Thursday, February 11, 2021

BIASHARA KATI YA TANZANIA, SAUDI ARABIA YAZIDI KUIMARIKA

 Na Mwandishi wetu,

Urari wa kibiashara kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Saudia Arabia umezidi kukuwa ambapo mpaka sasa miradi 14 ya uwekezaji kutoka nchini humo imesajiliwa katika kituo cha taifa cha uwekezaji (TIC)huku kampuni nane za Kitanzania zikipata kibali cha kuuza minofu ya samaki nchini humo.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ameyasema hayo katika mazungumzo yake na  Balozi wa Saudi Arabia hapa nchini, Mhe. Mohamed Bin Mansour Al Maliki anayemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini.

“Kwa hakika kipindi hiki mahusiano ya Saudi Arabia na Tanzania yameimarika vizuri kwa manufaa ya pande zote mbili, ambapo katika sekta ya uwekezaji kumekuwa na miradi 14 iliyoandikishwa katika Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC) ambapo uwiano wa biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Saudi Arabia unazidi kuongezeka na kuimarika,” Amesema Balozi Ibuge

Balozi Ibuge ameongeza kuwa zipo fursa nyingi za uwekezaji ambazo kupitia juhudi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na wadau wa sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya kilimo, kampuni kubwa kampuni kubwa ya Serikali ya Saudi Arabia ipo katika hatua za mwisho za kuja kuwekeza katika sekta za mifugo na kilimo hapa nchini.

Balozi Ibuge ameeleza kuwa kwa upande wa Tanzania “kampuni nane zimepata kibali cha kuuza minofu ya samaki katika soko la Saudi Arabia ikiwa ni moja kati ya juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa na Balozi Al Maliki kwa kushirikiana na Serikali katika kuimarisha mahusiano ya nchi zote mbili,”.

Kwa upande wake Balozi, anayemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini Mhe. Al Maliki ambaye amekuwa hapa nchini kwa kipindi cha miaka minne amesema anajisikia fahari na bahati kupata fursa ya kuiwakilisha nchi yake hapa Tanzania na kwamba katika kipindi chake chote  amepata ushirikiano mkubwa.

“Kwa kweli wakati wote wa uwakilishi wangu, nimekuwa nikipata ushirikiano wa kutosha wakati wa kutekeleza majukumu yangu jambo hili limenifurahisha sana……........na nitakuwa balozi mwema kwa Tanzania,” Amesema Balozi Al Maliki

Balozi Al Maliki amewasihi watanzania kuendelea na utamaduni wao unaowafanya kuheshimika duniani kote hususani katika suala la umoja, amani na mshikamano bila ya kujali itikadi za kisiasa na dini.

Tanzania na Saudi Arabia zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu katika sekta ya kilimo, elimu, afya, biashara na uwekezaji, maji, utalii, kwa lengo la kuhakikisha utekelezaji wa diplomasia ya uchumi unafikiwa kwa wakati.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiongea na Balozi wa Saudi Arabia hapa nchini, Mhe. Mohamed Bin Mansour Al Maliki wakati balozi huyo alipokuwa anamuaga katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Balozi wa Saudi Arabia hapa nchini, Mhe. Mohamed Bin Mansour Al Maliki akimueleza jambo Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akimkabidhi zawadi ya picha ya Mlima Kilimanjaro Balozi wa Saudi Arabia hapa nchini, Mhe. Mohamed Bin Mansour Al Maliki katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Balozi wa Saudi Arabia hapa nchini, Mhe. Mohamed Bin Mansour Al Maliki akimkabidhi zawadi Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam




 









Wednesday, February 10, 2021

MHE. OLE NASHA ASHIRIKI MKUTANO WA BUNGE LA NNE LA AFRIKA MASHARIKI

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. William Tate Ole Nasha (Mb) ashiriki katika Mkutano wa Pili, Kikao cha Nne, Bunge la Nne la Afrika Mashariki uliofanyika kwa njia ya mtandao. 

Kikao hicho kimefunguliwa na Spika wa Bunge hilo Mhe. Martin Ngoga na baadaye kuendelea kuliongoza Bunge katika utekelezaji wa majukumu yake ya siku. Shughuli ziliyofanywa na Bunge hilo na kufuatiliwa na Mhe. Ole Nasha ilikuwa ni kusomwa kwa mara ya kwanza Muswada wa Afrika Mashariki kuhusu Mifugo wa mwaka 2021, uwasilishwaji wa taarifa ya Kamati ya Kilimo, Utalii na Maliasili ambayo inaangazia tathmini ya utekelezaji wa shughuli za Kamisheni ya Bonde la Ziwa Viktoria na uwasilishwaji wa Hoja ya Azimio la Bunge la kulishawishi Baraza la Mawaziri la Afrika Mashariki kuhusu uharakishwaji wa kuanzisha mfuko wa dharura wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko katika Jumuiya. 

Bunge la Afrika Mashariki linaendelea na vikao vyake kwa njia ya mtandao ambavyo vitafanyika kwa kipindi cha wiki tatu kuanzia tarehe  28 Januari hadi 17 Februari 2021. 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. William Tate Ole Nasha akifuatilia Kikao cha Bunge la Afrika Mashariki kilichokuwa kikiendelea kwa njia ya video 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. William Tate Ole Nasha akifuatilia Kikao cha Bunge la Afrika Mashariki kilichokuwa kikiendelea kwa njia ya video

TANZANIA YACHAGULIWA KUNUFAIKA NA MRADI WA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 8 WA INTRA – ACP

 


Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji ambaye pia anaiwakilisha Tanzania katika Umoja wa Ulaya Mhe. Jestas Nyamanga akifafanua kuhusu upatikanaji wa soko la migebuka na dagaa wa Kigoma katika soko la Umoja wa Ulaya jijini Dar es Salaam


BALOZI IBUGE AWATAKA MABALOZI KUKUZA DIPLOMASIA YA UCHUMI

 Na Mwandishi wetu,

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amewataka mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani kuongeza jitihada za kuhakikisha Diplomasia ya Uchumi inaleta tija iliyokusudiwa.

Balozi Ibuge ametoa kauli hiyo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo kwa nyakati tofauti na Balozi wa Tanzania nchini Zimbambwe, Mhe. Prof. Emmanuel Mbennah pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Wilson Masilingi katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Balozi Ibuge katika mazungumzo yake na Balozi wa Tanzania nchini Zimbambwe Prof. Mbennah amemtaka kuhakikisha kuwa anafanya kazi kwa weledi katika kuimarisha uhusiano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Zimbabwe pamoja na kukuza diplomasia ya uchumi kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali. 

“Balozi nakusihi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kufanikisha azma na malengo ya Serikali katika kuhakikisha tunaimarisha uhusiano wetu wa kidiplomasia na Zimbabwe lakini pia kukuza diplomasia ya Uchumi kati yetu na Zimbabwe,” Amesema Balozi Ibuge.

Kwa upande wake, Balozi Prof. Mbennah amemhakikishia Katibu Mkuu kuwa uhusiano wa Jamhuri ya Muungano na Tanzania na Zimbabwe ni mzuri na imara.

Katika tukio jingine, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Wilson Masilingi ambapo pamoja na mambo mengine wamejadili umuhimu wa kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika ipasavyo na uhusiano mzuri wa kidiplomasia ilionao na Marekani. 

Katika kuhakikisha hilo, Balozi Ibuge alimsisitiza Balozi Masilingi kuendelea kufanya kazi kwa bidii katika kutekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa manufaa ya Taifa.  

Nae balozi Masilingi amemhakikishia Katibu Mkuu kuwa Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani unaendelea kutekeleza diplomasia ya uchumi kwa kasi inayotakiwa.

Balozi wa Tanzania nchini Zimbambwe Mhe. Prof. Emmanuel Mbennah akimuelezea jambo Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wakati wa mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiongea na Balozi wa Tanzania nchini Zimbambwe Mhe. Prof. Emmanuel Mbennah 


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Zimbambwe Mhe. Prof. Emmanuel Mbennah 


Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Wilson Masilingi akimuelezea jambo Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wakati wa mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam 


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akimsikiliza Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Wilson Masilingi mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam. Kulia ni Msaidizi wa Katibu Mkuu Bi. Eva Ng’itu 


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiongea na Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Wilson Masilingi


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Wilson Masilingi



Sunday, February 7, 2021

TANZANIA, AFRIKA KUSINI ZAWASILISHA OMBI MAALUM AU

 Na Mwandishi Wetu

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja Jamhuri ya Afrika Kusini zimewasilisha ombi maalumu kwa Umoja wa Afrika kuzitambua rasmi njia zilizotumika na wapigania uhuru kutoka Dar es Salaam kupitia nchi mbalimbali Kusini Mwa Bara la Afrika hadi Namibia kuwa urithi wa Kimataifa.

Ombi hilo limewasilishwa na Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Cyril Ramaphosa katika Mkutano wa 34 wa kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika unaofanyika kwa njia mtandao na kuungwa mkono na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) ambaye alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.  

Tanzania pia imeuomba Umoja wa Afrika kuitambua lugha ya Kiswahili kama lugha ya asili na ya ukombozi katika Bara la Afrika kwa kuwa ndiyo lugha iliyotumika kwa ajili ya mawasiliano na mafunzo kwa wapigania uhuru ikizingatiwa kuwa kauli mbiu ni Sanaa, Utamaduni na urithi.

“Tumeuomba Umoja wa Afrika kuitambua lugha ya Kiswahili kama lugha ya asili na ya ukombozi katika Bara la Afrika kwa kuwa ndiyo lugha iliyotumika kwa ajili ya mawasiliano na mafunzo kwa wapigania uhuru ikizingatiwa kuwa kauli mbiu ni sanaa, utamaduni na urithi,” Amesema Prof. Kabudi.

 

Akiufunga Mkutano huo wa siku mbili, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ambaye pia ni rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mhe. Felix Tshisekedi amesisitiza kuwa umoja, mshikamano na amani katika bara la Afrika ndiyo nyenzo pekee itakayoliwezesha bara hilo kuendelea kiuchumi ili kuendana na rasilimali ilizonazo.

“Umoja, mshikamano na amani katika bara la letu la Afrika ndiyo nyenzo pekee itakatuwezesha sisi kuendelea kiuchumi ili kuendana na rasilimali tulizonazo kwa maslahi yetu mapana,” Amesema Rais Tshisekedi

Pamoja na mambo mengine, mkutano huo umejadili mambo mbalimbali ikiwemo uundaji wa Kamati mpya ya uongozi wa Umoja wa Afrika (the AU Bureau of Assembly) kwa mwaka 2021, uzinduzi wa Kaulimbiu ya Umoja wa Afrika kwa mwaka 2021 inayohusu “Sanaa, Tamaduni na Urithi katika kufikia azma ya Afrika Tuitakayo”

Mengine yaliyojadiliwa ni taarifa ya Maendeleo ya Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu COVID-19 Barani Afrika, taarifa ya Utekelezaji wa Mabadiliko ya Kitaasisi ya Umoja wa Afrika; na Uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitumia fursa hiyo kueleza utayari wake kuendelea kushirikiana na Umoja wa Afrika na Nchi Wanachama wa Umoja huo katika kutekeleza jitihada zinazolenga kuiwezesha Afrika kujitegemea.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akifuatilia Mkutano wa 34 wa kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika unaofanyika kwa njia Video Conference ambapo ujumbe wa Tanzania umehudhuria mkutano huo jijini Dar es Salaam. Kulia mwa Prof. Kabudi ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge. Prof. Kabudi anamuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli katika mkutano huo. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb), Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge pamoja na Maafisa mbalimbali wakifuatilia Mkutano wa 34 wa kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika unaofanyika kwa njia Video Conference. Prof. Kabudi amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli katika mkutano huo. 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb), Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wakifuatilia Mkutano wa 34 wa kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika unaofanyika kwa njia Video Conference. Prof. Kabudi amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli katika mkutano huo. 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb), akifuatilia Mkutano wa 34 wa kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika unaofanyika kwa njia Video Conference. Prof. Kabudi amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli katika mkutano huo. 


Mkutano ukiendelea 



Friday, February 5, 2021

TZ YATOA MUELEKEO WAKE KATIKA AWAMU YA PILI YA UONGOZI WA RAIS MAGUFULI

Na Mwandishi wetu, 

Serikali ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema katika kipindi cha muhula wa pili wa miaka mitano ya Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli itajikita zaidi katika diplomasia ya uchumi, kuimarisha sekta binafsi, kukuza biashara pamoja na mahusiano na Mataifa mengine duniani. 

Msimamo wa Tanzania umetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi Jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wake na Mabalozi wanaoziwakilisha Nchi zao hapa Tanzania pamoja na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na kuongeza kuwa ni dhamira ya Tanzania kuhakikisha kuwa ina uwezo wa kukuza biashara na kuuza bidhaa katika nchi mbalimbali duniani.

“Katika mwaka huu unaoanza sasa na miaka ijayo katika mhula wa pili awamu ya tano ni wakati muafaka wa Tanzania kuimarisha diplomasia ya uchumi na uhusiano mwema baina yake na nchi mbalimbali kwa kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchi hizo katika maeneno ya uzalishaji, viwanda na kuongeza biashara kwa manufaa ya mataifa yote,” Amesema Prof. Kabudi 

Pamoja na mambo mengine, Prof. Kabudi amewaambia Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa hapa Nchini kuwa hali ya kisiasa na amani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla imeimarika kuliko wakati wowote hususani mara baada ya uchaguzi mkuu uliomalizika Octoba, 2020 na kwamba uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar unachochea kuongezeka kwa uwekezaji na ufanyaji wa biashara kwa lengo la kukuza uchumi. 

Kwa upande wake Kiongozi wa Mabalozi Dkt. Ahmada El Badasui ambaye pia ni Balozi wa Comoro hapa nchini ameshukuru kwa uwepo wa mkutano huo ambao unawapa fursa mabalozi kufahamu masuala mbalimbali yanayoendelea hapa nchini.

“Nakupongeza Mhe. Waziri na uongozi wa Wizara kwa kuandaa mkutano huu ambao unatupa fursa sisi mabalozi kujadili na kujua mambo mbalimbali yanayoendelea hapa nchini, mikutano kama hii ni muhimu sana kwetu kwani inatusaidia na kutuwezesha kuboresha mahusiano yetu ya kidiplomasia,” Amesema Dkt. El Badasui

Kwa upande wake Balozi wa Umoja wa Ulaya Mhe. Manfredo Fanti ameipongeza Tanzania kwa kuingia uchumi wa kati na kwamba Umoja wa Ulaya uko tayari kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha Uchumi wa Tanzania unaendelea kukua na kuimarika.

Mkutano huo wa Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa umehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe William Tate Ole Nasha, Katibu Mkuu Balozi, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge na Wakurugenzi na Wakuu wa Idara na vitengo vya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiongea na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania pamoja na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wakati wa mkutano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe William Tate Ole Nasha (Mb) akiongea na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania pamoja na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wakati wa mkutano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiongea na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania pamoja na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wakati wa mkutano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam


Balozi wa Comoro hapa nchini na kiongozi wa Mabalozi Dkt. Ahmada El Badasui akitoa neno la shukrani kwa viongozi wakuu wa Wizara (hawapo pichani) kabla ya kumalizika kwa mkutano 


Sehemu ya Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wakifuatilia mkutano 


Balozi wa Canada Mhe. Pamela O’Donnel akichangia jambo wakati wa Mkutano   


Balozi wa Umoja wa Ulaya Mhe. Manfredo Fanti akichangia jambo wakati wa Mkutano. Kulia kwake ni Balozi wa Rwanda hapa nchini, Mhe. Meja Jenerali Charles Karamba.  



 


Thursday, February 4, 2021

IOM YAIPONGEZA TANZANIA KWA KUWASAMEHE RAIA WA ETHIOPIA

Shirika la Kimataifa la Uhamaji (IOM) limeipongeza Serikali ya Tanzania kwa hatua iliyochukua ya kuwaachia huru Raia 1789 wa Ethiopia waliokuwa wakishikiliwa kwa kuingia nchini kinyume cha sheria.

Pongezi hizo zimetolewa na Bw. Mohammed Abdiker Mohamud Mkurugenzi wa IOM Kanda ya Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi ofisini kwake jijini Dodoma.

Bw. Mohamud amesema kitendo kilichofanywa na Rais Magufuli hivi karibuni ni cha kuigwa na kupongezwa na mataifa mengine kwani uhamaji wa watu umekuwepo kwa miaka mingi kwa ajili ya kutafuta maisha amani na usalama wao.

“Tunashukuru sana na kuipongeza Serikali ya Tanzania kwa kitendo cha kuwaachia huru raia 1789 wa Ethiopia waliokuwa wakishikiliwa, kitendo hicho ni cha mfano na kinapaswa kuigwa na mataifa mengine,” alisema.

Viongozi hao pia wamezungumzia namna ya kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na Taasisi hiyo ya IOM na kuzijengea uwezo taasisi na mashirika wa kukabiliana na masuala ya uhamaji ikiwa ni pamoja na kusaidia kituo cha mafunzo ya uhamaji cha IOM kilichopo mjini Moshi kuwa kituo cha Umahiri cha masuala ya uhamaji katika bara la Afrika.

Akizungumza katika kikao hicho Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi ameishukuru IOM kwa kuipongeza Tanzania na kuahidi kuwa Serikali ya Tanzania itatoa ushirikiano kwa Shirika hilo katika kutekeleza kazi zake hapa nchini.

Amesema Uhamaji sio jambo linalokataliwa na nchi ila kinachotakiwa ni kufuata sheria na taratibu za nchi husika na kuongeza kuwa Kitendo hicho kitawafanya Waethiopia hao kurejea nchini kwao na kushiriki harakati za kiuchumi na hivyo kuiletea maendeleo nchi yao..

Prof. Kabudi ameiahidi IOM kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano na kituo hicho kinachotoa mafunzo ya kuongeza uwezo wa masuala ya uhamaji kwa Bara la Afrika ili kiwe kituo cha umahiri.

Amesema Tanzania itahakikisha Kituo hicho kinatambulika na Umoja wa Afrika ili kiweze kupata misaada ya kifedha na kitaalamu na hivyo kukamilisha azma ya IOM ya kuwa na kituo cha umahiri katika masuala ya uhamaji wa watu kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine.

Ameitaka IOM kuelekeza nguvu katika kusaidia nchi zenye machafuko na hali mbaya za kiuchumi na kuongeza kuwa Shirika ka IOM lazima lijikite katika kuwafanya Waethiopia waone kuwa hakuna faida kwa kuikimbia nchi yao na kwenda Afrika Kusini na kwingineko duniani na kwamba wanatakiwa kubaki nchini mwao ili kuijenga nchi yao.

Hivi karibui Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipokutana na Rais Sahle –Work Zawde wa Ethiopia Chato mkoani Geita alitangaza kuwaachia huru raia zaidi 1700 waliokuwa wakishikiliwa kwa kuingia nchini kinyume cha sheria.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akisalimiana Bw. Mohammed Abdiker Mohamud Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Uhamaji (IOM) Kanda ya Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika alipomtembelea Mhe. Waziri ofisini kwake jijini Dodoma

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akiwa na Bw. Mohammed Abdiker Mohamud Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Uhamaji (IOM) Kanda ya Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika walipokutana kwa mazungumzo ofisini kwake jijini Dodoma.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi na Bw. Mohammed Abdiker Mohamud Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Uhamaji (IOM) Kanda ya Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika katika picha ya pamoja baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika jijini Dodoma

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi, Bw. Mohammed Abdiker Mohamud Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Uhamaji (IOM) Kanda ya Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika (kulia) na Bw.Qasim Sufi Mkurugenzi Mkaazi wa IOM nchini (kushoto) katika picha ya pamoja baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika jijini Dodoma.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi na Bw.Qasim Sufi Mkurugenzi Mkaazi wa IOM nchini wakitakasa mikono baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika jijini Dodoma.

Wednesday, February 3, 2021

BALOZI BRIGEDIA GENERALI IBUGE AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI LUVANDA

Balozi Brigedia Generali Wilbert Ibuge,Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki leo amekutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Baraka Luvanda Balozi wa Tanzania nchini India katika ofisi za Wizara zilizopo Mtumba, jijini Dodoma. 

Mazungumzo hayo yalilenga kubadilishana mawazo na uzoefu baina yao kuhusu masuala mbalimbali hususan katika kudumisha na kuboresha uhusiano na ushirikiano uliopo katika ya Tanzania na India, kutangaza fursa zilizopo Tanzania ili kuvutia zaidi biashara na uwekezaji nchini kutoka India. 

Jitihada za kutangaza fursa zinazopatikana nchini zimekuwa zikiendelea kufanywa na Wizara, kupitia Balozi zake ikiwa ni utekelezaji wa maagizo na maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuhakikisha kuwa Diplomasia ya Uchumi inatekelezwa ili kuinufaisha nchi kupitia fursa zilizopo.

Tanzania na India zimekuwa na ushirikiano mzuri na wakudumu wa kidipolomasia na kiuchumi ambao umeendelea kuzinufaisha nchi zote mbili. Mfano, Juni 2015 Tanzania ilinufaika na mkopo kutoka nchini India wa upanuzi wa mradi wa maji kutoka Ziwa Vikitoria kwenda Mkoani Tabora, mradi huu ambao unanufaisha zaidi ya watu 1,433,004 ulikamilika mwaka 2019.

India ilianzisha Ubalozi wake nchini Tanzania mwaka 1961 (wakati huo ilijulikana kama Tanganyika), hii ilikuwa kabla Tanganyika haijapata uhuru, na Tanganyika ilianzisha Ubalozi wake nchini India mwaka 1962, mara baada ya kupata Uhuru.

Balozi Brigedia Generali Wilbert Ibuge, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mhe. Baraka Luvanda Balozi wa Tanzania nchini India wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kuhitimisha mazungumzo yao yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara zilizopo Mtumba, jijini Dodoma

Balozi Brigedia Generali Wilbert Ibuge, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mhe. Baraka Luvanda Balozi wa Tanzania nchini India wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kuhitimisha mazungumzo yao yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara zilizopo Mtumba, jijini Dodoma


Balozi Brigedia Generali Wilbert Ibuge, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akisalimiana na Mhe. Baraka Luvanda Balozi wa Tanzania nchini India alipowasili Wizarani kufanya mangumzo na Katibu Mkuu.

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akifuatilia ufunguzi wa Mkutano wa 38 wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika unaofanyika kwa njia ya video. Anayeonekana katika Screen pichani ni Waziri wa Ushirikiano na Uhusiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini na Mwenyekiti wa Baraza hilo Mhe. Dkt. Naledi Pandor anayeongoza mkutano huo


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akifuatilia Mkutano wa 38 wa Baraza la Mawaziri Umoja wa Afrika unaofanyika kwa njia ya video

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi na ujumbe wa Tanzania wakifuatilia ufunguzi wa Mkutano wa 38 wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika unaofanyika kwa njia ya video.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akifuatilia ufunguzi wa Mkutano huo unaofanyika kwa njia ya video. 


Mkutano wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika unaofanyika kwa njia video (video conference) umeanza.Mkutano huo umefunguliwa na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Umoja huo na Waziri wa Ushirikiano na Uhusiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini Mhe. Dkt. Naledi Pandor

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi ameongoza ujumbe wa Tanzania kutokea katikaa mji wa Serikali Mtumba ulioko Makao Makuu ya nchi jijini Dodoma.

Mkutano huo wa kawaida wa siku mbili unaongozwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo Mhe. Dr. Naledi Pandor Waziri wa Ushirikiano na Uhusiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini pamoja na mambo mengine utaandaa rasimu ya agenda za Mkutano wa 34 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika utakaofanyika tarehe 6 na 7 Februari, 2021 kwa njia video  

Mkutano huo unajadili na kupitisha mapendekezo ya taarifa ya Mkutano wa 41 wa Kamati ya Kudumu ya Uwakilishi (Permanent Representatives Committee –PRC),taarifa ya hali ya ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu (COVID-19) Barani Afrika na taarifa ya Mkutano wa Pamoja wa Kamati ya Baraza la Mawaziri ya Tathimini na Kamati ya Mawaziri 15 wa Fedha.

Mkutano pia utafanya uchaguzi na Uteuzi wa Wajumbe Sita (6) wa Bodi ya Ushauri ya Masuala ya Rushwa ya Afrika, Makamishna wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika na Majaji wanne (4) wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.

 

 

Tuesday, February 2, 2021

MKUTANO WA 38 WA BARAZA LA MAWAZIRI WA UMOJA WA AFRIKA KUFANYIKA KWA NJIA YA MTANDAO

 


Mkutano wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika unatarajiwa kufanyika tarehe 3 na 4 Februari, 2021 kwa njia mtandao (video conference).

 Katika Mkutano huo Tanzania itawakilishwa na Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye atashiriki Mkutano huo kutokea makao makuu ya nchi jijini Dodoma. Mkutano huo unafanyika baada ya kukamilika kwa Mkutano wa 41 wa Kawaida wa Kamati ya Uwakilishi ya Kudumu uliofanyika tarehe 20 hadi 26 Januari, 2021.

 Mkutano huo wa kawaida wa siku mbili utaongozwa na kufunguliwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo Mhe. Dr. Naledi Pandor Waziri wa Ushirikiano na Uhusiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini. 

Mkutano huo pamoja na mambo mengine utaandaa rasimu ya agenda za Mkutano wa 34 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika utakaofanyika tarehe 6 na 7 Februari, 2021.

Mkutano huo utajadili na kupitisha mapendekezo ya taarifa ya Mkutano wa 41 wa Kamati ya Kudumu ya Uwakilishi (Permanent Representatives Committee –PRC),taarifa ya hali ya ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu (COVID-19) Barani Afrika na taarifa ya Mkutano wa Pamoja wa Kamati ya Baraza la Mawaziri ya Tathimini na Kamati ya Mawaziri 15 wa Fedha.

Mkutano pia utafanya uchaguzi na Uteuzi wa Wajumbe Sita (6) wa Bodi ya Ushauri ya Masuala ya Rushwa ya Afrika, Makamishna wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika na Majaji wanne (4) wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.