizigo ambalo pia limejengewa ukuta kwa ajili ya kuzuia mashambulizi ya maguruneti.

Scanner inayotumika kukagua malori ya mizigo ambayo ina nguvu kubwa ya kubaini vifaa vilivyobebwa katika lori kimoja baada ya kingine. kutokana na nguvu ya scanner hiyo harusiwi mtu kukaa karibu inapofanya kazi. 

Waziri Mahiga akionesha moja ya mitambo iliyofungwa kwa ajili ya kuzuia bomu lisilipuke kabla halijasababisha madhara.



Wednesday, May 9, 2018

Katibu Mkuu akutana kwa mazungumzo na Kaimu Balozi wa Marekani nchini

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda akizungumza na Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Bi. Inmi Patterson alipofika Wizarani kwa ajili ya mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani.
Mazungumzo yakiendelea

Katibu Mkuu afanya mazungumzo na Balozi wa Vietnam nchini

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Adolf Mkenda amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Vietnam nchini Mhe. Nguyen Doanh, tarehe 09 Mei,2018, Jijini Dar es Salaam.

Balozi Doanh alitumia fursa hii kujitambulisha na kumpongeza Prof. Mkenda kwa kuteuliwa kuwa Katibu mkuu wa Wizara. Aidha,  mazungumzo hayo pia yalilenga kuboresha mahusiano yaliyokuwepo kati ya Tanzania na Vietnam, pia Prof.Mkenda amemhakikishia Balozi  ushirikiano  kipindi chote cha utekelezaji wa majukumu yake hapa nchini.
Balozi Doanh naye akifafanua jambo katika mazungumzo hayo.
Mazungumzo yakiendelea

Katibu Mkuu afanya mazungumzo na Balozi wa Ujerumani nchini

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda(kulia) akiwa katika mazungumzo na  Balozi wa Ujerumani nchini Mhe. Detlef Waechter alipomtembelea wizarani tarehe 9 Mei,2018, Jijini Dar es Salaam.

Pamoja na mambo mengine mazungumzo hayo yalilenga katika kuendelea kuboresha mahusiano yaliyopo kati ya Tanzania na Ujerumani.
Mazungumzo yakiendelea, wanaofuatilia mazungumzo hayo ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy( Katikati kulia), kushoto kwake ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, Bw. Justus Nyamanga na kulia kwake ni Afisa Mambo ya Nje, Bi Lilian Kimaro.



Dkt, Mahiga afungua Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania, Israel



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afriika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akikata utepe kuashiria ufunguzi wa ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Israel Ufunguzi huo ulifanyika jijini Tel Aviv tarehe 08 Mei 2018. Wengine katika picha ni Waziri wa Sheria wa Israel, Mhe. Bibi Ayelet Shaked na Balozi wa Tanzania nchini Israel, Mhe. Job Masima.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afriika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Sheria wa Israel, Mhe. Bibi Ayelet Shaked na Balozi wa Tanzania nchini Israel, Mhe. Job Masima.wakigongesheana glasi kwa ajili ya kuwatakia afya njema viongozi wa mataifa yao, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afriika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga wakisalimiana na Waziri wa Sheria wa Israel, Mhe. Bibi Ayelet Shaked walipowasili kwa ajili ya kushiriki ufunguzi wa ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Israel.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afriika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akiweka saini Kitabu cha Wageni baada ya kuwasili kwenye ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Israel kwa ajili ya kuzifungua rasmi. Anayemwangalia ni Waziri wa Sheria wa Israel, Mhe. Bibi Ayelet Shaked Add caption

Waziri wa Sheria wa Israel, Mhe. Bibi Ayelet Shaked akiweka saini Kitabu cha Wageni baada ya kuwasili kwenye ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Israel kwa ajili ya kushiriki ufunguzi rasmi wa ofisi hiyo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afriika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akibadilishana mawazo na Waziri wa Sheria wa Israel, Mhe. Bibi Ayelet Shaked walipowasili kwa ajili ya kushiriki ufunguzi wa ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Israel.

 caption

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afriika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akiwahutubia mamia ya watu hawapo pichani waliohudhuria hafla ya ufunguzi wa ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Israel. Pembeni yake ni Waziri wa Sheria wa Israel, Mhe. Bibi Ayelet.

Waziri wa Sheria wa Israel, Mhe. Bibi Ayelet Shaked akiwahutubia mamia ya watu hawapo pichani waliohudhuria hafla ya ufunguzi wa ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Israel. Kushoto ni Waziriwa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afriika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga na kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Israel, Mhe. Job Masima.

Balozi wa Tanzania nchini Israel, Mhe. Job Masima akiwahutubia mamia ya watu hawapo pichani waliohudhuria hafla ya ufunguzi wa ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Israel. Waliokaa ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afriika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga na Waziri wa Sheria wa Israel, Mhe. Ayelet Shaked.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afriika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watanzania wanaoishi Israel.



Bi. Kisa Doris Mwaseba (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Watanzania wanaoishi Israel.

Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani ambaye anaiwakilisha pia Tanzanaia nchini Uswisi, Mhe. Dkt. Abdallah Possi akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afriika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga katika Uwanja wa Ndege wa Zurich. Dkt. Possi alikuja kumpokea na kumsindikiza Mhe. Waziri akiwa njiani kuelekea Israel.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Dkt, Mahiga afungua Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania, Israel

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga amezindua rasmi ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Israel na kuitaka Israel nayo iharakishe kufungua ofisi ya ubalozi nchini Tanzania.

Ufunguzi wa ofisi hiyo ya ubalozi iliyopo katika mji wa Tel Aviv ulifanyika leo na ulihudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo Waziri wa Sheria wa Israel, Mhe. Ayelet Shaked, Mabalozi wa nchi za Afrika na Watanzania wanaoishi nchini humo.

Katika hotuba yake, Dkt. Mahiga aliitaja Israel kama nchi ya kupigiwa mfano kwa sababu licha ya changamoto za kimahusiano na baadhi ya jirani zake lakini bado nchi hiyo imepiiga hatua kubwa za kimaendeleo katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo cha umwagiliaji, viwanda, matibabu, TEHAMA, ulinzi na usalama, uhifadhi wa maji na masuala ya nishati ikiwemo nishati ya kutumia joto ardhi.

Kwa upande wa ulinzi na usalama, Waziri Mahiga alisema Watanzania hawataisahau Israel kwa kuwa ndiyo nchi iliyoisaidia Tanzania kuanzisha Jeshi la Kujenga Taifa ambalo mafanikio na mchango wa jeshi hilo unajulikana na kila Mtanzania. Alisema JKT baada ya lugha ya Kiswahili ndiyo chombo cha pili kilichosaidia kwa kiasi kikubwa kuunganisha makabila zaidi ya 120 ya Watanzania na kuwa wamoja hadi leo.

Dkt. Mahiga alieleza kuwa Israel ni nchi yenye mafanikio makubwa duniani ambapo imepelekea raia wake wengi kushinda tuzo za Nobel na hiyo imetokana na harakati zao kwa ajili ya wanadamu.

Aliishukuru Israel kufuatia mawaziri wake wawili kufanya ziara za kikazi nchini Tanzania hivi karibuni. Mawaziri hao ni Waziri wa Ulinzi, Mhe. Avigdor Liberman aliyetembelea Tanzania tarehe 20 hadi 22 Machi 2018 na Waziri wa Sheria, Mhe. Ayelet Shaked ambaye alikuwa nchini tarehe 23 na 24 Aprili 2018.

Katika ziara hizo masuala mbalimbali yaliafikiwa ikwemo Israel kuisaidia Tanzania kuanzisha chombo cha kutoa msaada wa kisheria kwa wasiojiweza ambacho kwa upande wa Israel kimeshaanzishwa na kina mafanikio makubwa.

Dkt.Mahiga aliwakaribisha Waisrael kuja Tanzania kwa ajili ya kufanya utalii kwa kuwa Tanzania ina vivutio lukuki vya utalii. Alisema zaidi ya watalii elf 50 wanakuja Tanzania kila mwaka lakini hawatoshi kutokana na uwingi wa vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

Kwa upande wake, Mhe. Shaked alibainisha kuwa Israel ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo kusaidia teknolojia ya kisasa kwenye kilimo ili kuongeza tija katika uzalishaji.
Aidha, Balozi wa kwanza wa Tanzania nchini Israel, Mhe. Job Masima alishukuru wadau wote ikiwemo Serikali ya Israel kwa kumpa ushirikiano wa kutosha uliofanikisha upatikanaji wa ofisi hiyo na kufunguliwa rasmi tarehe 08 Mei 2018. Aliwahakikishia umma uliohudhuria hafla hiyo na wadau wengine kuwa wasisite kufika kwenye ofisi hiyo kwa ajili ya kupata huduma watakazozihitaji.      
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Israel
09 Mei 2017


Tuesday, May 8, 2018

Balozi Mushy akutana na Mabalozi kutoka nchi zinazounda kundi la Unitedfor Consensus


       
     
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy(kulia) akisisitiza jambo kwa Balozi wa Italy Nchini Mhe. Roberto Mengoni(kushoto), kwenye mazungumzo na Mabalozi wa Nchi zinazounda kundi linaloitwa United for Consensus ambazo zinakaa na kujadiliana kwa pamoja kuhusu mabadiliko yanayotakiwa kufanyika katika Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa  ( UN Security Council), walipotembelea Wizarani, tarehe 08 Mei,2018, Dar es Salaam.

Mabalozi kutoka Nchi zinazounda kundi linaloitwa United for Consensus wakifuatilia mazungumzo hayo kutoka kulia ni Balozi wa Pakistan nchini, Mhe. Amir Mohamed Khan, balozi wa Hispania nchini, Mhe. Felix Costales, Balozi wa Canada nchini, Mhe. Alexander Leveque, Balozi wa Korea Kusini nchini, Mhe. Song Geum Yong na Mwisho ni Balozi wa Uturuki nchini, Mhe. Ali Davutaglu.
Mhe. Roberto Mengoni akifafanua jambo kwenye mazungumzo hayo.
Mkutano ukiendelea.
Picha ya pamoja baada ya mazungumzo.




Katibu Mkuu afanya mazungumzo na Kampuni ya kutengeneza magari ya Foton.

Katibu Mkuu  Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Adolf Mkenda amekutana na kufanya mazungumzo na Bw. Apple Sun, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Kutengeneza Magari ya Foton Motors Group Kenya,
 Mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Wizara, Tarehe 08 Mei,2018, Dar es Salaam.

Katika kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli za Tanzania mpya ya Viwanda na pia katika kuendelea kutekeleza Diplomasia ya Uchumi, Prof.Mkenda alitumia mazungumzo hayo kuishawishi kampuni hiyo kujenga kiwanda cha kutengeneza magari hapa nchini, Kampuni hiyo iwapo itajenga kiwanda hicho hapa nchini itachangia kwa kiwango kikubwa kuongeza ajira kwa Watanzania na pia kusaidia katika juhudi za kutunza mazingira kwani itapunguza uagizaji wa magari yaliyotumika ambayo huchangia katika uharibifu wa mazingira. 

Prof. Mkenda amewahakikishia ushirikiano kutoka Serikalini iwapo watajenga kiwanda hicho hapa nchini.Kampuni hiyo kutoka nchini China inatengeneza magari mbalimbali kama vile pick-up, magari ya kawaida, SUV, maroli, matrekta n.k yenye kutumia teknologia ya hali ya juu na  ubora mkubwa.   
Kwa sasa Kampuni hiyo ina Kiwanda cha kutengeneza magari (Assembling Plant) nchini Kenya. 

Naye Bw. Sun alisema Kampuni yake iko tayari kwa mazungumzo na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuona uwezekano wa kujenga Kiwanda hicho hapa nchini, hata hivyo kwa sasa wameishafungua ofisi ya uwakilishi hapa nchini. 

Bw. Justin Kisoka(Kushoto) na Bw. Bernard Msuya, Maafisa Mambo ya Nje kutoka Wizarani wakifuatilia Mkutano huo.
Bw. Apple Sun akisisitiza jambo katika mazungumzo hayo.


Mkutano ukiendelea

Picha ya Pamoja baada ya mazungumzo

Sunday, May 6, 2018

TAARIFA KWA VYOMBO HABARI


TAARIFA KWA VYOMBO HABARI
Waziri Mahiga kuzuru Israel
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) atafanya ziara ya kikazi nchini Israel kuanzia tarehe 07 hadi 10 Mei 2018. Ziara hiyo imekuja kufuatia mwaliko wa mwenyeji wake ambaye ni Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Mhe. Benjamin Netanyahu. Dkt. Mahiga anakuwa Waziri wa kwanza wa Mambo ya Nje kutoka Tanzania kufanya ziara nchini Israel.
Atakapowasili nchini Israel, Dkt. Mahiga atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Mhe. Netanyahu na kushiriki uzinduzi rasmi wa Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini humo.
Ikumbukwe Israel ni moja kati ya nchi sita ambazo Serikali ya awamu ya tano imefungua Balozi Mpya. Mhe. Job Masima aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kuwa Balozi wa kwanza wa Tanzania nchini humo.
Waziri Mahiga ataitumia ziara hiyo sio tu kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia uliopo bali pia kuishawishi Serikali ya Israel iunge mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa viwanda.
Israel ni moja ya nchi zenye maendeleo makubwa duniani katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, viwanda, uhifadhi wa maji, matibabu, ulinzi na usalama, mawasiliano na nishati ya joto ardhi. Hivyo kupitia ziara hiyo, agenda ya uchumi wa viwanda ya Tanzania inaweza kupata ushirikiano mkubwa wa Israel kutokana na hatua kubwa ya kimaendeleo iliyofikia.
Kabla ya Tanzania haijafungua ofisi ya Ubalozi Israel, ilikuwa inawakilishwa kupitia ubalozi wake Misri na Ubalozi wa Israel nchini Kenya unawakilisha pia Tanzania hadi sasa.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam
 06 Mei, 2018