Friday, November 24, 2023

SHIRIKISHO LA JAMHURI YA SOMALIA LAKUBALIWA KUJIUNGA NA JUMUIYA YA EAC



Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwa kwenye Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika katika viwanja vya Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha

Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umeridhia ombi la Shirikisho la Jamhuri ya Somalia kujiunga na Jumuiya hiyo katika Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Jumuiya hiyo uliofanyika jijini Arusha.

Mkutano uliopitisha ombi hilo umehudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. William Ruto, Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Evereste Ndayishimiye, Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Sudani Kusini Mhe. Silver Kiir, Waziri Mkuu wa Rwanda aliyemwakilisha Rais Paul Kagame na Makamu Rais wa DRC aliyemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Mhe. Antonie Tshisekedi.

Mkutano huo pia ulihudhuria na Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Somalia Mhe. Hassan Sheikh Mahmoud ambaye alialikwa kuhudhuria mkutano huo.

Mkutano huu pia ulipokea na kuridhia kwa kauli moja mapendekezo ya Majadiliano ya Juu kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi na Usalama wa Chakula yaliyofanyika jijini Arusha tarehe 23 Novemba na kuhudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Mawaziri wa Kisekta.

Kuridhiwa kwa mapendekezo hayo kunaifanya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwenda katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabia Nchi (COP28) utakaofanyika nchini UAE kuanzia tarehe 28 Novemba 2023 na msimamo mmoja wa nchi wanachama.

Mkutano huo ulijadili na kukubaliana juu ya masuala mbalimbali ya Mtangamano wa Afrika Mashariki ambapo wameazimia kuendelea kuulinda na kuukuza mtangamano huo kwa lengo la kuwaenzi waasisi wake na kuinua kipato cha watu na kutoa rai za kutokuruhusu tofauti ndogondogo kuleta mtafaruku ndani ya Jumuiya

Viongozi hao wameitakia heri Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika nchini humo.

Katika Mkutano huo Wanafunzi sita kutoka nchi wanachama walishinda tuizo ya uanjdishi wa Insha na kupatiwa vyeti na zawadi ya fedha taslimu. Wanafunzi walioshinda tuzo hizo ni Lalom Joselin kutoka Sudani Kusini aliyepata Dola 550 za Marekani, Ilimfuwe Aija kutoka Burundi alipata dola 600 za Marekani, Amoron Evelyn kutoka Uganda alipata Dola 770 za Marekani, Irasore sania kutoka Rwanda alipata Dola 1000, Idirisa Musa Hamadi kutoka Tanzania alipata Dola 1200 za Marekani na Austin Alego Angoya 1kutoka Kenya alipata Dola 1500 za Marekani.

Wanafunzi hao washindi wa Tuzo hizo pia wamepata zawadi ya kutembelea Hifadhi ya Taifa Tarangire, Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro na Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro kuanzia tarehe 25 -27 Novemba 2023.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia kwenye Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika katika viwanja vya Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha

Rais wa Burundi Mhe. Évariste Ndayishimiye ambaye amemaliza muda wake wa Uenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki akimkabidhi vitendea kazi Mwenyekiti Mpya wa Jumuiya hiyo Rais wa Sudan Kusini Mhe. Salva Kiir Mayardit wakati wa Mkutano wa kawaida wa 23 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha.
Viongozi mbalimbali wakifuatilia Mkutano wa kawaida wa 23 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliokuwa ukiendelea jijini Arusha.
Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwa wamesimama wakati wimbo wa Afrika Mashariki unapigwa kwenye Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika katika viwanja vya Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akifuatilia Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliokuwa ukiendelea katika viwanja vya Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha
Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato (Mb.) akifuatilia Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliokuwa ukiendelea katika viwanja vya Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akifuatilia Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliokuwa ukiendelea katika viwanja vya Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha
Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Dkt. William Ruto akizungumza kwenye Mkutano wa 23 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika katika Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha
Rais wa Somalia Mhe. Hassan Sheikh Mohamud akizungumza kwenye Mkutano wa 23 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika katika Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha. Somalia imekuwa Mwanachama mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya ombi lake la kujiunga na Jumuiya hiyo kuridhiwa kwenye mkutano.
Rais wa Burundi Mhe. Évariste Ndayishimiye akitoa hotuba ya ufunguzi kwenye Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika katika viwanja vya Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha
Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Museveni akihutuba ya ufunguzi kwenye Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika katika viwanja vya Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha

Idirisa Musa Hamadi kutoka Tanzania akipokea zawadi ya uandishi wa Insha

NAIBU WAZIRI BYABATO AKUTANA NA NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA JAMHURI YA KOREA

Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato akisalimiana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea, Bi. Oh Youngju walipokutana kwa mazungumzo pembezoni mwa Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha.


Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato, amekutana na kuzungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea, Bi. Oh Youngju, pembezoni mwa Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha.

Katika mazungumzo yao viongozi hao wamekubaliana kuendelea kuimarisha uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea kwa manufaa ya pande zote mbili.

Akizungumza katika mkutano huo Naibu Waziri Mhe. Byabato alimuelezea Bi. Youngju kuridhishwa kwa Tanzania juu ya ushirikiano na uhusiano uliopo kati yake na Jamhuri ya Korea na kuahidi kuendelea kushirikiana na nchi hiyo kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

Naye Bi. Youngju alimuelezea Naibu Waziri Byabato juu ya mpango wa Jamhuri ya Korea wa kuandaa Mkutanoo kati ya Nchi yake na Viongozi wa Bara la Afrika uliopangwa kufanyika mapema mwezi Juni 2024 na kwamba anaialika rasmi Tanzania ishiriki katika mkutano huo.
 Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato akimsikiliza Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea, Bi. Oh Youngju walipokutana kwa mazungumzo pembezoni mwa Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha.
Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea, Bi. Oh Youngju yaliyofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha.
Mazungumzo yakiendelea

KISWAHILI NYENZO MUHIMU KATIKA KUKUZA BIASHARA KATI YA TANZANIA NA MALAWI

Serikali ya Tanzania itaendelea kukuza na kuhamasisha matumizi ya Lugha ya Kiswahili ili kuimarisha biashara inayovuka mipaka hususan katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ikiwemo Malawi.



Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Agnes Kayola alipokitembelea Chuo Kikuu cha Biashara na Sayansi cha nchini humo kwa lengo la kujadiliana na Uongozi wa Chuo hicho kuhusu namna bora ya kuanzisha ushirikiano baina na taasisi za elimu za Tanzania hususani katika kufundisha Lugha ya Kiswahili.



Katika mazungumzo yake na Mkuu wa Kitivo cha Elimu, Mawasiliano na masuala ya Habari wa Chuo hicho, Dkt. Kizito Elijah, Mhe. Balozi Kayola alisema kuwa, upo mwingiliano mkubwa wa kibiashara baina ya Tanzania na Malawi unaosababisha mahitaji makubwa ya kujifunza lugha ya Kiswahili ili kurahisisha mawasiliano katika biashara.



Aliongeza kusema Serikali ya Tanzania itaendelea kusimamia na kutekeleza makubaliano yote yaliyofikiwa wakati wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoifanya nchini humo mwezi Julai 2023 ikiwemo masuala ya ufundishaji wa Kiswahili nchini Malawi.



Kwa upande wake, Dkt. Elijah alisema kuwa, Chuo hicho kimepanga kuanzisha Kituo cha Lugha na kuonesha nia ya kushirikiana na Tanzania hususan Taasisi za Elimu na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ili kutekeleza azma ya kufundisha Lugha ya Kiswahili chuoni hapo na kwamba chuo hicho kipo tayari kuanzisha ushirikiano na Vyuo Vikuu vya Tanzania ikiwa ni pamoja na kubadilishana wakufunzi na wanafunzi.



Wakati huohuo, Mhe. Balozi Kayola ameitembelea Kampuni ya Kitanzania ya Bakhresa ambayo imewekeza nchini Malawi tangu mwaka 2003 katika viwanda vya uzalishaji Unga wa ngano, sabuni za kufulia na inatarajia kukamilisha kiwanda cha kutengeneza mafuta ya kupikia mwezi Mei 2024.



Akiwa katika Kampuni hiyo Mhe. Balozi Kayola amepongeza uwekezaji mkubwa uliofanyika na kuwahamasisha kuendelea kukuza wigo wa uwekezaji wa bidhaa mbalimbali nchini humo kwani mahitaji bado ni makubwa.



Kadhalika, Mhe. Balozi Kayola alipata fursa ya kukutana na Jumuiya ya Watanzania waishio katika Mkoa Kusini, Malawi ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu ateuliwe kuiwakilisha Tanzania nchini humo.



Katika mazungumzo yake na Jumuiya hiyo aliwaasa kuendelea kuwa wawakilishi wazuri wa nchi yao kwa kufuata sheria za nchi waliyopo  ili kulinda taswira nzuri ya Tanzania.



Pia alisisitiza umuhimu wa wao kuendelea kujiandikisha kwenye Mfumo wa Kidigitali wa kuwatambua Diaspora (Diapora Digital Hub) ili iwe rahisi kuwaunganisha na fursa mbalimbali za biashara, masoko, na uwekezaji zilizopo nchini pamoja na kurahisisha utoaji wa msaada wakati wa dharura zinazoweza kuwapata katika nchi wanazoishi.



Mhe. Balozi Kayola alitumia fursa hiyo pia kuwajulisha kuhusu hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa  na Mhe. Rais Dkt. Samia huku akitaja Miradi mikubwa inayokamilishwa ikiwemo Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Nyerere, Mradi wa Reli ya Kisasa ya SGR na miradi mingine kwenye sekta ya Kilimo, Biashara na Uwekezaji.



Vilevile, Mhe. Balozi Kayola aliwaeleza Diapora hao kuwa, Ubalozi upo tayari kushirikiana nao na kuwasisitiza kuwa huru katika kuwasilisha maoni, mapendekezo na ushauri kwa manufaa mapana ya Tanzania. 

Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Agnes Kayola akizungumza  na Mkuu wa Kitivo cha Elimu, Mawasiliano na masuala ya Habari wa Chuo Kikuu cha Biashara na Sayansi cha Malawi,  Dkt. Kizito Elijah alipokitembelea Chuo hicho kwa lengo la kujadiliana na Uongozi wa Chuo hicho kuhusu namna bora ya kuanzisha ushirikiano baina na taasisi za elimu za Tanzania hususani katika kufundisha Lugha ya Kiswahili.
Mkuu wa Kitivo cha Elimu, Mawasiliano na masuala ya Habari wa Chuo Kikuu cha Biashara na Sayansi cha Malawi,  Dkt. Kizito Elijah wakati wa mkutano kati yake na Balozi Kayola (hayupo pichani)
Mhe. Balozi Kayola akiagana na Dkt. Elijah mara baada ya kukamilisha mazungumzo baina yao 

Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Agnes Kayola akipata maelezo alipotembelea Kampuni ya Kitanzania ya Bakhresa iliyowekeza nchini Malawi tangu mwaka 2003 kwenye viwanda vya kutengeneza unga wa ngano na sabuni za kufulia.
Mhe. Balozi Kayola akiendelea kupata maelezo wakati wa ziara yake kwenye moja ya kiwanda cha Kamapuni ya Kitanzania ya Bakhresa ambayo imewekeza nchini Malawi

Mhe. Balozi Kayola akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Kampuni ya Bakhresa Malawi Limited akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Bw. Mahesh Josyabhatla (wa pili kulia)
Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Agnes Kayola akizungumza na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi Mkoa wa Kusini mwa Malawi alipowatembelea kwa ajili ya kujitambulisha ikiwa ni mara ya kwanza tangu ateuliwe kuiwakilisha Tanzania nchini humo
Sehemu ya Watanzania wanaoishi Mkoa wa Kusini, Malawi wakifuatilia mkutano kati yao na Mhe. Balozi Kayola (hayupo pichani)

Mwenyekiti wa Watanzania wanaoishi Mkoa wa Kusini Malawi, Bw. Suleiman Marijani akizungumza wakati wa Mkutanoo kati ya Jumuiya hiyo na Balozi Kayola