Saturday, December 5, 2020

Tanzania yafungua ofisi ya Mwakilishi wa Heshima jijini Mumbai

Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda kwa pamoja na Mwakilishi wa Heshima Mteule wa Tanzania jijini Mumbai Bwana Nayan Patel wakisaini Mkataba wa Kazi wa kumwezesha Bwana Patel kuwa Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania katika mji huo. Mkataba huo ulisainiwa jijini Mumbai, India tarehe 04 Desemba 2020.
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda na Bwana Nayan Patel wakibadilishana Mkataba wa Kazi wa kumwezesha Bwana Patel kuwa Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania katika mji wa Mumbai.

Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania Jijini Mumbai Bwana Nayan Patel akihutubia katika hafla ya ufunguzi rasmi wa ofisi ya Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania Jijini humo iliyofanyika tarehe 04 Desemba 2020.

Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda akitoa hotuba kumpongeza Bwana Patel kwa kukubali kuiwakilisha Tanzania jijini Mumbai na kumtaka kuiwakilisha vema nchi.


Balozi wa Tamzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda na Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania Jijini Mumbai Bwana Nayan Patel wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wageni walioshriki halfla ya uwekaji saini wa Mkataba wa Kazi wa Mwakilishi wa Heshima.


-------------------------------------------------------------------------------
Na. Mwandishi Maalum, India

Tanzania yafungua ofisi ya Mwakilishi wa Heshima jijini Mumbai

Serikali ya Tanzania imefungua rasmi ofisi ya Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania katika Jiji la Mumbai katika hafla iliyofanyika jijini humo tarehe 04 Desemba 2020.

Mumbai ni jiji kuu la biashara na viwanda nchini India (commercial and industrial hub) ambapo linachangia zaidi ya asilimia 6 la pato la India na pia linachangia zaidi ya asilimia 25 ya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali za viwandani nchini India (25% of industrial output).

Aidha, Mumbai ni jiji mojawapo kati ya majiji kumi duniani, yanayoongoza kwa biashara, hususan katika mzunguko wa fedha duniani (global financial flow). Vilevile, Mumbai ni Jiji linaloongoza kuwa na mabilionea wengi nchini India, ambapo linashika nafasi ya 9 kuwa na mabilionea wengi duniani.

Kadhalika, shughuli za biashara na huduma za kifedha katika Jiji hilo lenye watu zaidi ya milioni 20 zinachangia mzunguko wa fedha katika uchumi wa India kwa zaidi ya asilimia 70.

 

Ni kutokana na umuhimu wa Jiji hilo, Serikali iliamua kusogeza karibu huduma za kikonseli, biashara, uwekezaji, utalii na mengineyo kwa kuwa na Mwakilishi wa Heshima atakayeratibu shughuli hizo kwa karibu. Ikumbukwe India ni nchi kubwa yenye uchumi mkubwa na idadi kubwa ya watu duniani wanaofikia bilioni 1.2. Hivyo, si rahisi kwa nchi zenye uwakilishi mjini New Delhi kuweza kuhudumia kwa ukamilifu nchini India bila kuwa na ofisi za aina hii.

 

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda alielezea juu ya umuhimu wa ofisi ya Mwakilishi wa Heshima jijini Mumbai kuwa itasaidia kutoa huduma za Kikonseli kwa karibu zaidi na pia itasaidia zaidi kuvutia na kutangaza fursa mbalimbali za biashara, uwekezaji zilizopo nchini, kutafuta masoko ya bidhaa za kilimo na viwanda vya Tanzania pamoja na vivutio mbalimbali vya utalii wa Tanzania ili kukuza sekta ya utalii nchini.

Aidha, Balozi Luvanda alieleza kuwa ofisi hiyo itachangia katika kukuza biashara zaidi kati ya Jiji la Dar es Salaam na Mumbai kufuatia kuimarishwa kwa huduma za usafiri wa anga baada ya Shirika la Ndege la Tanzania (Air Tanzania) kuanza safari zake za ndege za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam kwenda Mumbai tangu mwezi Julai 2019. Vilevile, majiji haya yanaunganishwa na bandari kuu muhimu ambazo ni Bandari ya Dar es Salaam, kwa upande wa Tanzania, na Bandari ya Mumbai, kwa upande wa India.

 

Bwana Nayan Patel, ni raia wa India na mfanyabiashara mwenye mtaji mkubwa jijini Mumbai na amekwishaanza rasmi kazi ya Uwakilishi wa Heshima baada ya kukamilika kwa taratibu zote za kidiplomasia. 

 

Bwana Patel aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kumpa heshima kubwa ya kuiwakilisha Tanzania jijini Mumbai na maeneo mengine ya jirani na akaahidi kuitendea haki nafasi hiyo kadri atakavyoweza.


Friday, December 4, 2020

WIZARA YA MAMBO YA NJE YAJIPANGA KUWAJENGEA UWEZO WA KAZI WATUMISHI WAKE

Mkurugenzi wa Kitengo cha Dispora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Anisa Mbega akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brig. Gen. Wilbert Ibuge wakati wa ufunguzi rasmi wa Awamu ya Kwanza ya  Mafunzo Maalum kwa Maafisa Waandamizi wa Wizara kuhusu Utaalamu katika Uchambuzi wa masuala mbalimbali (Analytical Skills). Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo Maafisa hao ili kuboresha utendaji kazi wao wa kila siku. Kadhalika, Mafunzo hayo ambayo yalifanyika jijini Dodoma hivi karibuni, yaliandaliwa na Wizara kwa kushirikiana na Taasisi ya UONGOZI na Shirika la UNDP.

Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Peter Pinda akizungumza na mmoja wa Washiriki wa Mafunzo hayo alipotembelea eneo hilo akiwa kwenye shughuli zake za ujenzi wa Taifa na kuwasalimia Washiriki 

Sehemu ya Washiriki wa Mafunzo ya Utaalam katika Uchambuzi wakifurahia jambo

Washiriki wengine wakiwa tayari kuanza kujifunza mbinu mbalimbali za kufanya uchambuzi

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo akiwasilisha Mada kwa Washiriki kuhusu "Umuhimu wa Uchambuzi katika Kufanya Maamuzi".

Sehemu ya Washiriki wakimsikiliza Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Singo (hayupo pichani) 

Sehemu nyingine ya Washiriki wakifuatilia mafunzo

Mwezeshaji kutoka Taasisi ya UONGOZI, Bibi Zuhura Muro akiwasilisha Mada kwa Washiriki kuhusu "Umuhimu wa Kutumia Akili Hisia (Emotional Intelligence) katika Uongozi". 

Mmoja wa Washiriki, Bw. Suleiman Magoma akichangia jambo wakati wa mafunzo hayo

Mwezeshaji kutoka Taasisi ya UONGOZI, Prof. Joseph  akiwasilisha Mada kwa Washiriki kuhusu "Umuhimu wa Uchambuzi katika Kutafuta Suluhisho la Matatizo mbalimbali".

Mmoja wa Washiriki, Bw. Ismail akieleza jambo kwa Washiriki wenzake ikiwa ni sehemu ya Washiriki kufanyia kazi yale waliyojifunza 

Washirki wakiwa kwenye mjadala

Sehemu nyingine ya Washiriki wa Mafunzo hayo.

 

TANZANIA, INDONESIA ZAAHIDI KUENDELEA KUKUZA BIASHARA

 Tanzania na Indonesia zimeahidi kushirikiana na kuendeleza kukuza biashara kwa kuanzisha kwa manufaa ya nchi zote mbili.  

Akihutubia katika usiku wa shukrani kwa ajili ya wafanyabiashara wa Tanzania na Indonesia kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kukuza biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili, Balozi wa Indonesia nchini Tanzania Mhe. Prof. Ratlan Pardede amesema kuwa maendeleo yaliyopatika kwenye sekta ya biashara nzuri inayofanywa na wafanyabiashara kutoka nchi zote mbili.

"Sisi Indonesia na Tanzania tumekuwa tukifanya biashara yenye manufaa kwa mataifa yetu mawili, bidhaa tunazouza ni imara na zimekuwa na ubora mzuri ambapo kwa sasa biashara imeongeza mapato zaidi ya asilimia 10," Amesema Balozi Pardede  

Ameongeza kuwa mwaka 2017 aliahidi kuwaleta wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Indonesia kuja Tanzania kwa ajili ya kuwekeza, ambapo hadi sasa tayari wameanzisha kiwanda cha Sabuni na Losheni Mkuranga

Kwa upande wake Mgeni Rasmi, ambaye ni Waziri wa Biashara na Uwekezaji kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga amempongeza Balozi kwa hatua na mipango mizuri ya kuinua uchumi wa mataifa yote mawili na kumuahidi ushirikiano katika kuhakikisha kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuwaboreshea mazingira wawekezaji na wafanyabiashara ili kuwawezesha kufanya biashara vizuri katika mazingira salama.

Nataka nikuhakikishie kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara kati ya Indonesia na Tanzania kwa kiwango cha juu." Amesema Soraga. Pia Mhe. Waziri alielekeza wakati mwingine Baraza la kuundwe Biashara la Tanzania na Indonesia (TIBC) ili mpango huo uweze kujumuisha zaidi na kuwafikia wadau wengi nchini Tanzania.

Kulingana na rekodi za Ubalozi wa Indonesia, bidhaa takribani 54 za Kiindonesia zipo kwenye soko la Tanzania kama vile mafuta ya Mawese, nguo, karatasi pamoja na sabuni. Kwa upande mwingine, Indonesia imekuwa ikiagiza bidhaa kadhaa kutoka Tanzania, ambazo ni karanga, pamba, kakao, kahawa, chai, viungo na tumbaku.

Balozi wa Indonesia nchini Tanzania Mhe. Prof. Ratlan Pardede akiongea na wafanyabiashara (hawapo pichani) katika hafla ya usiku wa shukrani kwa ajili ya wafanyabiashara wa Tanzania na Indonesia iliyofanyika jana Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Biashara na Uwekezaji kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga akihutubia hadhara ya wafanyabiashara (hawapo pichani) katika hafla ya usiku wa shukrani kwa ajili ya wafanyabiashara wa Tanzania na Indonesia iliyofanyika jana Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Biashara na Uwekezaji kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Soraga akipokea zawadi kutoka kwa Balozi wa Indonesia nchini Tanzania Mhe. Pardede jijini Dar es Salaam   


Waziri wa Biashara na Uwekezaji kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Soraga (katikati) akiwa pamoja na Balozi wa Indonesia nchini Tanzania Mhe. Pardede katika picha ya pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia Bw. Caesar Waitara (kushoto) na Afisa Mkuu Mambo ya Nje, Bw. Francis Luangisa jijini Dar es Salaam   


Washiriki (wafanyabiashara) wakifuatilia mkutano  


Baadhi ya Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Waziri Bw. Soraga pamoja na Mhe. Balozi, Pardede



Ubalozi wa Tanzania, Qatar Washiriki Tamasha la Kumi la Kiasili la Majahazi

Ubalozi wa Tanzania Qatar ukishirikiana na Wanadiaspora kutoka Tanzania unashiriki kwenye Tamasha la Kumi la Kiasili la Majahazi lijulikanalo kama 10th Katara Traditional Dhow Festival.Tamasha hilo  linafanyika Doha kuanzia tarehe 1-5 Disemba 2020 ambapo Tanzania inaelezea utamaduni wa kiasili wa jahazi wa mwambao wa Afrika Mashariki na Zanzibar ambapo ndio kitovu cha utamaduni huo. 

Utamaduni huo ulipelekea kuibuka muingiliano wa utamaduni wa lugha, mavazi, chakula na dini pamoja na matumizi ya Majahazi. Ubalozi umepata fursa pia ya kutangaza bidhaa za kitanzania kama viungo(spices) asali, korosho na kahawa pamoja na kutangaza utalii wetu. 

Mgeni Rasmi, Mhe. Hamad bin Abdulaziz Al Kawari, Waziri wa Nchi na Mkurugenzi wa Maktaba ya Taifa pamoja na Meneja Mkuu wa kijiji hicho cha Katara, Dr. Khalid bin Ibrahim Al Sulaiti  wakipata maelezo kwenye banda la Tanzania walipotembelea wakati wa uzinduzi wa Tamasha hilo.

Mabalozi wa Nchi za Afrika Mashariki waliopo Qatar wakiwa katika picha ya pamoja kwenye Banda la Maonesho la Tanzania

 

Thursday, December 3, 2020

HABARI KATIKA PICHA MATUKIO MBALIMBALI ALIYOFANYA PROF. KABUDI

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akipokea barua ya pongezi kutoka kwa Balozi wa Ufaransa hapa Nchini Mhe. Frederic Clavier  iliyoandikwa na  Rais wa Ufaransa Mhe. Emmanuel Macron kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kumpongeza kwa Tanzania kuingia katika uchumi wa kati


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akiteta jambo na Balozi wa Ufaransa hapa Nchini Mhe. Frederic Clavier katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam



Msajili wa Mahakama ya Kimataifa ya Kesi Masalia za Mauaji ya Kimbari (International Residual Mechanism for Criminal Tribunals -IRMCT) Bw. Abubacar Tambadou akimsikiliza Prof. Palamagamba John Kabudi wakati walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akiwa katika picha ya pamoja na Msajili wa Mahakama ya Kimataifa ya Kesi Masalia za Mauaji ya Kimbari (International Residual Mechanism for Criminal Tribunals -IRMCT) Bw. Abubacar Tambadou mara baada ya mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akimkabidhi zawadi ya picha ya Mlima Kilimanjaro Balozi wa Italia hapa nchini, Mhe. Roberto Mengoni ambaye amamaliza muda wake wa utumishi hapa nchini


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akimkabidhi zawadi ya picha Balozi wa Namibia hapa nchini, Mhe. Theresia Samaria ambaye amamaliza muda wake wa utumishi hapa nchini

 

 










RAIS WA UFARANSA AMTUMIA BARUA YA PONGEZI RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA DKT JOHN POMBE MAGUFULI KWA KUIWEZESHA TANZANIA KUINGIA KATIKA ORODHA YA NCHI ZA UCHUMI WA KATI

Monday, November 30, 2020

BALOZI IBUGE ATAMBELEA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI ETHIOPIA

 Na Mwandishi wetu, Addis Ababa

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ametembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia kwa lengo la kujionea utendaji kazi wa Ubalozi pamoja na kukagua mali za Serikali nchini humo.

Balozi Ibuge kabla ya kuanza kukagua mali za Serikali, alikutana na watumishi katika mkutano ambapo amewataka kufanya kazi kwa bidii, weledi na uaminifu kwa kuweka mbele maslahi ya Taifa.

"Nawasihi sana kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake tufanye kazi kwa bidii na kuwa wabunifu wa kuitangaza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," Amesema Balozi Ibuge

Pamoja na Mambo mengine, Balozi Ibuge amewasihi Ubalozi huo kuhakikisha kuwa wanatekeleza vyema vipaombele vya Serikali ya awamu ya tano kama ilivyoelekezwa kwenye ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (2020 - 2025) katika Sura ya Saba, ambapo sura hiyo imeelekezwa kuwa Balozi zote kutekeleza Diplomasia ya Uchumi pamoja na Diplomasia ya Siasa.

Pia Balozi Ibuge amekagua mali mbalimbali zinazomilikiwa na Serikali ya Tanzania nchini Ethiopia kwa lengo la kuijionea na kujiridhisha juu ya uwepo wa mali hizo.

Kwa upande wake Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Bibi Elizabeth Rwitunga amemhakikishia Balozi Ibuge kuwa watafanya kazi kwa umoja, bidii, weledi na ubunifu kwa maslahi ya Taifa.

Bibi. Rwitunga ameongeza kuwa mashirikiano kati ya Tanzania na Ethiopia ni mazuri na yanaendelea kuimarika ikiwemo ushirikiano katika masuala ya usafiri wa anga ambapo Shirika la Ndege la Ethiopia linashirikiana na Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) katika masuala mbalimbali ikiwemo mafunzo na matengenezo ya ndege ambapo tayari watanzania watatu (3) wameshapatiwa mafunzo ya ndege.

Kuhusu Sera ya Diplomasia, Kaimu Balozi, Bibi. Rwitunga ameahidi kusimamia sera ya Diplomasia ya uchumi pamoja na Diplomasia ya siasa kwa kuhakikisha kuwa ubalozi utaendelea kuwasiliana na wawekezaji mbalimbali wa kuwekeza nchini Tanzania katika sekta za Nishati, Usafirishaji, Utalii pamoja na Biashara.

Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia unaiwakilisha Tanzania pia katika nchi za Djibouti, Yemen pamoja na Umoja wa Afrika na kamisheni ya Umoja wa Mataifa inayosimamia masuala ya Uchumi Barani Afrika (UNECA).

Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge akisaini kitabu cha wageni katika Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia  


Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akisisitiza jambo kwa watumishi (hawapo pichani) wakati wa mkutano  


Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge akiendesha kikao na wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini  


Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Bibi. Elizabeth Rwitunga (mwenye gauni la rangi ya bluu) akimpatia maelezo Balozi Ibuge wakati alipokuwa akikagua mali zinazomilikiwa na Serikali ya Tanzania nchini Ethiopia   


Balozi Ibuge akipatiwa maelekezo kutoka kwa Afisa wa Ubalozi wakati wa ukaguzi wa mali zinazomilikiwa na Serikali ya Tanzania nchini Ethiopia  

 



PROF. KABUDI AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA CHINA, FINLAND NA SWEDEN

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Finland hapa Nchini Mhe. Riitta Swan.Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushiriki
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika mazungumzo na Balozi wa China hapa Nchini Mhe. Wang Ke. Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Sweden hapa Nchini Mhe. Anders Sjoberg.Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Balozi wa Sweden hapa Nchini Mhe. Anders Sjoberg. Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Finland hapa Nchini Mhe. Riitta Swan. Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam.

Saturday, November 28, 2020

UBALOZI WA TANZANIA AFRIKA KUSINI WAPEWA CHANGAMOTO YA KUTEKELEZA DIPLOMASIA YA UCHUMI, SIASA

Na Nelson Kessy, Pretoria

Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini wapewa changamoto ya kuhakikisha kuwa unatekeleza Diplomasia ya Uchumi pamoja na Diplomasia ya Siasa iliyopo ndani ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM (2020-2025).

Changamoto hiyo imetolewa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge wakati alipotembelea Ubalozi huo jijini Pretoria nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kujionea utendaji kazi wa Ubalozi na mali za Serikali nchini humo. 

Balozi Ibuge ameutaka Ubalozi huo kuhakikisha kuwa unatekeleza diplomasia ya uchumi pamoja na diplomasia ya siasa kwa weledi ili kuleta manufaa ya Taifa.

"Nawapongeza kwa utendaji kazi wenu na nawasihi muendelee kujituma katika kazi (proactive) katika kuwapata wawekezaji na kutengeneza kuwa ni sehemu ya mfumo wa kuleta mabadiliko ambayo Serikali imeyapanga kupitia Ilani ya CCM ya 2020-2025," Amesema Balozi Ibuge.

Balozi Ibuge pia alipongeza utendaji wa Ubalozi huo ambao pamoja na Afrika Kusini unaiwakilisha Tanzania katika Ufalme wa Lesotho, Jamhuri ya Botswana, Jamhuri ya Namibia na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Kadhalika Balozi Ibuge alipokea changamoto mbalimbali zinazoikumba Ubalozi huo na Kuahidi kuzifanyia kazi ili kuongeza tija na ufanisi wa Ubalozi.

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania Nchini Afrika Kusini, Meja Jenerali Gaudence Milanzi amemueleza Balozi Ibuge mafaniko mbalimbali ya Ubalozi katika kutekeleza diplomasia ya uchumi na siasa nchini Afrika Kusini.

Moja kati ya mafanikio hayo ni pamoja na kuenezwa kwa lugha ya Kiswahili ambapo Serikali ya Tanzania na ya Afrika Kusini zinatarajia kusaini mkataba wa kutumika lugha ya Kiswahili kama katika shule za Afrika Kusini mwezi wa Machi 2021.

"Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Afrika Kusini tutasaini mkataba wa kutumika kwa lugha ya Kiswahili katika shule za Afrika Kusini mwezi wa Machi 2021," Amesema Balozi Milanzi.

Pamoja na mambo mengine Balozi Milanzi ameahidi kusimamia sera ya Diplomasia ya uchumi pamoja na Diplomasia ya siasa kwa kuhakikisha kuwa ubalozi utaendelea kuwasiliana na wawekezaji mbalimbali wa kuwekeza nchini Tanzania katika sekta za Biashara, Madini na Mawasiliano.


Balozi wa Tanzania Nchini Afrika Kusini, Meja Jenerali Gaudence Milanzi akiwatambulisha baadhi ya wafanyakazi kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ibuge wakati alipowasili Ubalozini leo tarehe 27 Novemba 2020


Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge akisaini kitabu cha wageni katika Ubalozi wa Tanzania Nchini Afrika Kusini leo tarehe 27 Novemba 2020


Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akisisitiza jambo kwa watumishi (hawapo pichani) wakati wa mkutano  


Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge akiendesha kikao na wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini  


Balozi wa Tanzania Nchini Afrika Kusini, Meja Jenerali Gaudence Milanzi akimuonesha baadhi ya mali Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi wakati alipokuwa anakagua mali za Serikali Ubalozini