Thursday, December 15, 2022

BALOZI SIRRO AWASILISHA HATI ZA UTAMBULISHO KWA RAIS WA ZIMBABWE

Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Mhe. Simon Sirro amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Emmerson Mnangagwa, Ikulu Zimbabwe.

Julai 20, 2022 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alimteua aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe.

Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Mhe. Simon Sirro akiwasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Emmerson Mnangagwa, Ikulu Zimbabwe

Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Emmerson Mnangagwa akisalimiana na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Mhe. Simon Sirro Ikulu Zimbabwe baada ya kuwasilisha Hati za Utambulisho

Picha ya pamoja 



Tuesday, December 13, 2022

AFRIKA MASHARIKI WAHIMIZWA KUTUMIA BIDHAA ZA NDANI

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma (kulia) akiangalia bidhaa za mjasiriamali kwenye maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu Juakali yanayoendelea jijini Kampala, Uganda.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma ametoa wito kwa wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kujivunia na kutumia bidhaa zinazozalishwa katika Jumuiya ili kuijenga Afrika Mashariki yenye uchumi stahimilivu na maendeleo endelevu. 

Waziri Riziki Pembe Juma ameeleza hayo alipokuwa akizungumza kwenye sherehe za SIKU YA TANZANIA (TANZANIA DAY) katika maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu kama “Juakali”, yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru vya Kololo Jijini Kampala, Uganda. 

“Nimepata fursa ya kutembelea baadhi ya mabanda ya maonesho na nimefurahishwa kuona bidhaa mbalimbali kutoka kwa wajasiriamali, kwa kweli bidhaa zilizopo zina ubora na ubunifu na zinavutia sana. Nitoe rai kwa wana Afrika Mashariki kutumia bidhaa hizi zinazozalishwa katika Jumuiya ili kuunga mkono juhudi za Serikali za kubadilisha sekta isiyo rasmi kuwa rasmi ili wananchi waweze kushiriki katika kuchangia maendeleo endelevu na pato la Jumuiya”. alisema Waziri Riziki Pembe Juma

Maadhimisho ya TANZANIA DAY yaliambatana na shughuli mbalimbali zilizofanywa na wajasiriamali wa Tanzania kwa lengo la kucherehesha maonesho na kuonesha utamaduni wa Tanzania pamoja na bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini. Miongoni mwa shuguli zilizofanywa ni pamoja na maonesho ya mavazi ya asili, maonesho ya vito vya thamani na madini, vyakula vya asilia, ngoma za asili na muziki. 

Akizungumza na maelfu ya washiriki wa maonesho hayo Waziri Riziki Juma Pembe mbali na kutoa wito kwa wana Jumuiya kununua bidhaa za ndani alielezea hatua mbalimbali zinazo endelea chukuliwa na Serikali za Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kutatua changamoto zinazowakabili wajariamali, ambapo kwa upande wa Serikali ya Tanzania amezitaja hatua zilizochukuliwa kuwa ni pamoja na; kutoa mikopo yenye masharti nafuu, kuanzisha maeneo maaalum ya kufanyia biashara na kutoa elimu ya ujasiriamali.

“Serikali za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinaendelea kuhakikisha wajasiriamali hawa hawaendelei kubaki wadogo bali wanapaswa kukua ili waweze kushiriki katika sekta rasmi kama wajasiriamali wakubwa. Vilevile kwa kushirikia na Sekretarieti ya Jumuiya tutahakikisha maonesho haya yanaendelea kufanyika kwa lengo la kuwapatia fursa wajasiriamali wa sekta hii ili waweze kutambua fursa zilizopo katika nchi zetu na kushiriki katika uzalishaji na maendeleo ya nchi zetu”. Alieleza Waziri Riziki Pembe Juma

Hii ni mara ya tano kwa Jamhuri ya Uganda kuwa mwenyeji wa maonesho haya tokea kuanzishwa kwake mwaka 1999.
Mkurugenzi anayesimamia masuala ya Diapora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi James Bwana akiangalia bidhaa za mjasiriamali kwenye maonesho ya 22 yaJuakali yanayoendelea jijini Kampala, Uganda

Meza Kuu wakiwa wamesimama wakati wimbo wa Taifa ukipigwa wakati wa maadhimisho ya SIKU YA TANZANIA kwenye maonesho ya 22 ya Juakali ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yanayofanyika jijini Kampala, Uganda

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma akihutubia wakati wa maadhimisho ya SIKU YA TANZANIA kwenye maonesho ya 22 ya Juakali ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yanayofanyika jijini Kampala, Uganda

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma akifurahia muziki wa asili pamoja na wajasiriamali iliokuwa ukipigwa wakati wa maadhimisho ya SIKU YA TANZANIA kwenye maonesho ya 22 ya Juakali yanayoendelea jijini Kampala, Uganda.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma (kulia) akiangalia bidhaa za mjasiriamali kwenye maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu Juakali yanayoendelea jijini Kampala, Uganda.

Balozi wa Tanzania nchini Uganda Mhe. Aziz Mlima akitoa salaam kwa wajasiriamali wakati wa maadhimisho ya SIKU YA TANZANIA kwenye maonesho ya 22 ya Juakali ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yanayofanyika jijini Kampala, Uganda

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma (kulia) akiangalia bidhaa za mjasiriamali kwenye maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu Juakali yanayoendelea jijini Kampala, Uganda

Wajiriamali wa Tanzania wakiwa kwenye maonesho ya mavazi yaliyofanyika kwenye maonesho ya 22 ya Juakali yanayoendelea jijini Kampala, Uganda

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi na Watendaji wa Serikali na wajasiriamali`kwenye maonesho ya 22 ya Juakali yanayoendelea jijini Kampala, Uganda.


Monday, December 12, 2022

UBUNIFU, UBORA WA BIDHAA ZA WAJASIRIAMALI WATIA FORA MAONESHO YA JUAKALI

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma ameeleza kuridhishwa na namna Wajasiriamali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanavyoongeza viwango vya ubora na ubunifu katika huduma na bidhaa wanazozalisha. 

Waziri Riziki Pembe Juma ameeleza hayo alipozungumza kwenye sherehe za ufunguzi wa maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu kama Juakali, zilizofanyika tarehe 11 Disemba 2022 katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda. 

Amesema hatua iliyofikiwa na Wajasiriamali hao ni dalili nzuri ya kufikiwa kwa lengo la kuyafanya maonesho hayo y’a Juakali kuwa jukwaa la fursa ya kukuza masoko, kubadilishana uzoefu na teknolojia. 

Ameongeza kuwa hali hiyo inatokana na ukweli kuwa wajasiriamali hao bado wanahitaji kuendelea kujifunza zaidi, kubadilishana uzoefu na teknolojia baina yao katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Sote tumeshuhudia bidhaa mbalimbali zinazouzwa katika baadhi ya mabanda yaliyopo katika maonesho haya ambayo yamejumuisha nchi zote wanachama, bidhaa zina ubora na ubunifu wa hali ya juu. Ongezeko hili la ubunifu na ubora wa bidhaa za wajasiriamali hawa kila mwaka, ni dalili njema kuwa wana Afrika Mashariki katika siku za usoni tutakuwa na bidhaa zinazotosheleza mahitaji yetu kwa ubora na wingi hali ambayo itasaidia kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje” alisema Mhe. Waziri Riziki

Mhe. Waziri Riziki pia ameeleza kuridhishwa na namna Wanawake walivyojitokeza kushiriki katika maonesho hayo. 

Asilimia 87 ya idadi ya Wajasiriamali zaidi ya 300 wa Tanzania kwenye maonesho haya ni Wanawake, hali hii inadhirisha na uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan unatoa kipaumbele kwa wanawake kwa kuzingatia kuwa mwanamke ni kiungo thabiti katika maendeleo ya familia na nchi kwa ujumla, alisema Mhe. Waziri.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Robinah Nabbanja ambaye alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni katika sherehe hiyo ya ufunguzi wa maonesho, ametoa wito kwa Serikali za Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuendelea kufanya mabadiliko muhimu ya sera za uchumi ili ziweze kuleta msukumo katika kuongeza uzalishaji wa bidhaa na kurahisha zaidi ufanyaji wa biashara katika Jumuiya. 

“Kundi la wajasiriamali wadogo na wakati linachangia asilimia 60 ya pato la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, huku 99% ya biashara ndogo na kati zikimilikiwa na wazawa wa Afrika Mashariki, ni muhimu kukumbuka kuwa katika kila Waafrika 10; 6 kati ya hao wamejiajiri katika sekta ya biashara ndogo na kati, hivyo ni sawa na kusema kuwa, biashara ndogo na za kati zinazalisha wastani wa ajira 8 katika kila ajira 10 mpya,” alisema Mhe. Waziri Mkuu Nabbanja

Mheshimiwa Nabbanja alisisitiza kuwa endapo sera zitakuwa rafiki zaidi kiasi cha kutatua changamoto zinazowakabili wazalishaji wadogo italeta manufaa makubwa ya kiuchumi kwa Jumuiya, kwa kuwa asilimia 99 ya Wajasiriamali ni wazawa wa Afrika Mashariki hivyo maboresho hayo yatawanufaisha wao moja kwa moja na kuleta mchango mkubwa katika maendeleo ya viwanda na upatikanaji wa ajira za kutosha kwa Vijana na wanawake.

Mhe. Nabbanja amesema maonesho ya juakali ni jukwaa muhimu linalowawezesha Wajasiriamali kuonesha na kuuza huduma na bidhaa wanazozalisha, vilevile yanatoa fursa hadhimu kwa Wajasiriamali kuongeza wigo wa soko, kujifunza zaidi kuhusu ubunifu na kubadilishana uzoefu na teknolojia katika masuala mbalimbali kama vile kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na mifugo.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma (wa kwanza kulia) akisalimiana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Robinah Nabbanja (mwenye barakoa) kwenye sherehe ya ufunguzi wa maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu Juakali, iliyofanyika jijini Kampala, Uganda. 
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma akihutubia kwenye sherehe ya ufunguzi wa maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu Juakali, iliyofanyika jijini Kampala, Uganda. 
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Jamhuri ya Uganda Mhe. Robinah Nabbanja  akihutubia kwenye sherehe ya ufunguzi wa maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu Juakali, iliyofanyika jijini Kampala, Uganda. 
Viongozi na Watendaji wa Serikali, Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Taasisi mbalimbali wakiwa kwenye picha ya pamoja kwenye ufunguzi wa maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu Juakali, iliyofanyika jijini Kampala, Uganda. 
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Robinah Nabbanja wakiangalia bidhaa za mmoja wa wajasiriamali kwenye maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu Juakali, yanayoendelea jijini Kampala, Uganda. 
Mjasiriamali wa Tanzania alikimwonjesha mvinyo mteja kwenye maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu Juakali, yanayoendelea jijini Kampala, Uganda. 
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma (katika) akiwasili katika Viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda kushiriki ufunguzi rasmi wa maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu Juakali yanayoendelea nchini humo.

Tanzania na Oman Zainisha Maeneo ya Kushirikiana

Tanzania na Oman zimedhamiria kuchukua jitihada za makusudi kuimarisha ushikiano wa kiuchumi baina ya nchi hizo zenye uhusiano madhubuti wa kihistoria.

Hayo yamebainishwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi hizo, Mhe. Dkt. Stergomena L. Tax (Mb) na mwenyeji wake, Mhe.  Sayyid Badr Al Busaidi walipokutana pembezoni mwa Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Oman uliohitimishwa jijini Muscat tarehe 11 Desemba 2022.

Katika hotuba zao za kufunga Mkutano wa Pili wa JPC, Viongozi hao walieleza kuwa nchi zao zimekubaliana kuanzisha Kamati ya Pamoja ya Kufuatilia Utekelezaji wa Maazimio ya Mkutano huo ili kuwa na tija kwa pande zote mbili.

Kamati hiyo pamoja na mambo mengine, itahakikisha kuwa rasimu zote za mikataba na makubaliano zinakamilika na kutiwa saini ili kujenga mazingira ya kisheria ya kuimarisha uhusiano wa kindugu uliopo baina ya Tanzania na Oman.

Maeneo yaliyojadiliwa na ujumbe wa nchi hizo na kuwekewa mikakati ya utekelezaji ni pamoja na kilimo, elimu, nishati, biashara, uwekezaji, mawasiliano, mifugo na usafirishaji. Maeneo mengine ni uvuvi, utalii, michezo, utamaduni, madini, uhamiaji, fedha na udhibiti wa majanga ya moto.

Mkutano wa JPC kati ya Tanzania na Oman ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena L. Tax; Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato; Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu; Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab; Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Ndugu Kheri Mahimbali; na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar, Ndugu Mwanahamisi Adam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena L. Tax (Mb) na mwenyeji wake, Mhe.  Sayyid Badr Al Busaidi wakiwa katika mazungumzo pembezoni mwa Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Oman uliohitimishwa jijini Muscat tarehe 11 Desemba 2022.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena L. Tax (Mb) akiwa katika picha ya pamoja  na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Mhe.  Sayyid Badr Al Busaidi waliipokutana pembezoni mwa Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Oman uliohitimishwa jijini Muscat tarehe 11 Desemba 2022.

Meza Kuu wakati wa Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Oman uliohitimishwa jijini Muscat tarehe 11 Desemba 2022.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena L. Tax (Mb) akibadilishana nyaraka zenye masuala yaliyoafikiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Mhe.  Sayyid Badr Al Busaidi wakati wa Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Oman uliohitimishwa jijini Muscat tarehe 11 Desemba 2022.

 

Sunday, December 11, 2022

ZAIDI YA WAJASIRIAMALI 300 WASHIRIKI MAONESHO YA JUAKALI UGANDA


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikisha ushiriki wa Wajasiriamali zaidi ya 300 katika maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu Juakali yanayofanyika katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda kuanzia terehe 8 - 18 Disemba 2022.

Maonesho hayo yanayoongozwa na kauli mbiu “Nunua Bidhaa za Afrika Mashariki, ili kujenga Uchumi Stahimilivu na Endelevu wa Afrika Mashariki” yanalenga kutoa fursa kwa Wajasiriamali ya kuonesha huduma na bidhaa mbalimbali wanazozalisha na kubadilishana uzoefu, ujuzi na taarifa na wajasiriamali wenzao katika Jumuiya, sambamba na kukuza wigo wa masoko mapya.

Maonesho hayo ambayo yamevutia Wajasiriamali zaidi 1500 kutoka Nchi zote saba (7) Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, na ikikadiriwa 75% kati yao kuwa ni wanawake, yamesheheni bidhaa mbalimbali zenye asili ya Jumuiya. Kwa upande wa wajisiriamali wa Tanzania miongoni mwa bidhaa na huduma wanazozionesha ni pamoja na mavazi ya asili, bidhaa za baharini, bidhaa za kilimo zilizoongezewa thamani, mashine za kuzalisha bidhaa mbalimbali, madawa ya asili, vito vya thamani na madini, utalii, na bidhaa za ngozi kama vile viatu, mabegi na mikoba. 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Wajasiliamali wa Tanzania wameonesha kuridhishwa kwao na kupongeza juhudi na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania chini ya Uongozi madhubuti wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya biashara ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kushiriki katika maonesho hayo. 

“Kutokana na gharama kubwa za kusafirisha bidhaa zetu hadi hapa nchini Uganda, wengi wetu tusingeweza kumudu, hivyo tusingeweza kuwa na uwakilishi wa kutosha katika maonesho haya. Hata hivyo kutokana na dhamira ya Serikali ya kutusaidia wajasiriamali kukua kibiashara kupitia kupata masoko mapya ya huduma na bidhaa tunazozalisha na kutuongezea ujuzi na uzoefu imeona ni vyema ituwezeshe katika maeneo mbalimbali ikiwemo kugharamia usafiri wa kutuleta hapa nchini Uganda na kuturudisha nyumbani baada ya maonesho”. Ameeleza Lilian Sambu mjasiliamali. 

Maonesho ya Juakali yalifanyika kwa mara ya kwanza mwezi Novemba 1999 jijini Arusha, ambapo yaliambatana na tukio la kihistoria la kusainiwa kwa Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika maonesho hayo, Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki walielekeza kuwa yafanyike kila mwaka kwa mzunguko kati ya Nchi Wanachama ili kuimarisha mtangamano wa jamii na uchumi wa watu wa Afrika Mashariki.
Bw. Joseph Ndunguru (kulia) mzalishaji wa bidhaa za vyakula kutoka mjini Mtwara akielezea bidhaa zake kwa mteja aleyetembelea banda lake kwenye maonesho ya 22 ya Juakali yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda.
Wateja wakichangamkia bidhaa za mmoja wa wajasiriamali wa Tanzania (kulia) walipotembelea banda lake katika maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu Juakali yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda.
Sehemu ya wajasiriamali wa Tanzania wakipanga bidhaa zao kweye maonesho 22 ya Juakali yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda 
Wateja wakiangali bidhaa za mmoja wa wajasiriamali wa Tanzania (kulia) walipotembelea banda lake kwenye maonesho ya 22 ya Juakali yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda.
Mkurugenzi Mtendaji wa Just Products Bi. Judith M. Lugembe akifuatilia taarifa ya biashara yake katika maonesho ya 22 ya Juakali yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda
Naibu Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala Mhandisi Steven Mlote akifuatilia maelezo ya mjasirimali alipotembelea banda la Tanzani kwenye maonesho ya 22 ya Juakali yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda
Mkurungenzi wa Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,Ajira,Vijana na Wenye Uemavu) Bw. Ally Msaki akizungumza na Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza na Waziri anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki wa Uganda Mhe. Rebecca Alitwala Kadaga alipotembelea banda la Tanzania kwenye maonesho ya 22 ya Juakali yanayoendelea jijini Kampala, Uganda
Mkurugenzi Msaidizi wa Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji Bw. Athuman Nkungu akiangalia bidhaa ya mmoja wa wajasiriamali alipotembelea meza yake kweye maonesho 22 ya Juakali yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda 
Sehemu ya wajasiriamali wa Tanzania wakimsalimia Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza na Waziri anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki wa Uganda Mhe. Rebecca Alitwala Kadaga (yupo kwenye gari inayoonekana pichani) alipotembelea banda la Tanzania kweye maonesho 22 ya Juakali yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda 
Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza na Waziri anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki wa Uganda Mhe. Rebecca Alitwala Kadaga (mwenye chupa ya mvinyo mkononi) akipokea zawadi kutoka kwa mmoja wa wajasiriamali wa Tanzania kwenye maonesho ya 22 ya Juakali yanayoendelea jijini Kampala, Uganda

Wednesday, December 7, 2022

MHE. DKT. TAX AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI KUTOKA VIETNAM


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amewakaribisha wawekezaji kutoka Vietnam kuja nchini kuwekeza katika sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano pamoja na Kilimo.


Mhe. Waziri Tax ameyasema hayo alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Habari na Mawasiliano  wa Vietnam na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha nchi hiyo Mhe.  Nguyen Manh Hung alipomtembelea Ofisini kwake jijini Dodoma hivi karibuni.


Mhe. Dkt Tax amesema Tanzania inathamini ushirikiano kati yake na Vietnam ambayo imepiga hatua  kubwa katika maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano na kwamba kupitia ushirikiano huo Tanzania  imejipanga kunufaka katika sekta hiyo na nyingine zenye manufaa kati ya nchi hizi mbili.


Ameongeza kusema nchi hiyo ambayo tayari imewekeza kwenye sekta ya Mawasiliano hapa nchini kupitia Kampuni ya Simu ya Halotel, bado inakaribishwa kuwekeza zaidi katika sekta hiyo hususan kwenye miundombinu ya kidijiti na kwamba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuhakikisha wawekezaji wanafanikisha malengo yao lakini pia Taifa linanufaika kupitia uwekezaji.


“Tanzania inaendelea kujiimarisha katika Sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi. Kama ulivyosema Mhe. Waziri, Vietnam ni miongoni mwa nchi 10 duniani zilizopiga hatua kubwa katika sekta hiyo,  naendelea kuhimiza wawekezaji zaidi kutoka nchini kwako kuja kuwekeza kwenye sekta hiyo lakini pia na sekta nyingine kama Kilimo hususan kile cha biashara na usindikaji wa mazao ya kilimo” alisema Dkt. Tax.

 

Kwa upande wake, Mhe. Nguyen Manh Hung amepongeza jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji na kwamba nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali yanachangia maendeleo ya wananchi.


Akizungumzia uwekezaji kupitia kampuni ya Viettel ambayo ni kampuni mama ya mtandao wa simu wa Halotel hapa nchini, amesema nchi yake imewekeza mtaji wa takribani Dola bilioni moja katika miundombinu ya mtandao huo ambao umejikita kuwahudumia zaidi wananchi wa vijijini na kwamba hadi sasa Mtandao huo umeajiri watanzania 1,000.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Habari na Mawasiliano wa Vietnam na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha nchi hiyo Mhe. Nguyen Manh Hung alipomtembelea Ofisini kwake jijini Dodoma hivi karibuni.
Sehemu ya ujumbe ulioambatana na Mhe. Mahn Hung akiwemo Balozi wa Vietnam nchini Mhe. Nguyen Nam Tien (kulia) wakifuatilia mazungumzo
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania ulioshiriki mazungumzo. Kushoto ni Bw. John Kambona, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki 

 

VACANCY ANNOUNCEMENT