Friday, October 27, 2023

TANZANIA, SADC ORGAN TROIKA KUIMARISHA USHIRIKIANO

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeahidi kuendelea kushirikiana na Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Organ Troika).

Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) alipokutana na Mkurugenzi wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, Prof. Kula Ishmael Theletsane katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo yao, Balozi Mbarouk amemhakikishia Prof. Theletsane kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Sekretarieti ya SADC katika kuhakikisha kuwa taasisi hiyo inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi na ufasaha. 

Viongozi hao wamezungumzia pia mipango ya uendelezwaji wa Kituo cha Kupambana na Ugaidi cha Kanda cha (SADC-RCTC) ambacho Tanzania ni mwenyeji wake. Mipango hiyo ni pamoja na mkakati wa kukifanya kituo hicho kuwa Kituo cha Umahiri pamoja na kupata watumishi na rasilimali kwa ajili ya uendeshaji wa kituo hicho. 

Kwa upande wake Prof. Theletsane ameishukuru Tanzania kwa ushirikiano ambao imeutoa katika kuanzisha kituo hicho na kueleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika uendelezwaji wake.  “Tunaipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada zake za kuendesha kituo kwa ufanisi, nasi pia tunaahidi kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha kuwa ulinzi na usalama vinaimarika kikanda,” alisema Prof. Theletsane. 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akimkaribisha Mkurugenzi wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, Prof. Kula Ishmael Theletsane katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akimsikiliza Mkurugenzi wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, Prof. Kula Ishmael Theletsane walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akimsikiliza Mkurugenzi wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, Prof. Kula Ishmael Theletsane walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam




WAFANYABIASHARA WA ALGERIA KUSHIRIKI MAONESHO YA SABASABA MWAKA 2024

Rais wa Kituo cha Uwekezaji na Maendeleo cha Waarabu na Afrika (Arab-African Centre for Investment and Development-CAAID), Dkt. Amine Boutalbi amesema kuwa CAAID inaratibu ushiriki wa wafanyabiashara wa Algeria kwenye maonesho ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) maarufu Maonesho ya Saba Saba kwa mwaka 2024.

Amesema hayo wakati wa mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Iman Njalikai yaliyofanyika kwenye Ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Algiers tarehe 26 Oktoba 2023.

Aidha, Dkt. Amine Boutalbi ameahidi kuwa CAAID itashirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Algeria kuratibu kongamano maalum la wafanyabishara wa Algeria litakalofanyika nchini Tanzania mwaka 2024 kwa lengo la kuimarisha uwekezaji na biashara kati ya wafanyabiashara wa nchi hizi mbili.

Kwa upande wake, Balozi Njalikai ameahidi kuwa atashirikiana na kituo hicho ambacho ni kiungo muhimu kati ya Ubalozi na Sekta Binafsi nchini Algeria. 

Mhe. Balozi amehidi pia ofisi yake itashirikiana na mamlaka za Tanzania hususan TPSF, TIC na TANTRADE ili kufanikisha ushiriki wa wafanyabiashara wa Tanzania kwenye makongamano ya uwekezaji na biashara yanayoandaliwa na Kituo cha CAAID mwezi Mei 2024.

Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Iman Njalikai akimkaribisha ofisini kwake Rais wa Kituo cha Uwekezaji na Maendeleo cha Waarabu na Afrika (Arab-African Centre for Investment and Development-CAAID), Dkt. Amine Boutalbi kwa ajili ya mazungumzo

Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Iman Njalikai akiwa katika mazungumzo na Rais wa Kituo cha Uwekezaji na Maendeleo cha Waarabu na Afrika (Arab-African Centre for Investment and Development-CAAID), Dkt. Amine Boutalbi 

Thursday, October 26, 2023

TANZANIA YAPONGEZWA KWA KUWEKA MIUNDOMBINU WEZESHI KWA WALEMAVU


Serikali ya Tanzania imepongezwa kwa kuendelea kusimamia haki za binadamu kwa makundi maalum ya  wazee na watu wenye ulemavu kwa kuweka miundombinu wezeshi ya kuwapunguzia adha mbalimbali ikiwemo matumizi ya lugha ya alama kwenye mikutano.

 

Pongezi hizo zimetolewa tarehe 26 Oktoba 2023 wakati wa uwasilishwaji agenda kuhusu Utekelezaji wa Haki za Binadamu kwa Makundi Maalum ya Wazee na Watu wenye Ulemavu kwenye Kikao cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kinachoendelea jijini Arusha.

 

Akizungumza kuhusu nafasi ya Tanzania katika kusimamia haki za binadamu kwa makundi maalum ya wazee na wenye ulemavu, Mkurgenzi Msaidizi wa Idara ya Haki za Binadamu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Richard Kilanga amesema kuwa Serikali imepiga hatua katika kuhakikisha makundi haya maalum ya watu wanapata haki zao za msingi kama wananchi wengine ikiwemo chakula, malazi na mavazi.

 

Amesema kutokana na kuthamini mchango wa wazee  na watu wenye ulemavu kwenye maendeleo ya  nchi Ibara ya 11 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inaelekeza mamlaka ya nchi kuweka utaratibu wa kuwawezesha kupata elimu na msaada kutoka kwa jamii wakati wa uzee, maradhi  au hali ya ulemavu na katika hali nyinginezo za mtu kama hajiwezi.

 

Ameongeza kusema katika kutekeleza jukumu la kusimamia kikamilifu ulinzi wa haki za binadamu kwa makundi  ya wazee na walemavu, mwaka 2004 ilianzishawa Sera ya Watu wenye Ulemavu kwa upande wa Tanzania Bara na Sera ya aina hiyo ilianziswha Zanzibar mwaka 2018. Sera hizi zimeainisha namna watu wenye ulemavu wanavyopata huduma za elimu jumuishi, kazi, ajira na huduma za utangamano.

 

Pamoja na kuwepo kwa Sera hizo Serikali zote zimeweka Sheria ya Utekelezaji wa Sera hizo  mwaka 2010 kwa Tanzania Bara na mwaka 2022 kwa upande wa Zanzibar. Sheria hizi pamoja na mambo mengine zinaweka misingi muhimu kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu zinahifadhiwa na kulindwa ikiwa ni pamoja na kuheshimu utu wa mtu, uhuru wa mtu kufanya maamuzi, kutobaguliwa na kushiriki katika masuala yote ya kijamii, kupata taarifa, kuzingatia usawa wa wanawake na waaume na mahitaji yao na upatikanaji wa kiwango cha maisha yanayotakiwa na hifadhi ya jamii.

 

Pia mabaraza ya taifa kuhusu watu wenye ulemavu pamoja na Idara maalum kushughulikia masuala ya watu wenye ulemavu yameanzishwa Tanzania Bara na Zanzibar.

 

Kuhusu Wazee. Bw. Kilanga amekieleza kikao hicho kuwa, Serikali ya Tanzania imeendelea kuwatambua na kutoa huduma za msingi za chakula, malazi, mavazi na matibabu kwa wazee wasiojiweza na watu wasiokuwa na watu wa kuwahudumia katika makazi 14 kwa upande wa Tanzania Bara.

 

“Zaidi ya wazee milioni mbili wametambuliwa katika mikoa 26. Kati ya wazee hao wananawake ni 735,169 na wanaume ni 1,382,468 kati ya wazee 586,772 sawasawa na asilimia 27 wamepatiwa vitambulisho vya bima ya afya kwa ajili ya matibabu ambapo wanawake ni  331,103 na wanaume ni 255,669,” alifafanua Bw. Kilanga.

 

Kikao cha Kawaida cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kilifunguliwa rasmi jijini Arusha tarehe 20 Oktoba 2023 na kinatarajiwa kumalizika tarehe 09 Novemba, 2023. Pamoja na mambo mengine kikao kinapokea na kujadili agenda mbalimbali zinazohusu haki za binadamu katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Richard Kilanga  akitoa maelezo ya nchi kuhusu nafasi ya Tanzania katika kusimamia haki za binadamu kwa makundi maalum ya wazee na wenye ulemavu  wakati wa vikao vya Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu vinavyofanyika jijini Arusha.Wakati wa kkao hicho, Tanzania ilipongezwa kwa kutekeleza sheria zinazosimamia makundi hayo iikiwemo kuweka mazingira wezeshi kwa watu wenye ulemavu ikiwemo matumizi ya lugha ya alama

Mkutano ukiendelea

 

WATANZANIA WAWILI HAWAJULIKANI WALIPO NCHINI ISRAEL


 


TWO TANZANIANS ARE MISSING IN ISRAEL


 

Wednesday, October 25, 2023

TANZANIA, AUSTRIA KUSHIRIKIANA ELIMU YA UFUNDI, UTALII, BIASHARA NA UWEKEZAJI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Austria zimekubaliana kuimarisha sekta za elimu ya ufundi pamoja na utalii, biashara na uwekezaji.

Makubaliano hayo yameafikiwa katika Mkutano wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angelah Kairuki (Mb) na Waziri wa Kazi na Uchumi wa Austria, Mhe. Prof. Martin Kocher walipokutana katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Jijini Dar es Salaam.

Waziri Kairuki amesema kuwa wamekubaliana kushirikiana katika masuala ya kilimo, elimu ya ufundi ambapo Tanzania kwa sasa msukumo wake ni elimu ya ufundi na tayari serikali imeanza kuboresha sera ya elimu na mitaala ya elimu.

“Austria wameonesha nia ya kushirikiana na Tanzania katika masuala ya tasnia ya ukarimu na utalii, wenzetu kwa mwaka wanapata watalii takriban milioni 40 na wamepiga hatua kubwa, nimefurahishwa pia kuona katika ujumbe alioambatana nao Prof. Kocher kuna wafanyabiashara na wawekezaji ambao wameonesha nia ya kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya utalii, uwekezaji wa hoteli na mnyororo mzima wa thamani katika sekta ya utalii alisema Waziri Kairuki.

Waziri Kairuki aliongeza kuwa pamoja na mambo mengine, wamekubaliana kushirikiana katika sekta za afya, pamoja na sekta binafsi nchini kwa kuwa mazingira ya biashara na uwekezaji ni salama na rafiki. 

Naye Waziri wa Kazi na Uchumi wa Austria, Mhe. Prof. Martin Kocher amesema Austria itaendeleaa kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali hususan miundombinu, kilimo, usindikaji wa chakula, elimu ya ufundi, afya, ajira/kazi, nishati pamoja na utalii kwa maslahi ya pande zote mbili.

“Tanzania kufungua Ubalozi wake nchini Austria, umetuwezesha kushirikiana katika sekta mbalimbali mathalan sekta ya elimu ya ufundi pamoja na utalii,” alisema Prof. Kocher 

Prof. Kocher aliongeza kuwa asilimia 40 ya vijana nchini Austria wamekuwa wakipatiwa elimu ya ufundi katika fani tofautitofauti, hivyo Austria inaamini kuwa endapo watashirikiana na Tanzania kuwapatia vijana elimu ya ufundi itasaidia kuwawezesha kupata fani mbalimbali zitakazo wasaidia kujenga Maisha yao na kuinua uchumi wa taifa kwa ujumla.

Akiongelea kuhusu sekta ya utalii, Prof. Kocher amesema kuwa Austria itaendelea kushirikiana na Tanzania kuhakikisha kuwa Austria na Tanzania zinakuwa na utalii endelevu pamoja na kuhakikisha kuwa mataifa hayo yanakuwa na vivutio bora vya utalii kwa miongo ijayo. 

Pamoja na mambo mengine, mazungumzo ya viongozi hao yalijikita katika kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Austria kwa manufaa ya pande zote mbili.

Mhe. Waziri Kocher yupo nchini Tanzania kwa ziara yake ya kikazi ya siku moja na ameambatana na ujumbe wa wawekezaji 20 kutoka Austria wanaolenga kuwekeza nchini Tanzania katika sekta za utalii, afya, nishati, elimu, ujenzi na miundombinu.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angelah Kairuki akizungumza na Waziri wa Kazi na Uchumi wa Austria, Mhe. Prof. Martin Kocher (hayupo pichani) wakati walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Kazi na Uchumi wa Austria, Mhe. Prof. Martin Kocher akizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angelah Kairuki (hayupo pichani) wakati walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Jijini Dar es Salaam

Mazungumzo baina ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angelah Kairuki na Waziri wa Kazi na Uchumi wa Austria, Mhe. Prof. Martin Kocher  yakiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angelah Kairuki akiagana na Waziri wa Kazi na Uchumi wa Austria, Mhe. Prof. Martin Kocher  baada ya kumalizika kwa mazungumzo yao katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angelah Kairuki akimkabidhi zawadi ya picha ya Mlima Kilimanjaro Waziri wa Kazi na Uchumi wa Austria, Mhe. Prof. Martin Kocher baada ya kumalizika kwa mazungumzo yao katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Jijini Dar es Salaam



Tuesday, October 24, 2023

SERIKALI YAWEKA MIKAKATI YA KUINUA VIJANA KIUCHUMI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha inainua ustawi wa vijana kiuchumi.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Maliasili na Utalii,  Mhe. Angellah Kairuki (Mb.) kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) katika Maadhimisho ya miaka 78 ya Umoja wa Mataifa yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam. 

Waziri Kairuki amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikutumia njia mbalimbali kuhakikisha vijana wanapiga hatua kiuchumi.

"Kwa upande wa Tanzania Bara, Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 inafanyiwa mapitio ili kuakisi hali ya sasa ya maendeleo ya vijana, vipaumbele na changamoto," Mhe. Kairuki alisema. 

Waziri Kairuki ametaja moja ya mkakati ni kuwezesha vijana kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) ambalo hutoa mikopo kwa vijana wajasiriamali na uanzishwaji wa zaidi ya mifuko 45 maalum katika wizara na idara mbalimbali ili kuhakikisha kuwa vijana wanawezeshwa kiuchumi. 

Waziri Kairuki ameongeza kuwa Tanzania imehakikisha kuna ongezeko la upatikanaji wa huduma za ushauri nasaha rafiki kwa vijana kupitia programu ya Afya ya Ujinsia na Haki za Uzazi na kuongeza upatikanaji wa huduma za matunzo na matibabu ya VVU. 

Amesema kupitia Mpango wa Kujenga Kesho Bora – YOUTH INITIATIVE FOR AGRIBUSINESS, Serikali inatarajia kuongeza ushiriki wa vijana katika sekta ya kilimo na kuharakisha kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo kwa ajili ya maisha endelevu na bora. 

Waziri Kairuki  amewaasa vijana kuwa wabunifu na kutumia teknolojia ambayo ni nguzo muhimu za kukuza uwezeshaji wa vijana.

"Ni muhimu kusaidia wajasiriamali wachanga katika kubadilisha mawazo yao kuwa biashara zinazofaa, endelevu kupitia kujenga uwezo na upatikanaji wa masoko na matumizi ya teknolojia na uvumbuzi." amesema.

Naye Mratibu Mkazi wa UN Tanzania, Bw. Zlatan Milišić alisema Umoja wa Mataifa pamoja na taasisi zake utaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuandaa na kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) pamoja na kuwawezesha vijana kutimiza malengo yao.

Bw. Milisic amesema Umoja wa Mataifa utaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuwawezesha vijana kutimiza malengo yao na ya Serikali kwa ujumla.

Maadhimisho ya mwaka huu yameongozwa na kaulimbiu isemayo “Kuwekeza leo kwa ajili ya kesho kwa kuinua vijana wa Kitanzania”.

Waziri wa Maliasili na Utalii,  Mhe. Angellah Kairuki akihutubia katika Maadhimisho ya miaka 78 ya Umoja wa Mataifa yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Maliasili na Utalii,  Mhe. Angellah Kairuki akikagua gwaride katika Maadhimisho ya miaka 78 ya Umoja wa Mataifa yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Maliasili na Utalii,  Mhe. Angellah Kairuki katika picha ya pamoja wanafunzi na Viongozi mbalimbali wakati wa Maadhimisho ya miaka 78 ya Umoja wa Mataifa yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam




BALOZI MBAROUK ASAINI KITABU CHA MAOMBOLEZO UBALOZI WA FINLAND

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) amesaini kitabu cha maombolezo Ubalozi wa Finland kufuatia kifo cha Rais wa zamani wa nchi hiyo Mhe. Martti Ahtisaari kilichotokea tarehe 16 Oktoba 2023. 

Mhe. Ahtisaari amefariki akiwa na umri wa miaka 86, alikuwa Rais wa Finland kuanzia mwaka 1994 hadi 2000 na Balozi Mstaafu wa Finland nchini Tanzania mwaka 1973 hadi 1976

Mara baada ya kusaini kitabu cha maombolezo, Balozi Mbarouk amesema Hayati Ahtisaari atakumbukwa daima kama mwanadiplomasia mashuhuri ambaye alijitolea maisha yake yote katika masuala ya upatanishi

“Kiongozi huyo atakumbukwa kama kiongozi mahiri wa Finland aliyeimarisha ushirikiano wa karibu Kati ya Finland na Tanzania kupitia cheo chake cha Ubalozi alichohudumu nchini mwaka 1973-1976 . 

Kupitia nyadhifa hiyo Hayati Ahtisaari alifanya kazi kama rafiki wa karibu na Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Hayati Benjamin William Mkapa na Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete.

Kupitia urafiki huo, Hayati Ahtisaari alishirikiana na MaRais Wastaafu kuanzisha mikakati ya kutafuta amani kwenye nchi zenye migogoro barani Afrika hususan Burundi kupitia Taasisi ya Mpango wa Utatuzi wa Migogoro (CMI) ambaye ndiye mwanzilishi.

Kwa kutambuliwa kama mpatanishi wa amani, Hayati Ahtisaari alitunukiwa medani ya amani duniani ya Nobel mwaka 2008 na alisifiwa kwa kukuza undugu baina ya Mataifa kwa mtindo wake wa kujitolea bila kujionesha

“Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunapenda kutoa salamu zetu za pole kwa wananchi na serikali ya Finland pamoja na familia kwa kuondokewa na kiongozi bora na mpenda amani. Mungu ampumzishe kwa amani,” aliongeza Mhe. Balozi Mbarouk
Balozi wa Finland nchini, Mhe. Theresa Zitting akimkaribisha Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk katika Ofisi za Ubalozi huo wakati Balozi Mbarouk alipowasili kusaini kitabu cha maombolezo kufuatia kifo cha Rais wa zamani wa nchi hiyo Mhe. Martti Ahtisaari kilichotokea tarehe 16 Oktoba 2023

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akisaini kitabu cha maombolezo Ubalozi wa Finland kufuatia kifo cha Rais wa zamani wa nchi hiyo Mhe. Martti Ahtisaari kilichotokea tarehe 16 Oktoba 2023

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akisaini kitabu cha maombolezo Ubalozi wa Finland kufuatia kifo cha Rais wa zamani wa nchi hiyo Mhe. Martti Ahtisaari kilichotokea tarehe 16 Oktoba 2023



Monday, October 23, 2023

TANZANIA YAPONGEZWA KWA KUWEKA MIFUMO SHIRIKISHI KATIKA KUIMARISHA HAKI ZA BINADAMU NA WATU

Mwenyekiti  wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kutengeneza mifumo shirikishi yenye lengo la kukuza na kuimarisha haki za binadamu na watu nchini.

 

Mhe. Jaji Mwaimu ametoa pongezi hizo leo tarehe 23 Oktoba 2023 wakati akihutubia wajumbe wa Kikao cha Kawaida cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kinachoendelea jijini Arusha.

 

Mhe. Jaji Mwaimu amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanikiwa kuweka mifumo shirikishi inayowezesha wadau mbalimbali kujadili mambo muhimu ya kitaifa ikiwemo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi ikiwa ni jitihada za Serikali za kuensdelea kuimarisha na kuboresha usimamizi wa haki za binadamu na watu.

 

Akizitaja  hatua za Serikali zinazodhihirisha mwenendo mzuri wa kuimarika na kustawi kwa haki za bianadamu na Watu nchini kuwa ni pamoja na  kuwekwa mfumo shirikishi  wa kujadili mambo muhimu ya Kitaifa na kuimarika kwa demokrasia ambapo Mhe. Rais Samia aliunda Kamati Maalum kwa ajili ya kutathmini mwenendo mzima wa masuala ya siasa nchini.

 

“Tunapenda katika mkutano huu kuweka msisitizo katika masuala machache ambayo Tume imeona kwamba yana mwelekeo chanya na yamejipambanua kutokana na umuhimu wake. Kwanza ni hatua ya Serikali ya Tanzania ya kuweka mfumo shirikishi wa kujadili mambo muhimu ya kitaifa. Mfano hivi karibuni Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kushirikiana na vyama vya siasa nchini walikaa pamoja jijini Dar es Salaam kujadili taarifa ya kamati Maalum iliyoundwa ba Mhe. Rais Dkt. Samia  kwa ajili ya kukuza mwenendo mzima wa masuala ya siasa ikiwemo demokrasia ya vyama vingi.

 

Pia amepongeza hatua ya kuzinduliwa kwa Kampeni ya miaka mitatu ya Mama Samia ya Msaada wa Kisheria ambayo mpaka sasa imetekelezwa kwenye mikoa mitano na kuwafikia zaidi ya wananchi 2,870 waliopo kwenye maeneo 39 ya vizuizi  na zaidi ya wananchi 361,740 waliopo uraiani wamehudumiwa kwa ukamilifu na kufaidika.

 

Amesema, miongoni mwa waliofaidika na Kampeni hii ni wahamiaji raia wa Ethiopia zaidi ya 80 ambao walirejeshwa nchini kwao baada ya kuwa vizuizini kwa changamoto za uhamiaji.

 

Mhe. Jaji Mstaafu Mwaimu pia aliutaja mchakato ulioanzishw ana Mhe. Rais Dkt. Samia wa kupitia upya mfumo wa Taasisi zinazoshughulikia masuala ya Haki Jinai kuwa ni wenye tija kubwa  na wa kupigiw amfano kwenye kuimarisha  Nyanja za haki za binadamu na watu nchini.

 

“Tume imeona suala la Mhe. Rais Dkt. Samia la kuanzisha mchakato wa kupitia upya mfumo wa taasisi zinazoshughulikia masuala ya haki jinai kuwa ni jambo kubwa na lenye tija. Mchakato huu ambao unalenga kufanya mapitio ya mnyororo mzima wa haki jinai kwa kushughulikia dosari za upatikanaji wa haki za binadamu utaleta tija na kuimarisha haki za binadamu hapa nchini pale utakapokamilika,” alisisitiza Mhe. Jaji Mwaimu.

 

Pia Tume hiyo imepongeza utayari wa Serikali wa kuanza kuandaa Mpango Kazi wa Taifa wa Biashara na Haki za Binadamu ambao ukikamilika utawezesha kuingiza katika mfumo Kanuni za Umoja wa Mataifa za masuala ya Haki za Binadamu na Biashara na kuwahakikishi a Watanzania kufanya shughuli za biashara kwa namna inayozingatia na kuhifadhi haki za binadamu.

 

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ni Idara huru ya Serikali iliyoanzishwa mwaka 2001 ambayo pamoja na mambo mengine husimamia utekelezaji wa haki za binadamu na watu nchini.

 

Kikao cha Kawaida cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kilifunguliwa rasmi tarehe 20 Oktoba 2023 na kinatarajiwa kumalizika tarehe 09 Novemba, 2023


Mwenyekiti  wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu akizungumza wakati wa Kikao cha Kawaida cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kinachoendelea jijini Arusha.  Katika hotuba yake Mhe. Jaji Mwaimu ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuanzisha mifumo shirikishi ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kuimarisha masuala ya haki za binadamu na watu na demokrasia nchini. Kikao cha 77 kilifunguliwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi tarehe 20 Oktoba 2023 na kitamalizika tarehe 09 Novemba 2023
Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na watu, Mhe. Janet Ratatouille Sallah-Njie (wa tatu kushoto) akiendesha kikao cha 77 cha Tume hiyo kinachoendelea jijini Arusha.
Sehemu ya Washiriki wa Kikao cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu naWatu wakifuatilia kikao

Sehemu nyingine ya washiriki

Kikao kikiendelea