Saturday, July 16, 2022

MAKATIBU WAKUU WA SADC WAANZA MAANDALIZI YA MKUTANO WA 24 WA KAMATI YA MAWAZIRI

Mkutano wa 24 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO) utafanyika jijini Pretoria, Afrika Kusini kuanzia tarehe 16 hadi 19 Julai, 2022. 

 

Mkutano huo umetanguliwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu unaofanyika tarehe 16 na 17 Julai 2022 ambapo ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Kamati hii unaongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma M. Rajab ambaye anamwakilisha Katibu Mkuu, Balozi Joseph Sokoine. 

 

Mkutano wa 24 unalenga pamoja na mambo mengine kupokea na kujadili agenda mbalimbali zikiwemo mapitio ya utekelezaji wa maamuzi ya Mkutano wa 23 wa MCO na Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC; Hali ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya kanda; na tathmini ya hali ya Ulinzi na Usalama katika Kanda pamoja na Tathmini ya athari zitokanazo na mgogoro unaoendelea katika bara la Ulaya.

 

Viongozi wengine kutoka Tanzania wanaoshiriki Mkutano wa Makatibu Wakuu ni pamoja na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala, Mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi, Lt. Jenerali Salum Othman, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. Meja Jenerali (Mst) Gaudence Milanzi, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kuzuia na  Kupambana na Rushwa,  Kamishna wa Polisi Salum  Hamduni, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga.

 

Ujumbe wa Tanzania kwa ngazi ya Mawaziri unatarajiwa kuongozwa na Mhe. Balozi Liberata Mulamula, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye ataambatana na Mhe. Dkt. Stergomena Tax, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Mohammed Rajab akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Makatibu Wakuu unaofanyika kwa ajili ya kuandaa Mkutano wa 24 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC MCO) utakaofanyika jijini Pritoria, Afrika Kusini kuanzia tarehe 16 hadi 19 Julai 2022.

Mwenyekiti wa Mkutano wa Makatibu Wakuu (kulia) na Mjumbe kutoka Sekretarieti ya SADC  wakati wa ufunguzi wa mkutano huo unaofanyika jijini Pretoria, Afrika Kusini tarehe 16 na 17 Julai 2022 kwa ajili ya kuandaa Mkutano wa 24 wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC.

Sehemu ya Ujumbe wa Serikali ya Angola ukishiriki Mkutano wa Makatibu Wakuu

Sehemu ya Ujumbe wa Serikali ya Botswana ukishiriki Mkutano wa Makatibu Wakuu

Wakati huohuo Mhe. Balozi Fatma ameongoza kikao kati yake na ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mkutano wa Makatibu Wakuu. Pichani Balozi Fatma akizungumza na ujumbe huo (hawapo pichani) kuhusu namna ya kushiriki kikamilifu kama Tanzania kwenye Mkutano wa 24 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola.

Viongozi mbalimbali kutoka Serikalini akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kuzuia na  Kupambana na Rushwa,  Kamishna wa Polisi Salum  Hamduni (kushoto) wakimsikiliza kiongozi wa ujumbe wa Tanzania, Balozi Fatma (hayupo pichani) wakati wa kikao cha maandalizi ya ushiriki wa Tanzania kwenye Mkutano wa Makatibu Wakuu

Viongozi wengine akiwemo Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala (kushoto) wakati wa kikao cha maandalizi

Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Bw. Shija akifuatilia kikao cha maandalizi cha ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mkutano wa Makatibu Wakuu

Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga akishiriki kikao cha maandalizi kilichohusisha ujumbe wa Tanzania.


 

TANZANIA YATOA WITO KWA BARA LA AFRIKA KUIMARISHA AMANI NA USALAMA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) ametoa wito kwa nchi za Umoja wa Afrika (AU) kuendelea kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na umoja huo katika kutafuta suluhu ya migogoro ili kudumisha amani na usalama barani Afrika. 

Waziri Mulamula ametoa wito huo alipokuwa akichangia ajenda iliyohusu masula ya nafasi za uanachama katika Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika kwenye Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika uliofanyika jijini Lusaka Zambia tarehe15 Julai 2022.

Akitoa mchango wake kwa lugha ya Kiswahili Waziri Mulamula alieleza kuwa Tanzania inaunga mkono juhudi zinazofanywa na AU kwa lengo la kuimarisha utendaji wa Baraza la Umoja na Usalama la Umoja wa Afrika ikiwemo kuendelea kuwa na idadi ya wanachama waliopo katika baraza hilo. 

“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni muumini mkubwa wa usawa wa uwakilishi wa kanda na nchini wanachama ndani ya Umoja wa Afrika na Taasisi nyingine za kimataifa. Hii ni kutokana na imani yetu kuwa endapo usawa utazingatiwa tutaendelea kudumisha umoja na mshikamano wetu ambao kwa muda mrefu umeendelea kuwa nguzo ya amani na usalama katika bara letu” Alieleza Waziri Mulamula. 

Sambamba na hilo katika Mkutano huo wa Baraza la Mawaziri miongoni mwa ajenda zilizojadiliwa ilikuwa ni kupitisha bajeti ya Umoja wa Afrika kwa mwaka 2023. Kitu muhimu katika mkutano huu ni kuwa bajeti hiyo imeweka kifungu kwa ajili ya utekelezaji wa maamuzi ya Mkutano wa 35 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika yaliyopitsha Kiswahili kuwa Lugha ya Kazi ya Umoja wa Afrika. 

Akizungumzia suala hilo Waziri Mulamula ameeleza kuwa amefarijika kuona kipengele maalumu cha kutekeleza maamuzi ya kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya kazi ya Umoja wa Afrika inafanyiwa kazi kwa vitendo. Aliongeza kusema hatua hiyo itaharakisha utekelezaji wa maamuzi hayo kwa kuwa itarahishisha utendaji wa shughuli mbalimbali muhimu kama vile kugharamia zoezi la kutafsiri nyaraka mbalimbali, kulipa au kuajili wakalimani na kuwajengea uwezo wa lugha hiyo wataalamu wa ngazi mbalimbali katika Kamisheni ya Umoja wa Afrika na Taasisi nyingine za umoja huo. 

Aidha katika mkutano huo wa 41 wa Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika kwa mara ya kwanza wameanda baadhi ya taarifa zinazotokana na mkutano huo kwa lugha ya Kiswahili.

Vilevile Waziri Mulamula kwenye Mkutano huo alichangia mjadala wa kupitisha bajeti ya Umoja wa Afrika kwa mwaka 2023 ambapo kwa niaba ya Tanzania ameunga mkono mapendekezo ya bajeti ya umoja huo. Pia alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa Kamisheni ya Umoja wa Afrika na Taasisi zake kuendelea kuchukua hatua za kupunguza matumizi ili kuendana na uhalisia wa hali ya uchumi wa nchi zetu za Afrika katika nyakati hizi.

 

“Tunatoa wito kwa Kamisheni na Taasisi nyingine za Umoja wa Afrika kuweka mipango mizuri ya miradi na shughuli zake ili kuendana na uwezo wa kutekeleza miradi hiyo na kuweka kipaumbele kwa miradi yenye tija kwa wananchi wa Bara la Afrika” Alisema Waziri Mulamula.

Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika umeongozwa na mwenyekiti wake Mhe. AissataTall Sall ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Senegal.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akichangia jambo kwenye Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika jijini Lusaka, Zambia
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akifuatilia mjadala uliokuwa ukiendelea kwenye Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika uliofanyika jijini Lusaka, Zambia.
Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika uliofanyika jijini Lusaka, Zambia ukiendelea. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Tanzania ulioshiriki katika Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika jijini Lusaka, Zambia.

Friday, July 15, 2022

TANZANIA, UBELGIJI ZAKUBALIANA KUANZA MASHAURIANO YA KUANZISHA USHIRIKIANO UBORESHAJI WA HUDUMA ZA BANDARI

 








TANZANIA, UFARANSA ZAAHIDI KUENDELEZA USHIRIKIANO

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Ufaransa zimeahidi kuendeleza ushirikiano katika nyanja za elimu, afya, maji, usafirishaji, kilimo na utalii kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.

Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk aliposhiriki hafla ya kuandimisha Siku ya Taifa ya Ufaransa  iliyofanyika Jijini Dar es Salaam tarehe 14 Julai 2022.

Balozi Mbarouk alisema Tanzania na Ufaransa zimekuwa na uhusiano mzuri tangu mwaka 1961 na mataifa hayo yamekuwa na ushirikiano katika nyanja za elimu, afya, maji, usafirishaji, mawasiliano, utalii, kilimo, biashara na uwekezaji.

“Ufaransa imekuwa mdau mkubwa katika masuala ya uchumi ambapo kampuni mbalimbali kutoka Ufaransa zimewekeza nchini na zimekuwa zikichangia kutoa ajira kwa watanzania na kuongeza pato la taifa,” alisema Balozi Mbarouk 

Balozi Mbarouk aliongeza kuwa Ufaransa imekuwa mdau mkubwa wa utalii ambapo idadi ya watalii imekuwa ikiongezeka kutoka 25,000 kwa mwaka 2020 hadi 50,000 kwa mwaka 2022.

“Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikiboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuwavutia zaidi wawekezaji kutoka nje kuja kuwekeza  nchini…….pia Serikali inatambua na kuthamini mchango wa wafanyabishara wa Ufaransa katika kukuza sekta uchumi,” alisema Balozi Mbarouk.

Awali Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Nabil Hajlaoui alisema Ufaransa imefurahishwa na ushirikiano mzuri inaoupata kutoka Serikali ya Tanzania na kuahidi kuwa Ufaransa itaendelea kudumisha uhusiano huo kwa maslahi ya mataifa yote mawili.

Balozi Hajlaoui aliongeza kuwa Ufaransa itaendelea kushirikiana na Tanzania kuunga mkono juhudi mbalimbali za kukuza maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania.

“Tanzania imekuwa na uhusiano mzuri na Ufaransa kwa muda mrefu nawaahidi hapa kuwa uhusiano huu tutaendelea kuudumisha na kuulinda wakati wote,” alisema Balozi Hajlaoui

Balozi Hajlaoui aliongeza kuwa Ufaransa inaridhishwa na jitihada za Tanzania katika kuhakikisha usawa wa kijinsia katika jamii, uhuru wa demokrasia, kulinda amani na usalama ndani na kwenye kanda.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda, Mabalozi mbalimbali na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini, asasi za kiraia, viongozi wa vyama vya siasa na wafanyabiashara.  
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akisalimiana na Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Nabil Hajlaoui wakati wa hafla ya kuandimisha Siku ya Taifa ya Ufaransa  iliyofanyika Jijini Dar es Salaam tarehe 14 Julai 2022

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akitoa hotuba yake katika hafla ya kuandimisha Siku ya Taifa ya Ufaransa  iliyofanyika Jijini Dar es Salaam tarehe 14 Julai 2022

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akitoa hotuba yake katika hafla ya kuandimisha Siku ya Taifa ya Ufaransa  iliyofanyika Jijini Dar es Salaam tarehe 14 Julai 2022

Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Nabil Hajlaoui akiwasilisha hotuba yake katika hafla ya kuandimisha Siku ya Taifa ya Ufaransa  iliyofanyika Jijini Dar es Salaam tarehe 14 Julai 2022


Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda akijadili jambo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk katika hafla ya kuandimisha Siku ya Taifa ya Ufaransa  iliyofanyika Jijini Dar es Salaam tarehe 14 Julai 2022

Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda katika picha ya pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Nabil Hajlaoui na Afisa Mtendaji Mkuu NMB Bank, Bibi. Ruth Zaipuna pamoja na maafisa kutoka Ubalozi wa Ufaransa na Wasanii wa muziki wa kizazi kipya

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akiteta jambo na Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Nabil Hajlaoui wakati wa hafla ya kuandimisha Siku ya Taifa ya Ufaransa  iliyofanyika Jijini Dar es Salaam tarehe 14 Julai 2022



TANGAZO LA KAZI KATIKA SEKRETARIETI YA JUMUIYA YA MADOLA