Thursday, October 31, 2013

Jumuiya ya EAC na talaka rejea


Mhe. Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akielezea kuhusu hisia za kutengwa kwa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).   Waziri Membe alikuwa katika mahojiano maalum na Mwandishi Fredy Mwanjala wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten ofisini kwake leo, jijini Dar es Salaam.

Waziri Membe akiendelea na mahojiano hayo, wakati Bi. Fauzia Yusuph wa Channel Ten akirekodi tukio hilo. 




Jumuiya ya EAC na talaka rejea

Na TAGIE DAISY MWAKAWAGO


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb) ameelezea hisia za sintofahamu kuhusu kutengwa kwa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), na kuhoji kuwa iwaje nchi yetu itengwe na nini maana ya Jumuiya hiyo?

Aliyasema hayo katika mahojiano maalum na Mwandishi Fredy Mwanjala wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, yaliyofanyika ofisini kwake leo, jijini Dar es SalaamMazungumzo hayo yalijikita zaidi katika kujua msimamo wa Tanzania kidiplomasia wakati huu wa sintofahamu ya Jumuiya hiyo inayoendelea, hususan Tanzania ikionekana kutengwa na nchi za Uganda, Rwanda na Kenya.

“Huu ni muungano wa watu wenye woga,” alisema Waziri Membe na kuongeza kuwa Jumuiya hiyo ilishawahi kuvunjika mnamo mwaka 1977.  

“Jumuiya hiyo ilishawahi kuvunjika na kuungwa tena, na Tanzania hatukuathirika.  Tuko tayari kupewa au kutoa talaka, na ikiwezekana labda kutakuwa na talaka rejea,” alisema Waziri Membe.  Jumuiya hiyo ya EAC inazijumuisha nchi za Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi na Tanzania.

“Sisi ndio ‘center of gravity’ na ndio soko kubwa la bidhaa katika ukanda wa Afrika Mashariki - tuna rasilimali zaidi ya majirani zetu, tuna utajiri wa ardhi na bandari nne ambazo ni ufunguo wa kutumia bahari kubwa na kufikia nchi nyingine duniani,” alifafanua Waziri Membe.  Bandari hizo ni za Mtwara, Tanga, Dar es Salaam na bandari ya Bagamoyo ambayo ipo katika ujenzi wa kuifanya iwe bandari kubwa ya kimataifa barani Afrika.

Waziri Membe alisema cha kushangaza ni kwamba majirani zetu wanatakiwa kutambua kuwa Tanzania ni nchi ambayo ni mfano pekee wa kuigwa kwa uzoefu wa muungano.  “Sisi ni taifa na sio muungano wa makabila matatu au manne,” alisema Waziri huyo.

“Hauwezi leo ukaitaifisha ardhi ya nchi nyingine na kuviacha vizazi vijavyo bila mali,” alisema Waziri Membe na kuongeza kuwa “kwa vyovyote vile, jumuiya hii ya Afrika Mashariki lazima iende kwa taratibu.”

Aidha, Waziri Membe alienda mbali zaidi na kusema kuwa huenda chokochoko ya kutengwa kwetu inatokana na wivu au gere kwa Tanzania kupeleka majeshi yake huko Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, jambo alilosema huenda halijawafurahisha baadhi ya watu katika Jumuiya hiyo.

Vilevile alisema kuwa kitendo cha Tanzania kukataa ardhi kuwa sehemu ya mali ya Afrika Mashariki huenda pia imepelekea mchango mkubwa kwenye choko choko hizo.

Waziri Membe amewaambia Watanzania kuwa “wakae wakijua kwamba akufukuzae hakwambii toka, utaona tuu mambo yanabadilika.”


Mwisho.



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.